Rais wa Ujerumani aacha gumzo, aenda Zanzibar kwa boti

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akisalimiana na mgeni wake Rais wa Ujerumani Mhe, Joachim Gauck mara alipowasili kwa boti bandari ya Malindi, Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein akisalimiana na mgeni wake Rais wa Ujerumani Mhe, Joachim Gauck mara alipowasili kwa boti bandari ya Malindi, Zanzibar

Zanzibar/Arusha. Ziara ya rais wa Shirikisho la Ujerumani, Joachim Gauck imeacha mjadala mzito kisiwani hapa kutokana na kitendo chake cha kutumia usafiri wa boti kuja Unguja na kutembea kwa miguu hadi Hoteli ya Serena ya Zanzibar.

Rais huyo, akiwa na mwenyeji wake, Dk Ali Mohamed Shein, alikuwa akitembea mitaa ya Mji Mkongwe, huku akisalimiana na wananchi waliokuwa pembeni ya barabara kushuhudia ujio wake.

Tofauti na viongozi wengi wa juu, Rais Gauck alisafiri kutoka Dar es Salaam kwa kutumia boti ya Kilimanjaro 4 na kuwasili saa 5:30 asubuhi. Alipokewa na mwenyeji wake, Shein pamoja na wananchi wakiwamo na wanafunzi.

Baada ya kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride maalum la heshima, kiongozi huyo alianza kutembea huku akisalimia wananchi na wengine kudiriki kuwashika mikono.

Akiwa katika ulinzi wa kawaida, alipita mitaa ya Malindi, Mizigani na Forodhani ambako wananchi walikuwa wamejipanga pembeni huku wakicheza ngoma ya Beni. Siku hiyo maduka yalifungwa kutokana na sababu za kiusalama.

Mbali na hatua hiyo Wafanyabiashara wa Forodhani walitakiwa kufunga biashara zao siku moja kabla ya mgeni kuwasili na mitaa hiyo kufanyiwa usafi mkubwa, hasa kwenye barabara zote alizopita pamoja na ufukwe wa Forodhani.

Wachukuzi wa mizigo kwenye Bandari ya Malindi walipata pigo baada ya kuzuiwa kutekeleza majukumu hadi kiongozi huyo alipoondoka kuelekea Hoteli ya Serena.

Mfanyabiashara Ahmed Mwinyi  Muhamad (29) Mkazi wa Bububu alisema kitendo cha Rais Gauck kutumia usafiri wa gharama nafuu, kimewavua nguo viongozi wa Afrika ambao hutumia usafiri ghali bila ya kuwapo sababu za msingi.

Alisema kitendo cha kiongozi huyo kusalimiana na wananchi kwa kuwapa mikono kinaonyesha upendo na kuwa karibu na watu bila ya kujali wadhifa wake na kuwataka viongozi wengine kufuata nyayo zake.

“Tatizo kubwa viongozi wetu wanawahitaji wananchi wakati wa uchaguzi, wakipata huwezi kuwasogelea wala kuwaona na ukifanya mchezo utachezea virungu,” alisema Muhamad.

Katibu mkuu wa Tadea, Juma Ali Khatibu alisema Rais Gauck amewatukana kisayansi viongozi wa Afrika kutokana na kusafiri na wasaidizi wake kwa boti.

Alisema viongozi wa Afrika wakipata madaraka, hutumia magari ambayo hutembea kwa mwendo wa kasi na vioo vya giza na wakati mwingine kuhatarisha hata usalama kwa wapita njia.

“Rais Joachim ametoa fundisho kubwa kwa viongozi wa Afrika wajenge utamaduni wa kuwa karibu na wananchi badala ya kuwaogopa,” alisema Khatibu.

Mkurugenzi wa uenezi na mawasiliano ya umma wa CUF, Salum Bimani alisema kiongozi huyo amewafungua macho viongozi wenzake kuacha tabia ya kuwatumia wananchi wakati wa mahitaji yao na badala yake waonyeshe upendo.

Alisema ziara hiyo imeacha somo kubwa kwa viongozi kuwa tayari kupunguza gharama za matumizi kama kuna huduma mbadala zinapatikana badala ya kuonyesha ufahari katika matumizi.

Wakati huohuo, Ujerumani, imeahidi kuendelea kushirikiana na mataifa ya Afrika kujenga misingi ya utawala bora, haki za binadamu kama nyenzo ya kujenga, kulinda na kudumisha amani na utulivu endelevu.

Rais Gauck wa Ujerumani alitoa ahadi hiyo wakati akihutubia wafanyakazi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kwenye ukumbi wa Bunge la Eala.

“Amani na usalama ni mambo yasiyostahili kuchukuliwa kimzaha. Haya ni masuala ya msingi yanayostahili kupiganiwa na kusimamiwa kwa juhudi na nguvu zote, siyo tu ndani ya EAC, bali duniani kote,” alisema Rais Gauck

Alisema msingi mkuu wa amani na utulivu ni kutenda haki kwa kila kada ndani ya jamii husika, huku akizitaka serikali za nchi wanachama wa EAC kutunga na kutekeleza sera zinazolenga kuwaunganisha raia katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Rais Gauck aliyetembelea pia Mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na katika mazungumzo ya faragha na rais wa Mahakama hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu, Agustino Ramadhani, aliyataka mataifa ya Afrika kuzingatia utawala wa sheria na haki za binadamu.

“Uvunjaji wa haki za binadamu ni suala lisilovumilika. Wahusika wote wa uvunjaji wa haki za binadamu lazima wawajibishwe kwa kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria na kuhukumiwa kwa makosa yao,” alisisitiza Rais huyo wa Ujerumani anayemaliza ziara yake nchini leo

Katika mazungumzo yao, Jaji Ramadhani alimuomba Rais Gauck kusaidia kuhimiza Mataifa ya Afrika kuridhia mkataba wa kuanzishwa kwa mahakama hiyo na kutoa tamko kuruhusu raia wake kufungua kesi mahakamani hapo.

Hadi sasa, ni Mataifa 28 pekee, kati ya 54 Barani Afrika ambayo yameridhia mkataba wa kuanzishwa kwa mahakamani hiyo, huku saba pekee yakitoa tamko kuruhusu raia wake na mashirika yasiyo ya kiserikali kufungua mashauri mbele ya mahakama hiyo.

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s