Wahafidhina wanapiga ngumi ukuta

Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein
                                        Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein

Na Jabir Idrissa

NINAAMINI Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) haiendi vizuri kama ilivyotarajiwa. Ninathubutu kusema naweza kuingia katika mjadala popote pale wa kuzieleza sababu za hali hiyo. Zipo sababu za wazi na zilizojificha za kwanini serikali iliyoundwa kutokana na mabadiliko ya 10 ya Katiba ya Zanzibar, haijakidhi matarajio ya wananchi.

Ninaelewa matatizo ya mfumo mpya uliotokana na maridhiano ya kisiasa yaliyofikiwa na wakuu wa CCM na CUF, na umma kuyaridhia kwa kura ya maoni Julai 2010.

Ila pamoja na yote hayo, sijafikiria kujiingiza katika kushawishi watu kwamba mfumo huu alioanza nao Dk. Ali Mohamed Shein, hauifai nchi.

Wapo watu, wengine wakiwa wanasiasa wakubwa katika Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanajenga hoja kuwa tunapoingia katika maandalizi ya uchaguzi mkuu, kuna ulazima wa kuwepo mjadala wa kuivunja serikali ya umoja.

Siamini kwa sababu nyingi. Lakini haraka ninajipa wasaa wa kushangaa mbona katika suala hili walio mbele ya kupiga kelele na kujitahidi kutaka majadiliano yatakayoishia na kuvunjwa kwa mfumo wa serikali ya ushirikiano, wanatoka CCM pekee?

Nimesoma makala za mahojiano yaliyofanywa kwa wanasiasa na wasomi na kubaini wanaotaka mabadiliko, kwamba Zanzibar irudi enzi za chama kinachoshinda uchaguzi kuchukua kila kitu, si wale wanaotoka nje ya CCM.

Nazungumzia watu makini kifikra, sio wanaofanya siasa za mzaha kama wanavyosomeka baadhi ya wanasiasa wanaoufuja mfumo kwa sababu tu umewaengua katika kupata ulwa.
Wanasikika wanasiasa wakisema mfumo wa serikali ya ushirikiano haufai kwa kuwa “umenufaisha vyama vya CCM na CUF tu.”

Kwao, mfumo ulio bora ni ule unaowahakikishia nao kuwemo serikalini, bila ya kujali kama wametimiza kigezo au sharti lililowekwa na katiba.

Ni rahisi kusema wanasiasa hawa wanajipigia debe kwa sababu kwao mfumo halali ni wao kuwemo katika serikali. Ni kwa kiasi gani vyama wanavyoongoza vinakubalika kwa umma, si la muhimu kwao.
Sharti mojawapo kuu la chama kushirikishwa katika uundaji wa serikali ya umoja wa kitaifa, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, ni kupata asilimia ya kura wakati wa uchaguzi mkuu.

Hakuna chama zaidi ya CCM na CUF, kilichotimiza sharti hilo; na ndio maana ni vyama hivyo tu vilivyoshinda sharti hilo, vimeshirikishwa katika serikali.

Basi sijawahi kusikia mawazo haya ya kuvunja serikali ya ushirikiano yakitolewa na mwanasiasa atokae CUF, chama kinachoishika shingo CCM katika ushindani wa siasa Zanzibar, kiasi cha kuvuruga matumaini yake ya kuendelea kushika dola kimazoea.

Kwanza, ni muhimu kubainisha mapema msimamo wangu kuwa viongozi waandamizi ndani ya CCM wanalalamikia mfumo huo kwa kuwa umewakosesha sauti ya moja kwa moja katika utawala wa nchi.
Ni tofauti na ilivyokuwa kabla ambako CCM wakiamua kila kitu wapendavyo na wajisikiavyo baada ya uchaguzi. Kisingizio cha mwenendo huo ni katiba ndivyo inaelekeza – chama kinachoshinda uchaguzi kiunde serikali peke yake.

Fursa hiyo haipo tena sasa kwani imeonekana ilitumika vibaya kwa kuendeleza ukandamizaji wa misingi thabiti ya demokrasia, mmoja ukiwa wa kuzuia mgawanyiko wa jamii katika utawala.

Ndani ya nyoyo za viongozi wa CCM kuna chembechembe za uhafidhina. Hawataki kubadilika na hawapendi kuamini kuwa Zanzibar si nchi miliki yao, bali nchi ya kila mtu aliyehalali kikatiba.
Ujinga wa watu hao ni kule kuamini kuwa hakuna mwenye akili ya kuongoza Zanzibar, zaidi ya wao walioko CCM. Nje ya chama hicho, kilichozaliwa kwa kuuliwa vyama vya ukombozi, Tanganyika (TANU) na Zanzibar (ASP), hakuna haki ya mwingine kuongoza.

