Amran Umbaya Vuai (1933-2015): Lulu iliyotutoka

Marhum Amran Umbaya Vuai
Marhum Amran Umbaya Vuai

Na Ahmed Rajab               Toleo la 390  28 Jan 2014

KUNA watu na watu. Kuna wasio na haya wala staha. Mfano wao ni baadhi ya wanasiasa uchwara wa Zanzibar. Hawa mara hupanda majukwaani wakitukana na kuwatisha wananchi wenzao. Mara hutishia kuidhibiti mitandao ya mawasiliano ya kijamii.

Kazi yao kubwa ni kutia fitina, kupalilia chuki katika jamii na kuvurumisha matusi na shutuma zisizo na ukweli bila ya kuzingatia athari zake.

Kuna na wengine wenye adabu na heshima zao. Aghalabu watu wa aina hii thamani yao huwa haitambuliki mpaka wanapoiaga dunia. Wanapokuwa hai huonekana kuwa ni watu wa kawaida tu wanaohangaika na maisha.

Wanapofariki ndipo tunapotanabahi kwamba lulu imetuponyoka. Ndipo huhuzunika tukibaki kusema: “amma tumeondokewa na mtu.”

Maneno hayo ndiyo tuyasemayo tuliokuwa tukimjuwa Amran Umbaya Vuai tangu afariki jijini London Januari 17, siku tatu baada ya mdogo wake Mohamed kufariki Unguja. Tungali twayasema maneno hayo kwa sababu marehemu Amran alikuwa na mengi ya kupigiwa mfano. Nitayataja mawili tu: hulka yake na msimamo wake wa kisiasa.

Hulka yake yote ilikuwa ni mchanganyiko wa uungwana na uzalendo. Mchanganyiko huo ndio uliomfanya awe “mtu wa watu.” Uliwafanya Wazanzibari wenzake wampende, wamsikilize kwa hekima yake, watake ushauri wake na wamheshimu kama yeye alivyokuwa akiwaheshimu; na akiwaheshimu wakubwa na wadogo zake.

Uungwana wa Amran Umbaya ulikuwa ule unaopatikana Uswahilini tu. Ni uungwana uliojikita kwenye mienendo, mila na desturi za Waswahili. Kwa ufupi, msingi wa uungwana wake ulikuwa ni utamaduni wa Kiswahili.

Hapa inafaa niongeze kwamba Amran akikerwa na jinsi Kiswahili kisemwacho Uswahilini, iwe Pwani ya Kenya, Unguja, Pemba au sehemu za Mrima, kinavyopotoshwa na wasio Waswahili na hata na baadhi ya Waswahili wenyewe wanaoshikilia kwamba lazima kifuatwe kile kiitwacho “Kiswahili sanifu.”

Ilikuwa rahisi kwake kuwa na muamala mzuri na kila aliyekutana naye kwa sababu ya uungwana aliokuwa nao.

Ijapokuwa alikuwa myenyekevu, mcheshi, karimu na mpole katika mazungumzo yake hata hivyo ghafla akipandisha hamaki alipohisi kwamba wananchi wanaendewa kinyume na viongozi wao. Akiwa mpigania haki hakuweza kuvumilia uonevu au madhila ya aina yoyote.

Ama uzalendo wake hausemeki. Ulikuwa wa hali ya juu kabisa, ukivuka mipaka ya kikabila na ya vyama vya siasa. Katika miaka ya karibuni hadi kufa kwake alikuwa akiwashajiisha Wazanzibari wasahau tofauti zao za kivyama, wawe kitu kimoja katika kupigania haki zao na wahakikishe kwamba nchi yao inarejeshewa mamlaka yake kamili.

Sikumbuki siku yoyote niliyozungumza naye asinitajie Zanzibar na kujadili mustakbali wake. Alipokuwa anakuuliza kama kuna chochote akikusudia iwapo kuna habari zozote za nyumbani, za Tanzania, kwa jumla, na hususan za Zanzibar.

Nina hakika kwamba Zanzibar ndiyo iliyokuwa ikimwenda akilini alipokuwa akilala usiku na ndiyo aliyokuwa akiamka nayo.

Halikuwa jambo la ajabu kwamba aliwausia watu wasiopungua watano kwamba atapofariki maiti yake isafirishwe ikazikwe Zanzibar, tena kwao Chwaka. Na huko ndiko alikozikwa na umati wa watu Jumamosi iliyopita karibu na kaburi la mzee wake Sheikh Umbaya Vuai Shirazi.

