Maalim Seif: Nipo tayari kufa kutetea wapigakura

Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akimtambulisha rasmi Mansour Yussuf Himid kwa wananchi wa jimbo la Kiembesamaki, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jimboni humo
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akimtambulisha rasmi Mansour Yussuf Himid kwa wananchi wa jimbo la Kiembesamaki, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jimboni humo

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema yupo tayari kufa kwa kutetea misingi ya haki na utawala wa sheria katika kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu.

Alisema hayo jana wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Bustanini, Kiembesamaki, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja katika mkutano ambao waziri wa zamani wa SMZ, Mansour Yussuf Himid aliutumia kutangaza kugombea uwakilishi katika jimbo hilo.

Maalim Seif alisema tayari Jeshi la Polisi limeanza kuweka mizengwe katika upatikanaji wa viwanja vya mikutano ya hadhara kwa madhumuni ya kuibeba CCM, jambo ambalo halikubaliki kwa kuzingatia misingi ya demokrasia.

Alisema kitendo cha Polisi Wilaya ya Magharibi kuzuia Uwanja wa Baraza la Wawakilishi ambao ulipangwa kutumika kwa mkutano huo kinaonyesha kuwa baadhi ya watendaji wa jeshi hilo bado hawajabadilika.

“Nakwambieni safari hii kama polisi mmeleta mabomu ya kupiga watu wakati huu wa kuelekea uchaguzi, basi safari hii mtamuua Makamu wa Kwanza wa Rais, sitakubali kuona haki na misingi ya utawala wa sheria ikivunjwa,” alisema Maalim Seif.

Alisema mikutano ya vyama vya siasa inasimamiwa na Sheria namba tano ya Vyama vya Siasa, lakini masheha na viongozi wa wilaya wamekuwa kikwazo kwa mikutano ya wapinzani kufanyika, jambo ambalo ni kinyume na misingi ya demokrasia.

Kuhusu Mansour

Alisema Mansour ni kiongozi mwenye dira na uchungu wa kweli wa kuwatumikia wananchi na kulinda haki za Zanzibar.

Akihutubia katika mkutano huo, Mansour alisema atatumia nguvu zake zote kufanya kampeni nyumba kwa nyumba, tawi kwa tawi, hadi jimbo hilo alitie mikononi.

Aliyekuwa Mwakilishi wa Kiembesamaki (CCM), Mansour Yussuf Himid, akizungumza na wanachama na wapenzi wa CUF katika jimbo hilo.
Aliyekuwa Mwakilishi wa Kiembesamaki (CCM), Mansour Yussuf Himid, akizungumza na wanachama na wapenzi wa CUF katika jimbo hilo.

“Sitoona haya kuingia tawi kwa tawi kusaka kura kwa ajili ya CUF, matawi yote ya CCM katika jimbo hili nimeyajenga mwenyewe nitafanya kampeni za nyumba kwa nyumba na sina kinyongo na kufukuzwa CCM,” alisema.

Alikumbushia kukamatwa kwake na Jeshi la Polisi na kufunguliwa kesi ya kupatikana na risasi kinyume na sheria na kuwataka wananchi wa Zanzibar kuacha kushabikia mambo yanayokwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu hasa wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.

Alisema Zanzibar imepita katika misukosuko mingi na kuwataka wananchi kuendelea kulinda na kuthamini misingi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo imesaidia kupunguza chuki.

Viongozi wengine waliohutubia katika mkutano huo ambao ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Kamati ya maridhiano, Hassan Nassor Moyo, ni Mwakilishi wa Mji mkongwe Ismail Jussa Ladhu, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Salim Bimani na naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Nassor Ahmed Mazrui.

Chanzo: Mwananchi

Wakati huo huo; Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) Maalim Seif Sharif Hamad, amemtambulisha rasmi Mansour Yussuf Himid kwa wananchi wa Jimbo la Kiembesamaki na kuwaomba wamuunge mkono.

