Profesa Lipumba avuruga Bunge

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam jana baada ya kusomewa shtaka la kuhamasisha wafuasi wa chama hicho kutenda kosa la jinai. Juu kulia- Spika wa Bunge Anne Makinda akizungumza baada ya wabunge wa upinzani (kushoto), kusimama mfululizo wakipinga kuahirishwa kwa hoja ya kujadili suala la Profesa Lipumba kukamatwa.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam jana baada ya kusomewa shtaka la kuhamasisha wafuasi wa chama hicho kutenda kosa la jinai. Juu kulia- Spika wa Bunge Anne Makinda akizungumza baada ya wabunge wa upinzani (kushoto), kusimama mfululizo wakipinga kuahirishwa kwa hoja ya kujadili suala la Profesa Lipumba kukamatwa.

Dodoma. Kwa mara ya pili, Spika Anne Makinda jana alilazimika kuahirisha kwa muda shughuli za Bunge la Jamhuri ya Muungano baada ya wabunge wa vyama vya upinzani kukataa kukaa, wakishinikiza kitendo cha polisi kumpiga na baadaye kumkamata Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kijadiliwe kwa masilahi ya Taifa.

Profesa Lipumba, ambaye pamoja na wanachama wengine 32 walikamatwa juzi eneo la Mtoni Mtongani wakati alipokuwa akielekea Zakhem, Mbagala jijini Dar es Salaam kuwataka wafuasi wa CUF kutawanyika kwa amani baada ya Jeshi la Polisi kuzuia maandamano, jana alikamatwa tena akiwa nje ya Kituo Kikuu cha Polisi muda mfupi baada ya kuachiwa kwa dhamana, akidaiwa kuongea na waandishi wa habari wakati akiwa mtuhumiwa.

Wakati akiwa mbaroni, Profesa Lipumba alijisikia vibaya na hivyo kupelekwa hospitali kabla ya kufikishwa Mahakama ya Kisutu jioni, akishtakiwa kwa kufanya maandamano bila ya kibali.

Jana bungeni, Spika Makinda alijikuta akipambana na nguvu ya wabunge wachache wa upinzani ya kuzuia kuendelea kwa shughuli za Bunge kama ilivyokuwa mwishoni mwa mwaka jana wakati walipotumia staili hiyo ya kusimama wakati wote kushinikiza Bunge kusikiliza matakwa yao kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya wahusika kwenye sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.

Wakati huo ilibidi Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Nchi, Sera na Utaratibu wa Bunge, William Lukuvi kumfuata mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe kuzungumza naye kabla ya Bunge kuahirishwa.

Tafrani ya jana iliyodumu kwa dakika 12 na sekunde 8 ilianza baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu. Baada ya kumalizika kwa kipindi hicho, wabunge zaidi ya watano wa upinzani walisimama kutaka kutoa hoja na Spika Makinda alimpa nafasi ya kwanza James Mbatia, ambaye ni mbunge wa kuteuliwa, aliyeomba mwongozo akitumia Kanuni ya 47 inayohusu kuahirishwa kwa shughuli za Bunge ili kujadili jambo la dharura.

Mbatia, ambaye aliisoma kanuni yote ya 47 yenye vipengele vinne, aliomba kutoa hoja ya kutaka kitendo cha kupigwa kwa Profesa Lipumba wakati akiwa katika mkutano wa hadhara, kijadiliwe.

Mbatia alisema: “Jana (juzi) tarehe 27 mwezi Januari mwaka huu wilayani Temeke jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CUF Profesa Lipumba alikuwa na ratiba ya kufanya mkutano wa hadhara pamoja na maandamano na walifuata taratibu zote za kisheria na za kikatiba za kujumuika, kuandamana na kuweza kubadilishana mawazo.

“Cha kushangaza, dakika za mwisho polisi walikataza jambo hilo lisiendelee na Profesa Lipumba akaonyesha ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoendelea na jambo hilo, lakini Jeshi la Polisi likafika baadaye kidogo kuamua kutumia nguvu dhidi ya raia ambao hawafanyi fujo yoyote, raia ambao wameonyesha ushirikiano na utii kwa Jeshi la Polisi.”

Mbatia alisema pamoja na ushirikiano huo polisi waliamua kumpiga Profesa Lipumba na raia wengine wa Tanzania hata watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano, kauli ambayo ilifanya wabunge wampigie makofi mwenyekiti huyo wa Chama cha NCCR-Mageuzi.

Aliendelea kusema waandishi wa habari walipigwa virungu na kudhalilishwa, jambo ambalo alisema linaondoa utulivu, amani nchini.

“Mimi binafsi nilisikitika sana baada ya vyombo vya habari kuonyesha moja kwa moja. Nilichukua hatua ya kuwasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kuwa mambo ya aina hii yalipokuwa yakitokea huko nyuma, sisi vyama vya siasa tuliwahi kumuhusisha hata Rais.”

Chanzo: Mwananchi

 

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s