Mambo, vijambo na majambo ya 2015

Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete akiongoza kikao cha kamiti kuu ya CCM, kisiwani Zanzibar hii leo. Pembeni yake ni Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein
Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete akiongoza kikao cha kamati kuu ya CCM, kisiwani Zanzibar hii leo. Pembeni yake ni Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein. Picha: Othman Mapara

Na Ahmed Rajab

MWAKA uliopita ndo umepita ingawa nchini Tanzania si yote ya mwaka uliomalizika yaliyomalizika.  Mwaka mpya nao umeshaingia na yake mapya. 2015 umeingia kwa mguu wa shari. Tumewashuhudia polisi wakiwatia nguvuni vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) waliotembea kwa amani kilomita 1,200 kutoka mkoa wa Geita kwenda Ikulu, Dar es Salaam. 

Vijana hao wanadai ifufuliwe serikali ya Tanganyika.  Baadhi ya vijana wengine waliokwenda kuwachukulia dhamana wenzao nao walitiwa mbaroni.

Tukio jengine la kushtusha lilitokea Ijumaa usiku pale genge la majambazi lilipozivamia sehemu kadhaa za Dar es Salaam. Majambazi hao wajiitao “Panya Road” na “watoto wa mbwa” ni hatari. Kwa muda mfupi walisambaa maeneo mbalimbali ya jiji hilo wakiwa na marungu, mapanga, visu na bisibisi.

Kusudio lao lilikuwa ni kuwashambulia watu na kuwapora walichokuwa nacho. Walifanikiwa kuwafanya wakazi wa Dar es Salaam waingiwe na kiwewe na kuwa katika mtafaruku mkubwa. Baadhi yao walikimbilia polisi kutaka hifadhi.

Haya ni mageni Tanzania. Viroja kama hivi aghalabu huvisikia nchi za mbali kwa mfano Mexico kwenye magenge kama yale ya Mara Salvatrucha (MS13) na Bario 18 au Colombia.

Majambo haya yanatisha hasa katika mwaka kama huu wa uchaguzi ambapo wanasiasa wasio na maadili wanaweza wakayatumia magenge ya wahalifu dhidi ya wapinzani wao au dhidi ya wafuasi wa wapinzani wao.

Yanayojiri nchini kutoka kumalizika kwa mwaka jana na kuingia mwaka huu ni mwendelezo wa yale yaliyotokea kabla.  Ni matukio ambayo bado hayakuhitimika au kukamilika.

Jambo moja lakini haliepukiki. Tukitaka tusitake mwaka huu mpya umeingia na changamoto zake zikiwa pamoja na ulizozibeba kutoka 2014.  Lakini unatupatia pia fursa mpya za kukabiliana na changamoto hizo.

Lazima tujiandae kwa yote.  Tujiandae kuzikabili changamoto hizo na tujiandae kuzitumia fursa zilizopo.  Hizi ni fursa zitazotuwezesha kukabiliana na masaibu ya maisha.

Masaibu ninayoyakusudia ni yale yenye kusababishwa na utawala mbovu. Masaibu haya hufinyangwa na wanadamu waliokula yamini kututumikia na kuyafanya maisha yetu yawe bora. Lakini badala ya kuyatekeleza hayo wametutumbukiza katika shimo la nakama na wenyewe wakiwa hata mshipa hauwapigi.

Mwaka huu Tanzania imekabiliwa na changamoto nyingi.  Akthari zao si mpya. Zilianzia tangu mwaka jana na hata kabla ya hapo. Kubwa kupita yote ni hitimisho la mchakato wa kulipatia taifa Katiba mpya.

Hitimisho hilo litakuwa katika umbo la kura ya maoni itayopigwa kuwauliza wananchi iwapo wanaikubali  au wanaikataa Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba. Hiyo ni fursa adhimu watayokuwa nayo wananchi.

Vyama vya siasa navyo mwaka huu vitakabiliwa na changamoto ambazo havikuwahi kuzikabili. Na ni vyama vyote kutoka kinachotawala hadi vya upinzani.  Huu ni mwaka wao. Ama vitaimarika au vitaanza kumomonyoka na kuyoyoma.

Kwa upande wa Chama cha Mapinduzi (CCM) huu ni mwaka wa mitihani mingi.  Ni mwaka ambapo chama hicho kitavuna kilichokipanda.  Mavuno hayo tutayaona wakati wa kura ya maoni kuhusu Katiba na wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanywa Oktoba.

