Bendera za ASP zazua taharuki Zanzibar

Iliyokuwa bendera ya Afro Shiraz Party
Iliyokuwa bendera ya Afro Shiraz Party

Zanzibar. Chama cha CUF kimesema hakihusiki na bendera za Afro Shiraz Party (ASP) zinazoonekana katika mikutano yake ya hadhara inayofanyika Unguja na Pemba. Kupepea kwa bendera hizo kumeibua mjadala mkubwa miongoni mwa  viongozi wa CCM visiwani humo.

Msimamo huo wa CUF umeleezwa na Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano  kwa Umma, Salum Abdallah Bimani baada ya UVCCM Zanzibar kulalamika kuwa CUF kimekiuka  sheria Namba 5 ya mwaka 1992 ya vyama vya siasa  huku mamlaka zikifumbia macho suala hilo.

 “Wanaopepeprusha bendera hizo ni Wazanzibari wanaoguswa na sera pamoja na misingi ya ASP.  CUF haihusiki na bendera hizo,” alisema Bimani.

Alisema ni kweli bendera hizo zimekuwa  zikionekana kwenye mikusanyiko na mikutano ya hadhara inayoandaliwa na CUF ila hubebwa na wananchi wenye hisia za kukiunga mkono ASP kisera, kimsimamo na kihistoria.

Bimani alisema CUF kinaweza kuhusishwa na bendera hizo iwapo zingekuwa zinapepea kwenye milingoti ya ofisi zake za matawi, wadi, jimbo, mikoa au Taifa lakini kupeperushwa kwenye mikutano hakuna uhusiano wowote na chama hicho.

Hata hivyo alisema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia sheria na si vyama vya siasa na kumtaka Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Shaka Hamdu Shaka kuacha kuihusisha CUF na bendera hizo.

Kwa upande wake Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa Zanzibar, Rajab Baraka alipoulizwa kuhusiana na madai ya UVCCM, alisema ni kweli wamepokea malalamiko kuhusiana na kupeperushwa kwa bendera hizo na tayari suala hilo limewasilishwa Makao Makuu ya Ofisi ya Msajili jijini  Dar es Salaam.

“Tayari tumelizungumza suala hilo na kinachosubiriwa ni maamuzi ya kisheria baada ya wanasheria wetu kulifanyia kazi na kulitolea ufumbuzi, uamuzi wake hauhitaji kukurupuka ila lazima kuwe na tafakuri na hekima kabla ya kutoa maamuzi mazito,” alisema Baraka.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za UVCCM huko Gymkhana mjini Zanzibar, Shaka alisema CUF kimeamua kuleta chokochoko za kisiasa ambazo zinaweza kuitingisha na kuzorotesha amani, utulivu na maridhaino yaliofikiwa visiwani humu. “Kitendo cha kubeba alama za chama chetu cha zamani ASP na kuzitumia kwenye mikutano yao ya hadhara  licha ya kuwa ni uvunjaji wa sheria lakini kinaweza kuibua mitafaruku na mapigano yasiohitajika, tunaonya kwa mara ya mwisho ikishindikana tutazilinda bendera zetu,” alisema Shaka.

Naibu huyo Katibu Mkuu wa UVCCM alisema inashangaza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kushindwa kuchukua hatua za kisheria huku  ikiridhia uvunjaji wa sheria.

“Kikundi kinachojiita mguu mbele, mguu nyuma kinachotambuliwa na Katibu Mkuu wa CUF Seif Sharif Hamad hubeba bendera na kuimba nyimbo za harakati za Mapinduzi ya Zanzibar, ZNP hakina mnasaba na ASP, iweje CUF kitumie sera za ASP kilichozaa CCM,” alihoji Shaka.

Wananchi katika Manispaa ya Zanzibar wamekuwa wakikusanyika na kujadili kiini cha CUF kupeperusha bendera za ASP  na kushindwa kupata majibu kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu,  huku sheria ikikataza kutumika kwa nembo, alama. bendera na kauli mbiu za vyama vya zamani.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s