Tusidangayane imeingia siasa kwenye ZanID

Mkurugenzi wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZanID) Zanzibar, Mohemmed Ame
Mkurugenzi wa Vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi (ZanID) Zanzibar, Mohemmed Ame

Na Ally Saleh

Katika hali ya kawaida wallahi hata mtu asingetarajia jambo hili liwe la ubishi seuze kuwa la kufikia hata Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuingiana maungoni na hata kikao hicho kuahirishwa kwa ajili ya
vurugu.

Katika hali ya utawala bora na kuheshimu sheria mtu hata asingetarajia ifike hadi Serikali inakataa kutekeleza sheria iliyutungwa na ambayo ina mguso na maisha ya kila siku ya mwananchi na kujikinga na
kujilinda kwa sababu za kisiasa.

Mtu angekuwa akitarajia kuwa suala hilo hivi sasa lisingekuwa kabisa hoja maana kwa hali yoyote ingekuwa tayari hivi sasa, kama kungekuwa na nia njema, hivi sasa kila mtu angekuwa na kitambulisho cha
Mzanzibari Mkaazi au maarufu kama ZanID.

ZanID inatakiwa kwa sheria itolewe kwa kila Mzanzibari anaeishi Zanzibar na ambaye ametimiza umri wa miaka 18, na kusema kweli kama kungekuwa na mipango na utekelezaji makini sidhani kwamba Mwakilishi
wa Jimbo la Ole Hamad Masoud angetaka kufikisha Hoja Binafsi katika Baraza la Wawakilishi.

Lakini Hamad Masoud akaamua wiki iliyopita kufanya hivyo kwa sababu kuna Wazanzibari kadhaa wenye sifa na kupindukia ambao kwa makusudi mazima wanakoseshwa haki hiyo ikiaminika ni kwa sababu ya kisiasa. Na hilo la kila kitu kuingizwa katika siasa kwa Zanzibar sio jambo geni.

Sheria ya Vitambulisho inasema wazi kuwa kila mtu lazima atembee na kitambulisho na Polisi wanayo haki kumuuliza mtu yoyote kitambulisho hicho wakati wowote, lakini Serikali inashindwa kutekeleza jambo hilo
kwa kuwa inajulikana kuwa kuna watu hawapewi vitambulisho hivyo na kwa hivyo jambo hilo likifanywa Serikali itaaibika.

Hivi sasa kila ajira ya Serikali; kila ombi Serikalini kama vile leseni na mambo mengine mtu hutakiwa kuonesha kitambulisho chake cha ZaniD na kila mwanafunzi anaeingia Chuo Kikuu hutakiwa kuwa na ZanID
kiasi ambacho inatia shaka kwa nini bado suala la vitambulisho liwe la kusuasua.

Suala la watu wangapi, wapo wapi na wa aina gani hawana vitambulisho hivyo limefanywa kuwa gumu sana. Juzi katika Baraza la Wawakilishi wajumbe wa CCM waliungana na upande wa kusema kuwa vitambulisho vinatolewa kihalali na hapakuwa na haja ya kukubali Hoja Binafasi iliyowasilishwa kutaka Kurugenzi inayohusika ichapuze utoaji vitambulisho na katika hali ya uwazi.

Ilikuja ikadhihirika Barazani hapo wajumbe wengi wa CCM wakichanganya siasa za ushindi wa uchaguzi na suala la vitambulisho vya ZanID wengi wakielekea kusema wazi kuwa Hoja Binafsi hiyo imekuja ili kujaribu
kupata wapiga kura zaidi kwa chama cha CUF kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Baadhi ya wajumbe waliochangia hawakuwa hata wakijua mahitaji ya sheria hiyo ili mtu aandikishwe yanasemaje huku wakipinga ukweli ambao upo wazi hapa Zanzibar kwamba kuna watu wengi wasiohusika kabisa kupata vitambulisho hivyo ambao wanatokea Tanzania Bara ambao wanavyo vitambulisho hivyo.

