Rais huyu hadanganyi, hadanganyiki

Rais Kikwete akiwa ameongozana na mgeni wake Rais Gauck mara baada ya kumpokea
Rais Kikwete akiwa ameongozana na mgeni wake Rais Gauck mara baada ya kumpokea

KWA kawaida, Mkuu wa Taifa anapojiwa na mgeni rasmi wa kitaifa kuna mambo fulani ya huyo mgeni ambayo hutakiwa ayajuwe. Tena ayahifadhi kabla ya kumpokea mgeni wake.

Baadhi ya mambo hayo huwa anapaswa ayajuwe hasa ikiwa ni mara yake ya mwanzo kutembelewa na huyo mgeni.
Kwa upande wake huyo mgeni naye atakuwa amekwishaelezwa mambo binafsi kumhusu mwenyeji wake.

Kwa mfano, kabla ya Rais Joachim Gauck wa Ujerumani kufunga safari hivi majuzi kuelekea Tanzania alikuwa tayari amekwishapewa maelezo kuhusu mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete.

Alikwishamjuwa ni mtu wa aina gani.

Kadhalika alikuwa amekwishaelezwa namna ya kuzungumza naye na atarajie kuambiwa nini na mwenyeji wake au mwenyeji wake huenda akajibu vipi maswali atayomuuliza kuhusu sera za Tanzania na mwenendo wa serikali yake.

Alikuwa amekwishazitalii na kuzijuwa sera hizo na misimamo ya serikali na ya chama kinachotawala Tanzania.
Gauck alikuwa amekwishaelezwa kiwango cha uhuru wa kusema na kutoa maoni kilivyo Tanzania na jinsi upinzani nchini humo unavyodhalilishwa na vyombo vya dola, hasa na Polisi.

Aidha alikuwa amekwishafahamishwa mahusiano yalivyo baina ya serikali ya Muungano na serikali ya Zanzibar, namna mfumo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ulivyo Zanzibar na jinsi wakorofi wachache wanavyojaribu kuuchimba.

Baadhi ya maelezo hayo, Gauck aliyapata kutokana na utafiti uliofanywa na maofisa wa upelelezi na wa kijasusi walio katika ubalozi wa Ujerumani mjini Dar es Salaam.

Takriban balozi zote, zaidi zile za madola makuu, zilizo Dar es Salaam zina maofisa wenye kazi ya kukusanya habari kwa njia za kijasusi.

Siku hizi habari za kijasusi huitwa habari za “kiintelijensia” lakini ujasusi ni ujasusi tu. Hata hivyo, hauepukiki kwani dunia haiwezi kwenda bila ya ujasusi.

Kwa hakika, ujasusi umekuwako tangu azali. Ndo pakaja ule usemi wa kwamba ujasusi ndio kazi ya pili iliyo kongwe kabisa duniani. Ya kwanza, inavyosemekana, ni umalaya.

Ujasusi umekuwako tangu wanadamu walipoanza kujikusanya na kujiendesha kwa utaratibu wa watawala na watawaliwa.
Una historia ndefu sana. Maandishi ya kale ya magwiji wa mikakati ya vita kama Sun-Tzu wa China au Chanakya wa Bara Hindi yana maelezo mengi kuhusu ujasusi.

Wamisri wa kale walikuwa na mfumo wao wa kijasusi wa kupatia habari. Waebrania (Wayahudi wa kale) nao walikuwa na majasusi wao. Kadhalika majasusi walizagaa katika milki za kale za Wagiriki na Warumi.

Hata Mtume Muhammad (SAW) alitumia sana majasusi wakati wa vita; alianza kuwatumia pale Waislamu walipolivamia eneo la Hamra al-Asad kuwashambulia watu wa Makkah wa kabila la Quraysh waliokuwa wakiupiga vita Uislamu na Mtume wake.

Tumerudi sana nyuma katika historia lakini kwa upande wake Rais Kikwete naye aliwajibika kuzitumia asasi zake za kijasusi kuyajuwa mengi kuhusu wasifu wa mgeni wake. Haitoshi kwamba ajuwe anatembelewa na Rais mwenzake tu.

Pamoja na kuzijuwa sera za Ujerumani na misimamo yake, Kikwete alitakiwa ayajuwe mambo ya kibinafsi ya Gauck. Kwa mfano, ni vitu gani vinavyomsisimua Gauck, nini kinamchusha na kumkirihisha, ana watoto wangapi, wajukuu wangapi na vitukuu vingapi, anapenda kusoma vitabu vya aina gani au kuangalia filamu za aina gani?