Hakuna kilichokuwa kikimtia uchungu zaidi ya kuwaona baadhi ya viongozi wa Zanzibar walivyo tayari kuitosa nchi yao kwa maslahi yao ya kibinafsi. Angelikuwa hai angekwisha watafutia majina wanaoandaa mkakati wa kuukaba uhuru wa mawazo na wa kujieleza.

Alivunjwa moyo na viongozi wa siasa wa Zanzibar kwa kukosa kuwa na msimamo mmoja kuhusu majaaliwa ya nchi yao. Ndio maana mwishoni mwa uhai wake akiamini kwamba ufumbuzi wa suala la Zanzibar utapatikana Bara kwa juhudi za wenye kudai serikali ya Tanganyika yenye mamlaka yake.

Kwa vile alikuwa na dongo zuri Amran alikuwa haonyeshi kwamba alikuwa na umri mkubwa (Februari hii inayotupigia hodi angetimia miaka 82). Si kipindi kirefu alipoanza kuugua maradhi yaliyosababisha kifo chake.

Nilikuwa naye kwa muda wa saa kadhaa kabla hajakata roho. Siku hiyo nilitambua kwamba alikwishachungulia kwingine na karibu ataihama dunia hii. Juu hayo nilipoarifiwa kuwa ametutoka nilihisi kama kwamba mauti yalimjia ghafla.

Kifo chake kilinifanya niyakumbuke aliyowahi kuyasema mshairi mmoja wa kale wa Pwani ya Kenya:

Mauti ‘sidhani, yana muhula

Milele viumbe, hufa ghafula

Muumini hwamba: “Chenda hilala

Sipambaukiwi, nili mzima”

Daima hali huwa ndiyo hiyo. Ukenda kulala hujui kama utaamka u hai. Leo upo, kesho hupo.

Amran Umbaya alikuwa wadinasi, yaani mtoto wa watu.

Alizaliwa katika ukoo maarufu sehemu za shamba huko Chwaka kwenye mwambao wa mashariki mwa Unguja. Siku alizozaliwa yeye Chwaka ilikuwa kijiji, siku hizi ni mji mdogo. Ni sehemu yenye mandhari ya kuvutia. Watu kutoka mjini hupenda kwenda mandari Chwaka katika siku zao za mapumziko.

Chwaka ina umaarufu mwingine, wa Maulidi makubwa ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) ambayo yalianzishwa kusomwa huko kila mwaka na Sheikh Umbaya, mzee wake Amran.

Sheikh Umbaya alikuwa mtu mahashumu aliyeenziwa na watu wa tabaka na kabila tofauti. Na Maulidi yake yakihudhuriwa na masheikh wakubwa wakubwa wa Unguja.

Katika siku za ukoloni Sheikh Umbaya alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Utawala la Chwaka na akithaminiwa na viongozi wa vyama vyote vikuu vya siasa. Wakati wa Mapinduzi aliwahifadhi wafuasi kadhaa wa chama cha Hizbu, Zanzibar Nationalist Party (ZNP), wasije kuuliwa.

Baada ya Mapinduzi Sheikh Umbaya aliteuliwa mbunge na alitukuzwa na mshairi mwenzake Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwani Sheikh Umbaya alikuwa mshairi mahiri aliyekuwa na kipaji cha kutunga mashairi papo kwa papo.

Mwaka 1969 Rais Abeid Amani Karume alimchagua Sheikh Umbaya kuwa miongoni mwa wananchi 21 aliowapa dhamana ya kusimamia, bila ya malipo, ujenzi wa Chuo cha Kiislamu kilicho Mazizini, Unguja.

Chwaka ndiko Amran aliposoma Qur’an chuoni na kuanza kusoma katika shule ya msingi. Baadaye aliendelea na masomo yake mjini alipopelekwa kuishi na familia ya mmoja wa mashekhe na waalimu maarufu wa siku hizo Sayyid Hassan Sheikh.

Alikuwa miongoni mwa wanafunzi 40 wa mwanzo kutoka Zanzibar waliopelekwa na serikali ya kikoloni kwenda kusomea unahodha katika taasisi ya Mombasa Institute of Muslim Education (MIOME). Taasisi hiyo ilianzishwa ikiwa na lengo la kuwapatia elimu ya mambo ya ufundi wanafunzi wa Kiislamu kutoka Kenya, Tanganyika, Uganda na Zanzibar.

