Kila uchochoro Mji Mkongwe akina ‘William’ wanaona gaidi

Lukuvi* Ila kama ni balaa wataleta Wazungu na…
* Wanaopiga kampeni za chuki kanisani
* Sio hizi porojo za Waarabu wa Oman

Na Omar Msangi

Hivi karibuni mwandishi Mohammed Ghasani aliandika makala ndani yake akahoji, kosa la Wazanzibari nini hata ‘Tanganyika’ iwang’ang’anie hivyo na kutowapa fursa ya kupumua na kuamua aina ya muungano wanaotaka.

Jibu la swali hilo analieleza vizuri Waziri Mheshimiwa William Lukuvi wakati akiongea na waumini wenzake Wakristo kanisani. Anaeleza Mheshimiwa Lukuvi akianza kwa kuwahoji Wakristo wenzake:

“Eti tuwaache Wazanzibari wajitawale wenyewe na Watanganyika… Wazanzibari kule waliko, asilimia 95 ni Waislamu. Tunataka wajitangazie serikali ya Kiislamu kule!”

“Hapana.” Sauti inasikika baadhi ya waumini wakijibu. Kisha anaendelea kuuliza Lukuvi:

“Mnajua madhara yake?” Inasikika sauti ya waumini wakijibu: “Makubwa sana.”

Waziri Lukuvi anaeeleza: “Wale Waarabu watarudi. Watazalisha siasa kali kule watakuja kutusumbua.”

“Mimi najua, kabisa. Kwa hiyo ndugu zanguni, mnaposikia mjadala kule, kuna watu unaweza kuona kama wana nia njema wanataka kuwasemea wale wanaoitwa Tanganyika, lakini wana siri yao moyoni. Kwamba labda ikipatikana hii serikali na sisi tutashinda tutatawala.”

“Zanzibar ni nchi ndogo sana. Ina watu milioni moja na laki tatu. Sisi tuna milioni arobaini. Unaweza ukauliza, kwa nini sisi tunaing’ang’ania sana ile? Lakini sisi tunaangalia mbele. Madhara ni makubwa kuicha Zanzibar kama ilivyo….bora tuwe nao.”

Bwana Ghasani, hilo ndio jibu. Zanzibar ikiachwa, Waarabu watarudi, watazalisha “Waislamu siasa kali”, wataisumbua Tanganyika.

Labda sasa swali ni je, kwa nini Zanzibar nao wasiwe na wasiwasi kuwa wakiwa chini ya makucha ya ‘Watanganyika’, Wakristo watawapa tabu Waislamu wa Zanzibar?

Mheshimiwa William Lukuvi na wale aliokuwa akiwahubiria kanisani, hawana wasiwasi huo kwa sababu Wazanzibari wenyewe wanaimba wimbo huo huo, wagawe uwatawale-Hawana agenda ya Uzanzibari wala ya Uislamu. Lao ni Pemba Vs Unguja na hofu ya kurudi Muarabu!!! Inalillahi waina ilaihir rajiuun!

Maadhali hiyo ndiyo hali ya Wazanzibari, sina haja ya kuwazungumzia hapa. Agenda yangu itakuwa pana zaidi. Hili la ‘Waislamu siasa kali’ ambao Mheshimiwa Lukuvi anadai kuwa watazalishwa Zanzibar kukiwa na serikali ya Kiislamu.

Japo suala la Zanzibar/Tanganyika na mfumo wa Muungano lina historia ndefu toka wakati wa Mwalimu, lakini anachozungumza hapa Mheshimiwa Lukuvi, ni propaganda ile ile iliyobuniwa na mabeberu katika kutekeleza malengo yao. Naye sasa anaitumia kufanikisha siasa za Tanzania katika suala la muungano, lakini pia katika kuendeleza ile Crusade aliyotangaza Bush.

Kama walivyosema wataalamu mbalimbali kuwa hakuna mtu mwenye akili yake timamu anayeweza kuamini kuwa kuna gaidi anayeweza kutoka Afghanistan au Uarabuni na kufanya gharika kama ile ya Septemba 11, Marekani, hakuna pia mtu mwenye akili yake timamu anayeweza kuamni kuwa Waarabu wa Oman au Wafursi wa Iran, wana mpango wa kuja kuikalia Zanzibar. Lakini ni uwongo tu unaozuliwa, ikapigwa propaganda na wakapatikana wajinga wa kuamini propaganda hiyo ili yatimie yanayotakiwa katika siasa.

Kama ni kuvamia nchi, na kama ni kuvurugwa nchi zetu, zitavurugwa na Wazungu wanaoivuruga Ukraine hivi sasa kwa sababu ya kupigania mafuta na gesi na kusimika hegemonia (hegemony) yao katika eneo hilo.

