Makuukuu ya tai si mapya ya kengewa

ZimbabweNa Ahmed Rajab                            Toleo la 388  14 Jan 2014

TANZANIA na Zimbabwe si nchi zenye kufanana sana isipokuwa labda kwa moja au mawili.  La kwanza ni kwamba zote zimekabwa na chama kimoja kilicho madarakani tangu uhuru wa nchi hizo.

La pili ni kuwa mwaka nenda mwaka rudi hali za wananchi wao zimeselelea palepale kama hazikudidimia zaidi.  Viongozi wao wameshika uzi uleule wa kupora mali ya taifa au kujitajirisha kwa njia za kifisadi. Na vigogo wa vyama vyao vinavyotawala wamezoea kupikiana majungu.

Kuna kuzidiana na nadhani kwa wakati huu ya Zimbabwe yameyapiku kidogo ya Tanzania.

ZANU-PF, chama kilichopigania ukombozi wa  Zimbabwe, hii leo kimegeuka pango lenye  kuwaficha baadhi ya mafisadi wakubwa wa taifa hilo.  Ni chama chenye utamaduni wa hofu, kilichogawika mapande mapande na chenye viongozi wasioona haya kuadhiriana hadharani.

Mwishoni mwa 2014 tulishuhudia jinsi mke wa Rais Robert Mugabe, Grace, alivyoibuka ghafla na kuwa kiongozi wa Umoja wa Wanawake wa ZANU-PF.  Huo ushindi wake ulikuwa sehemu ya mkakati wake dhidi ya aliyekuwa Makamu wa Rais Joice Mujuru, kizuka wa aliyekuwa mkuu wa majeshi Jenerali Solomon Mujuru.

Lengo lilikuwa ni kumg’oa kwenye madaraka Mujuru aliyekuwa makamu wa Mugabe kwa miaka10 na aliyekuwa akidhaniwa na wengi kwamba atakuwa Rais wa mwanzo wa kike wa Zimbabwe atapofariki ama atapojiuzulu Mugabe, atayetimia miaka 91 mwezi ujao.

Grace alihakikisha kwamba Mujuru hatolifikia lengo hilo. Mujuru alifukuzwa kazi Desemba iliyopita kwa uchochezi wake Grace.  Kabla Mugabe hajamfukuza,  Grace alitishia kwamba atamshughulikia Mujuru yeye mwenyewe iwapo Mugabe hatomchukulia hatua.

Habari hizo zilizidi kuthibitisha kwamba Mugabe anamsikiliza sana mkewe katika mambo ya utawala. Imekuwa Mugabe anaiendesha Zimbabwe na mkewe anamwendesha yeye.

Grace alimuandama Mujuru akishirikiana na Emmerson Mnangagwa, aliyekuwa waziri wa sheria.  Kwa hivyo, kama ilivyotarajiwa baada ya Mujuru kuanguka Mnangagwa ndiye aliyeteuliwa kushika nyadhifa zake zote katika chama na serikali.  Bakhshishi kubwa aliyopewa ni ya umakamu wa Rais.

Watu wakifikiri kwamba baada ya kupikiwa jungu Mujuru mambo yataishia hapo.  Wakifikiri kwamba Grace alizicheza karata zake vizuri na ataridhika kuwa hasimu yake hayuko tena madarakani.

Wadadisi wakihisi kwamba Mnangagwa naye amefurahi kuwa amepiga hatua kubwa ya kuelekea kumrithi Mugabe.  Pakaanza uvumi kuwa Mnangagwa akiwa Rais atamteua Grace awe Makamu wake.

Kumbe mambo hayakwisha. Majungu yanaendelea kupikwa.  Waliokuwa juzi wakilikoroga jungu pamoja dhidi ya Mujuru na walio katika kambi yake sasa wanapikiana majungu wenyewe kwa wenyewe.

Kundi la akina Mnangagwa halina tena umoja; limekwishaanza kumomonyoka.  Mapande hayo mawili yanapigania ngawira za kisiasa, vyeo katika chama na serikali.

Mnangagwa na wafuasi wake ndio wanaopigwa vita na kikundi cha watu wanne kinachoitwa “Genge la wanne.”  Wote ni wajumbe wa Kamati Kuu ya ZANU-PF. Nao ni waziri wa habari Jonathan Moyo, Savior Kasukuwere, Patrick Zhuwao ambaye ni mpwa wa Mugabe na Oppah Muchinguri.

