JK awaambia polisi wakae mguu sawa

Rais Jakaya Kikwete akikagua gwaride maalumu wakati wa hafla ya kuwatunukia vyeo maofisa 289 wa Polisi katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam jana Picha: Mwananchi
Rais Jakaya Kikwete akikagua gwaride maalumu wakati wa hafla ya kuwatunukia vyeo maofisa 289 wa Polisi katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam jana
Picha: Mwananchi

Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete amelikata Jeshi la Polisi nchini kujiandaa kikamilifu ili kukabiliana na vurugu zozote zitakazojitokeza wakati wa uandikishaji wapigakura, upigaji Kura ya Maoni ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.

Akifunga mafunzo ya maofisa warakibu wasaidizi katika Chuo cha Taaluma ya Polisi, Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema dalili zinaonyesha kwamba kuna watu wenye nia ya kuhatarisha amani katika matukio hayo.

“Tunayoyasikia na tunayoyaona yanaashiria kuwapo kwa dalili za wenzetu kukwamisha shughuli hizi za kitaifa kwa kufanya vurugu, Jeshi la Polisi jiandaeni na vitendo vyote vitakavyofanywa kwa lengo la kuhatarisha amani,” alisema akijibu maombi ya kupatiwa vifaa yaliyowasilishwa kwake na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Ernest Mangu.

Alisema Serikali itahakikisha kazi ya uandikishaji katika daftari la wapigakura, upigaji wa kura ya maoni na uchaguzi mkuu vinafanyika kwa amani na utulivu kwa gharama zozote.

Alisema ili kufanikisha kazi hiyo, Serikali italiwezesha Jeshi la Polisi ili litekeleze kikamilifu majukumu yake ya kulinda amani na utulivu.

“Tutawawezesha kwa kuwapa vifaa ili kuhakikisha mnafanya kazi yenu ya kutunza amani kwa umakini zaidi,” alisema Rais Kikwete anayemaliza muda wake wa mihula miwili ya urais baada ya uchaguzi mwaka huu.

Iwapo mambo yote yatakwenda kama yalivyopangwa, Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa itapigwa Aprili 30 wakati Uchaguzi Mkuu utafanyika Oktoba.

Profesa Lipumba apinga

Akizungumzia kauli hiyo ya Rais Kikwete, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema, “Rais Kikwete yeye ndiye mtu wa kwanza kuivuruga amani kwa kutangaza tarehe ya kufanyika kwa kura ya maoni wakati siyo jukumu lake na jukumu hilo ni la NEC, Serikali yake kushindwa kuratibu vyema mchakato wa uandikishaji.

“Kama uandikishaji hauendi vizuri mpaka sasa, anavunja sheria za nchi halafu yeye mwenyewe tena anakwenda kwa vyombo vya dola na kuvieleza vijiandae wakati yeye huyohuyo ndiye ameanzisha uvunjifu wa amani tunashindwa tumweleweje,” alisema.

Profesa Lipumba alisema kinachotakiwa kufanyika kwa sasa ni NEC kutangaza tarehe kamili ya uchaguzi na uandikishaji uende kwa utaratibu tofauti na ilivyo sasa kwa mkoa mmoja wa Njombe kusuasua mambo ambayo yanaashiria uvunjifu wa amani.

Kuhusu rushwa

Akizungumzia tuhuma za rushwa dhidi ya polisi, Rais Kikwete alisema tafiti mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanyika nchini zinaonyesha kwamba taasisi hiyo bado inaongoza kwa rushwa.

“Bado kuna wenzenu wachache ambao wanachukua rushwa, wachukulieni hatua ili mwondokane na aibu hii, msikubali watu wachache waharibu sifa nzuri ya Jeshi la Polisi,” aliagiza.

Roho mbaya

Kikwete aliutaka uongozi wa Jeshi la Polisi kujenga utamaduni wa kuwapandisha vyeo askari polisi ili kuwaongezea ari ya kufanya kazi.

“Zamani viongozi wa polisi walikuwa na roho mbaya hawakuwa wakiwapandisha vyeo askari, nikawauliza kwa nini, lakini hawakuwa na majibu, inasikitisha vyeo vipo lakini mtu anasota kwa miaka mingi na kacheo kale kale, acheni roho mbaya pandisheni vyeo askari kila inapobidi,” alisema.

Alisema kuna umuhimu wa kuwa na jeshi lenye wasomi wengi ili waweze kukabiliana na mbinu mpya za uhalifu.

“Wahalifu wanaendelea kubuni mbinu za kila aina, tunatakiwa kuwa na wasomi ambao wataweza kukabiliana na mbinu hizo,” alisema.

Aliutaka uongozi wa jeshi hilo kuongeza idadi ya polisi wanawake ili kuimarisha dawati za jinsia kwenye vituo vya polisi, kitendo kitakachopunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Ujambazi

Kuhusu ujambazi, Rais Kikwete alisema katika kipindi chake, jeshi hilo limefanya kazi kubwa katika kukabiliana na ujambazi.

“Wakati naingia madarakani nilikuta matukio ya majambazi kuingia na kuiba fedha hadi benki, matukio hayo yalikuwa ya kawaida kuyasikia, nikasema majambazi hayawezi kuachwa yatambe,” alisema.

Alisema hivi sasa matukio hayo yamepungua kwa kiasi kikubwa na akalipongeza jeshi hilo kwa kazi nzuri ingawa bado kuna matukio machache.

Awali,  IGP Mangu alimwomba Rais Kikwete kuliwezesha jeshi hilo kivifaa ili liweze kujiandaa mapema na upigaji wa kura ya maoni na uchaguzi mkuu.

“Tunaomba tuwezeshwe vifaa mapema ili tuweze kuvifanyia mazoezi kabla ya upigaji wa kura ya maoni na uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani baadaye mwaka huu,” alisema.

Mkuu wa Chuo cha Maofisa wa Polisi Dar es Salaam, Ali Lugendo alisema askari 290 wamehitimu mafunzo hayo na hivi sasa watakuwa warakibu wasaidizi wa polisi.

Alisema wahitimu hao watakwenda kuwa viongozi kwenye vituo mbalimbali vya polisi vya wilaya na hivyo kuwa wasimamizi wa nidhamu kwa askari.

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s