Uchaguzi unapokuwa marikiti ya kura

Rais Jakaya Kikwete akihutubia mkutano wa hadhara katika kampeni za uchaguzi mwaka 2010
Rais Jakaya Kikwete akihutubia mkutano wa hadhara katika kampeni za uchaguzi mwaka 2010

Na Ahmed Rajab              Toleo la 389  21 Jan 2014

KUNA dalili kwamba mwaka huu, mwaka wa uchaguzi nchini Tanzania, mbingu zitanyesha fedha. Zitavyonyesha Watanzania wataziona jinsi hizo fedha zitavyochezewa.  Hayo hayatokuwa mageni.  Tumeyasikia kabla wakati wa chaguzi zilizopita. 

Kama ilivyokuwa siku hizo safari hii pia fedha hizo watalishwa wapiga kura pamoja na wale wanaoonekana kuwa na uwezo wa kuyabadili maoni ya wapiga kura. Miongoni mwao watakuwa waandishi wa habari pamoja na watangazaji wa vipindi muhimu vya kisiasa vya redio na televisheni.  Watapewa zile zinazojulikana kama “bahasha za kaki.”

Yote hayo yatakuwa katika njama za wanasiasa za kununua kura na ni sehemu muhimu ya mikakati ya kampeni za uchaguzi. Lakini hata kabla ya kampeni hizo kuanza kwa dhati hongo zitaanza kutolewa kwanza ndani ya vyama pale wanasiasa watapokuwa wanachujana nani asimamishwe na chama chao.

Zitaendelea wakati wa kampeni za uchaguzi na hadi wakati wa uchaguzi pale wagombea wa vyama tofauti watapokuwa wanachuana kuzinyakua kura za wananchi wenye haki ya kupiga kura.

Wataozichezea fedha watakuwa ni wanasiasa wanaotaka wachaguliwe katika ngazi mbalimbali za madaraka — urais, ubunge na udiwani.

Itakuwa tunawaonea wanasiasa tukiwafanya watu waamini kwamba ni wote wataofanya hivyo. Ni mafisadi tu wataohusika. Wengi wao watakuwa ni wale walioingia katika siasa kwa minajili ya kujitajirisha.

Wanasiasa aina hiyo huwa wanazitumia siasa kuwa kama ngazi za kupandia ili wafike juu watakoweza kuyatumia madaraka watayoyapata kujineemesha.

Nchini Tanzania chama kilichofurutu ada katika mambo haya ya ununuzi wa kura na ubadhirifu wa fedha za umma katika kampeni za uchaguzi ni Chama cha Mapinduzi (CCM).  Hatukisingizii kwani hata baadhi ya viongozi wake katika nyakati mbalimbali wamekuwa wakipiga kelele wakiikemea tabia hiyo iliyo ovu na inayoitishia misingi ya kidemokrasia.

Safari moja Desemba 2013 Stephen Wasira, waziri wa nchi katika ofisi ya Rais, alinukuliwa akisema kwamba tabia hiyo ndiyo iliyosababisha uoza wa maadili na uongozi ndani ya chama chao. Wasira, anayetajwa kuwa na azma ya kugombea urais, aliwasihi wana CCM wawapuuze wale wataojaribu kununua vyeo au madaraka katika uchaguzi wa mwaka huu.  Vigogo kama John Malecela na Kingunge Ngombale-Mwiru nao pia wamejitokeza kukemea kitendo hivyo.

Kwa hakika, kwenye uchaguzi ujao vigogo wenye fedha nyingi kwenye mbio za urais wa Muungano wanatajwa na wapambe wao kuwa eti ndio vipenzi vya wengi.

Kuna na wengine waliolalamika kwamba wenye fedha wamekuwa wakizitumia fedha zao kuwahonga wenzao ili wawachague katika ngazi tofauti za uongozi chamani mwao.

Nchini Tanzania, na hususan ndani ya CCM, hata msamiati wa rushwa nao umebadilishwa kwa kusudi ili kuificha au kuihalalisha rushwa.  Siku hizi unasikia watu “wakifadhiliwa”  kwa “takrima.”  Ni sawa na neno lililokuwa likitumiwa sana zamani nchini Misri la “bakhshishi.”

