Lipumba agonganisha mihimili yote ya nchi

Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia akizungumza wakati wa kuhitimisha hoja yake kuhusu vurugu zilizotokea juzi jijini Dar es Salaam wakati viongozi na wafuasi wa CUF walipopigwa na kukamatwa na polisi. Picha: Mwananchi
Mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia akizungumza wakati wa kuhitimisha hoja yake kuhusu vurugu zilizotokea juzi jijini Dar es Salaam wakati viongozi na wafuasi wa CUF walipopigwa na kukamatwa na polisi. Picha: Mwananchi

Dodoma. Mjadala kuhusu sakata la polisi kumpiga na kumtia mbaroni Profesa Ibrahim Lipumba jana ulikuwa mkali, lakini uliweka bayana kugongana kwa mihimili mitatu ya nchi baada ya Bunge kujadili suala hilo wakati likiwa limeshafika mahakamani.

Mgongano huo umetokea katika kipindi kisichozidi miezi miwili baada ya Bunge kugoma kupokea zuio la Mahakama la kujadili kashfa ya uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escow na kuendelea na mjadala ambao ulifikia maazimio ya kuwawajibisha wahusika.

Tukio lililojadiliwa jana lilitokana na Profesa Lipumba kukamatwa Jumanne wiki hii wakati akielekea Zakhem, Mbagala ambako alidai alikuwa akienda kutawanya wafuasi wa chama hicho baada ya Jeshi la Polisi kuzuia maandamano na mkutano wa hadhara wa chama hicho ulioandaliwa kwa ajili ya kukumbuka wafuasi 22 waliouawa mwaka 2001 wakati wakiandamana kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000.

Wakati mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia aliwasilisha hoja juzi majira ya saa 5.00 asubuhi kutaka Bunge lisitishe shughuli zake na kujadili suala hilo aliloliita “la dharura, kwa maslahi mapana ya Taifa”, Jeshi la Polisi lilimfikisha Profesa Lipumba mahakamani siku hiyohiyo lakini alasiri.

Jana, baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe kutoa taarifa ya Serikali kuhusu tukio hilo na kuomba radhi kwa yaliyotokea huku akiahidi uchunguzi kwa waliohusika kutumia nguvu kupita kiasi, Spika Anne Makinda alimsimamisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju kuzungumza.

Masaju alijaribu kuzima mjadala huo kwa maelezo kuwa tayari Profesa Lipumba ameshafunguliwa mashtaka mahakamani, hivyo haingekuwa busara kwa Bunge kujadili suala hilo.

Kila alipojaribu kusoma vifungu vya sheria vinavyozuia muingiliano wa mihimili mitatu ya nchi, Serikali, Bunge na Mahakama, wabunge walipiga kelele.

Hata hivyo aliendelea kuwa Bunge linaongozwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria, na katika Kanuni ya 64 (1), Bunge haliruhusiwi kujadili jambo lolote ambalo liko mahakamani.

“Mihimili mitatu ni lazima isiingiliane, jambo hili lipo bungeni kujadiliwa kwa ajili ya kutolewa maamuzi, na lipo mahakamani kwa ajili ya kutolewa maamuzi, lakini mahakama ndiyo inayoweza kutoa maamuzi ya mwisho,” alisema Masaju.

“Kutokana na mazingira haya, naomba nilishauri Bunge lisijadili jambo hili,” alisema mwanasheria huyo aliyeteuliwa mapema mwezi huu.

Lakini baada ya kumaliza hoja zake, wabunge walipiga kelele na baadhi wakisema wanataka muongozo. Baadaye Spika Makinda alisema Bunge litajadili suala hilo.

Wabunge walijadili kwa kina tukio lote la kupigwa na kukamatwa kwa Profesa Lipumba kujaribu kuonyesha kuwa kiongozi huyo hakufanya kosa kwa kuwa chama kilifuata taratibu zote za kulitaarifu Jeshi la Polisi na kwamba baada ya amri ya kuzuia maandamano na mkutano, alitii amri, hoja ambazo zinaonekana kupinga mashtaka yaliyoko mahakamani kuwa Lipumba na wafuasi 32 wa CUF waliandamana bila ya kibali.

