Wanaitembeza Katiba isiyowafaa Watanzania

Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Abdulrahman Kinana akihutubia wananchi wa Mikoa miwili ya Kisiwani Pemba kwenye mkutano wa hadhara
Katibu Mkuu wa CCM Ndg. Abdulrahman Kinana akihutubia wananchi wa mikoa miwili ya kisiwani Pemba kwenye mkutano wa hadhara

SINA shaka, viongozi wakuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) tayari wanatumikia adhabu ya kupazwa. Wamekuwa wakila kwa matonge na kufakamia. Wanaonesha jeuri iliyozidi kiwango. Wakiwa wameshiba, bila ya kujali kushiba kwao kwa kufuru ni kudhulumu wananchi, wanathubutu hata kunengua viuno mchana kweupe, mbele ya kamera.

Wanajua wanachokula ni chakula kilichoandaliwa kwa gharama ya fedha za wananchi – kununulia unga wa ngano, sukari, mafuta ya kupikia, mchele, nyama, kuku, chumvi na viungo.

Lakini wamesahau yote hayo. Wameongeza kula kwa fujo na kutupa masalio katika kudhihaki wanyonge wanaonuka umasikini. Hawakujua mwezeshaji ana siku yake na wakati huamua kuadhibu wafisidi juu ya ardhi yake.

Sasa viongozi hawa wanaandamwa na walichokula kwa fujo. Wakiwa hai duniani wanalipa kimtindo gharama ya kudhulumu wanyonge, kiasi cha kukaribia kusokomezwa kule wasikokutarajia. Ama kweli asiyesikia la mkuu huvunjika guu.

Baada ya kuipitisha Katiba inayopendekezwa, kwa njia ya kinajimu, iliyofanikishwa kwa fedha nyingi za umma huohuo, tena wakiitumia Zanzibar kujitangazia ushindi, viongozi wa CCM wanaweweseka.

Wameivamia Zanzibar wakidhihirisha walivyojimilikisha nchi pamoja na jamhuri. Wanatukana, mumo kwa mumo wakidhihaki wananchi kwa kuwataka waikubali na kuipigia kura.

Ingawa wanajua kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni, kipindi cha kampeni kwa umma hakijafika bado, wao kwa kuwa ndio “wenye nchi” na kila kitu, wameanza kampeni rasmi.

Wanajua vilevile kuwa wanachokifanya ni kitu kisicho cha haki, maana wanashawishi wananchi waikubali katiba bila ya kuwahakikishia wanayo mikononi kwa ajili ya kuisoma ili kuielewa vilivyo, wameendelea kupanda majukwaani wakitunisha mishipa ya shingo kuitakia ridhaa.

Ratiba ya Kura ya Maoni, kwa ajili ya kuifanyia uamuzi Katiba inayopendekezwa, haijatangazwa.

Watangazaji wa ratiba hii sio Rais ambaye inaeleweka alitimiza wajibu wake kuelekeza amri ya serikali ichapishwe katika Gazeti Rasmi baada ya yeye kukabidhiwa katiba inayopendekezwa, wala sio wao viongozi wa CCM.

Kwa mujibu wa sheria iliyopo nchini, Tume ya Taifa ya Uchaguzi – National Electoral Commission (NEC) – ndio yenye wajibu huo. Haijatangaza.

Tume hii ilichoeleza ni utaratibu wa kuandikisha wananchi kwa ajili ya kuandaa Daftari la Kudumu la Wapigakura. Katika kueleza hili, ilibainisha ratiba lakini si ya kuchukuliwa kuwa ni uamuzi kwamba kura itafanyika siku ya 30 Aprili kama inavyopigiwa debe na CCM.

Kwanza kuitishwa kwa kura hii kunategemea sana kukamilika kwa maandalizi yanayofanywa na Tume ya Uchaguzi. Ni maandalizi yanayofanywa baada ya tume kupata fedha kutoka serikalini. Makisio ya tume katika kufanya kazi ya kuandaa daftari la wapigakura ni Sh. 293 bilioni.

Uongozi wa Tume haujawahi kuthibitisha kama umepatiwa fedha ilizotaka. Taarifa za kichunguzi zinasema hata nusu ya fedha hizo haijafikia kutolewa.

Tuseme serikali imetoa fedha zote. Uandikishaji wapigakura hauwezi kukamilika kwa Februari na Machi, kuna kazi ya kuhakiki kilichoandikishwa. Chini ya mfumo mpya wa kielektroniki, hii kazi haitakamilika.

Sheria inatoa kipindi cha elimu kwa umma kuieleza katiba. Ni kipindi ambacho Tume inatakiwa kuunda kamati mbili, moja ya kuhamasisha wananchi wairidhie na nyingine ya kuhamasisha wananchi waikatae katiba inayopendekezwa.