Maelezo kama hayo huwa si ya kipuuzi bali humpa fursa mwenyeji kuwa na vibwagizo vya kuyachangamsha mazungumzo na mgeni wake ili mazungumzo yao yanoge.

Muhimu zaidi Kikwete alipaswa apatiwe taswira kamili na historia ya kisiasa ya mgeni wake. Alitakiwa amjuwe ni mtu wa aina gani; ni mtu wa kubabaisha mambo tu na kuwatoa watu njiani au ni mtu asiyedanganya na asiyedanganyika?

Sidhani kama Kikwete alipewa maelezo ya kutosha kumhusu Gauck. Lazima wasaidizi wake hawajamueleza yote aliyostahili ayajuwe kumhusu Gauck.

Lau Kikwete angeyajuwa ya Gauck sifikiri kama angethubutu kuyasema aliyoyasema alipowatetea polisi wa Tanzania mbele yake kwa kuyavamia maandamano ya Chama cha Wananchi (CUF) na kumpiga Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

Maandamano hayo yalikuwa ni ya kuwakumbuka wanachama wa CUF waliouliwa na majeshi na polisi visiwani Zanzibar Januari 26 na 27, 2001.

Nayo lazima yalimkumbusha Gauck siku zake za maandamano.
Katika miaka ya 1980 pale Kanisa katika Ujerumani ya Masharki lilipokuwa likiunga mkono vuguvugu la kidemokrasia, Gauck ndiye aliyekuwa akiongoza maombi kanisani kabla ya kuanza maandamano makubwa ambayo hatimaye yaliuporomoa utawala wa Kikomunisti.

Kikwete alisema kwamba polisi walibidi wayavunje kwa nguvu maandamano ya CUF kwa sababu wana CUF walivunja sheria kwa kuandamana bila ya kibali.

Kweli sheria ni sheria na ni lazima ziheshimiwe. Uvunjwaji wa sheria ni utovu wa nidhamu na utovu wa aina hiyo hauwezi kuvumiliwa katika jamii yoyote ile hususan ile inayojigamba kwamba ni ya kidemokrasi.

Lakini kutumia hoja hiyo kama kisingizio cha kuwatumilia mabavu wapinzani ni jambo ambalo Gauck lazima aliling’amua mapema. Ni mtu aliyekaramka; hadanganyiki.

Amekwishayapitia hayo na zaidi ya hayo katika maisha yake ya uanaharakati dhidi ya Ukomunisti.
Gauck si mtu ambaye ninakubaliana naye kiitikadi.

Na kuna mengi katika nadharia anazoziamini ambayo ninayapinga. Hata hivyo, sina budi ila nimheshimu, tena sana. Ninamheshimu kwa sababu ya msimamo wake wa kupigania haki na kupinga dhulma.

Habari za bwana huyu Gauck ni nyingi mno na zimeanzia mbali tangu ujanani mwake alipokuwa mpinzani wa udhalimu na mateso ya mfumo wa Kikomunisti.

Gauck alizaliwa katika ukoo wa mabaharia mjini Rostock, Ujerumani ya Mashariki. Baada ya sehemu hiyo kuvamiwa na majeshi ya Warusi vilipomalizika vita vikuu vya pili vya dunia, Ujerumani ilikatwa sehemu mbili: Ujerumani ya Magharibi iliyokuwa katika kambi ya nchi za Magharibi na Ujerumani ya Mashariki iliyokuwa ikifuata mfumo wa Ukomunisti.

Mwaka 1951 alipokuwa na umri wa miaka 11 babake aliyekuwa nahodha alikamatwa na majeshi ya Kirusi na akahamishwa kupelekwa Siberia, Urusi.

Kilichomchongea akamatwe ni harakati zake za kupigania haki za raia. Alifungwa, akateswa na kupewa kazi ngumu kwa muda wa miaka minne.

Kwa hivyo, upinzani wa Gauck dhidi ya udhalimu umekuwa ukimwenda ndani ya damu yake akimrithi babake katika uanaharakati wa kupigania haki.