“Jeshi la Polisi lilifanya uhuni kuwahisha kumpeleka Profesa Lipumba mahakamani,” alisema Mbatia.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mjadala huo, Mbatia alisema kitendo hicho cha kuwahisha mahakamani suala la Profesa Lipumba, kililenga kulizuia Bunge kutekeleza azma yake ya kujadili tukio hilo lililotokea Mtoni Mtongani jijini Dar es Salaam.

Awali katika taarifa ya Serikali, Chikawe alieleza mtiririko mzima wa tukio hilo na kuagiza idara ya malalamiko katika wizara yake kufanya uchunguzi wa malalamiko kwamba katika kadhia hiyo polisi wametumia nguvu nyingi kuliko ilivyotakiwa.

“Jeshi la polisi halipaswi kutumia nguvu kuliko zinazohitajika katika kukamata watuhumiwa wa makosa ya jinai… haipo kwenye sheria ipo kwenye Police General Orders (maagizo ya jumla ya polisi). Serikali inaomba radhi wananchi wote waliokumbana na kadhia hii bila ya wao kujihusisha.”

Alisema ni muhimu wananchi wakajiweka mbali na matukio yote ya uvunjifu wa sheria kwa kuwa polisi itaendelea kutimiza wajibu wake kisheria nchini.

Wakati wa kujadili tukio hilo jana, wabunge wengi walimrushia lawama Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakidai kuwa kauli aliyotoa bungeni mwaka juzi ya kutaka wananchi wapigwe iwapo hawatatii amri, imechochea vitendo hivyo vya polisi.

Mjadala huo pia ulionyesha mgawanyiko baina ya wabunge wa CCM, ambao walitetea vitendo hivyo vya polisi wakidai kuwa amani lazima ilindwe, huku wa vyama vya upinzani wakipinga.

Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ambaye alikuwa wa kwanza kuchangia, alisema Pinda na Chikawe hawafai kukaa kwenye viti vyao hata kwa dakika moja kwa kuwa kauli ya wapigwe tu ni ya Serikali nzima.

Alisema sheria haiwapi polisi mamlaka ya kukataza maandamano, bali kulinda na kupanga lini na njia za maandamano.

“Lipumba hakukataa… Jeshi la Polisi limetekwa na element (chembechembe) za kifashisti na wamebadilisha hata namba za magari yao kutoka STK na kuwa PT yaani Piga Tu. Mawaziri Pinda, Chikawe na IGP tunahitaji kuwawajibisha,” alisema Lissu.

Alisema inabidi kubadilisha sheria na sera za nchi ili polisi wawe wanalinda maandamano na si kupiga watu hovyo.

“Wakuu wa mikoa na wilaya waondolewe kwenye kamati za ulinzi na usalama za mikoa kwani ni makada wa CCM na ndiyo wanaotupiga na tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu, hivyo tunapopiga kelele sasa hivi ni kwa sababu maafa makubwa yanatusubiri,” alisema Lissu.

Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mnyaa aliungana naye akisema kuwa kuzuiwa kwa maandamano siku ya tukio wakati yaliombwa siku sita kabla, ni jambo la kusikitisha.

“Waziri aache kutudanganya kwamba Lipumba hakusitisha maandamano. Kilichotokea juzi tusikichukulie kivyama… kwani wabunge hawa wa CCM wameshapigwa na polisi?”alihoji.

Alisema inaonyesha kwenye jeshi hilo kuna mgawanyiko hivyo Bunge liwe na maazimio ya kusimamia mambo hayo ili kuwa na mabadiliko kwenye chombo hicho.

“Nguvu zilizotumika Mbagala kwa nini zisitumike kutafuta majambazi waliovamia kituo cha polisi Ikwiriri, au Tanga? Kauli ya Waziri Mkuu kusema ‘piga tu’ ni kauli mbaya,” alisema Mnyaa.

Naye mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali alisema ripoti ya Jumuiya ya Madola kuhusu polisi nchini inaeleza kuwa bado lina mfumo wa kikoloni kwa kuwa linafanya yale yale yaliyokuwa yakifanywa wakati wa ukoloni.

“Siyo sisi tunasema ni hii ripoti inasema sheria ya polisi ibadilishwe kwa kuwa ina mfumo wa ukandamizaji na kwamba ikibaki hivyo italiingiza Taifa kwenye maafa makubwa,” alisema Mkosamali.