Matamshi ya “hongo” na “rushwa” yamepelekwa kwa dobi na kufuliwa. Sasa mafisadi wanadhani kwa kuyageuza na kuyaita “takrima” wanaweza kutudanganya tudhanie kwamba ni safi.

Ugonjwa huu wa ununuzi wa kura si ugonjwa ulioibuka leo au jana.  Ni ugonjwa wa zamani sana. Ulianza kuonekana katika siasa za Warumi wa kale takriban karne moja kabla ya kuzaliwa Nabii Issa (Yesu Kristo.)

Ugonjwa huo haukufungika ndani ya mipaka ya nchi moja au mbili au bara moja au mawili lakini umevuka mipaka na kuambukiza kwingi. Ni ugonjwa ambao si mgeni nchini Lebanon au Taiwan au katika nchi za Amerika ya Kusini za Nicaragua na Argentina.

Barani Afrika umeambukiza kwingi hata kwenye visiwa vidogo kama vya Comoro ambako wanasiasa bila ya kuona haya wanapenda kutumia usemi wa “mkaa na mali nde mbaba” yaani mwenye mali au fedha ndiye baba.

Kenya ni kati ya nchi za Kiafrika zenye sifa mbaya ya ununuzi wa kura wakati wa kampeni za uchaguzi.  Wapiga kura ama hulishiwa fedha au hupewa vijizawadi. Na kama ilivyo hulka ya binadamu waroho huwa rahisi sana kughilibiwa hata na vijizawadi visivyo na maana.

Vijipesa na vijizawadi hutosha kuwadodeshea wapiga kura na kuwalaghai wawaunge mkono wasiostahili kuungwa mkono.  Shilingi 150 za Kenya zinatosha kumfanya mtu asiyejiweza kimaisha aache shughuli zake na badala yake ende kuhudhuria mkutano wa hadhara wa chama cha siasa kitachompa hizo KSh150.

Fedha usizozilalia au kuziamkia huwa na utamu wake hata ikiwa ni kidogo vipi.  Kadhalika kijizawadi cha kijinga huwa na mvuto wa kushangaza. Madhali mtu anakipata bure hutosha kumzuzua.

Nchi inayotajwa sana barani Afrika kwa mchezo huu wa kununua kura ni Nigeria. Huko kama mwanasiasa hana fedha au hana mzito anayemfadhili basi asahau kupigania kiti chochote kile, kiwe cha urais, ugavana, ubunge au cha baraza la senate.

Kuna mwanasiasa mmoja wa huko aliyewahi kunambia kwamba kama huna naira bilioni 4 za kuhongea basi sahau kujaribu kuwania urais. Ukiutaka ugavana uwe tayari kuzimwaga fedha za thamani ya naira bilioni moja. Ukitaka uwe mjumbe wa baraza la senate itakubidi uwe na naira akali nusu bilioni za kuwapakia watu mafuta. Na huwezi kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kama huna naira milioni laki tatu za kuhongea. (Dola moja ya Marekani ni sawa na naira 165.)  Katika mchezo huu mlishaji wengi ndiye mwenye nafasi ya kuibuka mshindi.

Mwaka 2007 taasisi moja ya kimataifa inayohusika na uchaguzi, yenye makao yake makuu Washington,  iitwayo International Foundation for Electoral Systems (IFES) ilifanya utafiti kuhusu chaguzi za Nigeria. Katika utafiti huo iligundua kwamba Wanigeria saba kati ya kumi wanaamini ya kuwa kura hununuliwa nchini humo katika chaguzi zote au katika nyingi ya chaguzi za huko.

Yote hayo yanatendeka ndani ya nchi inayosema kwamba inafuata mfumo wa kidemokrasia.  Kwa hakika, chaguzi zenyewe nchini humo, kama zilivyo Tanzania, zinafanywa chini ya mfumo wa kidemokrasia.

Mfumo wa aina ni ule unaowaruhusu wananchi wawe wanashiriki katika harakati za kisiasa nchini mwao na wakati huohuo kuwafanya wananchi hao wawe wanawakilishwa na watu waliowachagua.

Uwakilishi huo unaweza kuwa katika mabaraza ya kutunga sheria, kwa mfano bunge, baraza la senate au mabaraza ya miji. Ilimradi popote pale panapokuwa panafanywa maamuzi yenye kuyaathiri maisha ya wananchi basi wananchi hao wawe na wawakilishi wao katika vyombo hivyo.

