Nilipomjulisha Nyerere kwa Nkrumah

Mwalimu Nyerere na Nkurmah
                       Mwalimu Nyerere na Nkurmah

MATUKIO mawili muhimu yalitokea Ghana wiki iliyopita. La kwanza zilikuwa sherehe za kuadhimisha miaka 58 tangu nchi ya Gold Coast ilipopata uhuru wake na kuwa Ghana chini ya uongozi wa Dakta Kwame Nkrumah.

La pili lilikuwa Kongamano la Nane la Vuguvugu la Umajumui wa Kiafrika (8th Pan-African Congress) lililofanywa jijini Accra. Maudhui ya kongamano hilo yalikuwa: “Ulimwengu wa Kiafrika Tuutakao.”

Kwame Nkrumah hatunaye tena; wala Julius Nyerere hatunaye tena. Lakini ilikuwa kama tulikuwa nao wote wawili katika kongamano hilo la Accra. Majina yao yalikuwa katika ndimi za wengi miongoni mwa walioshiriki kwenye kongamano hilo, hususani vijana.

Samia Nkrumah, binti wa Nkrumah, aliniona namwendea nikiwa nimemshika mkono jamaa mmoja. Huyo jamaa nilikwishamwambia kwamba nikitaka kumjulisha na mtu. Lakini hakujuwa ni nani.
Ulikuwa ni wakati wa kihistoria. Samia aliponijia, tusalimiane na kunambia: “Ah, Ahmed Rajab, ndipo nilipowaambia wote wawili — jamaa niliyekuwa naye na yeye Samia, “wacha niwajulishe.” Hawakupata kukutana kabla.

Nilimwambia Samia: “Huyu ni Madaraka, mtoto wa Julius Nyerere.” Na nikamwambia Madaraka: “Huyu ni Samia, binti wa Kwame Nkrumah.”

Historia hutokea katika nyakati kama hizo. Ulikuwa ni wakati wa kusisimua kuwaona watoto wa viongozi hao wawili walipotambuana.

Sikuongeza langu ila niliwaacha wazungumze na mimi akili zangu zikitembea kwenye kumbukumbu zangu za Kwame na Julius. Walikuwa na msimamo mmoja kuhusu Muungano wa Afrika lakini walitofautiana juu ya njia za kuufikia umoja huo.

Hata hivyo, nakumbuka niliwahi kuambiwa kwamba Nkrumah alipokuwa amekwishatambua kwamba ugonjwa aliokuwa nao ndio utaoyamaliza maisha yake aliandika barua kumpelekea Nyerere. Alitaka barua hiyo apelekewe Abdulrahman Babu ili amfikishie Nyerere.

Kwa hivyo, Nyerere ndiye aliyekuwa kiongozi wa mwanzo wa Kiafrika aliyekuwa akijuwa maradhi yaliyokuwa yakimla Nkrumah. Kadhia hii imethibitishwa na Bi. June Milne, aliyekuwa msiri wa Nkrumah.

Yale matukio mawili ya wiki iliyopita huko Accra yanafungamana. Na kiungo chao kikubwa ni Nkrumah na falsafa yake juu ya ukombozi wa Afrika. Ni yeye aliyesema kwamba uhuru wa nchi yake hautokuwa na maana endapo nchi nyingine za Kiafrika zitaendelea kutawaliwa na wakoloni.

Na ni yeye pia aliyesisitiza kwamba Waafrika wapiganie nchi zao ziwe huru na halafu mengine yatafuata. Hii leo kuna makoloni mawili tu yaliyobaki kukombolewa barani Afrika: nchi ya Sahara ya Magharibi inayotawaliwa na Morocco na kisiwa cha Mayotte (kimojawapo kati ya visiwa vya Comoro) ambacho kinatawaliwa na Ufaransa.

Nkrumah alikuwa ni muhubiri mkuu wa nadharia ya Umajumui wa Kiafrika — nadharia ambayo ina historia ndefu sana. Ilianza kuenezwa na watu wenye asili ya Kiafrika waliozaliwa Marekani na katika visiwa vya Caribbean. Miongoni mwao walikuwa W.E. B. Du Bois na Marcus Garvey.

