Hivi ndivyo wanavyotutawala

Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein katika picha ya pamoja wajumbe wa tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) Ikulu Mjini Unguja
Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein katika picha ya pamoja wajumbe wa tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC) Ikulu Mjini Unguja

MBONA mambo yanakwenda msegemnege? Mara mkuu huyu wa serikali husema hivi, mara mwengine husema kinyume na hivyo. Umma unababaika, haujui ulishike lipi. Huko ni kutawala kwa kubabaisha. Inamkinika kwamba ubabaishaji huu tunaoushuhudia ni wa kudhamiria. Inawezekana kwamba ubabaishaji huo wa watawala ni sehemu ya mkakati wa makusudi wa kulifanya taifa liyakubali wayatendayo na wayatakayo watawala.

Siku hizi tunayashuhudia mengi kwa watawala wetu yenye kutia wasiwasi. Kubwa kabisa ni jinsi watawala walivyoufanya ulaghai uwe kigezo muhimu cha kupima mafanikio yao katika uendeshaji wa serikali. Kila wanapozidi kuulaghai umma ndipo wanapohisi kwamba wameweza kweli kuudhibiti na kushurutisha wayatakayo.

Ulaghai utazidi Tanzania kila taifa litapozidi kuukaribia uchaguzi mkuu ujao. Kuna uwezekano kwamba huenda hata ukajitokeza katika uchaguzi wenyewe na hasa Zanzibar ambako vitimbi vya wizi wa kura si vigeni.

Ulaghai unaotumika sasa ni mkubwa na ni matokeo ya kuporomoka kwa maadili ya utawala na kuzuka kwa watawala wasio na insafu hata kidogo. Watawala wa aina hiyo huwa hawana budi ila kutumia ulaghai kama mojawapo ya mbinu zao za kutawala.
Kwa hakika, ulaghai, kama mbinu ya utawala, ulianza kutumika kwa dhati tangu palipotolewa pendekezo la kuundwa Tume Maalum ya kushughulikia utungwaji wa Katiba mpya. Wakati huo watawala walisisitiza kwamba kazi ya Tume hiyo itakuwa kukusanya maoni ya wananchi yatayokuwa msingi wa Katiba mpya. Wakaanza kuipigia debe Katiba hiyo kuwa itakuwa ‘Katiba ya wananchi’.

Umma ulifurahi. Watawala wakapongezwa. Kumbe ulikuwa ulaghai mtupu. Hayo yalidhihirika mara baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba, chini ya Jaji Joseph Warioba, kumaliza kazi yake na mswada wa Katiba wa Tume hiyo kufikishwa mbele ya Bunge la Katiba.

Hapo ndipo palipofanywa kiini macho cha kulazimisha papatikane theluthi mbili ya kura za Zanzibar, jambo ambalo kwa mambo yalivyokuwa, na yalivyo hadi sasa, ni muhali. Rais aliyeahidi kutouingilia mchakato wa Katiba alikuwa hana junaa alipouingilia na kusema anayoyataka na asiyoyataka alipokuwa analifungua rasmi Bunge hilo la Katiba.

Halafu pakazuka suala la kulazimisha kura ya maoni kuhusu Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa ambayo, kwa kweli, haikuwa tena Katiba ya wananchi kama taifa lilivyoahidiwa. Serikali ilishikilia kwamba kura hiyo itapigwa Aprili 30, ijapokuwa wengi walikuwa wakisema kwamba jambo hilo ni muhali. Mambo hayakuwa tayari.

Rais akaingilia kati na kutamka hadharani kwamba kura ya maoni itapigwa Aprili 30. Wakuu wengine wa serikali wakaungama juu ya kuwa kila mtu akitambua kwamba Daftari la Wapiga Kura halikukamilika. Hii ni kwa sababu vifaa vya kuwasajili watu kwa mfumo wa kutumia teknolojia (Biometric Voter Registration au BVR) havikuwasili nchini.

Ni kipi kilichowapelekea wakuu wa serikali washikilie kwamba kura hiyo ya maoni itapigwa mwishoni mwa Aprili ijapokuwa wenye macho na akili walikwishaona, na kusema wazi,kwamba jambo hilo haliwezekani?
Kuna umati mkubwa wa wananchi wenye haki ya kupiga kura ambao bado hawajasajiliwa. Watawala walikataa kuyasikia hayo. Walishikilia kwamba kura ya maoni lazima itapigwa Aprili 30.

Hatimaye, serikali imetoa kauli yake rasmi naya mwisho kuhusu suala hilo. Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Damian Lubuva ametangaza kwamba hakuna kura ya maoni itayopigwa Aprili 30. Inasema kwamba kura hiyo itapigwa baadaye. Tarehe halisi bado haijatangazwa lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba kwa hali ya mambo ilivyo huenda isiwe kabla ya uchaguzi mkuu ujao.

Uamuzi huo wa kuiahirisha kura ya maoni utaiwezesha Tume ya Taifa ya Uchaguzi ijitayarishe upya ili iweze kuhakikisha kwamba watu wengi zaidi wataandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura. Na kuna suala tete la Muungano. Katiba inayolazimishwa na watawala yenye kulazimisha paendelee kuwepo mfumo wa Muungano wenye serikali mbili haina nia njema kwa mustakabali wa Muungano. Hii ni kwa sababu inakwenda kinyume na matakwa ya wananchi wengi wenye kutaka muundo wa Muungano ubadilishwe.

