Dk Shein kioo kipya kwa uadilifu Z’bar

Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein (Kushoto) akimwapisha Katibu Mkuu wa Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, wakati wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa kitaifa (SUK), Novemba mwaka 2010
Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein (Kushoto) akimwapisha Katibu Mkuu wa Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, wakati wa kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa kitaifa (SUK), Novemba mwaka 2010

Watu wengi hawakuamini  kama Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, angehimili mikikimikiki na dhoruba  ya kuoengoza  Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) hatimaye  ifikishe miaka mitano madarakani na kuifikisha ngwe ya  uchaguzi wa mwaka 2015 bila Serikali hiyo kuyumba  au kugawanyika.
Pamoja na kumudu jambo hilo; Rais wa Zanzibar anabaki Kuwa ndiye kiongozi mwenye  sifa  pekee ya kuongoza nchi kwa  kufuata misingi ya uadilifu, uwazi, uwajibikaji na ushirikishaji hasa anapoitisha vikao vya kiutendaji na tathmini ya  mipango kazi ya  Serikali kila baada ya miezi mitatu, maarufu bango kitita.

Dk Shein ni kiongozi aliyebahatika kufanya kazi za kiserikali akiwa Naibu Waziri wa Afya chini ya Serikali ya Dk Salimin Amour Jumaa  na kuwa Waziri wa Utawala Bora  katika Serikali ya Dk Amani Abeid Karume  baadaye  Makamu wa Rais chini ya Rais Benjamini Mkapa pia akifanya kazi na Rais Dk Jakaya Kikwete kabla ya kuwa Rais wa Zanzibar mwaka 2010.

Kukabidhiwa kwake jahazi la kuongoza SUK inayovishirikisha vyama hasimu vya CCM na CUF na kufikisha miaka mitano; ni ukweli usiopingika Rais huyo ameonyesha ushujaa, umahiri, ujuzi wa kuendesha mambo huku akiwa hakabiliwi na tuhuma za ufisadi, rushwa, uporaji ardhi, matumizi mabaya ya rasilimali za nchi pia hatamani kujitajirisha.

Mara zaote katika uongozi wake akiwa Rais amekuwa akiheshimu misingi ya utawala wa sheria, kuenzi haki za binadamu, kutambua mipaka ya demokrasia na kufuata siasa za wastani katika kuwatumikia wananchi wake.

Katika maeneo yote ambayo amekuwa mtumishi wa umma  kwenye Wizara, Dk Shein hatajwi wala hajakumbwa na kashfa za odokozi,  ufisadi, ubadhirifu wa mali za umma, upendeleo, ubinafsi na kila wakati amesimama na kuonyesha kuheshimu  taratibu, kanuni na utii wa Katiba ya nchi.

Wakati huu nchi na Taifa zikielekea uchaguzi mkuu wa dola, ipo haja na umuhimu wa kupata viongozi wa aina yake kuanzia urais, ubunge, uwakilishi na udiwani kwani kutoka uchaguzi mmoja hadi mwingine kuna kipindi  cha miaka mitano ambacho  wananchi wakitegemea wapate unafuu katika ujenzi wa uchumi, kwa  maendeleo ya jamii na ya kisekta.

Viongozi wetu katika maeneo ya uwalilishi kwenye vyombo vya kutunga sheria kama Bunge na Baraza la Wawakilishi (BLW) yakiwemo na mabaraza ya madiwani, kunahitaji wapatikane  aina ya viongozi wasioongozwa na tamaa, uchu wa kupora maliasili na rasilimali, ufisadi au tabia ya kutumia madaraka  ili kujitajirisha na kuwaacha waliowachagua wakiishi kwa shida na dhiki.

Ukiacha tabia yake hiyo, Rais huyo wa Zanzibar amebaki si kiongozi anayeongoza kwa  vitisho, ubabe, maneno makali au anayeongoza  Serikali chini ya kivuli cha uvunjaji wa sheria au ukiukaji wa Katiba zote mbili ikiwamo ile ya Zanzibar ya mwaka 1984 na  ya Jamhumri ya Muungano  wa Tanzania ya mwaka 1977.

Mara zote amesimama kwa miguu yake na kuonyesha kutii  uzalendo, kutobabaishwa, hatikisiki wala kuongozwa na  matamshi ya vitisho ambayo wakati mwingine hutoka upande wa hasimu zake  kisiasa huku akiwa mgumu  wa kupoteza mwelekeo hata pale watu na viongozi wa upande wake wanapomshauri mambo ambayo yako kinyume na misingi iliyowekwa.

Kwa mfano mwanzoni mwa mwaka huu, akifanya ziara ya kuimarisha chama chake na kukutana na mabalozi wa nyumba kumi  wa CCM, aliambiwa ipo haja ya kuivunja Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK)  kwa madai kuwa chini ya mfumo huo Zanzibar imekumbwa na matatizo mengi ikiwamo watu kumwagiwa tindikali na kupigwa risasi kuliko ilivyokuwa katika mfumo wa anayeshinda achukue vyote.

Dk Shein aliwaeleza kinagaubaga wanachama wenziwe kuwa kuundwa kwa SUK ni mchakato ambao kuoondosha kwake lazima kufuate taratibu zile zile na si jambo la kukurupuka au kufumba macho na kufumbua. Akasema ili aongezewe nguvu za kiutawala na kuudhofisha upinzani mambo mawili yanahitajika.

