Mtanzania anayetuhumiwa kwa ugaidi Kenya kizimbani

Rashid Charles Mberesero
                                                           Rashid Charles Mberesero

Dar/Dodoma/Nairobi. Mtanzania anayedaiwa kuhusika katika shambulizi la kigaidi lililoua watu 148 katika Chuo Kikuu cha Garissa – Kenya, Rashid Charles Mberesero, jana alifikishwa mahakamani na kuwekwa kizuizini kwa mwezi mmoja wakati polisi wakiendelea kukusanya ushahidi dhidi yake.

Mtuhumiwa huyo ambaye pia anafahamika kwa jina la Rehani Dida alirejeshwa Nairobi kutoka Garissa alikopelekwa awali kwa ajili ya kuhojiwa baada ya kukiri kujihusisha na kundi la Al- Shabaab.

Mahakama jijini Nairobi ilisema jana kuwa mtuhumiwa huyo ambaye hakutakiwa kujibu tuhuma hizo na wenzake wanne watalazimika kuwa chini ya uchunguzi mkali wa polisi kwa kipindi cha mwezi mmoja na baadaye wanaweza kusomewa mashtaka ya kuhusika katika shambulizi hilo lililoua watu hao, wengi wao wakiwa ni wanafunzi.

Haikufahamika mara moja sababu za kuamuliwa kuwekwa kizuizini kwa muda huo mbali ya taarifa kueleza kuwa ‘watashikiliwa na polisi tena katika kituo cha siri’.

Mwendesha Mashtaka, Daniel Karuri aliiambia Mahakama hiyo kuwa Mtanzania huyo ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tano, alikuwa amepanga safari ya kuelekea Somalia kwa ajili ya kujiunga na makundi ya kigaidi.

Watuhumiwa hao ni kati ya 14 waliotiwa mbaroni hivi karibuni baada ya shambulizi hilo la kigaidi.

Mahakama hiyo pia imewaamuru washukiwa wengine kuendelea kushikiliwa na polisi kwa muda wa siku tano hadi 15.

Awali, Karuri aliiambia Mahakama hiyo kuwa polisi walikuwa wakifuatilia kwa karibu uhusiano baina ya wale waliofanya shambulizi hilo na mfanyabiashara mmoja anayemiliki hoteli mjini Garissa. Inasemekana kuwa watu waliotekeleza shambulio hilo walikuwa wamelala katika hoteli hiyo.

Hakula chakula cha shule

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Kigwe, mkoani Dodoma alipokuwa akisema Mberesero baada ya kufaulu kutoka Gonja, wamesema hakuwahi kula chakula chochote shuleni kwa kipindi cha mwezi mmoja aliokaa akisubiri kuhamishwa na kubadilishiwa mchepuo wa masomo.

Wakizungumza na mwandishi wetu shuleni hapo jana, wanafunzi wa kidato cha tano, Yoram James na Thomas Godwin, walisema siku zote alizoishi shuleni hapo alikuwa akila kwa mama lishe jirani na shule hiyo.

“Lakini alikuwa na mkarimu kwetu wakati mwingine alikuwa akitununulia maandazi ya kunywea chai,” alisema Yoram.

 Chanzo: Mwananchi

 

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s