Masheikh wataka maaskofu waliache Bunge lifanye kazi

Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Khamis Mataka wa kwanza kulia.
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Khamis Mataka wa kwanza kulia.

Dar es Salaam. Siku mbili baada ya Jukwaa la Wakristo Tanzania kutoa hoja zake kutaka Serikali kuondoa muswada wa sheria itakayosimamia kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu imelitaka jukwaa hilo kuacha kuingilia Bunge.

Wiki ijayo, Serikali inakusudia kuwasilisha bungeni muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali wa mwaka 2014 unaopendekeza, pamoja na mambo mengine, kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Tamko la Sheria ya Kiislamu, Sura ya 375.

Baadhi ya hoja zilizotolewa na jukwaa hilo ni pamoja na kutokuwapo kwa utaratibu wa kisheria unaoruhusu Mahakama za Kadhi na kwamba Serikali inachukua jukumu la kuanzisha taasisi za kidini kinyume cha Katiba na wasiwasi kuhusu matumizi ya fedha za umma kuendesha taasisi hizo.

Hoja nyingine ni mapendekezo yaliyopo kwenye muswada huo kuwa kimya kuhusu kesi zinazohusisha migogoro kati ya Waislamu na Wakristo na kwamba baadhi ya madhehebu na taasisi za Kiislamu hazikubaliani na mamlaka za ya Mufti.

Hata hivyo, taasisi hiyo ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu jana iliwasilisha hoja nane zinazofafanua suala hilo.

Hoja nane

Masheikh hao walisema kauli ya jukwaa hilo ni kutaka kuifanya Serikali iliyotoa ahadi kupitia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ionekane imewadanganya Waislamu ili waichukie Serikali yao… “Ikumbukwe kwamba ahadi ya marekebisho ya sheria kuitambua Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara ni ya Serikali.”

Taarifa hiyo ilitaka Bunge liachiwe uhuru na waumini wa Kikristo wa Bunge waujadili muswada huo bila ya shinikizo la kiimani la kuukataa.

“Mbinu zozote za kuwashawishi wabunge kiimani kutekeleza maazimio ya Jukwaa la Wakristo Tanzania, ni udini ambao ni hatari kwa umoja na mustakabali wa Taifa letu.”

Taarifa hiyo iliyosainiwa na katibu mkuu wa taasisi hiyo, Sheikh Hamisi Mataka ilisema; Serikali ya Tanzania ina vyombo vya uchunguzi na utafiti vyenye uwezo wa kubaini maeneo yanayovunja umoja wa kitaifa na yanayopingana na Katiba.

Ilisema hofu ya kuwapo Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara ni bandia, kwani kesi zinazohukumiwa kwa mujibu wa Sheria ya Kiislamu zinazohusiana na ndoa, talaka, mirathi, wasia, wakfu na malezi ya watoto zinapatiwa uamuzi katika Mahakama zilizopo na kwa miaka kadhaa na wala maaskofu hawajapata kudai ziondolewe kwa kuwa ni za kidini.

“Tunachoomba Waislamu ni kubadilishiwa hakimu ili aje kadhi ambaye ana taaluma na uelewa mpana wa Sheria za Kiislamu… Ni vipi kasoro ya dini ionekane baada ya kuletwa kadhi atakayezipatia hukumu za kesi hizo na isionekane sasa wakati zipo mahakamani kwa hakimu anayezikosea hukumu hizo?”

Kuhusu hoja kwamba baadhi ya taasisi za Kiislamu hazikubaliani na mamlaka ya Mufti, taarifa hiyo ilisema hayo ni mambo ya ndani ya Waislamu.

Taasisi hiyo ya Masheikh imesema itashangaa iwapo Serikali itaamua kuuondoa bungeni muswada huo kwa kisingizio cha kupingwa na baadhi ya taasisi za Kiislamu au shinikizo jingine.

Iliwataka wabunge kuzingatia viapo vyao vya kuitumikia nchi na watu wake kwa uadilifu na bila ya kuathiriwa na shinikizo la kiimani na kuwataka waupokee muswada huo na waupime kwa hoja na kutoa majibu yenye hoja na kamwe wasikubali kugawanywa kiimani.

Taasisi hiyo imesema haina pingamizi na dhamira ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju kuwafahamisha ‘wenye hofu’ na uwapo wa Mahakama ya Kadhi Tanzania Bara kuwa haina madhara yoyote kwa umoja, mshikamano na mustakabali wa Taifa.

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s