Gauck amewahi kusema kwamba alianza kuuchukia Ukomunisti tangu utotoni mwake kwa sababu ya madhila aliyoyapata babake. Amesema kwamba tangu akiwa na miaka tisa akiamini kwamba mfumo wa usoshalisti si mfumo wa haki.

Haya ni matamshi yenye walakin na sikubaliani nayo hata chembe. Lakini Gauck ni mtu mwenye kusema anayoyaamini na hayo ndiyo anayoyaamini.

Hata alipokuwa skuli, alikuwa hazifichi chuki zake dhidi ya Ukomunisti na alikataa katakata kujiunga na vuguvugu la vijana wa Kikomunisti. Kwa sababu hiyo alikosa mengi.

Moja alilolikosa ni kuwa mwandishi wa habari. Akitamani kusoma Kijerumani ili awe mwandishi wa habari lakini alikataliwa kwa vile babake alikuwa muasi na yeye hakuwa muumini wa Ukomunisti. Badala yake akasomea theolojia yaani elimu ya dini.

Lengo lake hasa halikuwa awe kasisi lakini masomo ya dini yalimpa fursa ya kusomea falsafa na itikadi ya Ukomunisti ilikuwa haikushamiri kanisani.

Hatimaye aliangukia ukasisi ingawa kazi hiyo ilikuwa ngumu kwa vile utawala wa Kikomunisti ulikuwa ukipinga dini.
Kwa miaka mingi Kasisi Gauck alikuwa akifuatwa na majasusi wa serikali na mara kwa mara akibughudhiwa na watu wa usalama wa idara ya polisi wa siri.

Ni wazi kwamba kutokana na historia yake ndefu, Gauck anafahamu vyema dola inapotumia mbinu za kuwabana wapinzani. Amekwishayapitia hayo alipokuwa akibanwa na utawala wa kimabavu wa Ujerumani ya Mashariki.

Ni mtu ambaye habaniibanii maneno, hupasua tu na kusema mambo kinagaubaga hasa anapokuwa anazungumza na watawala. Hiyo ndiyo sababu iliyowafanya wengi wammwagie sifa tele.

Kiongozi mwenzake wa Ujerumani ambaye ndiye mwenye kuendesha serikali, Angela Merkel, aliwahi kumsifu Gauck kuwa ni “mwalimu halisi wa demokrasia” na “mtetezi asiyechoka wa uhuru, demokrasia na haki.”

Wengine wamesema kwamba Gauck ni “Rais wa nyoyo’; wengine wamemwita “Rais bora.”
Kuna wasemao kwamba kama Ujerumani ina mtu mwenye kufanana na Nelson Mandela kwa uadilifu na kwa kupigania haki basi mtu huyo ni Gauck.

Anafananishwa pia na Lech Walesa wa Poland na Vaclav Havel wa Czechoslovakia. Wote watatu walikuwa safu ya mbele kupigania haki katika zile nchi zilizokuwa nyuma ya “pazia la chuma,” yaani nchi zilizokuwa zikitawaliwa na mfumo wa Kikomunisti.

Wapo pia waliombandika Gauck jina la “mwindaji wa Stasi,” yaani mwindaji wa yale majasusi au mashushushu au viwavi (kama tulivyokuwa tukiwaita Zanzibar) — watumishi wa idara ya polisi ya siri ya Stasi waliokuwa wakiwaadhibu wakaazi wa Ujerumani ya Mashariki.

Gauck ameitwa hivyo kwa sababu baada ya kuunganishwa Ujerumani kufuatia kuporomoka kwa utawala wa Kikomunisti Ujerumani ya Mashariki, Kasisi Gauck, aliteuliwa mkuu wa tume iliyochunguza vitendo vya hiyo polisi ya siri ya Stasi.
Sifa kubwa ya Gauck ni ya kusema kweli, hasa kuwaambia ukweli watawala; kwani amezoea kuwakabili wenye madaraka na kuwapasulia ukweli.

Hata akiwa Rais wa Ujerumani, dola yenye nguvu, Gauck hamezei maneno anapozungumzia serikali zenye kuzikiuka haki za binadamu.

Gauck si kiongozi mwenye kuyapima ayasemayo yasije yakayadhuru maslahi ya kiuchumi ya nchi yake.
Anaujali utu kinyume na walivyo wengi wa viongozi wetu. Muhimu zaidi ni kwamba Rais huyu hadanganyi wala hadanganyiki.

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

One Reply to “Rais huyu hadanganyi, hadanganyiki”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s