Hawa wenye kumpinga Mnangagwa wanasema kwamba hafai na hastahiki kuwa Makamu wa Rais. Wala asithubutu kusema kuwa atakuwa Rais kwa sababu mtu akiwa Makamu wa Rais haina maana ya kuwa ni lazima aurithi urais pale Mugabe atapofariki au atapostaafu. Mugabe mwenyewe anasema hauachi urais; atauacha atapotokwa na akili tu.

Wengine wanaoshambuliwa ni Phelekezela Mphoko, aliyeteuliwa Makamu wa Rais wa pili pamoja na waziri wa usafiri Obert Mpofu ambaye pia ni Katibu wa Fedha wa ZANU-PF.  Januari 2 mwaka huu watu wasiojulikana walivunja ofisi zake Harare wakijaribu kuingia ndani.

Siku kadhaa kabla kuna watu wasiojulikana waliojaribu mara mbili kuvunja na kuingia katika ofisi za Mnangagwa.  Mwezi Desemba unga wa sumu kali ya aina ya sianidi (cyanide) ulinyunyizwa juu ya meza ya Mnangagwa ofisini mwake.  Mugabe alidai kwamba hilo lilikuwa jaribio la kumuua Mnangagwa.

Mugabe akamshutumu Joice Mujuru kuwa anafanya uchawi na anakula njama za kutaka kumuua yeye Mugabe. Hata mkewe Grace Mugabe naye alimshutumu Mujuru kuwa anataka kumuua.

Tunasikia kwamba katika mkutano mmoja wa Kamati Kuu ya ZANU-PF uliofanywa kabla ya mkutano mkuu uliomng’oa Mujuru madarakani waziri wa habari Moyo na waziri wa usafiri Mpofu walipambana wakishambuliana vidole machoni.  Moyo alimtukana Mpofu kwa kumwambia kwamba akili zake ni kama za panya.

Usicheke kwa sababu haya si mambo ya dhihaka. Si masihara ya barazani. Ni vita vya kufa na kupona.

Mpofu ni pandikizi la jitu lakini Moyo alipoanza kubwabwaja na kumvurumishia matusi alinyweya kama kuku aliyepigwa na mvua.  Siku hiyo Mugabe alimuunga mkono Moyo na si Mpofu mwenye tabia ya kumaliza barua rasmi anazomwandikia Mugabe kwa kuandika “Mwanao aliye mtiifu sana kwako.”

Mpofu, aliyetoka kwenye familia ya wanyonge, si kigogo tu ndani ya ZANU-PF.  Ni tajiri mkubwa pia nchini mwenye kumiliki mengi.  Kampuni zake kubwa ni nne, zikiwa kampuni saba pamoja na benki moja. Lakini anasemekana kuhusika na kampuni nyingine zisizopungua 15. Moja inawakodisha helikopta waheshimiwa na wenye kujiweza. Nyingine ni za usafiri, za kuuza magari, boti za kusafiria au kustarehea katika Mto Zambezi, mikahawa, hoteli na duka kubwa la kuuza nyama.

Ana majumba saba anayoyapangisha katika miji mbalimbali ya Zimbabwe. Utajiri wake ulizidi kukua baada ya kuteuliwa waziri wa madini 2009 na hasa tangu alipoanza kuidhinisha leseni za uchimbaji dhahabu na almasi.

Si ajabu basi kuona kwamba siku hizi anamiliki mashamba makubwa saba.  Wala si ajabu kwamba yeye ni miongoni mwa mawaziri wa ZANU-PF walionunua mashamba makubwa yaliyokuwa zamani mali ya wazungu na yaliyotaifishwa na serikali.

Kadhalika ana haki ya eneo kubwa la ardhi alilolipata bure.  Mawaziri na vigogo wengine wa ZANU-PF wamekuwa wakipeana na kugawana wenyewe kwa wenyewe ardhi na mashamba yaliyo milki ya serikali.

Isitoshe Mpofu ana ng’ombe wapatao elfu nne. Inasemekana kwamba kila wiki anauza ng’ombe 500 na faida anayoipata si ndogo. Ni nadra sana kutomuona kila panapopigwa mnada wa ng’ombe .