Vuguvugu hilo liliasisiwa na watu watatu kutoka visiwa vya Carribean mwishoni mwa karne ya 19 kupambana na ukoloni barani Afrika. Waasisi hao watatu walikuwa vijana wawili wazaliwa wa Haiti, Anténor Firmin na Bénito Sylvain, na mwenzao Henry Sylvester Williams aliyezaliwa Trinidad.
Firmin, Sylvain na Williams ndio walioandaa mkutano wa kuzungumzia nadharia hiyo ya Umajumui wa Kiafrika uliofanywa London, Uingereza, Julai 1900. Du Bois alikuwa miongoni mwa wajumbe walioshiriki katika mkutano huo.

Du Bois alizaliwa Marekani 1868 na alifariki na kuzikwa Accra, Ghana, 1963. Alikuwa ni msomi wa hali ya juu na mwanaharakati aliyepigania Wamarekani wenye asili ya Kiafrika wapewe haki sawa kama walizokuwa nazo wenzao wa Kizungu. Alikuwa pia akipigania makoloni ya Kiafrika yapewe uhuru na yawe na mamlaka ya kujitawala wenyewe.

Wanafunzi wake aliokuwa akiwasomesha katika Chuo Kikuu cha Atlanta wakimuelezea kuwa ni mtu aliyekuwa mahiri sana, mwenye nidhamu ingawa akionekana kwamba hachanganyiki sana na watu.
Kongamano la mwanzo la Umajumui wa Kiafrika lilifanywa Paris mwaka 1919. La pili, lilifanywa 1921 katika miji mitatu — Paris, London na Brussels. La tatu lilifanywa Lisbon, Ureno, 1923. Lane liliandaliwa New York, Marekani, 1927.

La tano, lililo maarufu sana lilifanywa Manchester, Uingereza, 1945. Walioliandaa kongamano hilo walikuwa George Padmore aliyetoka Trinidad na Tobago, Nkrumah (aliyetoka Gold Coast, Ghana ya leo), Jomo Kenyatta (Kenya), Herbert Mackonnen (Ethiopia), Obafemi Awolowo (Nigeria) na Peter Abrahams (Afrika ya Kusini). Mkutano huo ulihudhuriwa pia na kizuka wa Marcus Garvey pamoja na Du Bois kutoka Marekani.

Umuhimu wa Kongamano hilo la tano la Umajumui wa Kiafrika ni ule wito wake wa kutaka nchi za Kiafrika zipewe uhuru wao. Miongoni mwa maazimio mingine ya kongamano hilo ni lile lililotaka ubaguzi wa kikabila uharamishwe na kuwa kosa la jinai. Kongamano hilo lilihudhuriwa na wajumbe kutoka makoloni mbalimbali ya Kiafrika na ya visiwa vya West Indies.

Miaka 13 baada ya Kongamano la tano baada ya Ghana kuwa huru na Nkrumah, akiwa rais wake, aliandaa mikutano miwili ya kihistoria na iliyokuwa muhimu kwa Afrika.
Kwanza Aprili, 1958 Nkrumah alikuwa mwenyeji wa nchi nane za Kiafrika zilizokuwa huru wakati huo (Ethiopia, Ghana, Libya, Tunisia, Morocco, Misri, Liberia na Sudan). Halafu Novemba mwaka huohuo wa 1958 Nkrumah aliandaa huko huko Accra mkutano wa All African People’s Conference.

Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo wa pili wa Accra walikuwa wapigania uhuru kutoka nchi nyingine za Kiafrika. Miongoni mwao walikuwa Patrice Lumumba, Abdul Rahman Babu, Nnamdi Azikiwe, Kenneth Kaunda, Frantz Fanon, Ali Muhsin Barwani na Abeid Amani Karume.
Baada ya hapo harakati za Umajumui wa Kiafrika zilipwaya kidogo hadi 1974 pale Julius Nyerere na Bill Sutherland walipoandaa Kongamako la Sita, Dar es Salaam, Tanzania. Sutherland, Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika aliyekuwa akiishi Tanzania, alikuwa katibu wa Kongamano hilo.

