Vita ya urais CCM nje nje

Sadifa Juma Hamisi
Sadifa Juma Hamisi

Arusha. Wakati joto la urais likizidi kupanda ndani ya CCM kutokana na hofu ya baadhi ya majina mazito ya wagombea wa nafasi hiyo kukatwa kwa mizengwe, vita vya wagombea sasa ni dhahiri baada ya mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kusema hakuna mtu atakayekatwa bila ya sababu za msingi.

Mjumbe huyo, Sadifa Juma Hamisi, ambaye ni mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), pia alisema umoja huo haujafikia uamuzi wala kumtuma mtu kumdhibiti mwanachama anayetajwa kuwania urais.

Katika siku za karibuni kumekuwapo mjadala mkubwa ndani ya CCM juu ya mtu atakayepitishwa kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho, na ilizidi baada ya Rais Jakaya Kikwete kueleza kuwa mwanachama ambaye atateuliwa na CCM kugombea urais hayumo miongoni mwa waliojitokeza na kuwataka wanachama kuwashawishi watu wenye sifa wajitokeze.

Siku chache baadaye, Dk Raphael Chegeni aliliambia gazeti la Mwananchi kuwa ametumwa na wanachama wa CCM wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kwenda kumshawishi Lowassa kujitokeza kuwania urais kuitikia wito wa Rais Kikwete wa kuwataka wanachama kuwashawishi watu wenye sifa kujitokeza.

Hadi sasa, wanachama waliojitokeza kuwania kuteuliwa na CCM kugombea urais ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, January Makamba (Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia), Hamisi Kigwangala, na Lazaro Nyalandu ambaye ni waziri wa Maliasili na Utalii.

Lakini pia wako wanaotajwa kuwania urais lakini hawajatangaza ambao ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sita, William Ngeleja, Emmanuel Nchimbi, Mwigulu Nchemba, Stephen Wasira, Bernard Membe na Edward Lowassa ambaye ameibua mjadala kati ya kambi yake na zinazompinga.

Mapema wiki iliyopita, katibu wa uhamasishaji na chipukizi wa UVCCM, Paul Makonda alikaririwa akisema kuwa vitendo vyake vya kumshambulia Lowassa vinatokana na kutumwa na umoja huo kumdhibiti, jambo ambalo limezidisha mjadala kuhusu mteule wa chama hicho.

Kutokana na hofu hiyo, viongozi wa UVCCM na CCM mkoani Arusha wametuma ujumbe wa maneno kwa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa za chama hicho wakitaka wanachama wasifanyiwe kile wanachokiita kuchafuana na vitisho vya baadhi ya wagombea kukatwa kimizengwe.

Ujumbe huo ulitumwa juzi na mwenyekiti wa CCM wa mkoa, Onesmo ole Nangole na mwenyekiti wa UVCCM, Robinson Meitinyiku ambao walitaka Sadifa Juma Hamis kueleza msimamo wa mkoa kwa vyombo hivyo viwili vya maamuzi, na mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM aliwahakikishia kuwa hakuna mgombea atakayekatwa kwa “sababu za kijinga”.

Akijibu ujumbe wa viongozi hao, Sadifa aliyekuwa jijini hapa kumsimika kamanda wa vijana wa wilaya ya Arumeru, Mathias Manga, aliwaondolea hofu katika hafla hiyo akisema hakuna mgombea wa urais wa CCM ambaye atakatwa bila sababu za msingi, lakini akawataka vijana kusubiri zamu yao hadi 2025.

Kauli ya Sadifa

“Niwaombeni mwenyekiti wa mkoa na mwenyekiti wa UVCCM, msiogope. Hakuna mtu atakayekatwa kijinga ndani ya Kamati Kuu au Halmashauri Kuu. Kikubwa tufuate maadili. Mimi mchapakazi ndiye nitamtetea,” alisema bila kutaja mgombea anayekusudiwa.

Alisema ni lazima kiongozi bora awe na mikakati na dira na upeo wa kuwa na mikakati bora ya kutekeleza ahadi zake kwani hatuwezi kuwa na kiongozi ambaye hana dira wala mikakati.