Uhamasishaji huu unapaswa kufanywa huku wananchi wakiwa na nakala za katiba hii. Mpaka sasa nakala za katiba hii ni lulu. Aliyenayo ameipata kibahati.

Unapoona hata asasi muhimu za kiraia, wabunge, vyama vya siasa, vyombo vya habari havijapatiwa nakala za katiba hii zaidi ya kubaki kwenye mitandao, jiulize hiyo elimu kwa umma itatolewaje?

Basi viongozi wa CCM wakafika Zanzibar majuzi. Wanahamasisha Unguja na Pemba waikubali katiba na siku ya kura ya maoni waipigie NDIO. Dhihaka iliyoje jamani?

Watu ambao wamesahauliwa kwa miaka yote katika kupewa mamlaka ya kuamua mustakbali wa Muungano na wakakosa maoni yao kujumuishwa kwenye katiba, wanashawishiwa kuiridhia katiba inayopendekezwa. Maajabu makubwa.

Niliwahi kueleza kwenye safu hii namna upitishaji wa katiba hii ulivyoandamana na uchafu unaonuka vibaya. Kulikuwa na harufu mbaya iliyohatarisha neva za pua za Wazanzibari wengi kukatika.

Utafutaji wa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uligubikwa na jitihada za kishetani zinazopaswa tu kutendwa na mashetani.

Kama lilivyoandaliwa na watawala tangu mwanzo, ndivyo lilivyoishia – mashetani kujiamini na kuthubutu kutumia elimu ya unajimu kufanikisha walichopanga.

Basi Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM, na Nape Nnauye, Katibu Mwenezi, wameungana na wasaidizi wao wa Zanzibar kuhimiza katiba iamuliwe kwa kura ya NDIO.

Kampeni yao imeandamana na maneno makali pia, wanafundisha Kiswahili Wazanzibari. Hawajui Wazanzibari wamebobea lugha hii hata itumiwapo kwa mafumbo. Ni chakula chao kila siku.

Siioni Katiba ya kushaawishiwa Wazanzibari waikubali. Tena sasa uongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ukiwa umeshapigilia msumari wa moto: Vyama vyao havitashiriki Kura ya Maoni.

Sababu ni zilezile – katiba yenyewe imebeba matakwa ya CCM ya kung’ang’ania utawala usiozingatia misingi ya utawala bora. Inalinda mifumo ya kulinda wafisidi wa uchumi; inaendeleza kuinyima Zanzibar mamlaka ya kutumia raslimali zake kujiendeleza.

Ni katiba iliyojaza ahadi za kizushi. Kusema Zanzibar sasa itakopa kimataifa bila kikwazo, au itajiunga na OIC, au itachimba mafuta yake, ni ulaghai mtupu.

Yote hayo hayatawezekana mpaka uongozi wa Serikali ya Muungano (SMT) utake. Siku zote SMT imekuwa ikiidhalilisha uongozi wa Serikali ya Mapinduzi (SMZ) linapokuja suala la kutaka idhini ya mambo kama hayo.

Zanzibar imeporwa serikali za mitaa, imeporwa ardhi yake ndogo iliyopo, maana haya yametiwa katika katiba inayopendekezwa.

Zanzibar imedanganywa miaka yote ya Muungano kama mtoto mdogo anayepewa pipi na baba ili asilie akiahidiwa kesho ndio atapewa atakacho. Kumbe hatapewa, na akili tena, anaongezwa pipi huku akiambiwa “kesho nitakuletea.” Ulaghai haukubaliki.

Kwa kuwa CCM wamewasakama wawakilishi wa vyama vya upinzani hata kugomea Bunge Maalum la Katiba, na wakaitumia vizuri nafasi kuvuruga Rasimu ya Katiba iliyobeba maoni ya wananchi, hakuna maneno matamu yatakayowatuliza Wazanzibari.

Kama Kinana, Nape na wenzao hawana lugha ya kushawishi Wazanzibari kuiridhia katiba mpya, sioni hilo kufanikishwa na Mzee Kingunge Ngombale-Mwiru, Hamad Rashid Mohamed na Dk. Francis Michael kupitia kampeni mpya ya Waziri wa Habari.

Maneno kwamba Wazanzibari wakubali ardhi yao itwaliwe na SMT kwa kuwa Mzee Aboud Jumbe Mwinyi aligawiwa ekari 50,000 Bara, hayatoshi kuonesha Zanzibar ina fursa ya kujitegemea ndani ya mfumo wa Muungano wa serikali mbili.

Kinana wanaitembeza katiba hii kwa sababu haifai maana chema chajiuza, kibaya ndio hujitembeza. Kimekosa soko eti! CCM wanaitembeza katiba isiyowafaa Wazanzibari na wenzao Watanganyika.

Chanzo: Mawio

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s