Inayoitwa vita dhidi ya ugaidi, vita dhidi ya ‘siasa kali’ hivi sasa ina miaka 14. Ilianza rasmi mwaka 2001 baada ya Sepetmba 11 ikafuatiwa na uvamizi Iraq. Kwa muda huo wa miaka 14 wa kuunda majinamizi na mazimwi kwa jina la Taliban, Osama bin Laden, Saddam Hussein, Gaddafi, Assad, Al-Shabaab, ISIS, IS, Boko Haram n.k, nchi zaidi ya saba zimevamiwa, kupigwa mabomu na kushambuliwa kwa makombora ya drones. Hawa akina Karl Peters wanaofanya haya, ndio wa kuhofiwa kuwa wana mpango wa kurudi kutukalia au kutuletea machafuko tuuwane wenyewe kwa wenyewe kisha wajifanye wasamaria wema wa kutusaidia kijeshi na kikachero. Na wakifanikiwa hilo, machafuko hayaishi. Ndio hali ya Nigeria, Yemen na kwingineko.

Mamilioni ya Waislamu wameuliwa kwa sababu ya uwongo na propaganda zao, mamilioni wakatiwa vilema na mamilioni hivi tunavyoandika, wamebaki kuwa wakimbizi. Kwa wenye chuki na Waislamu, mara nyingi huwa hawaangalii athari ya machafuko, vita na kuangamizwa kwa nchi wala ile agenda ya ujumla ya mabeberu. Wanachotizama ni kuwa Waislamu wameuliwa, wanabamizwa. Wanameza propaganda ya ugaidi na kuhalalisha kuuliwa Waislamu.

Ukirudi nyuma kulikuwa kuna kitu kinaitwa Operation Gladio (Italian: Operazione Gladio) au “stay-behind”. Walikufa sana Wazungu wa Ulaya. Na hawa walikuwa ni Wakristo. Mabeberu katika “Stay-behind operations” zao ndani ya nchi za NATO, hawakujali kuwa wanaokufa ni Wazungu wenzao na Wakristo wenzao pia.

Hivi sasa Ukraine kuna zogo kubwa. Watu wanauliwa. Kisa! Wenye uchu wa mafuta wanataka kuitia katika makucha yao nchi hiyo bila kujali watakufa watu wangapi au nchi kuharibikiwa kiasi gani kama ilivyoharibikiwa Iraq na Syria.

Hatukuwahi kuwa na ugomvi na wananchi wa Somalia wala kuwa na adui anaitwa ‘magaidi wa Kiislamu’ kutoka Somalia (Al-Shabaab). Lakini mabeberu kwa masilahi yao wameivuruga nchi ile wamezalisha Al-Shabaab, wamewatangaza kuwa ni magaidi wa Kanda hii ya Afrika na sisi kama vipaza sauti vinavyotumia betri badala ya akili, tumekuwa tukiimba wimbo huo huo.

Akizungumzia vita dhidi ya ugaidi, aliyewahi kuwa Mshauri wa Mambo ya Usalama wa Marekani (National Security Adviser), Zbigniew Brzezinski, anasema kuwa msamiati ugaidi na magaidi, umekuwa ni simulizi ya kutunga ya tangu zama ambayo hutumiwa na wanasiasa kisanii.

Brzezinski akieleza jinsi sababu za uwongo kuisingizia Iraq ugaidi na silaha za maangamizi zilivyoangamiza maelfu ya roho za watu wasio na hatia (collateral damage), anasema hiyo ni dhambi kubwa kwa Marekani ambayo inaiondolea heshma iliyo nayo duniani kama taifa kubwa. Katika maelezo yake marefu kwa Kamati ya Seneti, Brzezinski anasema kuwa, awali Marekani ilitumia uwongo wa Silaha za Maangamzi (WMD) kuivamia Iraq. Baada ya hapo inakuja tena na uwongo mwingine kuwa kuna magaidi wa Al-Qaida na ‘Muslim Fundamentalists’ ambao ni maadui hatari kwa usalama wa Marekani. Akasisitiza kuwa uwongo huo wa kusingizia kitisho cha ugaidi wa A-Qaidah katika nchi za Kiarabu ili kusimika alichokiita “U.S. regional hegemony”, utaleta madhara makubwa ikiwa ni pamoja na machafuko, mauwaji na kuifanya Marekani kuchukiwa duniani kote. ((SFRC Testimony — Zbigniew Brzezinski, February 1, 2007.)

Katika makala “Putting the Terror Threat In Perspective” iliyowekwa katika mtandao wa Washingtons Blog, inaelezwa kuwa matukio mengi ya ugaidi na kitisho cha ugaidi kwa ujumla, kinafanya kupandikizwa ili kutimiza malengo ya kisiasa na kiuchumi. Ikafafanuliwa kuwa nchi za kibeberu zimekuwa zikitumia kitisho cha ugaidi katika nchi zinazolengwa kupandikiza machafuko, uvamizi na kisha kufanikisha uporaji wa rasilimali.