Kwa upande wake mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari alilalamika kuwa wanachofanyiwa wapinzani, wamachinga, mamantilie, wanafunzi na watoto ni kitendo kisichoridhisha.

“Upinzani tumekuwa tukipewa kesi tu na sasa ni kila sehemu Mbowe, Lissu, Lema, Mdee mimi mwenyewe na juzi Lipumba (wana kesi). Iko siku haya yataisha,” alisema Nassari.

Rashid Abdallah, ambaye ni mbunge wa Tumbe, alisema: “Lipumba anapaswa kuheshimiwa kama ilivyo kwa (Rais Jakaya) Kikwete kwani ni mwenyekiti wa chama kama alivyo Kikwete. Polisi inatakiwa kubadilishwa hasa kwenye uongozi,” alisema na kupigilia msumari kuwa Waziri Pinda hafai.

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema, alisema kila wakiwasilisha taarifa za unyama unaofanywa na polisi, viongozi wamekuwa wakidharau.

“Kila tunapowapa taarifa nyie mnachukua ripoti kutoka kwa wanayofanya hayo halafu nyie mnakuja kuzisoma hapa bungeni,” alisema Mbowe huku akikumbusha tukio la kupigwa bomu wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika jijini Arusha.

Mbowe alisema Waziri Mkuu aliwahi kutoa taarifa za uongo bungeni, lakini Lema akamwambia ni uongo na jambo hilo halikuwahi kujadiliwa hadi leo.

Alisema alienda kumuona Profesa Lipumba alipofikishwa polisi na baadhi ya askari ambao hakuwataja walimweleza kuwa yalikuwa ni maagizo kutoka juu.

“Waziri Chikawe anasema Lipumba hakutii wakati alitimiza wajibu wake na televisheni zilionyesha,” alisema.

Alisema mbunge wa viti maalum (Chadema), Rose Kamili, ambaye alidaiwa kupigwa na polisi mkoani Iringa, hivi sasa amekuwa kilema na ametumia zaidi ya Sh 106 milioni za serikali kwa ajili ya matibabu.

Henry Shekifu (Lushoto) aliongoza wabunge wa CCM kutetea vitendo vya polisi akisema hawezi kutetea maovu.

“Hakuna nchi isiyokuwa na polisi au jeshi, vurugu zinatokea kutokana na watu kutotii sheria na kanuni, watu lazima watumie hekima na kufuata sheria,” alisema Shekifu na kuongeza kuwa polisi lazima wapambane hata kama kuna kuheshimu haki za binadamu.

Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba alisema hata kama Serikali inaundwa na CCM, lakini si kweli yanayofanywa na dola yote ni maagizo ya chama hicho.

“Kama kuna jambo linalohusu maslahi yetu, lazima tuwe pamoja, hivyo nashauri pia Serikali iangalie namna ya kutenganisha waandishi wa habari kwa kuwa na vifaa maalumu kutokana na kazi ngumu wanayoifanya,” alisema Nkumba.

Alisema katika nchi lazima kuwe na utii wa sheria hata kama chama gani kitawale.

Mbunge wa Donge, Sadifa Sadifa nusura azue tafrani wakati akitoa mchango wake baada ya kuifananisha CUF na vyama vya kuweka na kukopa (Saccos), jambo ambalo Spika alimtaka afute maneno hayo kutokana na wabunge wa upinzani, hasa CUF kumjia juu.

Alisema polisi walitumia nguvu ya kawaida kudhibiti maandamano hayo na kwamba Profesa Lipumba hakupigwa aliguswa tu, hivyo haki ya kuandamana isitumike vibaya.

Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde alifurahia tukio hilo akisema “ni sawa kwani alipigwa Kasanga Tumbo, ndo sembuse Lipumba.”

Akihitimisha mjadala huo, Mbatia alisema hakuna binaadamu mwenye mamlaka ya kuchukua uhai wa binadamu mwenzake na kwamba wapinzani si watu wa daraja la pili kwa kuwa nchi ni ya wote na kwamba kufanya hivyo ni ugaidi na kupiga akina mama ni ukatili.

“Tufanye marekebisho katika sheria ya polisi haraka ili Uchaguzi Mkuu ujao uwe wa amani na utulivu. Suala lililotokea juzi ni la kulaaniwa na tunaomba wote waliohusika wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema Mbatia.

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s