Kwa maelekezo makhususi watu kama hao wamesaidiwa na Masheha ambapo ni Masheha hao hao wamekuwa wakitajwa kuwa ni wakorofi kupita kiasi kuwazuia vijana na Wazanzibari wengine kuanza mchakato wa kupata ZanID kwa kukata kuwapa barua za kwenda kuwatambulisha afisi husika.

Malalamiko ya masheha yamekuwa makubwa hadi yamezibuwa masikio, lakini Serikali ya Zanzibar haisikii kabisa. Masheha mtu anajiuliza. wanapataje jeuri hii kama hawakupewa?

Basi baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika kukataa hoja hiyo wakasema kuwa watu kutoka Pemba wamekuwa wakijazana Unguja kuomba vitambulisho hivyo bila ya kujua kuwa kwa mujibu wa sheria
kitambulisho hicho hakitolewi kwa ukaazi ila hutolewa kwa Uzanzibari.

Kinyume na kitambulisho cha kura ambacho una kipata kwa Uzanzibari lakini pia kwa kutambua ni mpiga kura wa eneo fulani, unakipata pia kwa utambulisho wa Sheha kama wewe ni mkaazi wa jimbo fulani la
uchaguzi maana ni lazima tume ijue hesabu ya wapiga kura.

Lakini kwa kutoelewa na pia udhaifu wa sheria na kupewa nguvu Masheha wamekuwa wakihusisha ukaazi wa mtu na kitambulisho cha ZanID. Mimi ningefikiri kuwa Kurugenzi ya Vitambulisho ingekuwa na utaratibu
ambapo  tatizo hilo lingefanyiwa kazi.

Pia Kurugenzi hiyo kama ingekuwa na umakini wallahi hata kusingekuwa na zogo la vitambulisho hivyo. Kwa mfano toka ianzishwe ni miaka 10 ingekuwa kila mwaka inatoa vitambulisho kwa wanafunzi wote wa wa kuanzia Kidato cha Nne leo kusingekuwa na mlundikano hata wa watu ambao walipitia mfumo rasmi wa elimu kukosa vitambulisho hivyo.

Wawakilishi wengi wa CUF walienda na madai kadhaa ya watu ambao wamekoseshwa haki hiyo lakini wale wa CCM waliyapuuza wakisema utaratibu mtu akikwama kwa Sheha aende kwenye Kurugenzi na akikwama
aende Mahakamani huku wakifanya kama hawajui ugumu wa taratibu hizo kwa mtu wa kawaida.

Hapa napenda kutoa shuhuda mbili ambazo hata Mkurugenzi wa Vitambulisho Muhammed Juma Ame jambo hilo analijua vizuri na hakuna mtu yoyote ambaye ataniambia kuwa utaratibu huo unakwenda kwa haki na usawa.

Kwanza ni wa mke wangu Mwanakhamis kukataliwa na Sheha wetu Issa Ngwisa kupewa barua ya kwena kujiandikisha kwa miaka mitatu hadi nilipokwenda binafsi kwa Mkurugenzi Ame. Ikiwa mke wa mtu kama mimi anaweza kufanyiwa vitimbi vipi kwa watu wa kawaida?

Pili mwaka 2009 nilikusanya majina zaidi ya 800 ya wazee na vijana wasiokuwa na vitambulisho vya ZanID kwa Mji Mkongwe peke yake na kumpelekea Mkurugenzi Ame na kumjuburi kuwa nitawapeleka wote ukumbi wa Hoteli ya Bwawani aje kuwahakiki na kuwapa haki yao.

Lakini baada ya kuhangaika na majibizano ya barua kadhaa nadhani waliopata kuandishwa hawakuzidi 100 tena kwa juhudi zao binafsi. Huo ndio ukweli lakini Zanzibar panapoingia siasa ukweli hauonekani.

Tusijidanganye bure vitambulsho vya ZanID vimeingia siasa na ni suala la kuongeza au kupunguza nambari za wapiga kura. CUF wasiote kuwa watafanikiwa suala hili kwa urahisi maana CCM kwa kila hali na mali watataka kudhibiti rasilamali hii muhimu na kwa bahati mbaya zaidi ikisaidiwa na Kurugenzi yenyewe ambayo ilipaswa kutenda haki.

Chanzo: Mtanzania

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s