Juu ya kura ya maoni CCM ina kazi kubwa kuwashawishi wananchi waukubali msimamo wake kuhusu Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa hususan suala la muundo wa Muungano.

CCM inashikilia muundo wa sasa wa Muungano wenye serikali mbili uendelee wakati vyama vya upinzani vinataka Muungano wa aina ya shirikisho utaoitoa Tanganyika kutoka pango la Muungano na kuirejeshea serikali yake.

Uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanywa Desemba umetufungulia pazia kidogo kutuonyesha muelekeo wa matokeo ya chaguzi hizo mbili kwa upande wa Bara. Dalili zilizopo ni kwamba kwa mara ya mwanzo kabisa chama cha CCM kinaweza kikashindwa kwenye uchaguzi endapo uchaguzi huo utaendeshwa kwa uwazi bila ya kuzuka mizengwe.

Ama kwa Zanzibar CCM ki taabani; ni kama kinachokata roho kwa jinsi kinavyoachwa mkono kwa wingi na wafuasi wake, hasa vijana, katika mikoa ya Kaskazini na Kusini ya Unguja.  Hata baadhi ya wanaopiga makelele kukiunga mkono wakiwa faraghani wanakiponda.

Tunachosubiri ni kuona iwapo miongoni mwao watachomoza wenye ujasiri kama ule wa mwenzao aliyefukuzwa Mansour Yusuf Himidi. Kijana huyu ambaye sasa ametangaza rasmi kujiunga na Chama cha Wananchi (CUF) alikuwa kigogo wa CCM.  Ni kiongozi mwenye haiba ya kisiasa aliye na wafuasi wengi ndani ya chama chake cha zamani hasa vijana.

Upande wa upinzani nao una changamoto zake. Umoja uliopo wa upinzani umepatikana baada ya vyama vya upinzani kuwa na msimamo mmoja kupinga mchakato wa Katiba Mpya ulivyoendeshwa.  Hata jina la Umoja huo — Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) — linaainisha hayo. Kwa ufupi kinachoviunganisha vyama hivyo ni msimamo wao wa kuikataa Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalum la Katiba.

Hamna shaka yoyote kwamba uamuzi wa upinzani wa kuwa na umoja wao ni muhimu na wa busara.  Umewatia moyo wananchi na kuwapa tamaa kwamba kwa kuunganisha nguvu angalau kuna uwezekano wa wapinzani kuleta mageuzi.

Juu ya hayo, ili patokee mageuzi panahitajika zaidi ya umoja uliopo. Linalohitajika ni vuguvugu lenye dhamira iliyo bayana ya kuleta mageuzi. Vuguvugu hilo liwe linajuwa linapigania nini.   Tena liyahusishe makundi na jumuiya nyingine za kiraia na hata raia wa kawaida wasiofungamana na chama chochote cha siasa.

Kazi ya kuliandaa vuguvugu la aina hiyo haitokuwa rahisi.  Lazima patazuka mivutano na tofauti za fikra, na pengine hata itikadi, baina ya vyama na makundi mingine yaliyo katika vuguvugu hilo.  Kila upande utatoa rai zake kuhusu namna ya kuyafikia malengo fulani.

Kwa hivyo, ni muhimu vuguvugu hilo liwe na jukwaa litaloruhusu maoni yenye kukinzana yaweze kuzungumzwa na kujadiliwa kwa kufuata misingi ya kidemokrasia.  Mijadala aina hiyo ni muhimu si tu kwa kuuimarisha mshikamano wa upinzani lakini pia kwa ujenzi wa mfumo wa kidemokrasia nchini.  Hiyo ni njia moja ya kuustawisha uzoefu na, hatimaye, ueledi wa kutenda mambo kwa kuzifuata kanuni za kidemokrasia.

Kinachohitajika sasa ni kwa Umoja huo kuyatanua mas’ala yanayoviunganisha.  Unapaswa kushughulikia mambo kwa kina na upana zaidi ili uweze kupiga hatua na kuwa na Vuguvugu la Kuleta Mageuzi ya Kizalendo.

Hilo linawezekana kwa wepesi kwa vile vyama hivyo havitofautiani hivyo kiitikadi.