Akimtambulisha mwanachama huyo mpya wa CUF ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbali mbali katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ukiwemo wa uwaziri, Maalim Seif, amesema ameridhishwa na Mansour kutokana na ujasiri alionao katika kuwatetea wananchi.
aadhi ya wanachama na wapenzi wa CUF waliohudhuria mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika Kiembesamaki jana
Baadhi ya wanachama na wapenzi wa CUF waliohudhuria mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika Kiembesamaki jana
Kwenye mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika viwanja vya bustani ya Kiembesamaki Katibu Mkuu huyo wa CUF alisema Mansour ambaye pia alikuwa Mwakilishi wa jimbo la Kiembesamaki kupitia Chama Cha Mapinduzi ni mzalendo wa kweli anayeipenda nchi yake na maslahi kwa Wazanzibari.
“Tumempokea Mansour kwa mikono miwili, na kuombeni wananchi wa Kiembe samaki na wanachama wote mumuunge mkono Mansour”. Alisisitiza Maalim Seif.
Huku akishangiliwa na umati wa watu waliofurika hadi chini ya miti kutokana na mazingira ya viwanja vyenyewe, Maalim Seif aliendelea kummwagia sifa Mansour akimtaja kuwa ni kiongozi mkweli na anaye jiamini.
“Tunahitaji viongozi majasiri na wanaojiamini kama Mansour”, aliongeza.
Maalim Seif alitumia fursa ya mkutano huo kueleza maoni yake binafsi kuwa anamkubali Mansour Yussuf Himid kuwa mgombea makini wa uwakilishi katika jimbo hilo kupitia CUF katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Katika hatua nyengine Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amelitaka jeshi la polisi kuacha kushabikia vyama vya siasa na badala yake litende haki katika utendaji wake.
Amedai kuwa katika hali isiyokuwa ya kawaida, baadhi ya maofisa wa polisi wamekuwa wakitumiwa na viongozi wadogo wa Chama Cha Mapinduzi na kuacha kuwaheshimu viongozi wa wakuu wa CUF ambao amesema ni sehemu ya dola ya Zanzibar.
Amefahamisha kuwa Chama chake kitaendelea kuheshimu sheria za nchi katika kuandaa mikutano yake, lakini hakitokubali kuendelea kunyanyaswa kwa sababu zisizokuwa za msingi.
Kwa upande wake Mansour Yussuf Himid amewaambia wanachama wa CUF kuwa tayari ameshachukua na kurejesha fomu ya kugombea uwakilishi katika jimbo hilo kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
aadhi ya wanachama na wapenzi wa CUF waliohudhuria mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika Kiembesamaki jana. Picha: Khalfan Said
Baadhi ya wanachama na wapenzi wa CUF waliohudhuria mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika Kiembesamaki jana. Picha: Khalfan Said
Amewahimiza wazanzibari kuungana na kuendeleza umoja uliopo, ili kuona kuwa maridhiano yaliyoasisiwa hapa Zanzibar yanafanikiwa kwa maslahi na ustawi wa Zanzibar.
“Lengo la maridhiano ni kuwaunganisha Wazanzibari na kuondosha chuki zilizodumu kwa muda mrefu hapa Zanzibar, si vyenginevyo”, alisisitiza Mansour na kuongeza,
“Bila ya Wazanzibari kushikamana hatuwezi kupata maendeleo, hatuwezi kushinda”, alisema.
Amefafanua kuwa iwapo CUF kitampitisha kuwa mgombea wa uwakilishi katika jimbo hilo, hatoona tabu kupiga kampeni katika matawi ya CCM na nyumba nyumba, ili kuhakikisha CUF inashinda katika jimbo hilo.
Nae Mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu, amesema wataendelea kufuatilia haki ya vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi, ili kuwawezesha wote wenye sifa ya kupata kitambulisho hicho waweze kukipata na kushirikiri upigaji kura katika uchaguzi mkuu ujao.
Chanzo: OMKR
Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s