Kuzishughulikia biashara na kampuni zote hizo si kazi ndogo.  Ndipo tunapojiuliza anaupata wapi wakati wa kuutumikia umma?

Anapokuwa hazishughulikii biashara zake Mpofu anakuwa anajijenga kwa majenerali fulani wa kijeshi hususan wale wenye kuudhibiti utajiri wa eneo la Marange lenye machimbo ya almasi na walio katika kambi moja na Mnangagwa ndani ya chama chao cha ZANU-PF.

Wananchi wa Zimbabwe hupenda kuitaja neema ya ghafla iliyomwangukia Mpofu. Kuna wenye kushangaa kwa namna alivyojinyakula utajiri alio nao. Kuna wenye kuuliza iwapo ameupata utajiri huo kwa njia za halali.  Na kuna wenye kuuliza kuwa iwapo haijulikani ameipataje neema yote hiyo kwa nini hapachukuliwi hatua za kuhakikisha kwamba  ameipata neema hiyo kwa njia zilizo halali?

Na si yeye tu; wanasema vigogo wengine wa ZANU-PF nao pia wanastahiki kuchunguzwa. Usemi ulioko Zimbabwe ni kwamba vigogo wa chama hicho huwinda kwa vikundi na hula nyama kwa vikundi.

Utajiri wa Mpofu ni ishara ya jinsi mali ghafi ya Zimbabwe zinavyofisidiwa.  Ni ishara ya jinsi uroho na ufisadi ulivyokivaa chama hicho na jinsi ufisadi huo ulivyowagubika gubi viongozi wake.

Umoja wao na kulindana kwao ndiko kunakowapa nguvu; nguvu za kupora mali ya taifa. Lakini juu ya umoja walio nao viongozi hao hawaaminiani hata chembe.  Na ndio maana mara kwa mara hupikiana majungu.

Ikiwa tabia ya mawaziri wa Zimbabwe ni mithili ya mawaziri wa kwetu wenye kuzidi kujihusisha na biashara basi kuna haja ya kubadili namna mawaziri wetu wanavyoteuliwa.

Badala ya kumwachia Rais kuwa na dhamana ya kuteua mawaziri wa serikali labda kazi hiyo ikabidhiwe Bunge. Ndilo liwe na dhamana ya kuwateua mawaziri. Rais awe anawasimamia tu.

Mfumo wa aina hiyo utaondosha ile dhana ya kwamba mawaziri ni “wa Rais”.  Hawatokuwa tena “mawaziri wake”; watakuwa ni mawaziri wa umma kwani watakuwa wanateuliwa na wabunge, wawakilishi wa umma.

Nadhani bunge likiachiwa liteue mawaziri basi wataoteuliwa hawatojihisi kwamba wamefadhiliwa na Rais.

Kuna wasemao kwa masikitiko kwamba mna tai ndani ya ZANU-PF wenye nia ya kukiangamiza chama hicho kwa ndani. Hizi ni shutuma nzito. Kama tujuavyo tai hawana junaa ya kula mizoga. Hiyo ndiyo tabia yao na hicho ndicho chakula chao.

Kati ya wanaoshutumu kwamba mna tai wanaokichimba chama cha ZANU-PF ni Rugare Gumbo, msemaji rasmi wa zamani wa chama hicho, aliyefukuzwa Desemba kwa vile heshi kumkosoa Mugabe.

Huu mtindo wa kuwatia adabu wanachama wa ZANU-PF na hata wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwafukuza chamani ni mtindo mbaya. Ni mtindo wenye kupanda mbegu za ajabu. Kuna siku vyama hivyo vitavuna huzuni.

Waswahili tuna methali moja isemayo: “Makuukuu ya tai si mapya ya kengewa.” Siri za tai si ngeni kwa kipanga. Matendo  ya mtu na hata vitimbi vyake hujulikana na yule aliye karibu naye. Gumbo alikuwa karibu na wengi ndani ya ZANU-PF. Na anayajuwa mengi kama Mansour Yusuf Himidi ayajuavyo ya ndani ya CCM.

Baruapepe: ahmed@ahmedrajab.com

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s