Karume alitisha akikutolea jicho

Aliyekuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi ambaye baadae alihukumiwa kifo kwa kosa la uhaini na alikaa jela miaka 10
Aliyekuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi ambaye baadae alihukumiwa kifo kwa kosa la uhaini na alikaa jela miaka 10

Salma Said, Mwananchi

Miongoni mwa mambo ambayo watu waliomfahamu Mzee Abeid Amani Karume wanasema, ni pamoja na kuwa na hali ya kutisha hasa anapoambiwa jambo ambalo hakulipenda.

Hali hii ilishawahi kumkuta mzee Khamis Abdallah Ameir (85),anayesema aliwahi kutazamwa kwa jicho kali na Karume na tangu siku hiyo hakurudia kusema jambo lililomuudhi.

Akiwa mjumbe wa Baraza la Mapinduzi, anakumbuka siku moja Karume aliitisha kikao cha baraza na kuwapa taarifa za kutaka kuunganisha Tanganyika na Zanzibar.

Baada ya Mzee Karume kuwaeleza wajumbe, anasema walikaa kimya na kisha yeye akasimama na kushauri iitishwe kura ya maoni ili wananchi waulizwe kama wanakubaliana na kuunganishwa kwa nchi hizo.

Baada ya kutoa ushauri wake, Mzee Karume alimtupia jicho kali, hali iliyomfanya aufyate mkia hadi mwisho wa kikao.

‘’Alinitolea macho na macho yake yalikuwa ni makali, halafu akikutizama kwa muda mrefu unamuona kama ana kengeza hivi katika jicho lake moja” anasema mzee Ameir huku akicheka.

Anasema kuwa kwa hali ilivyokuwa ukumbini hasa baada ya jicho lile, hakuna aliyemuunga mkono na kimsingi wajumbe wengi walijawa na hofu.

Niligopa kwa sababu nilikuwa nasema sijui itakuwaje, lakini ndiyo nilishasema. Nilikuwa nafikiri nitakuja kuchukuliwa au vipi…’’ anaeleza.

Kiasili anasema Mzee Karume alikuwa mtu wa kuogopwa kutokana na ukali wake, na ndiyo maana watu wengi hawakuthubutu kumsogelea au kukataa kutekelezaa amri na maagizo yake.

‘’Alikuwa mcheshi lakini tabia yake ya kuogopwa ndiyo iliwafanya watu wengi waogope kushauriana naye mambo. Kila mmoja alikuwa anaogopa hajui atafikwa na jambo gani,’’ anasema.

Ameir ambaye baadae baada ya kifo cha Mzee Karume alikamtwa na kushitakiwa kosa la uhaini kwa kuhukumiwa kifo lakini alikata rufaa ndipo alipohukumiwa kufungwa jela miaka 30 lakini alikaa jela miaka 10 kisha akatolewa.

Hata hivyo anasema siku zile watu wakikamatwa kamatwa ovyo na kufunguliwa kesi hata kama hawana hatia lakini kwa kuwa waendesha mashitaka pamoja na majaji hawakuwa ni watu wenye elimu wakichukuliwa tu na kuwekwa wasimamia vyombo vya sheria bila ya elimu.

Siku zile watu walikuwa hawajasoma ndio wakitoa hukumu mimi nimehukumiwa kifo lakini huyo jaji anatwambia nyinyi nyote kama samaki wangu katika susu nikitaka nitamuawacha huyu na nisiyemtaka nitamtoa kwa hivyo hivyo ndivyo kesi zilivyokuwa zikiendeshwa…dhulma tupu na hakuna anayelalamika hakukuwa na vyombo vya kutetea haki za binaadam” alisema

Ameir anamsifu Mzee Karume kwamba alikuwa mtu mzuri lakini tatizo kubwa alililokuwa nalo alikuwa na washauri wabaya na hawajasoma wakiendesha mambo kwa utashi na chuki tu na hivyo kusababisha mambo mengi mabaya kutokea wakati wa uhai wake Mzee Karume.

Mzee Karume mbali na kukutolea mambo kama utatoa kauli ambayo haipendi lakini pia alikuwa ana tabia ya kutoa maamuzi ya haraka haraka bila ya kufikiria mfano anapoambiwa jambo na mmoja katika wajumbe wake wa baraza la mapinduzi.

Aidha pia alikuwa na tabia kuwashambulia watu bila hata ya wasiwasi na ndio maana mara kadhaa katika wajumbe wake wale ambao wakiendesha mambo ovyo aliwatishia kuwaondosha na kuwafukuza kazi.

Mfano mmoja Mzee Karume alishawahi kumwambia Edington Kisasi nitakurejesha kwenu Moshi kama utaendelea kufanya mambo ya ovyo hapa, na pia alishawahi kusema mtu mmoja nitakurejesha ukchume embe kwenu shamba huko”. alisema Mzee mmoja ambaye walikuwa pamoja kwenye chama cha ASP ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini

Karume pia alikuwa mwepesi kukusukumia ngumi na kukujibu jambo lolote ambalo lipo mbele yake bila ya kuzingatia nafasi yake aliyonayo kwa kuwa ameondokea katika ubaharia na wenzake wengi wa Bandarini Malindi walikuwa wakimfahamu kutokana na tabia hiyo ya ubabe na matusi.

“Yeye alikuwa anatukana tu wala hajali lakini ndio tabia yake kaizowea hiyo na sisi wenzake tuliomzowea tukenda naye hivyo hivyo lakini alikuwa mbabe na anayejiamini sana”  Alisema.

Aliongeza Mzee huyo kwamba “Karume akitisha bwana tena akitisha maana hakuwa anataka mchezo lakini ile kutukana alishazowea kama kule Malindi akenda kwa washihiri akiwatukana ovyo hata alipokuwa rais akiwaambia watu wake wa usalama msimkamate huyi tulikuwa tunasalimiana lakini kishatukana yeye anasema hiyo ni salamu” alisema Mzee huyo.

Wajumbe wa baraza la Mapinduzi waliobaki ni watano akiwemo yeye Khamis Abdallah Ameir, Mzee Hassan Nassor Moyo, Ramadhan Haji, Aboud Jumbe Mwinyi na Hamid Ameir.Said

 

Advertisements

One Reply to “Karume alitisha akikutolea jicho”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s