Kwa jumla, hao wawakilishi wa wananchi wanatakiwa wawe wanayapigania maslahi ya wanaowawakilisha, yaani wananchi waliopiga kura kuwachagua.

Katika demokrasia ya uwakilishi tuliyo nayo siku hizi vyama vya siasa ndivyo vinavyotumika kuwafanya wananchi washiriki katika harakati za kisiasa. Na vyama hivyo hivyo vya siasa ndivyo vinavyotumika kuwawakilisha wananchi kwani watetezi wa vyama hivyo ndio wanaosimama katika uchaguzi kuwataka wananchi wawachague.

Jambo la kushangaza ni kwamba ingawa chaguzi katika mfumo wa kidemokrasia huwa ni wa siri na hakuna ajuaye mtu anampigia kura nani hata hivyo wanasiasa bado wanawahonga wapiga kura wawapigie kura.  Si hasha kwa mpiga kura, kwa sababu ya umasikini au uroho wake, akakubali “anunuliwe” na vyama tofauti vya siasa na halafu akipigie kura anachokitaka yeye.

Hufanya hivyo akijuwa kwamba kwa vile kura yake ni ya siri hakuna atayeng’amua amekipigia kura chama gani. Lakini hilo linahitaji mwamko wa mpiga kura mwenyewe.

Ununuzi wa kura ni kitendo kisicho halali.  Hili ni jambo lililo wazi na linalopaswa kusisitizwa kila mara na wenye wajibu wa kuhakikisha kwamba uchaguzi ujao utaendeshwa kwa njia za halali bila ya mizengwe ya aina yote.

Hapa siwakusudii wajumbe wa Tume ya Uchaguzi peke yao bali hata na waangalizi wa jumuiya mbalimbali za Afrika ambao mara nyingi hukurukupa na kuelemea upande wa vyama vinavyotawala ikitegemea mrengo wao wa kisiasa.

Kitu kimoja kinachoweza kufanywa ni kuimarisha elimu watayopewa wapiga kura.  Kuwaelimisha wapiga kura kuhusu majukumu yao na upigaji kura wa haki kutaweza kupunguza kwa kiwango kikubwa athari za ununuzi wa kura katika matokeo ya uchaguzi.

Kuna jambo moja ambalo wapiga kura wanapaswa kufahamishwa hata kama watapokea zawadi au watazila fedha zitazomwagwa na wagombea uchaguzi au na vyama vya siasa.  Lazima wafahamishwe kwamba ni wajibu wao kupiga kura kwa kuzingatia hekima na maslahi ya taifa.

Haya yameonekana Zambia na Malawi ambako kumekuweko na maamuzi yaliyosababisha vyama kuingia na kutolewa madarakani kwa kura.

Katika nchi zetu changa matokeo ya uchaguzi hayaamuliwi na mashindano baina ya vyama vya siasa pekee. Ulimwengu wetu una mengi yaliyo ya ajabu kama hili la ununuzi wa kura.  Moja ya sababu za kuzuka kwa maajabu hayo ni udhaifu wa mchakato wa kidemokrasia katika nchi zetu.

Ununuzi wa kura sio tatizo pekee linalozichafua chaguzi zetu.  Kuna na mengine kama kutokua na tume huru ya uchaguzi, wizi wa kura na utumizi wa nguvu wakati wa upigaji kura au baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.  Haya ni mambo ambayo lazima yapigwe sana darubini katika uchaguzi mkuu ujao Tanzania.

Kuna wanaohoji kwamba ununuzi wa kura una faida yake. Kwamba unawashajiisha watu wazidi kushiriki katika uchaguzi.  Hoja hiyo, hata kama ina nguvu, haina uadilifu na inatupasa tuitupilie mbali jaani.

Kwa jumla, tukiyapima haya na yale tutaona tu kwamba ununuzi wa kura una madhara tu, tena makubwa, kwa demokrasia na utawala bora.  Hapawezi kuwapo uwajibikaji katika uchaguzi iwapo wapigaji kura watakuwa wananunuliwa na wagombea uchaguzi au na vyama vya siasa na wakiugeuza uchaguzi uwe marikiti ya kura.

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s