Wazanzibari mpo? Mnaletewa Lazaro Nyalandu

Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni mbunge wa Singida Kaskazini, Mh. Lazaro Nyalandu
Waziri wa Maliasili na Utalii ambaye pia ni mbunge wa Singida Kaskazini, Mh. Lazaro Nyalandu

Na Jabir Idrissa

UNAPOSIKIA majina ya wanasiasa wanaotaka urais wa jamhuri yetu, inashtua sana. Japo wengine wapo kweli maana labda wanazo sifa ikiwemo uwezo, wengine wanatania.

Ila, usije ukashangaa hata mende akaja kupitishwa. Itakumbukwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) imewahi kuita wananchi wapigie kura mgombea wake hata kama ni jiwe.

Ni kwa msingi huohuo, nataka kusihi mapema wapiga kura wa Zanzibar, wayatie akilini haya majina wanayoyasikia. Wakiletewa wasiostahili wasijepata uzito kuwatosa.

Katika makada wake waliotangaza nia ya kuomba ridhaa ya chama ya kuteuliwa kugombea urais Oktoba mwaka huu, yumo Lazaro Nyalandu, Mbunge wa Singida Kaskazini.

Huyu anajijuwa alivyojaa mawaa kiasi kwamba siamini kama kweli anautaka urais. Lakini sidharau, maana CCM hawatabiriki. Walivyozoea kutenda makosa, hasa kwa kigezo cha uadilifu, wanaweza kumteua.

Kabla sijaeleza ninayoyajua kwa uhakika hasa kumhusu Nyalandu, niseme wazi Rais Jakaya Kikwete anamjua vema Nyalandu. Alimpandisha uwaziri mapema 2014.

Alifanya hivyo baada ya Balozi Khamis Kagasheki kujiuzulu uwaziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii tarehe 28 Disemba 2013.

Kagasheki alitumia nguzo ya uwajibikaji kutokana na sokomoko lililotokea kwenye Operesheni Tokomeza Ujangili iliyovurugwa na waovu ili kutoa mwanya waendelee kunufaika na ujangili.

Wakati wa operesheni, Nyalandu alikuwa naibu waziri; na kiongozi kipenzi cha watendaji waliokuwa na jukumu la kulinda wanyama lakini ujangili ukishamiri waliko.

Nyalandu alitoa matamshi makali kupinga ripoti ya ufuatiliaji madhara ya operesheni ile ilipokuwa ikisomwa bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili, James Lembeli.

Alishutumu kuwa wajumbe walihongwa kuandaa ripoti ya uongo. Alipoteuliwa waziri kamili, alichekelea. Alijua amesogezwa kuchuma kwa upana.

Tatizo hapa, mwenyewe anasema wazi, kwa rais ni kama nyumbani kwao. Anafika Ikulu muda atakao, anapata kile atakacho na anajulikana anavyofurahia ushirikiano mzuri anaopewa. Walio karibu nae wanayaeleza hadharani.

Utaamini tu maana anasifika kwa maneno matamu ambayo sasa yamelegeza umakini katika ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi, ofisi muhimu katika kujenga taswira ya Ikulu.

Iwapo utendaji wa ofisi hii wa kiwango, Ikulu na Rais mwenyewe, hasa kama ni msikivu kweli, hupata sifa ya uzuri. Kinyume chake, ofisi itaonekana ovyo vilevile.

Rais Kikwete anajua kama hakumkataza waziri huyu, Tanzania ingeingizwa katika mtego wa kugharamia wanajeshi wastaafu wa Marekani, ambao alitaka waalikwe kuja kushiriki “mapambano dhidi ya ujangili.”

Kwa msimamo wa Nyalandu, aliona vikosi vyote vya majeshi vilivyopo chini ya Rais Kikwete havitoshi kudhibiti ujangili. Hapo ameonesha hana imani na askari wa wanyamapori tulionao.

Waziri Nyalandu alimuamuru Herman Kyeraryo, alipokuwa Kaimu Mkurugenzi wa Wanyamapori (ADW) awaalike wanajeshi hao. Kwa kuamini atavuka mipaka na kujipalia makaa, Keraryo alikataa.

Ndipo waziri alipomwambia rais walipokuwa ziarani Marekani katikati ya mwaka jana. Rais akamjibu, “wacha mambo yasiyokuhusu. Habari ya wanajeshi achana nayo… wanakuambia unauza nchi”

Rais anajua wazi Nyalandu amezusha mgogoro katika Wizara. Amevutana na watendaji akiwemo Maimuna Tarishi, aliyekuwa Katibu Mkuu kabla ya kuhamishwa, katika mabadiliko ya hivi karibuni.

Inajulikana Waziri Nyalandu amefurahia. Alitaka zamani kuondokana na Mama Tarishi, anayetajwa kama mtendaji makini anayetii sana sheria. Kwa Nyalandu alionekana kikwazo.