Zaidi ya kutumia ‘usanii’ wa kitisho cha ugaidi kuvamia na kupora nchi tajiri kwa rasilimali kama mafuta, kitisho hicho hutumika pia kuwasaidia watawala kudumu madarakani. Aliyekuwa Mkuu wa Usalama wa Ndani (Secretary of Homeland Security), Tom Ridge wakati wa George W Bush, akatoa mfano ambapo alilazimishwa kupandisha kiwango cha kitisho cha ugaidi ili kumsaidia Bush kushinda uchaguzi awamu ya pili.

Kwamba awatishe wananchi kuwa magaidi wa A-Qaidah karibuni tu wataiangamiza Marekani huku wakipewa kumbukumbu ya Septemba 11, halafu ionyeshwe kuwa Bush ndiye mwenye mipango sahihi ya kukabiliana na kitisho hicho hivyo apewe muda.

Ndio haya anayosema Mheshimiwa Waziri, Bwana William Lukuvi. Kwamba, maadhali kuna agenda ya kuidhibiti Zanzibar na maadhali hivi sasa bado kitisho cha ‘Waislamu siasa kali na ugaidi’ ni “dili”, kinafanya kazi; basi kinatumika kuwaunganisha Wakristo kupinga mabadiliko ya mfumo wa muungano. Kwa upande mwingine, kinatumika kuwagawa Wazanzibari, wabaki wakiogopa kitisho cha kurudi ‘Muarabu’, badala ya kusimama katika agenda moja ya Uislamu na Uzanzibari. Lakini kwa hapo hawezi kulaumiwa Lukuvi. Kama Wazanzibari wenyewe hawajitambui, Mheshimiwa William Lukuvi yeye afanye nini!

Mwezi Mei mwaka 2008 Chuo cha Kijeshi (United States Army War College) kule Carlisle, Pennsylvania, kiliandaa kitu kilichojulikana kama “Unified Quest 2008” (war games test). Katika ‘gemu’ hiyo ya siku tano, iliyohudhuriwa pia na makamanda wa kijeshi kutoka nchi za NATO na Israel, walisema kuwa walikuwa wakijiandaa ni kwa jinsi gani watalinda masilahi ya Marekani ndani ya nchi ya Nigeria ifikapo mwaka 2015.

Walisema kuwa inatarajiwa mwaka huo nchi hiyo itasambaratika kutokana na machafuko (vitendo vya kigaidi) na kwamba hata uchaguzi wa mwaka huo itabidi uahirishwe. Na kwamba kuna uwezekano mkubwa Nigeria kugawanywa kutoka katika hali yake ya sasa ya kuwa nchi kubwa Afrika yenye idadi kubwa ya watu na utajiri mkubwa wa mafuta. Pengine iwe Kaskazini na Kusini kwa Wakristo.

Akizungumzia suala hilo Februari 4, 2012, Balozi wa Marekani nchini Nigeria Bwana Terence McCulley, alitetea serikali yake akisema kuwa, waliofanya utabiri huo kuwa Nigeria itasambaratika ifikapo mwaka 2015 haikuwa serikali ya Marekani bali taasisi binafsi ikijulikana kwa jina la Rand Corporation and Booz-Allen.

Hata hivyo, taasisi hizo ndio wakala wa serikali na Jeshi la Marekani (Private Military Contractors) anayefanya kazi kwa maelekezo na kwa kulipwa na serikali.

Kilichokuwa kikitizamwa katika ‘bao’ hilo, ni namna ya kulinda masilahi ya kibeberu ya Marekani, ikiwa ni pamoja na kupeleka jeshi na namna AFRICOM itakavyofanya kazi ikifika mwaka 2015 ambapo ilitabiriwa kuwa nchi hiyo itasambaratika kutokana na machafuko. (Tazama: United States Army Allegedly Preparing For A Possible Break-Up Of Nigeria, Nigeria: U.S. Speaks On Nigeria’s Break-up. Na Cia And Mossad To Divide Nigeria Soon)

Mapema wiki hii, imetangazwa kuwa uchaguzi mkuu wa Nigeria umeahirishwa. Uchaguzi huo ambao ilikuwa ufanyike Februari 14, umeahirishwa hadi Machi 28. Sababu zilizotolewa ni za kiusalama, kwamba vyombo vya usalama vinahitaji muda zaidi wa kujiandaa kukabiliana na kitisho cha Boko Haram. Haijulikani iwapo ahadi hiyo itatekelezwa au ndio hatari ya kitisho itakuwa kubwa zaidi.

Zipo taarifa nyingi juu ya Boko Haram kwamba na wenyewe ni katika zile “Intelligence Assets” za mabeberu.

Kwa hakika kama yapo mambo ya kustahiki kuwashughulisha wanasiasa wetu, ni haya ya hawa wanaotuwangia na “war games test” pamoja na “Intelligence Assets” zao wakitutabiria machafuko huku wakiweka mikakati watakavyotukalia kikachero na kijeshi. Sio hizi porojo za kurudi Muarabu wa Oman.

Chanzo: An-Nuur

Advertisements

One Reply to “Kila uchochoro Mji Mkongwe akina ‘William’ wanaona gaidi”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s