Bila kutafuna maneno akasema lazima wana CCM waipigie kura nyingi nafasi ya urais,  pili chama  tawala kishinde viti vingi Pemba na Unguja  na tatu kikombea majimbo yaliopotea Unguja hapo ndipo kudhoofu kwa upinzani katika uendeshaji Serikali na  kupata nguvu za maamuzi,  utakapopatikana na si kuamka na mtu kufikiri anaweza kuifuta  Serikali iliowekwa na wananchi  kwa mujibu wa katiba na sheria.

Si hivyo ila mara zote Dk Shein amekuwa akisema anapata ushauri wa moja kwa moja toka kwa Makamu wa Kwanza na wa Pili wa Rais yaani Maalim Seif Sharif Hamad na Balozi Seif Ali Idd katika masuala ya uendeshaji Serikali, mawaziri chini ya SUK hufanya kazi kwa pamoja na ushirikiano hadi ikishindakana kuwabagua ni yupi CCM na yupi CUF.

Wakati SUK chini ya Dk Shein ikipasua anga na kuchana na mawimbi,  nchi kadhaa Barani Afrika zikiwamo Zimbabwe, Sudan Kusini na Kenya zimeshindwa kuhimili suluba ya uendeshaji wa Serikali zenye mifumo hiyo,  sasa baadhi ya nchi hizo ziko kwenye mapigano, kuvunjika na nyingine kushirikiana bila ya kuwepo umoja na kutofahamiana.

Katika kipindi hiki wakati  aliyekuwa Rais wa Namibia Hifikepunye  Pohamba akitwaa  Tuzo ya Mo Ibrahim na kujichukulia kitita cha Dola  milioni tano, najaribu kumtazama Dk Shein katika jicho jingine huku nikimuona ni kiongozi anayestahili kupigiwa mfano bora katika ukanda wa nchi za  Afrika Mashariki na Kati kwa utumishi wa uadilifu Visiwani hapa.

Licha ya Dk Shein kuonyesha unguli katika uendeshaji wa SUK tokea kuundwa kwake, ameonyesha ni madhubuti katika kutetea Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, mpambanaji na mlinzi wa misingi ya Mapinduzi ya Zanzibar pia alipoguswa na waliojaribu  kuvuruga haiba ya amani na umoja, Serikali yake ilichukua hatua za kuwakabili waliotaka kumchezea paka sharubu.

Kwa upande mwingine tunapoitazama Zanzibar katika historia ya siasa na chaguzi zake  kuu  tokea mwaka 1957 hadi mwaka 2009, tunaiona ilivyokumbwa na misukosuko mikubwa  ya kisiasa hali iliopekekea  viongozi   na wafuasi wa vyama vya kisiasa kukosa  maelewano  na azma ya  kufanya kazi pamoja.

Chini ya Serikali ya awamu ya saba Zanzibar hasa baada ya kufanyika maridhiano ya kisiasa vyama vikuu vimefanikiwa kuzika uhasama na sasa chini ya uongozi wa Rais huyo mambo yanakwenda kwa murua huku kiongozi mkuu wa Serikali akionekana kuongoza bila kutikisika.

Kuundwa kwa SUK mwaka 2010 mara baada ya uchaguzi mkuu na kupatikana utulivu, maelewano na vyama vya kisiasa vikuu kushirikiana katika uendeshaji wa Seikali kwa takriban miaka mitano sasa, hapo ndipo ninapolazimika kumuona na kumtafsiri Rais Dk Shein ni kioo kipya cha uadilifu na mhimili imara wa maridhiano yaliopatikana visiwani humu.

Hata hivyo Dk Shein mara zote amekataa  katakata kugeuka nyuma huku akikwepa siasa za makundi ambapo historia ikimuonyesha ndiye Rais pekee ambaye ameingia madarakani akiwa hana kundi toka ndani ya chama chake na hata alipokabidhiwa dhamana ya  kuongoza nchi amejiweka kando na miruzi ya ushabiki huo.

Si yeye wala watoto wake ambao wameingia  hamkani ya kulitumia jina la baba yao  kwa ajili ya kuhodhi  viwanja na majumba ya Serikali  kwa njia isiyo halali, kujiingiza kwenye kazi za biashara huku wakiwa hawana mitaji na rasilimali-fedha  vilevile mke wake Mwanamwema mara zote ni  mwanamama wa kawaida asiyeongozwa na mbwembwe wala mikogo ya  kulitumia jina la nafasi ya mumewe kujinufaisha.

Nafikiri hii si zama tena za kiongozi kusimama hadharani kutoa matamshi yanayotonesha vidonda vilivyoanza kupona, kupotosha umma kwa uzushi wa kitoto ili  kusaka ridhaa ya kupata madaraka kwa njia za hila au kufanya uchochezi wa maneno ya kuwagawa wananchi kama baadhi ya wanasiasa wengine  Zanzibar wafanyavyo majukwaani.

Mwaka huu ni mwaka ambao  kila mtu atavuna kile alichopanda; kama yuko aliyepanda maboga asitegemee kuvuna mpunga, aliyetoa jeuri atakula jeuri yake, bingwa wa hadaa, tapeli wa kisiasa  na asiyewatumikia wananchi kwa kuchapakazi, mbabaishaji, mwenye majibu   mkato au kujibadili sauti na namba ya simu,  asitarajia kama atafaa tena na kupata mtaji wa kura.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s