Kificho: Sheria Kura ya Maoni haijaridhiwa Z’bar

Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho

Zanzibar. Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), Pandu Ameir Kificho amesema Sheria ya Kura ya Maoni bado haijaridhiwa na Baraza la Wawakilishi kama masharti ya Katiba ya Zanzibar yanavyoeleza.

Kauli ya Kificho imekuja ikiwa ni siku moja baada ya Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS) na Taasisi ya Utafiti na Sera za Jamii Zanzibar (ZIRPP), kusema sheria imekiukwa katika utekelezaji wa mchakato wa Mabadiliko ya Katiba baada ya Baraza la Wawakilishi kutoridhia Sheria ya Kura ya Maoni Namba 11 ya Mwaka 2013.

Pia walidai kwamba Rais Jakaya Kikwete alivunja sheria kutokana na hatua alizochukua za kutangaza tarehe ya kufanyika Kura ya Maoni akiwa China, wakati jukumu hilo ni la Tume za Uchaguzi za Tanzania na Zanzibar kwa mujibu wa Kifungu cha 5(1)(B) cha Sheria ya Kura Maoni.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Salva Rweyemamu alisema juzi kuwa Rais ana washauri wake wenye taaluma zao akisema kuna Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Waziri wa Katiba na Sheria ambao wanamshauri kwenye masuala ya kisheria.

“Ifikie mahali watu waheshimu taaluma za wengine na wajue kwamba ni nani ambaye ametoa agizo, siyo kwa sababu wao ni wanasheria, basi wakae tu kikao na kusema ya kwao kwamba Rais alivunja sheria,” alisema Rweyemamu.

Kificho alisema tangu kutungwa kwa Sheria ya Kura ya Maoni na kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mwaka 2013, haijafikishwa katika Baraza na kwamba suala hilo linahitaji kuzingatiwa kwa kuhakikisha Sheria ya Kura ya Maoni inawasilishwa kabla ya Kura ya Maoni Aprili 30.

Alisema sheria yoyote itakayotungwa na Bunge kabla ya kutumika lazima iridhiwe na Baraza la Wawakilishi kama haina uhusiano na mambo ya Muungano.

Alisema Kifungu cha 132(1) cha Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 kimeweka sharti kuwa: “Hakuna sheria yoyote itakayopitishwa na Bunge la Muungano ambayo itatumika Zanzibar hadi sheria hiyo iwe ni kwa ajili ya mambo ya Muungano tu na ipitishwe kulingana na maelekezo yaliyo chini ya vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.”

Alisema ni sheria mbili tu zilizotungwa na Bunge na kuletwa Zanzibar kuridhiwa kabla ya kuanza kutumika; Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora na Sheria ya Kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Hata hivyo, Kificho alisema kwamba Sheria ya kura ya Maoni imetajwa katika Sheria ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo iliwasilishwa Barazani na kupata ridhaa ya Baraza la Wawakilishi kabla ya kuanza kutumika ikiwamo kazi ya kukusanya maoni ya wananchi. Pamoja na kutajwa katika Sheria ya Tume ya mabadiliko ya Katiba, Spika Kificho alisema inahitajika kuangaliwa kama inatosha kwa kutajwa katika sheria nyingine au la ili kufikia matakwa na masharti ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.

Kificho alisema kwamba Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ndizo zenye jukumu la kusimamia Kura ya Maoni.

Awali, Rais wa ZLS, Awadhi Ali Said alisema maandalizi na matokeo ya kura ya maoni yatakuwa batili kutokana na Sheria ya Kura ya Maoni kuwa bado haijaridhiwa na Baraza la Wawakilishi kinyume na Katiba ya Zanzibar.

Alisema haikuwa muafaka kwa NEC kutangaza suala hilo kabla ya sheria hiyo kupata Baraka za Zanzibar na kuridhiwa na Baraza.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

One Reply to “Kificho: Sheria Kura ya Maoni haijaridhiwa Z’bar”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s