Sasa zamu ni ya makabwela wa kwetu

New Delhi inavyoonekana wakati wa usiku
Mji wa New Delhi huko India unavyoonekana wakati wa usiku

Na Ahmed Rajab

NEW Delhi, mji mkuu wa India, pamoja na vitongoji vyake una wakazi milioni 25.
Kwa mujibu wa ripoti moja ya Benki ya Dunia, jiji hilo limepitwa na Tokyo tu, mji mkuu wa Ujapani, kwa idadi ya wakazi. Tokyo ina wakazi milioni 38 ushei.

Kwa kulinganisha, Dar es Salaam ina wakazi milioni 4. Tukiziacha idadi za wakazi wao jiji la Delhi linalipita sana jiji la Dar es Salaam kwa umri. Dar es Salaam ya leo ilianza kujengwa mwaka 1865 na Sultan Majid bin Said wa Zanzibar. Kwa hivyo Dar yetu, ambayo zamani ikiitwa Mzizima (yaani mji wenye afya), ni kama mji wa jana.

Delhi ni mji wa kale wenye historia ndefu. Ulitawaliwa na masultani kwa zaidi kidogo ya karne tatu (1206-1526). Muda wote huo masultani wa Delhi walikuwa wakitanua ardhi ya milki yao na wakijenga ngome nyingi kuuhami utawala wao.

Umati wa Delhi ya leo ni umati wa makabwela. Ukitembea mitaani Delhi, siku nenda siku rudi, utakutana na makabwela tu. Kuna wenye vibarua na kuna wasio na ajira. Wote wanalizwa na makali ya maisha.

Makabwela wa Delhi, akina Narendra, Manish na Gulshan, wanasononeka na maisha kama wanavyosononeka akina Msita, Jafari na Rehema huko Manzese, Dar es Salaam au akina Haji, Yusuf na Pandu huko Kwarara, Unguja. Hali zao zinafanana.
Ndiyo maana haishangazi kuwasikia wa Delhi, wa Dar na wa Unguja wakipiga kelele kwamba wanakabiliwa na maadui walewale: utawala mbovu na ufisadi.

Sababu iliyolileta jiji la Delhi Barazani kwetu ni zilzala iliyotokea huko Februari 7. Zilzala ya kura. Zilzala hiyo ilitokea wakati wa uchaguzi wa kulichagua bunge jipya la jiji hilo na waziri kiongozi mpya wa serikali itayoliendesha jiji hilo kwa muhula wa miaka mitano ijayo.

Download (1)

Zilzala hiyo imeibadili hata hali ya hewa ya Delhi. Upepo uvumao huko umegeuka. Siku hizi kuna upepo mpya usio na rihi mbaya ya ufisadi. Kuna waliofika hadi ya kusema kwamba kuna sayari mpya iliyoumbwa Delhi. Wanaiita “sayari ya makabwela.”

Wanasema kwamba sayari hiyo imeumbwa na wapiga kura wa Delhi waliokichagua chama cha Aam Aadmni Party (APP), yaani Chama cha Makabwela, kiliendeshe jiji hilo.
Makabwela wa APP na wafuasi wengine wa chama hicho walitumia ufagio kuwa alama ya chama chao katika uchaguzi. Wakiashiria kwamba dhamiri yao ni kuufyeka ufisadi. Ufagio huo ndio uliokinyanyua na kukipatia ushindi chama cha APP.

Alama ya ufagio, kama unakumbuka, ilitumiwa pia mwaka jana na makabwela wa Burkina Faso pamoja na wazalendo wenzao katika vuguvugu la kumuondosha kwenye madaraka Rais Blaise Compaoré.

Huo ni ushahidi kwamba wenye kunyanyaswa duniani kote si kwamba wana majonzi aina moja tu lakini huwa hata na lugha moja. Wanaweza wakawa na ndimi tofauti na misamiati tofauti lakini lugha yao ya kujikomboa huwa ni moja na wawe Burkina Faso, India, Tanzania au popote pale penye ugandamizi na ufisadi uliokithiri.

