Kwa nini tusimangwe tusiojua Kiingereza?

Vitabu mbali mbali vya lugha
Katika ujenzi wa ghorofa, Mhandisi anayejua Kiingereza anatumia mafundi wa Kiswahili wasiojua Kiingereza, lakini wana maarifa mapana kuhusu ujenzi. 

Abeid Poyo

Ona kioja cha nchi hii; mwalimu wa Kiswahili anafanyiwa usaili kwa lugha ya Kiingereza ili apate kazi. Dereva mzoefu na fundi hodari wa magari anakosa kazi katika mashirika ya umma au yale binafsi kwa sababu hajui Kiingereza.

Katika ujenzi wa ghorofa, mhandisi anayejua Kiingereza anawatumia mafundi wa Kiswahili wasiojua Kiingereza, lakini wana maarifa mapana kuhusu ujenzi.

Kuna wakati anapogundua kafanya kosa anaomba ushauri kwa mafundi haohao na kazi inaendelea kwa ubora stahiki.

Namalizia kioja kingine. Siku moja jirani yangu alijisifu kuwa tangu amhamishe mwanawe shule, sasa anazungumza kimombo si mchezo! Akatumia fursa hiyo kunishawishi na mimi kumhamisha mwanangu.

Nilfikiri angenambia mwanawe huyo ameongeza uwezo wa kusoma, kuandika, kuhesabu au kufikiri, la hasha, anafurahia mwanawe wa miaka minne kujua Kiingereza!

Si yeye, hata mimi mtoto wangu alipoanza chekechea siku ya kwanza alipokutana na mimi usiku na kunambia ‘Good morning madam’, japo alikosea salamu hiyo nilifurahi kuona anazungumza Kiingereza.

Ukweli ni kwamba fikra kuwa Kiingereza ndiyo kila kitu zimetuzonga Watanzania. Wengi hatuamini kama elimu na maendeleo vinaweza kupatikana bila kutumia lugha hiyo.

Ni kasumba tu tuliyonayo Watanzania, ndiyo maana ni kawaida hata kwenye mikusanyiko ya Waswahili watupu, washiriki wanaulizana watumie Kiingereza au Kiswahili.

Walipo Waswahili 200 na mzungu mmoja, watu watajiumauma na Kiingereza. Kisa, wamridhishe mgeni mmoja.

Eti msomi aliyezaliwa na kukulia Kariakoo anadai hawezi kuandika mada kwa Kiswahili!

Wanaowasilisha mada kwa Kiswahili nao wanajiona wana kasoro, hawajaiva kimaarifa kama wenzao ‘wanaotiririka’ kwa Kiingereza.

Nimeshawahi kuhudhuria mkutano fulani, mgeni mzungu ilibidi atoe ruhusa watu wazungumze Kiswahili kwa kuwa washiriki tungekuwa wazi na huru kuzungumza kilichokuwa kikijadiliwa. Ikumbukwe mada iliyokuwa ikijadiliwa ilihusu maendeleo yetu sisi Waswahili na siyo maendeleo ya mzungu huyo mgeni.

Chanzo: Mwananchi

 

Advertisements

One Reply to “Kwa nini tusimangwe tusiojua Kiingereza?”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s