Kufukuzwa CCM kumenipa fursa nzuri ya kufanya siasa za kuikomboa Zanzibar

Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akimpongeza Mhe. Mansour Yussuf Himid baada ya kuamua kujiunga na chama hicho na kumkabidhi rasmi kadi ya CUF katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.
Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akimpongeza Mhe. Mansour Yussuf Himid baada ya kuamua kujiunga na chama hicho na kumkabidhi rasmi kadi ya CUF katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja.

Jina la Mansoor Yussuf Himid limeendelea kupata umaarufu katika siasa kisiwani Zanzibar. Mwanasiasa huyo kijana ameendelea kupata umaarufu tangu alipotofautina hadharani kimsimamo na chama chake cha awali, (CCM).

Msimamo wake ulioonekana kwenda kinyume na ule wa viongozi wenzake ndani ya chama tawala na kwa sababu hiyo, alitimuliwa CCM na kuamua kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF).

Siku chache baada ya Mansoor kutangaza nia yake ya kujiunga na CUF, alikamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kumiliki silaha kinyume na sheria. Alidaiwa pia kukutwa na risasi kinyume na sheria.

Akiwa katika maisha mapya kisiasa, Mansour amekiri kukabiliwa na changamoto chungu mzima, lakini akisisitiza kusimama imara kutimiza ndoto yake kuwatumikia wananchi.

Anasema angependa kuona watu wanaheshimu uamuzi wake wa kujiuna na CUF kwa sababu ametumia fursa yake ya uhuru wa kuchagua demokrasia ya kweli.

“Sina sababu ya kuhofu jambo lolote, uamuzi wangu wa kujiunga na CUF ulikuwa sahihi,” alisema na kuongeza:

“Nilifahamu changamoto ambazo ningeweza kukutana nazo kwa uamzi wangu kujiunga CUF. Vizingiti na vitisho havikukosa nafasi, lakini hilo kwangu halikuwa tatizo, nimebaki kwenye msimamo wangu kama mtu huru wa kuamua wapi naweza kwenda.”

Anazungumza mengi baada ya uamuzi wake huo, lakini kubwa anasisitiza kuwa kwake ni changamoto kubwa kufikia uamuzi huo wa kujiunga na CUF kwa kuzingatia kuwa yeye ni muumini wa mapinduzi ambayo amerithi kutoka kwa wazazi wake.

“Nilijua yatatokea haya yanayonikuta hivi sasa na lazima niudhihirishie ulimwengu mtu kuwa na uamuzi wake ni jambo muhimu sana na siyo dhambi kuamua unaloliona linafaa,” anasema Mansoor.

Mansoor ni nani?

Mansoor ni mtoto wa Brigedia Yussuf Himid ambaye ni miongoni mwa watu wa mstari wa mbele katika Mapinduzi ya mwaka 1964 na aliyekuwa rafiki wa karibu wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Mwanasiasa huyu kijana aliyejizolea umaarufu mkubwa katika siasa za Zanzibar, anatoka katika nyumba ya wana-mapinduzi.

Mansoor aliwahi kuwa mweka hazina wa CCM na Waziri wa Maji, Ujenzi, Nishati na Ardhi, alishika wadhifa huo kwa muda wa miaka minane katika kipindi cha utawala wa Amani Karume na kumalizikia utawala wa Dk Ali Mohamed Shein kabla ya kutenguliwa nafasi hiyo na kufukuzwa katika chama chake.

“Mimi ni mwanamapinduzi na ni muumini wa mapinduzi, lakini ndiyo hivyo nimefukuzwa nyumbani…na mtu kufukuzwa kwao ni jambo zito sana kwa sababu ninapofukuzwa kwetu niende wapi? anahoji Mansoor.

Anasema kufukuzwa CCM kumempa fursa nzuri ya kuweza kujiamulia zaidi na kuacha mkondo wa demokrasia ufanye kazi yake kwa kujiamulia, kwani alipokuwa CCM hakuwa na uamuzi kama alivyo sasa.

“Kuna changamoto zake katika kuchukua uamuzi mzito kama huu na suala la kujiamulia lile unaloliamini wewe ambalo wenzako hawaliamini, pia ni changamoto nyingine lakini lazima uzikabili changamoto kama hizo,” anaongeza Mansoor.

Akitoa sababu zilizomsukuma kujiunga na CUF, Mansoor alisema kwanza ni dhana ya maridhiano kwa vitendo inayotekelezwa ndani ya CUF na pili demokrasia na sera za kuitetea Zanzibar kupata mamlaka yake.

