Maandamano ya vijana CUF yapigwa marufuku

Mwenyekiti wa Jumuia ya Vijana wa Chama cha CUF, Hamidu Bobali akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam hapo jana. Picha: Mwananchi
Mwenyekiti wa Jumuia ya Vijana wa Chama cha CUF, Hamidu Bobali akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam hapo jana. Picha: Mwananchi

Dar es Salaam. Licha ya Jumuiya ya vijana wa Chama cha Wananchi (CUF) kusisitiza azma yao ya kuandamana leo, polisi imepiga marufuku maandamano hayo na kusema halitosita kutumia nguvu endapo vijana wa chama hicho watakaidi amri ya kutoandamana.

Vijana wa chama hicho wamepanga kufanya maandamano leo kushinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuongeza muda wa kuandikisha wapiga kura kutoka siku saba mpaka 14. Pia, jumuiya hiyo inapinga uvunjifu wa haki za binadamu.

Januari 27, wafuasi wa chama hicho walifanya maandamano na kukabiliana na kipigo kutoka kwa polisi huku mwenyekiti wao, Profesa Ibrahimu Lipumba akikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kosa la uchochezi na kuhamasisha maandamano hayo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya chama hicho (Juvicuf), Hamidu Bobali alisema watafanya maandamano ya amani leo kuelekea Wizara ya Mambo ya Ndani na ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kupinga ukiukwaji wa haki za binadamu.

Maandamano hayo yanayoongozwa na makamu Mwenyekiti taifa, Babu Duni Haji yanatarajiwa kuanza saa mbili asubuhi kupitia Barabara za Uhuru, Bibi Titi na baadaye Barabara ya Ohio kisha kufika wizarani na ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Nec.

Bobali alisema pingamizi lililowekwa na jeshi hilo halina mashiko na kwamba hawajashawishika kuyasitisha. Aliwataka watu wote wapenda haki kujitokeza kwa wingi ili kushiriki katika maandamano hayo yatakayoanzia Buguruni Rozana.

“Tutakusanyika kuanzia saa mbili asubuhi na maandamano yataanza saa nne. Tutaanzia Buguruni-Rozana kupitia barabara ya Uhuru kisha Bibi Titi na baadaye Ohio. Tunaenda wizarani kuwaeleza mambo tunayoona kuwa hayaendi sawa.

Hakutakuwa na vurugu na hatujajipanga kupambana na polisi. Lakini endapo watatushambulia tutajilinda,” alisema Bubali.

Kwa maelezo ya CUF ni kwamba ufanisi wa mashine za BVR hautoweza kuandikisha wananchi wote wanaostahili kwa muda uliotengwa kwani zinauwezo wa kuandikisha watu 40 pekee kwa siku tofauti na inavyoelezwa na Tume kuwa ni watu 70.

Akizungumza na waandishi wa habari, kamanda wa polisi, kanda maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema wamezuia maandamano hayo kwa sababu vijana wa CUF hawana sababu za msingi za kuandamana, na waliwaambia wawasilishe madai yao Nec moja kwa moja.

Kova alisema sababu nyingine waliyoitoa kwamba wanapinga uvunjifu wa haki za binadamu haina mashiko kwa sababu suala la haki za binadamu linashughulikiwa kisheria baada ya uchunguzi kufanyika.

“Hatutakubali maandamano hayo kwa sababu tumebaini hayana lengo zuri. Tutatumia uwezo wetu kwa mujibu wa sheria kuhakikisha kuwa maandamano hayo hayafanyiki na kuleta kero kwa Watanzania wengine,” alisema.

Aliongeza kuwa kufanya maandamano kinyume na sheria za nchi ni kutaka nchi isitawalike, alisisitiza kuwa jeshi la polisi halitaruhusu hali hiyo kutokea.

Kamanda huyo alibainisha kuwa amepiga marufuku maandamano hayo chini ya kifungu cha 43 (1-6) cha sheria ya jeshi la polisi na polisi wasaidizi kinachompa mamlaka ya kufuta maandamano pale itakapobainika kuwa kutakuwa na uvunjifu wa amani.

“Kama hawakuridhika na maamuzi yetu tuliwashauri wakate rufaa kwa waziri wa mambo ya ndani. Lakini hawakutaka kufanya hivyo, hii si kutaka vita na jeshi la polisi,” alihoji Kamanda Kova na kusema polisi litapambana na kila mtu atakayejitokeza kuandamana.

Kova alisema kufanyika kwa maandamano hayo kutaathiri biashara za watu mbalimbali katika barabara zote walizopanga kupita. Alisema mtu hawezi kulala njaa kwa sababu vijana wa CUF wanaandamana.

Hata hivyo aliwataka wananchi kutojitokeza katika maandamano hayo ili kutojiingiza kwenye mapigano na jeshi la polisi bila sababu ya msingi. Alisisitiza kuwa hakuna mbadala wa amani, na masuala ya ukiukwaji wa haki za binadamu yanashughulikiwa kisheria

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

One Reply to “Maandamano ya vijana CUF yapigwa marufuku”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s