Falsafa ya Karume juu ya maisha na maendeleo

Majengo ya Michenzani ambayo yameachwa yakiharibika bila ya matengenezo
Majengo ya Michenzani ambayo yalianzishwa na Mzee Karume yameachwa yakiharibika bila ya matengenezo

Salma Said, Mwananchi

Miaka 43 baada ya kifo cha Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Sheikh Abeid Aman Karume, wananchi wengi wa Zanzibar wanakiri kuwa warithi wake wameshindwa kuendeleza falsafa yake kuhusu mapinduzi na maendeleo.

Katika makala haya, mwanadiplomasia maarufu wa Zanzibar, Muhammed Yussuf Mshamba, anazungumzia maisha na falsafa ya Sheikh Karume katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Dhana ya mapinduzi

Mshamba anasema: Kwa mtazamo wa Karume, dhana ya Mapinduzi Daima ilimaanisha kuondoa dhuluma na kuweka utawala wenye lengo la kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli na endelevu.

Kifo chake kimetuondolea kiongozi aliyeamini kwa dhati haja na umuhimu mkubwa wa kuwaletea wananchi wa Zanzibar maendeleo bila ya kujali itikadi zao za kisiasa, kabila, rangi wala dini.

Kimaisha alipenda kuona Wazanzibari wanaishi vizuri. Kwa hivyo, alijenga nyumba bora za maendeleo nchini kote, mijini na vijijini na kuwapatia wananchi bila ya malipo na bila ya ubaguzi wa aina yoyote ile. Alitoa huduma ya afya, matibabu na elimu bila ya malipo kwa wananchi wote bila ya ubaguzi. Alijenga shule za msingi na sekondari na hospitali na vituo vya afya nchini kote.

Alijiweka karibu na wananchi na ndiyo maana alianzisha wizara maalumu ya kuweka hali za wananchi sawa, kwa madhumuni ya kuwasaidia Wazanzibari wasiokuwa na uwezo wa kujikimu mahitaji yao ya kila siku.

Katika kujua thamani ya utu uzima na uzee, aliamua kujenga nyumba za wazee na kuwapatia huduma na makazi ya kudumu watoto mayatima pale Forodhani.

Zanzibar na maendeleo

Kuanzishwa kwa kituo cha televisheni ya rangi cha kwanza katika Bara la Afrika, inaelezwa kuwa ni miongoni mwa juhudi zake za kuiletea Zanzibar maendeleo.

Alipenda kuiona nchi yake ikiwa na maendeleo ya juu, na mfano mwingine wa juhudi hizo ni kujenga hoteli ya kisasa iliyojulikana kwa jina la Bwawani. Alifanya hivyo kwa kutambua kuwa visiwa ni sehemu nzuri kwa utalii.

Aidha, Mshamba anasema: Mzee Karume alianzisha viwanda, vikiwamo kiwanda cha sukari kilichopo Mahonda, kiwanda cha viatu Mtoni; na kiwanda cha kutengenezea zana za matrekta Mbweni.

Si maendeleo ya viwanda tu, lakini hata katika ajira. Mzee Karume hakuwa nyuma, alitoa ajira kwa wananchi wengi wa Zanzibar, kwa sababu hakupenda kuwaona vijana wa Kizanzibari wakitangatanga ovyo mitaani bila ya kuwa na kazi za kufanya tofauti na hivi sasa.

Wananchi na chakula

Mzee Karume alitaka Zanzibar ijitosheleze kwa chakula tena kutoka ndani badala ya kuagiza kutoka nje. Kutimiza azma hii, alianzisha mashamba ya mpunga Unguja na Pemba na kutoa wito kwa vijana kuendeleza mashamba hayo. Aliagiza matrekta ya kutosha kutoka China kwa ajili ya kutumika katika kilimo hicho kwa kutumia nyenzo na zana za kisasa

Alianzisha maduka ya Serikali nchini kote na kuyajaza bidhaa mbalimbali. Wafanyakazi wa Serikali waliwekewa utaratibu maalum wa kuwawezesha kukopa katika maduka hayo kila mwezi.

Karume na michezo

Mshamba anasema: Mzee Karume kama mchezaji wa zamani, aliupenda mchezo wa mpira wa miguu. Kwa hivyo, kwa msaada wa serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, alijenga kiwanja cha michezo cha kisasa chenye ubora zaidi kuliko vingine vyote katika Afrika Mashariki.

Alikipa kiwanja hicho jina la Amani, ili kuhakikisha kuwa timu zote zitakazocheza kiwanjani hapo zitafanya hivyo kwa amani bila ya kupigana. Alivipatia msaada wa kifedha vilabu vya Yanga na Simba vya Tanzania Bara, ili viweze kujiimarisha zaidi katika kukuza mchezo huo.

Hakuwa nyuma na utamaduni

Kuhusu mila na utamaduni wa Zanzibar, Karume aliendeleza ngoma za jadi na kienyeji za Zanzibar kama vile, kunguwia, bomu, msewe na taarab. Alivipatia misaada ya hali na mali vikundi vya taarab kama vile Culture, Malindi, Navy na vingi vinginevyo.

Mara kwa mara alihudhuria hafla maalumu za maonyesho ya ngoma za kienyeji na kutoa tunzo kwa wachezaji bora. Pia, Karume hakuwacha kuhudhuria maonyesho ya taarab katika kumbi mbali yaliyokuwa yakitumbuizwa na vikundi vya Culture na Malindi.

Mtu wa watu

Karume alikuwa ni mtu wa watu, ambaye hakusahau rafiki zake aliocheza au aliofanya nao kazi wakati wa ujana wake. Karibu wote wale aliojuana nao aliwasaidia kwa namna moja au nyingine; tena bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Kuna wale aliowapatia kazi katika utumishi wa Serikali au mashirika ya umma; na kuna wale aliowaweka karibu naye kwa ushauri au kucheza nao karata na dhumna

Chini ya utawala wa Karume, milango ya Ikulu ilikuwa wazi kwa kila mtu, kwa madhumuni ya kumuelezea shida au matatizo yake.

Mshamba anamalizia kwa kusema:“Kwa jumla, pamoja na mabaya yake, hapana shaka kuwa Wazanzibari wengi wa rika langu watamkumbuka Karume kwa mema yake haya; hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa viongozi wote waliomfuatia wameshindwa kutimiza angalau robo tu ya maendeleo yaliyopatikana chini ya utawala wake”.

 Chanzo: Mwananchi

 

Advertisements

One Reply to “Falsafa ya Karume juu ya maisha na maendeleo”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s