Masomo yaliyokuwa yakitiliwa mkazo MIOME ni uhandisi wa umeme na wa makanika, ubaharia na unahodha pamoja na useremala.

Mchango mkubwa wa fedha za kuanzishia taasisi hiyo ya MIOME zilitolewa na Sultani wa Zanzibar, nyingine zilitolewa na Jumuiya ya Mabohora wa Afrika ya Mashariki na Aga Khan. Ukoo wa Khamisi wa Mombasa ulitoa ardhi iliyojengewa taasisi hiyo ambayo siku hizi ni Chuo Kikuu cha Ufundi cha Mombasa, Technical University of Mombasa (TUM).

Bahati mbaya Amran na mwenzake mmoja hawakuweza kumaliza masomo ya unahodha MIOME kwa sababu walipopimwa macho walionekana kuwa ni vipofu rangi. Walikuwa na ugonjwa uliowafanya wasiweze kutofautisha rangi.

Kuweza kuona sawasawa ni kigezo cha lazima katika masomo ya unahodha. Kwa vile walikuwa vipofu rangi ilibidi wasimamishwe wasiendelee na masomo.

Wanafunzi wenzake wa Kizanzibari aliokuwa nao MIOME walimchangia fedha Amran na wakamfungia safari ende Uingereza kwa masomo mingine. Na huko akasomea umakanika wa magari.

Alirudi Zanzibar miaka michache baada ya Mapinduzi kwa kumridhia mzee wake na akateuliwa na Sheikh Abeid Karume kuwa meneja msaidizi wa Ofisi ya Utalii ya Tanzania Friendship Tourist Bureau.

Kwa bahati mbaya fitina za Mapinduzi zilimwandama na alifungwa gerezani kwa miaka kadhaa kwa kosa la kusingiziwa.

Alifunguliwa 1978 na baadaye akapata kazi ya kuwa meneja msaidizi wa hoteli za Zanzibar Hotel na Africa House. Baada ya hapo akaajiriwa katika meli ya MV Mapinduzi akiwa na kazi ya kuongoza meli. Mwaka 1980 aliihama Zanzibar na kurudi Uingereza.

Kwa muda wa miaka kadhaa aliingia katika shughuli za biashara akisafiri baina ya Uingereza na Gambia. Lakini baada ya mfumo wa vyama vingi vya siasa kuruhusiwa tena nchini Tanzania mshipa wa Zanzibar ulimpiga na akaamua kurudi akiyafanya maskani yake yawe Unguja na Uingereza.

Unguja akaanza kulima mboga na matunda ya aina mbalimbali ambayo akiyauza kwenye mahoteli.  Wakati huohuo siasa zikimwenda na alikuwa hakosekani akitoa rai zake kwenye mikutano na makongamano kuhusu mustakbali wa Zanzibar.

Kwa mfano, katika kongamano la kuadhimisha siku ya haki za binadamu lililofanywa Desemba 12, 2010 kwenye ukumbi wa EACROTANAL mjini Unguja Amran Umbaya alisimama na kushauri kwamba kwa kuongezeka magari serikali ilipaswa kuanza kufikiria mkakati wa kupunguza ajali za barabarani.

Uingereza pia akishiriki katika mikutano kadhaa iliyoandaliwa na jumuiya ya Mustakbali wa Zanzibar (MUWAZA), jumuiya ambayo imewaunganisha wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wa Civic United Front (CUF) hata kabla ya kupatikana Maridhiano huko Zanzibar.

Waliokuwa wakimjuwa Amran watamkumbuka kwa namna alivyokuwa akiwashauri wanaharakati kuhusu mbinu za kutumika kimataifa kuwapigania mashekhe wa Uamsho waliokamatwa. Alikuwa pia mshauri wa Salim Adi aliye mbele katika harakati za kuishitaki serikali kuhusu uhalali wa Muungano.

Amran Umbaya alikuwa mtu wa matumaini mema na dhana njema. Akiamini kwamba historia haifutiki, kwamba maelewano ya jadi na udugu wa Wazanzibari wenye asili mbalimbali utadumu na kusaidia kuijenga Zanzibar mpya.

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s