CUF: Ahadi ya JK ‘changa la macho’

Maalim Seif akihutubia wananchi wakazi wa Tandale, manispaa ya kinondoni
Maalim Seif akihutubia wananchi wakazi wa Tandale, manispaa ya kinondoni

Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimekosoa ahadi ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuanza kutoa elimu bure nchi nzima kuwa ni propaganda za kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Katika waraka uliotumwa kwa vyombo vya habari na Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Abdual Kambaya unaeleza kuwa haiwezekani Rais atoe ahadi ambayo haijajadiliwa na kupitishwa na chama chake kama sehemu ya malengo yatakayotekelezwa.

“Kitendo cha CCM kutangaza kufuta ada ya elimu ya msingi na sekondari ni changa la macho kwa Watanzania. Hii siyo mara ya kwanza kwa CCM kutoa ahadi ya elimu bure.

Alifafanua kuwa michango iliyoshindwa kuondolewa imeendelea kuwapo hadi leo bila ya dalili yoyote ya utekelezaji. Alisema licha ya kushindwa kufuta ada, michango inayoendelea kutozwa ni mingi na inazidi kwa kiasi kikubwa ada inayotozwa.

Rais Kikwete alitoa ahadi hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita mbele ya mabalozi wa nchi mbalimbali katika karamu aliyoindaa Ikulu kwa ajili ya kuukaribisha mwaka 2015, huku Rais wa Zanzibar, Dk Mohammed Shein naye akitangaza mpango huo wakati wa sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar.

Rais Kikwete alisema hatua hiyo inakuja baada ya Serikali kukamilisha Sera ya Elimu na Ufundi ili kuboresha sekta hiyo ambayo imepitishwa na Baraza la Mawaziri katika mkakati wa kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu kwa gharama itakayobebwa na Serikali.

Chama tawala kimetangaza azma hiyo ikiwa ni miaka 10 baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kubainisha kuwa hiyo ni moja ya mikakati yao ifikapo mwaka huu kama wangechaguliwa kuongoza dola.

“Bado kuna michango mbalimbali kama vile ya taaaluma, rim za karatasi, ulinzi, madawati, tahadhari, mtihani, mafunzo ya ziada, vitabu na nyingine nyingi. Ukijumlisha michango yote inazidi laki nne na bado pamoja na hali hii Serikali ya CCM inaibuka na kusema elimu itakuwa bure wakati utekelezaji wa kufuta michango hiyo shuleni bado ni kizungumkuti,” alisema Kambaya.

Chama hicho kimesema kilitegemea suala la elimu bure lingejadiliwa na kuwekwa kwenye maadhimio yaliyojadiliwa na kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichohitimishwa mjini Unguja jana ili kuonyesha kuwa ni huo mkakati wa kichama.

Chanzo: Mwananchi

Wakati huo huo; Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka viongozi wa Serikali za mitaa kutoka chama hicho waoneshe mfano kwa uongozi bora katika kuwatumikia wananchi na kukitangaza vyema chama hicho.

Maalim Seif alisema hayo leo wakati alipokuwa akizungumza na viongozi wa Serikali za mitaa kutoka CUF walioshinda katika uchaguzi wa mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika mwezi uliopita huko Makao Makuu ya CUF Buguruni.

Alisema wakati wa kampeni za uchaguzi wagombea wote walijinadi kwa wananchi na walitoa ahadi mbali mbali, hivyo ni jukumu lao kuzitekeleza kwa ufanisi mkubwa.

“Waheshimiwa viongozi uongozi ni dhamana msije mkawasahau wananchi waliokuchagueni, muwe wabunifu na muepuke ubinafsi kwa kujali matumbo yenu”, alionya Maalim Seif.

Wananchi wakimsikiliza Maalim Seif Sharif Hamad, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara Tandale, Manispaa ya Kinondoni
Wananchi wakimsikiliza Maalim Seif Sharif Hamad, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara Tandale, Manispaa ya Kinondoni

Mapema akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Tandale Kwatumbo kwa ajili ya kuwashukuru wana CUF na wananchi, Maalim Seif alisema ni dhahiri matokeo mazuri ya wapinzani yalitokana na uamuzi wa vyama vinne vinavyounda umoja wa Katiba ya Wananchi UKAWA kuunganisha nguvu.

Alisema katika uchaguzi huo CUF pamoja na vyama vinavyounda UKAWA vilisimama imara kuhakikisha wananchi wenye sifa za kuwa wapiga kura katika maeneo ndio wanaopiga kura na walioshinda ndio wanaotangazwa.

“Suala la kuendelea na UKAWA halina mjadala, kama kweli tunataka tukishinde CCM katika uchaguzi mkuu ujao mwezi Oktoba”, alisema Maalim Seif.

Katika uchaguzi huo wa Serikali za mitaa uliofanyika mwezi uliopita katika Kata ya Tandale, CUF kilishinda mitaa mitatu kati ya sita, ambapo mtaa mmoja hadi sasa matokeo yake yamekumbwa na utata.

Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Kwatumbo, Mohammed Kassim alisema ushindi huo unatokana na umakini wa wana CUF kuhakikisha wanalina ushindi wao.

Hata hivyo aliwataka wanachama wa CUF na wananchi wa Tandale wasitosheke na wasijisahau kwa ushindi huo, lakini wahakikishe wanajiimarisha zaidi na kuhakikisha wote wanajiandikisha katika daftari la kura, ili washiriki katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba.

Katika uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika mwezi uliopita CUF kilipata viti 19 katika Wilaya ya Ilala, viti 34 Temeke na viti 20 Kinondoni.

Chanzo: OMKR

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s