Maridhiano: Serikali ya Mseto Zanzibar yazua mjadala

dksheinmaalimseif

Zanzibar. Mustakabali wa uhai wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), upo shakani kutokana na wananchi kutofautiana kuhusu umuhimu wa kuendelea na mfumo huo wa uongozi, huku baadhi wakitaka iitishwe Kura ya Maoni kuamua hatma ya serikali hiyo.

SUK iliundwa mwaka 2010 baada ya vyama vikuu vya siasa visiwani hapa, CCM na CUF, kujadiliana na hatimaye kufikia muafaka wa kugawana madaraka ili kuondoa siasa za chuki zilizotokana na machafuko ya mwaka 2005 wakati wananchi walipokuwa wakipinga matokeo ya Uchaguzi wa Rais.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Mwananchi unaonyesha kuwa iwapo Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) haitakuwa makini katika usimamiaji wa kanuni na sheria za uendeshaji wa kampeni hadi kuelekea Uchaguzi Mkuu, kuna uwezekano mkubwa wa wanasiasa wa pande mbili kuyatumia vibaya majukwaa na kuiparaganyisha serikali hiyo.

Tatizo jingine linaloonekana kuinyemelea SUK ni  kuibuka kwa watu wanaotaka ifanyike Kura ya Maoni na wananchi kuulizwa kama wanataka mfumo huo wa uendeshaji serikali kwa pamoja unastahili kuendelea.

Kutoimarika kwa huduma za jamii chini ya SUK kama ilivyotegemewa na wananchi na malengo yake kutofikiwa kunaelezwa pia kuwa ni kati ya changamoto zinazoikabili SUK.

Akizungumza na Mwananchi, mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Jumuiya ya Asasi za Kiraia Zanzibar (Angoza), Mohamed Hafidh Khalfan alitetea SUK akisema kwamba faida zimeonekana, ikiwamo kudumishwa kwa amani na kuondoa mgawanyiko katika jamii, lakini akasema yapo mambo yanayohitaji kufanyiwa marekebisho ya msingi kulinda ustawi wa serikali hiyo.

Khalfan alisema viongozi wa juu wa SUK bado wanaona kwamba mfumo huo wa uendeshaji Serikali ni miliki yao binafsi isiyohusisha wananchi. “Ndani ya mwaka mmoja, wananchi walitakiwa kupewa elimu ya uraia kuhusu SUK kwa kuzishirikisha asasi za kiraia; Serikali imewaacha wananchi wakigawanyika na kuwa na ufahamu mdogo wa mfumo wenyewe.

Hili ni tatizo linalotishia uhai na mustakabali wa jambo hilo,” alisema Khalfan. Pia alisema kuwa kwa miaka minne, SUK imeshindwa kuleta na kuibua mabadiliko ya msingi serikalini kutokana na makatibu wakuu, makamishna, wakuu wa mikoa na wilaya kubaki watu wale wale huku wakiteuliwa kwa kuangaliwa itikadi zao kisiasa na kushindwa kusukuma uwajibikaji na utendaji wenye tija.

Kamishna mstaafu wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Simai Mohamed Said alieleza kuwa bado SUK ina umuhimu mkubwa licha ya kujitokeza baadhi ya watu kuipinga bila ya kuwa na nguvu ya hoja na kutojali kuhesabu mema yaliyopatikana, huku wakitoa kasoro haba zinazoweza kufanyiwa marekebisho ya msingi.

Simai alisema uhai wa SUK umetokana na hekima, uongozi bora na siasa safi ya Dk Shein katika kusimamia Serikali kisera.

Alisema zipo faida lukuki zilizopatikana tangu  kuundwa kwa mfumo huo, ikiwa ni pamoja na wajumbe wa  Baraza la Wawakilishi Zanzibar bila kujali itikadi zao za kisasa, kuikosoa serikali kila inapoteleza au kujisahau.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Serikali Zanzibar (Suza), Ali Haji Vuai alisema malengo ya SUK kimsingi yalikuwa matatu, moja ikiwa ni kuondoa hofu ya kisiasa.

Vuai anasema SUK imeishia katika hatua moja kati ya hizo, ambayo aliitaja kuwa ni kuiunganisha jamii kutokana na chuki za kisiasa, lakini akakosoa ujenzi na utendaji wa uendeshaji serikali hiyo, akisema bado haujabadilika kutokana na nyadhifa nyingi za watendaji wakuu kunufaisha upande mmoja.

Alisema kosa kubwa ni kukosekana kwa imani ya pamoja na badala yake vyama viwili vinaunda Serikali moja ambayo inatekeleza sera ya chama kimoja.

Mwenyekiti wa Taasisi ya Utafiti na Sera za Jamii Zanzibar, Mohamed Yussuf Mshamba alisema SUK bado ina umuhimu, lakini akaongeza kuwa ipo haja na ulazima katika kubadili muundo na utendaji wake.

Mshamba alisema wanaofikiria kuvunja mfumo wa SUK, hawajatafakari vizuri na hali hiyo itakuwa ngumu kufikiwa kutokana na kuhitajika kwa theluthi mbili ya uamuzi wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, lakini pia kuungwa mkono kwa hoja yenyewe  itakayoanzia kwenye vikao vya Baraza la Mapinduzi.

“Mvutano wa suala hilo kabla ya kufika Baraza la Wawakilishi utaibuka kwenye kikao cha mawaziri, kupita na kukubaliwa kwa jambo hilo kutazua mbinde na pengine hata hoja hiyo isifike Baraza la Wawakilishi kutokana na vyama vinavyoonda SUK kuwa na nguvu sawa za kiuamuzi,” alisema Mshamba.

Mnadhimu wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar upande wa CCM, Salmin Awadhi Salmin alisema kuna haja ya wananchi kuulizwa kama bado wanauafiki muundo huo au umewavunja moyo.

Salmin alisema tatizo lililopo ni kukosekana kwa nia njema ya kuundwa kwa mfumo wenyewe tangu awali na kwa upande wa pili ni viongozi wa SUK wanaotoka upinzani kutaka kuhakikisha wanawapora madaraka ya utawala wenzao wa chama tawala badala ya kuitumikia Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Chanzo: Mwananchi

One Reply to “Maridhiano: Serikali ya Mseto Zanzibar yazua mjadala”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s