Vyote vinajigamba kuwa kimsingi ni vyama vya kidemokrasia vyenye sera za kiuchumi zilizojikita katika mfumo wa ulibirali mamboleo.  Kwa hakika, vyama vyote hivyo vina sera za kiuchumi za kibepari ambazo hazina tofauti kubwa hata na zile za CCM ya leo.  Tofauti iliyopo ni ya utekelezaji — namna ya kuzitekeleza sera hizo na maadili ya wenye kuzitekeleza.

Sasa hasa ndipo inapoanza kazi ngumu ya UKAWA. Umoja huo lazima uonyeshe na mapema kwamba unaweza kupambana na vishindo utavyofanyiwa na hasimu yake mkuu, CCM.  Njia moja itayoweza kutumiwa kuudhofisha umoja huo ni kuvichafua vyama vyake kwa kujaribu kuwaingiza  baadhi ya viongozi wao katika mitandao ya kifisadi.  Tamaa ya ulwa na fedha ni adui mkubwa atayewaandama baadhi ya viongozi wa upinzani.

Kwa kusimama imara tu ndipo vyama hivyo vitapoweza kujikinga na vitimbi vitavyofanyiwa vya kuvifitinisha ili vianze kutiliana shaka.  Lengo litakuwa ni kuusambaratisha na hatimaye kuua umoja wao. Huu ni mwaka ambao tutashuhudia matukio ya ajabuajabu dhidi ya wapinzani.

Kuna wasemao kwamba historia huenda na kurudi. Na kwamba nchini Tanzania mambo yataendelea kuwa kama yalivyo, kwamba kila uchao yatakuwa yayo kwa yayo maji ya futi kwa nyayo.

Wenye fikra hizo wanakosea. Hali ya mambo haitoselelea kuwa hivi ilivyo daima abadan. Hilo ni hakika. Wananchi hawakulala.  Wanatambua kwamba wanao uwezo wa kuibadili hali ya mambo kwa kutumia kwa busara kura zao katika kura ya maoni na pia katika uchaguzi mkuu. Wanatambua kwamba wanapaswa kufanya hivyo ili waweze kujikinga na majanga yanayoweza kuwaangukia wasipofanya hivyo.

CCM si chama kilicho boza.  Si chama kinachojiachia kikumbwe na vimbunga bila ya kuwa na mikakati ya kupambana navyo.  Kwa hilo tu chama hicho kinastahili sifa.  Kwa hivyo, tutaraji kwamba CCM itaendesha kampeni kali wakati wa kura ya maoni juu ya Katiba mpya na wakati wa kuelekea uchaguzi mkuu.  Kampeni hiyo itatumia hoja na vitisho.

Kwa upande wa Zanzibar vitisho hivyo vitatisha zaidi hasa wakati wa kura ya maoni juu ya Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa. Ikiwa inapokaribia kura ya maoni itaonekana kwamba Wazanzibari bado wangali wanashikilia kuitumia haki yao ya kidemokrasia na watapiga kura kuikataa Rasimu ya Katiba basi tusishangae tukiyaona magenge kama ya kina “watoto wa mbwa” yakiingia mitaani.

Kwa bahati mbaya taasisi za utawala ni dhaifu Tanzania na hufanya kazi zake kwa upendeleo ijapokuwa zinatakiwa zisiwe zenye kumpendelea yeyote.  Aghalabu wanaonufaika ni chama kinachotawala na serikali yake. Ndio maana tunaona jinsi vyombo vya dola kama vile kwa mfano polisi na hata mahakama yanavyotumiwa kwa urahisi dhidi ya wapinzani na hata wale wanaodhaniwa tu kuwa ni wapinzani.

Kuna mianya mingi katika siasa za Tanzania na kuna maswali mengi ambayo ni mapema kuyauliza seuzi kuyapatia jawabu. Wafuasi wa falsafa ya  Ubudha wana methali isemayo kwamba mwanadamu husimama katika kivuli chake mwenyewe na halafu hushangaa kwamba kuna kiza.

Hatupaswi kuwa hivyo.  Tujiandae kwa yajayo kwani kwa jumla kwa hali ilivyo 2015 ni mwaka utaotushangaza kwa mambo, vijambo na majambo ya siasa za Tanzania.

Baruapepe: ahmed@ahmedrajab.com

Chanzo: Raia Mwema

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s