“Tunataka kiongozi mwenye kujiamini, awe ana vision (dira) na mission (mikakati), msikivu… hatuwezi kuchagua rais ambaye hana sifa hizi,” alisema.

Akizungumzia maombi ya Nangole kuhusu tabia ya kuwachafua baadhi ya wagombea na kuwatisha, Sadifa alisema hakuna kiongozi aliyetumwa na CCM na UVCCM kutukana mtu wala kumtisha.

“Mzee wangu, watu wengi wanajua wanamtaka nani, ukiona mtu anapanda kwenye majukwaa anamchafua mwenzake, ujue huyo ana mapungufu ya malezi, hakuna haja ya kumjibu kwani utaonekana na pia wewe una mapungufu,” alisema.

Akionekana kujibu kauli ya Makonda, Sadifa alisema UVCCM haijatuma mtu amtukane mwingine. Alisema akiwa mjumbe wa Kamati Kuu, hawajawahi kumtuma kiongozi yoyote kumtukana mwanachama mwingine wa CCM.

Alipoulizwa kuhusu hofu hiyo, kwa kifupi katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema: “Mimi siwezi kuwa msemaji wa Umoja wa Vijana, nikisema niwajibu nitakuwa nimepotoka.”

Mapema wiki iliyopita, Makonda alikaririwa akisema kuwa amekuwa akimshambulia Lowassa, ambaye anatajwa kuwania urais kupitia CCM, kwa sababu ametumwa na umoja huo.

Makonda amekuwa akikaririwa mara kwa mara akisema kuwa Lowassa hafai kuwa mteule wa CCM wa kuwania urais na mikanda ya kauli zake imesambaa kwenye mitandao ya kijamii, jambo lililofanya uteuzi wake kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni uhojiwe na watu wengi na hivyo kujikuta akilazimika kusema ametumwa na umoja wake kumdhibiti waziri mkuu huyo wa zamani.

Katika mazungumzo yake juzi, Sadifa hakutaka kutaja jina la mgombea atakayemtetea wala mtu anayemshambulia, badala yake alisema muda ukifika, kila kitu kitajulikana kwa kuwa watu wanamjua mgombea wanayemtaka.

“Mwenyekiti, dawa ya mjinga ni kukaa kimya, watu wanamjua mtu ambaye wanamtaka. Rais Jakaya Kikwete ni mtu ambaye hatabiriki, hana ushemeji… nyie subirini tu wakati ukifika,” alisema.

Vijana na urais

Akizungumzia vijana ambao wanautaka urais, Sadifa aliwataka kusubiri zamu yao hadi 2025 ili wazee waliopo wamalize muda wao.

Alisema utakapofika mwaka 2025 vijana watakuwa katika nafasi nzuri sana ya kushika uongozi na hawatakubali kuona viongozi wazee wakitaka kupewa nafasi.

“Wazee tutawaomba radhi mwaka wenu ni 2015 hadi 25, mkimaliza hapo, miaka yenu imekwisha, msije tena,” alisema.

Kauli ya Nangole

Awali, Nangole, ambaye aliwahi kusema kuwa Lowassa ni kiongozi msikivu na makini na ambaye ni tegemeo la Watanzania katika kuwaunganisha kuwa kitu kimoja, aliomba Kamati Kuu ipelekewe ujumbe kuwa CCM mkoani Arusha hairidhishwi na matendo ya baadhi ya viongozi kuwatukana na kuwatisha wengine.

Nangole alirejea kauli aliyowahi kuitoa kuwa CCM ni ya wanachama wote na ndani yake hakuna sisimizi au tembo wa kumtisha mwingine ili mradi anafuata taratibu za chama hicho.

Alisema imeibuka tabia ya baadhi ya viongozi wa CCM, kuwatisha wengine na kuwatukana kana kwamba wao ndio wana hatimiliki ya CCM.

Naye mwenyekiti wa UVCCM mkoani Arusha, Robinson Meitinyiku alisema kuna kiongozi mmoja ametoa kauli kuwa mgombea mmoja hata kama akisafishwa na madodoki hawezi kuwa msafi.

Badala yake alisema kiongozi aliyetoa maneno hayo ndiye hawezi kusafishika hata kwa gunzi kwani kuna taarifa aliwahi kusaliti na kujiunga na chama kingine.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s