Wanajuwa kinachowaua na wanajuwa namna ya kukishinda.
Kusema kweli ushindi wa APP haukushangaza. Wengi tukitaraji kwamba chama hicho kitashinda. Lakini kilichoishangaza dunia ni jinsi hicho Chama cha Makabwela kilivyoshinda. Kilishinda kwa kishindo; tena si kishindo kidogo.

Bunge la Delhi lina viti 70. Chama cha APP kimejinyakulia viti 67 na kile cha Bharatiya Janata Party (BJP) kilishinda viti vitatu.

BJP ndicho chama cha Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, ambaye naye alishinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa Mei mwaka jana.

Inafaa tukumbushe, na hasa tukikumbushe Chama cha Mapinduzi (CCM), kwamba chama kikongwe cha Congress chenye mahusiano ya muda mrefu na CCM, kimejiondokea patupu. Kimekwenda kapa.
Chama cha Congress, kama kilivyo CCM, ni chama cha Uhuru. Ni chama cha akina Mahatma Gandhi na Jawaharlal Nehru (babu na baba wa Uhuru wa India). Chama hicho kililitawala jiji la Delhi kwa miaka 15 hadi 2013. Hii leo hakina hata mguu wa kiti katika bunge la Delhi.

Congress ni chama ambacho miaka saba tu iliyopita kilikuwa na viti zaidi ya 43 katika bunge hilo. Wakati huo chama cha makabwela cha AAP kilikuwa hata hakijazaliwa.
Ingawa chama cha APP ndicho kilichoshinda uchaguzi wa Februari 7 kwa kweli ushindi huo ni ushindi wa makabwela. Makabwela wa Delhi wamethibitisha kwamba umma hauwezi kushindwa endapo utaazimia na utakuwa na uongozi imara.

Arvind Kejriwal, kiongozi wa APP, aliapishwa Februari 14 awe waziri kiongozi wa Delhi. Ilikuwa mara yake ya pili kula kiapo hicho. Mara ya mwanzo ilikuwa Desemba 28, 2013. Lakini baada ya siku 49 alijiuzulu uwaziri kiongozi Februari 14, 2014.

Kejriwal, kijana wa miaka 46, alijiuzulukwa sababu kwa vile serikali yake haikuwa na wingi mkubwa wa viti bungeni ilikwamishwa humo bungeni kupitisha mswada wa kupinga ufisadi.
Kwa mwaka mzima hadi Jumamosi iliyopita jiji kubwa la India, Delhi, lilikuwa halina serikali iliyochaguliwa. Katika kipindi hicho shughuli za jiji hilo zikawa zinaendeshwa na Rais wa India, Pranab Mukherjee.

Hivi sasa Kejriwal anasema kwamba suala kuu katika ajenda yake ni kufanya kila njia ule mswada wa kupinga ufisadi upite bungeni na uwe sheria. Mswada huo ulipendekeza paundwe chombo cha kuchunguza visa vya ufisadi na kuchukuliwa hatua za kuufyeka kabisa. Wabunge wa upinzani waliungana kuupinga mswada huo. Safari hii hamna shaka kwamba utapita bila ya hata kujikwaa.

Hatua nyingine muhimu ambazo Kejriwal anasema atazichukua ni kuendelea kupunguza gharama za maisha. Alipokuwa waziri kiongozi mara ya kwanza alipunguza kwa asilimia 50 malipo ya stima.
Sasa anasema serikali yake itaendelea kupunguza malipo ya umeme na itawapatia wakazi wa Delhi maji safi kwa bei ya nafuu watayoweza kuimudu, atawapa wakazi hao mamlaka ya kujiendesha katika ngazi za chini za utawala na atapigania jiji la Delhi liwe na hadhi ya jimbo lenye mamlaka makubwa zaidi.

Suala jingine ambalo anasema serikali yake italishughulikia ni suala la usalama wa wanawake. Hili ni suala muhimu sana hasa Delhi ambako ubakaji wa wanawake umekuwa ugonjwa sugu.

Kadhalika, serikali ya APP itaunda kikosi maalum cha usalama cha wanawake wapatao 10,000. Wanawake wataoingizwa katika kikosi hicho ni wale ambao kwa sasa wanafanya kazi za upishi, usafishaji au za udereva wa kuyaendesha magari ya wakuu wa serikali. Yote hayo yamo kwenye ilani ya uchaguzi ya chama hicho cha makabwela.