“Kwenye CUF, kila mmoja ana uhuru wa kuongea kwa mujibu wa maoni yake na mtazamo wake, watu wanatoa maoni yao bila ya kukemewa bila ya kushikiwa bakora, nimeona huku watu wana mawazo tofauti,” anasema na kuongeza

“Wapo wanaoutaka muungano kama ulivyo wapo wenye kuutaka muungano wa usawa pia wapo wenye kutaka mfumo wa Serikali tatu na wasioutaka Muungano kabisa, lakini kila mmoja anasema na hakuna aliyefukuzwa”.

Kwanini CCM ipo kimya?

Ali Mbarouk ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Anaelezea sababu za kukaa kimya huko kwa CCM Zanzibar.

“Siyo bure hasa ikizingatiwa kuwa utamaduni wa CCM kwa viongozi wakuu wa chama hicho ni kutoa matamko makali na kuonyesha misimamo yao binafsi na misimamo ya chama chao pale yanapotokea matukio makubwa kama hili la uamuzi wa Mansour,” anasema.

Anasema hali hiyo ya CCM kwa sasa inadhihirisha mshtuko mkubwa na fadhaa iliyokikumba chama hicho, huku akidai hiyo inatokana na nafasi ya historia ya familia ya Mansour kwa Zanzibar na Wazanzibari.

“Vyovyote iwavyo, kushindwa kwa CCM na viongozi wake wakuu kuendeleza utaratibu na utamaduni wao wa vijembe katika suala hili la Mansour ni ishara tosha kuwa pigo limewapata na kuwajeruhi ipasavyo” anasema msomi huyo.

Anaendelea kusema kuwa, kwa mazingira ya siasa za Zanzibar, uamuzi huu wa Mansour hauishii kuiathiri CCM Zanzibar pekee bali athari yake itachukua mawanda mapana zaidi na taathira zake zitajionyesha katika eneo kubwa maradufu.

“Athari hizi zinaweza kujitokeza hata kwa Mansour mwenyewe na familia yake, hasa ikizingatiwa uamuzi wake huu unaonyesha kwenda sambamba na matukio kadhaa ya familia yake ya kujaribu kurekebisha kasoro kadhaa za kihistoria zilizoshika kasi siku za hivi karibuni, hasa uzinduzi wa vitabu viwili uliyofanywa na mama mzazi wa mwanasiasa huyo hivi karibuni,” anasema.

Msomi huyo anasema Siasa za Zanzibar hazijazoea kuwa na wanasiasa na wafuasi wa aina kama ya Mansour kwa miaka kadhaa.

“Mansour ni muwazi kuelezea misimamo yake, mkweli kudhihirisha hisia zake anapoguswa moyo wake kwa kumuweka Mungu wake mbele na mtulivu na mtaratibu kuelekeza wenzake kumfahamu kile anachokiamini” anasema.

Omar Said Shaaban ni Msomi na Mwanasheria wa Zanzibar anasema Mansoor amefanya uamuzi sahihi kisiasa kwa kujua wapi anaekelea na upepo unavyokwenda katika zama hizi za demokrasia.

Anasema Mansoor ni kiongozi mwenye maono na alitaka kutimiza mtizamo wake ndani ya CCM lakini kwa bahati mbaya hakupewa nafasi hivyo uamuzi aliochukua ulitokana na kukatishwa ndoto zake. Kijana huyo licha ya kumuunga mkono kutokana na uamuzi wake wa kujiamulia kile anachokiamini lakini pia anasema bado Mansoor ana nafasi ya kutimiza ndoto zake nje ya CCM na kwa mazingira ya siasa za Zanzibar anadhani kuwa CUF ndio chagua sahihi.

Licha ya kumuunga mkono, anasema hakupaswa kujiunga na chama cha siasa kama kweli alikuwa na haja ya kuitetea Zanzibar alipaswa aache siasa

“Mansour angeingia kwenye Asasi zilizokuwa za kisereikali (NGO’S) angefanya kazi nzuri na hata wale ambao wamechoka na wana siasa wangekuwa pamoja na yeye” anasema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Zanzibar, Faiza Ali Salum yeye anasema Mansoor atapaswa kujitathmini zaidi juu ya yale aliyoyataenda wakati akiwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi na alipokuwa waziri

Alisema mtazamo wa Mansoor ni mzuri wa kujiamini na kutetea nchi, lakini jambo hilo linahitaji zaidi vitendo kuliko maneno kwa sababu wanasiasa wengi hawatekelezi yale wanayoyasema.

Kwa upande wake, Mwanaharakati wa Haki za Wanawake, Jamila Ahmed Mohammed anasema mtazamo wa Mansour hautakuwa na mustakbali mwema wa moja kwa moja katika maisha yake ya kisiasa.

“Hii inatokana na ukweli kwamba aina ya siasa zetu ni za kujikomba komba kufurahisha baadhi ya watu wenye nafasi na hautoi fursa kwa mtu kufanya kazi anasema.

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s