Dhana hiyo si sahihi hata kidogo. Zanzibar ina watu wengi wenye elimu nzuri, wala siyo ya kubahatisha, na uwezo wa kuongoza. Isitoshe, kuna watu nje ya vyama vya siasa wenye uwezo mkubwa wa kutambua mahitaji muhimu ya Wazanzibari.

Lakini ukweli ni kwamba ilipofikishwa Zanzibar, nchi yenye uchumi duni usiojiweza hata kwa kugharamia mishahara ya watumishi wake, pamechangiwa na uwezo na dhamira ya kiuongozi ya viongozi wa CCM. Si ndio chama kilichoshika dola miaka yote hiyo? Sasa yule aliyepewa dhamana ya uongozi, ndiye anayewajibika kwa hali iliyopo.

Mtu ajiulize ni kwanini viongozi wawili wale – Amani Abeid Karume, aliyekuwa Rais wa Zanzibar, akitoka CCM, na Maalim Seif Shariff Hamad aliyegombea urais akitoka CUF – waliona haja ya kuiingiza nchi katika mabadiliko ya mfumo wa kuiongoza.

Waliacha ubinafsi wakaangalia hatima ya nchi. Waliacha maslahi ya vyama walivyo (ninayoamini ni madogo) na kufikiria maslahi mapana ya nchi na watu wake.

Karume na Maalim Seif waliamua kwa dhati ya nyoyo zao kufikiria nje ya mduara. Wanasiasa hao walipima hali za wananchi walio nyuma yao.

Walijitoa mhanga huku wakijua haitakuwa rahisi kueleweka haraka ndani ya vyama vyao. Si uongo, Karume alisemwa sana na wenzake, kama vile alivyosakamwa Maalim Seif na wafuasi wake.
Wapo wanasiasa ndani ya makundi yao mpaka leo wanahoji ilikuaje Karume na Maalim Seif wakafikiria maelewano kwa siri namna ile.

Wanauliza wale walikuwa na siri gani wasishirikishe wenzao. Ni umasikini wa fikra tu kudhani kwamba maridhiano lazima yaanzie kwa watu elfeni. Kumbe asili yake hutokana na wazo la mtu, akaliuza kwa mtu wa pili. Huyo wa pili husaidia wazo kukuzwa na kufanyiwa kazi mpaka mafanikio.
Ndani ya CCM suala la maridhiano lingali linazua fitna. Baadhi ya viongozi wanaendelea kuulizana maridhiano yalianzaje.

Ukweli, watabakia hapohapo kwa sababu ndivyo walivyo – hawataki kufikiria nje ya maslahi yao huku wakiamini hiyo ndiyo hasa siasa nzuri.

Hawa ni wahafidhina wasioona maana ya utulivu uliopo. Basi tuseme wanauona utulivu, tatizo kwao ni kutoamini kuwa umesababishwa kwa sehemu kubwa na maridhiano yaliyohalalishwa na wananchi kwa kura ya maoni. Hili hawalioni.

Ni wanasiasa hao wanaoamini kuwa chini ya sera za “mapinduzi daima” ndiyo Zanzibar inaendeshwa vizuri na kuendelea mbele. Kwao, mfumo wa mapinduzi daima, ndio unaoifaa Zanzibar.
Wanajua kuwa kutokana na mfumo huo ndio maana serikali inaendelea kuamini ina haki ya kusaidia CCM kupata ushindi wakati wa uchaguzi mkuu.

Kwamba serikali ina haki ya kutumia fedha zilizo kodi ya wananchi wote, na zile za misaada, kwa ajili ya kugharamia mipango ya kukipatia ushindi CCM.

Wazanzibari, kote Unguja na Pemba, wanaamini Zanzibar imefuta zama hizo za ujuha kutawala akili za viongozi.

Zile ni zama hoi zilizochangia kuidhoofisha nchi iliyopaswa kuwa kileleni mwa mafanikio ya uchumi unaozalisha ajira milioni kwa mwaka kama ilivyokuwa miaka ya 1950.

Mfumo uliojengwa kwa gharama kubwa, haustahili kufutwa kirejareja kama wanavyofikiri wahafidhina. Hata kidogo.

Wale wanaodhani bado wanayo nafasi ya kurudisha nyuma fikra mpya za kuiendeleza Zanzibar, wasahau. Wanapiga ngumi ukuta.

Chanzo: Mawio

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s