Wako Waafrika wasiofurahishwa na ushindi wa APP kwa vile mwaka jana walikashifiwa na kiongozi mmoja wa chama hicho.

Somnath Bharti, aliyekuwa waziri wa sheria wa Delhi katika muda mfupi ambao APP kilitawala jijini humo, aliwaamrisha polisi wende kuipekua nyumba moja ambayo akishuku kuwa ni danguro. Polisi walikataa kwa kutokuwa na waranti ya kuipekua nyumba hiyo.

Bharti na wasaidizi wake wakaingia kwa nguvu ndani ya nyumba hiyo na wakawazuia wanawake wanne wa Kiganda. Kisa hicho kilizusha uhasama kati ya India na Uganda na kiliwafanya baadhi ya wamahiaji wa Kiafrika wahame Delhi.

Arvind Kejriwal, waziri kiongozi mpya wa Delhi, ni wa kizazi kipya. Ni kiongozi asiye na makuu na anayechagizwa na kikohozi kisichomwisha. Amejifunza mengi tangu achaguliwe mara ya kwanza kushika hatamu za serikali ya Delhi, halafu ajiuzulu baada ya siku 49 na achaguliwe tena.

Download (3)
Kuna makosa aliyoyafanya njiani lakini inavyoonyesha ni kwamba wakazi wa Delhi wamempa fursa nyingine awaongoze. Amejifunza mengi na nina hakika naye amewafunza wengi hata nje ya mipaka ya India.

La kwanza ni kwamba makabwela wakishikamana wanaweza kuwashinda walio kwenye vyama vikongwe, vyenye fedha nyingi na uzoefu mkubwa wa kutawala.
Si kuwashinda kwa mapanga na mashoka lakini kwa karatasi za kura ilimradi uchaguzi uwe wa wazi na usio na ghiliba.

Kabla ya kujitosa katika siasa Kejriwal, aliyesomea uhandisi, alikuwa akifanya kazi idara ya kodi. Kwa kawaida wafanyakazi wa idara kama hiyo mikono yao huwa si mitupu. Alijiuzulu 2006 na akajiingiza katika harakati za kupigania haki, serikali safi, utawala bora na kupinga ufisadi.

Download
Kufika 2011 Kejriwal akaanzisha vuguvugu lisilo la kisiasa lenye kupinga ufisadi. Hapo ndipo alipoanza kupata umaarufu India. Vuguvugu lake liliwavutia makabwela pamoja na Wahindi wengine wa tabaka la kati waliochoka na ufisadi.
Vuguvugu hilo halikudumu. Palizuka suitafahamu ndani yake na Kejriwal akashutumiwa kwamba akilitumia ili apate madaraka.

Muda si mrefu akaunda chama cha Aam Admi party, akisema yeye ndiye Gandhi wa leo atayeufyeka ufisadi. Alikuwa hajitwezi, hajionyeshi wala haringi. India ikampenda; jiji la Delhi likamkumbatia. Likampa ushindi 2013. Akazidi kupendwa alipopunguza bei za umeme na maji na kwa msimamo wake dhidi ya ufisadi.

Juu ya yote hayo alijikwaa kwenye jambo moja. Hakuziweza siasa za “nipe, nikupe.” Hakujuwa namna ya kupatana na kuwa na maafikiano na mahasimu wake. Mwisho akakata tamaa na akajiuzulu.
Lakini miezi michache baadaye alifanya jambo asilowahi kufanya kiongozi yeyote wa India. Aliomba radhi.
Alitoa taarifa Mei akisema kwamba ingawa alijiuzulu kwa sababu za kimaadili lakini “ninawaomba radhi watu waliotaka serikali ya AAP iendelee kutawala Delhi.” Kuomba radhi kwake kulimnyanyua na kumsukuma mbele katika medani ya siasa.

Baada ya kutangazwa kwamba chama chake kimeshinda uchaguzi wa Februari 7 Kejriwal aliwasihi wafuasi wake kwa kuwaambia: “Msiwe na kiburi. Vyama vingine vilishindwa kwa sababu ya kiburi, nasi yatatufika kama hayo tukiwa na kiburi.”

Chanzo: Raia Mwema

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s