Lipo jingine. Rais hakosi kujua kwamba ni Nyalandu aliyemfikisha kuzorotesha uhusiano wa Tanzania na Mamlaka ya Imarati – United Arab Emirates (UAE) – ambayo kiongozi wake muhimu alizuiwa kuingia nchini Julai 2014, kuja kufanya uwindaji wa kitalii.

Suala hilo lilifikia hapo kwa fitna za kutengeneza: eti eneo ambalo kiongozi huyo wa Imarati angewinda, lilikuwa na mgogoro ulioko mahakamani na limezuiwa na Bunge la Tanzania kwa uchunguzi. Uongo uliopitiliza mpaka.

Wakati huo, Waziri Nyalandu alikuwa anakamilisha utaratibu wa kuzuia leseni za vitalu ambazo serikali iliwapa kampuni ya Green Miles Safari (GMS) ambayo mmoja wa wamiliki wake ni raia wa Imarati.

Mbia mwenzake ni Abdallah Awadh, Mtanzania mzaliwa wa Iringa, aliyepata ufadhili wa UAE wa zaidi ya Dola 10 Milioni za Marekani kuwekeza katika sekta hii.

Vyombo vya usalama ambavyo humjulisha kila wakati Rais mambo ya nchi yakiwemo ya viongozi wake, wa karibu na mbali, vinamjua Nyalandu.

Vinajua nyendo zake katika mtandao unaofanikisha wanyamapori walio hatarini kutoweka wauliwe na vipusa kukusanywa.

Wasimjue vipi wakati ipo ripoti ya uchunguzi iliyombaini? Jamaa wanajua watu wanaotumika kufanikisha ujangili, simu wanazotumia, vituo vya kukusanyia pembe za faru na meno ya tembo. Wanajua hadi wanaomiliki silaha isivyo.

Sasa katika kuzidi kujiachia kwa wawekezaji Wamarekani, akasaidiwa ndege ndogo. Akajinasibu anasimamia vita vya ujangili; kumbe ndege yenyewe ni mbovu. Kwa miaka mitatu ilikuwa imelala Uwanja wa Kimataifa wa Dar es Salaam.

Warushaji walikataa kuirusha wakihofia gharika. Akashinikiza. Lahaula. Iliporushwa, ikaanguka puu; ikaua rubani pamoja na askari wa serikali.

Nani hajui namna Nyalandu anavyowasaidia wawekezaji wa kigeni kutoka Marekani waliowekeza katika sekta ya uwindaji wa kitalii kuvuruga wawekezaji wengine?

Nani hajui ni huyu anayesikiliza na kutii matakwa ya matajiri na mawakala wao wanaotaka waachiwe kuua wanyama kwa muda mrefu zaidi kuliko inavyoshauriwa na wataalamu?

Wala si kwamba hajui mantiki ya serikali kupitia Balozi Kagasheki, kurekebisha mwaka 2012, udhaifu uliotokea kutokana na Kanuni ya Hifadhi ya Wanyamapori ya 2010, iliyoweka muda wa uwindaji wa miezi tisa.

Tarehe 30 Desemba, Nyalandu akageuka jiwe kwa kusaini marekebisho mapya ikiwa ni hatua mbaya inayoridhia matakwa ya wadau aliokutana nao Arusha na kumshawishi kuongeza muda wa uwindaji.

Alipoingia ofisini, aliamrisha wasaidizi wake waandae Tangazo la Serikali (GN) ili kufurahisha marafiki zake wanaohangaika kila wakati kutafuta mianya ya kuvuna hazina ya taifa hata kwa hila.

Nyalandu anaidhinisha uwindaji uanze Machi hadi Disemba, badala ya Julai hadi Disemba kama alivyoacha Balozi Kagasheki ambaye alifanya hivyo kwa kufuata ripoti ya utafiti ya Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori nchini (TAWIRI).

Wataalamu wanasema wanyama wanahitaji muda wa kuzaana na kukua kabla ya kuwindwa. Kuingilia mfumo wao wa maisha, ni sawa na kuruhusu waangamizwe.

Hajawa mlinzi wa wanyamapori, maana askari katika kikosi cha kudhibiti ujangili, wasingemlilia Profesa Alexander Songorwa alipoondolewa Aprili 2014 na Nyalandu kuwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Huzuni zao zilitokana na kujisikia vibaya kwani wiki kadhaa kabla, walikula, kulala na kulinda pamoja na profesa huyo, akijifunza mazingira ya kazi ya ulinzi maporini katika kukabiliana na majangili.

Walinzi hao kwa siku tatu walilala doria na Prof. Songorwa alipofanya ziara maporini. Alichochea ari, nguvu na kasi mpya katika kulinda wanyama, waleta uchumi.

Tanganyika wanamjua Nyalandu. Jimboni kwake wanamjua sana alivyowaangusha huku akishibisha kundi lake. Ninaweka akiba kwenu Wazanzibari msisahau, sawasawa?

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s