Lengo kuu la kongamano la sita lilikuwa kujiandaa dhidi ya tawala za wazungu wachache zilizokuwako kusini mwa Afrika.

Ingawa mapambano dhidi ya utawala wa wachache yaliendelea kusini mwa Afrika na mafanikio makubwa yalipatikana hata hivyo shughuli na harakati za Umajumui wa Kiafrika zilipwaya tena hadi 1994.

Mwaka huo wanaharakati wakiongozwa na Abdul Rahman Babu, Karim Essack, mzalendo wa Afrika ya Kusini, aliyekuwa akiishi Tanzania, pamoja na Kanali Kahinda Otafiire wa Uganda waliandaa kongamano la saba, Kampala.

Nilikuwa miongoni mwa wajumbe zaidi ya 1,600 kutoka sehemu mbalimbali duniani waliohudhuria Kongamano la saba. Miongoni mwa wengine walikuwa Kwame Touré (Stokely Carmichael), Jenerali Farah Aidid kutoka Somalia na Betty Shabazz (mjane wa Malcolm X).

Kongamano hilo liliamua kuwa na ofisi ya kudumu jijini Kampala, Uganda, na Dakta Tajudeen Abdul-Raheem kutoka Nigeria alichaguliwa Katibu Mkuu wa Vuguvugu la Umajumui wa Kiafrika chini ya Uenyekiti wa Kahinda Otafiire, ambaye sasa ni waziri wa sheria wa Uganda. Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, akawa mlezi wa Vuguvugu hilo.

Mengi yalifanywa na ofisi ya Kampala katika kipindi cha miaka michache. Kwa bahati mbaya ofisi hiyo ilikabiliwa na changamoto nyingi, zikiwa pamoja na ukosefu wa fedha za kutosha za kuendesha miradi kadhaa. Vuguvugu zima likapata pigo kutokana na kifo cha Tajudeen aliyefariki katika ajali ya motokaa, Nairobi, Kenya, Mei, 25, 2009.

Yote hayo yalikuwa miongoni mwa sababu za kupwaya tena kwa harakati za Umajumui wa Kiafrika.
Mkutano wa wiki iliyopita uliofanywa Accra ulikuwa wa nane katika mfululizo wa mikutano mikuu ya Vuguvugu la Umajumui wa Kiafrika. Tofauti ya huo na mengine iliyopita, isipokuwa lile kongamano la pili la 1921, ni kwamba huu wa nane unafanywa katika mihula miwili. Muhula wa pili utakuwa Mei, 2016.
Jambo lililonitia sana moyo katika Kongamano la wiki iliyopita ni kuona shauku kubwa waliyokuwa nayo vijana, wake kwa waume, juu ya nadharia na historia ya Umajumui wa Kiafrika. Wengi wakitaka kujuwa zaidi na wale ambao tayari wanayajuwa madhumuni ya vuguvugu hilo wameonesha raghba ya kutaka kuushika usukani wa uongozi wake.

Kinyume na wale waliosahau mchango wa Vuguvugu hilo katika ukombozi wa Afrika, niliwaona vijana hao kwamba wako tayari kuendeleza fikra za waasisi wa Vuguvugu hilo.
Na ndio maana juu ya makosa waliyoyafanya baadaye walipokuwa wanazitawala nchi zao, viongozi hao wangali wakienziwa na vijana.

Hawa ni vijana waliokaa wakaitafakari hali halisi ya Afrika —ilivyokuwa enzi za ukoloni, ilivyo sasa na namna wanavyoitaka iwe miaka ijayo.

Nkrumah, Ahmed Ben Bella wa Algeria, Ahmed Sekou Toure wa Guinea, Modibo Keita wa Mali, Frantz Fanon wa Algeria, Nyerere, Patrice Lumumba wa Congo, Jomo Kenyatta wa Kenya pamoja na Mu’ammar Qadhafi wa Libya ni miongoni mwa wana wa Afrika walioshangiliwa kwa nguvu na Kongamano hilo.

Chanzo: Raia Mwema

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s