Kushikilia pawepo serikali mbili ni kudharau matakwa ya wananchi na kuwanyima haki yao ya kukipata wakitakacho. Hatari iliyopo ni kwamba muundo huu wa sasa ukiendelea kutazidi kutokea mvutano kuhusu suala la Muungano.
Septemba 8, 2014, Rais Jakaya Kikwete alikutana na viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Viongozi hao wanasema kwamba waliafikiana kuhusu mambo manne ambayo wanataka yaingizwe katika Katiba ya 1977 itayokuwa inatumika wakati wa uchaguzi ujao. Mambo yenyewe ni:
– kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi;
– ushindi wa Rais kuamuliwa kwa asilimia zaidi ya 50;
– kuruhusiwa wagombea huru kuwania nafasi za udiwani, ubunge na urais; na
– kuruhusiwa matokeo ya uchaguzi wa urais kupingwa mahakamani.

Sio hayo tu yaliyokubaliwa katika huo mkutano wa Septemba 8 kati ya Rais na viongozi wa Ukawa. James Mbatia, aliye mwenyekiti mwenza wa Ukawa, amesema kwamba katika kikao hicho walitiliana saini kwamba endapo uchaguzi mkuu ujao utafanyika chini ya Katiba ya 1977 basi Bunge lingekutana Novemba mwaka jana kufanya marekebisho hayo 15 ya Katiba yaliyopendekezwa.

Na ikiwa Bunge lisingeliweza kukutana Novemba basi, Mbatia alisema, walikubaliana likutane Februari, mwaka huu. Inavyoonyesha ni kwamba watawala walifanya ulaghai tu wa kujidai wanayakubali mambo ambayo kwa kweli walikuwa hawana nia ya kuyatekeleza.

Mambo yote hayo manne yalikuwemo katika Rasimu ya Pili ya Katiba iliyopendekezwa na Tume ya Warioba lakini yalifutwa na watawala kupitia Bunge la Katiba. Mlikuwamo na mengi mengine katika Rasimu hiyo yaliyo na umuhimu kwa taifa na kwa kustawisha demokrasia na ambayo watawala, kupitia Bunge la Katiba, waliyatoa. Miongoni mwa hayo ni miiko ya uongozi na uwajibikaji wa wabunge.

Ni jambo la aibu kabisa na lenye kuhuzunisha kuona kwamba watawala wamethubutu kuondosha miiko ya uongozi katika Katiba inayopendekezwa na kuondosha kipengele kinachowataka wabunge wawe wanawajibika. Inathibitisha wazi kwamba hawa watawala tulio nao hawana nia safi na mustakabali wa taifa.

Wananchi,kwa jumla, wanataka wawe na viongozi wasio na doa kama matone ya mvua kutoka mbinguni. Lakini watawala wetu wao wako radhi kuliachia taifa liwe linaongozwa na watu walioukumbatia ufisadi, wasiojali ikiwa utawala wao ni mbovu na wala wasiojali ikiwa wananchi wananyimwa na kudhulimiwa haki zao.

Hawana haja na maadili. Wakishapata ridhaa ya wananchi huwa hawana haja nao tena, wangependelea hata watokomee ili wasiweze kuzidai haki zao. Si ajabu kuwa watawala wetu waliichezea hivyo Rasimu ya Katiba iliyopendekezwana wananchi kwa sababu ni kawaida yao kudanganya ili waweze kuliburuza taifa lende watakako, utadhani hili taifa ni punda.

Labda ndivyo walionavyo taifa hili kwamba ni sawa na punda na ndio maana wako tayari kutumia ulaghai na nguvu zao zote kulifanya liwasikilize, liwatii na lifikiri kuwa hakuna waokozi kama hao. Na ndio maana pia ikawa watawala wanakuwa tayari kuwatandika mikwaju wale wananchi wenye kuonyesha ujasiri wa kutetea haki zao ama kwa kuandamana au kwa kuchukuwa hatua nyingine za amani.

Lakini Watanzania si punda na wala hawana hulka ya punda. Ni binadamu wenye kufikiri na wenye kutambua kwamba kuishi si kuzaliwa, kufanya kazi na kufa tu. Wanatambua kwamba kuishi kunahitaji zaidi ya hayo.Kunahitaji maisha yenye maana yaliyoonja ladha ya ujasiri.

Kuishi kunahitaji kiwango fulani cha ujasiri. Mwenye kuishi atakuwa kweli ameishi endapo atathubutu kupigania haki na kupambana na madhalimu wa dunia hii. Ninaamini kwamba iko siku watanyanyuka na kuwaambia watawala: “Basi, yanatosha. Tumeshaung’amua ulaghai wenu. Mmetughilibu vya kutosha.”

Ujasiri wa aina hiyo hata ukiwa mgumu wa kutoa jasho, na mchungu wa kutoa nyongo,hatimaye huwa na ladha nzuri. Mara nyingi matokeo ya mapambano huwa na utamu usio na kifani. Mapambano hayo si lazima yawe ya kupigana kwa silaha. Yanaweza yakawa mapambano ya fikra kwa fikra. Ya wananchi kupambana na wanasiasa wenye kutumia ulaghai kwa kutowapa kura zao.

Huu ni wakati wa wapiga kura kuanza kufikiria namna ya kuwapima wataogombea kura zao. Wawe werevu na wazalendo kwa kutowachagua viongozi wenye kuwaahidi mustakabali usio na mustakabali. Huo ni mustakabali usio na maslahi kwa taifa kwa sababu hauzingatii haki za taifa na za wananchi. Kwa ufupi, ni mustakabali unaozaa dhana kinzani ya kuufanya usiwe mustakabali mwema. Kwa hivyo, unakuwa mustakabali usio na mustakabali.

Advertisements

One Reply to “Hivi ndivyo wanavyotutawala”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s