Mansour: Ninasonga mbele

Mwanachama mpya wa CUF Mansour Yussuf Himid akizungumza na wanachama wenzake , baada ya  kujiunga na chama hicho katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja
Mwanachama mpya wa CUF Mansour Yussuf Himid akizungumza na wanachama wenzake , baada ya kujiunga na chama hicho katika viwanja vya Paje, Wilaya ya Kusini Unguja

MIEZI minne iliyopita, mama mzazi wa Mansour Yussuf Himid, alinukuliwa akisema kamwe msimamo wake na familia yake wa kupendelea Zanzibar yenye mamlaka kamili, hautabadilika.

Alibainisha msimamo huo akisema hata kama gharama yake itakuwa ni kijana wake huyo kufungwa gerezani.

Ilikuwa ni kipindi ambacho Mansour ametupwa rumande baada ya kushitakiwa mbele ya Mahakama ya Mkoa ya Vuga, akidaiwa kukutwa na silaha pamoja na risasi kinyume cha sheria za nchi.

Msimamo huo, ulielezwa kwa wananchi na Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na umma wa watu katika uwanja wa Demokrasia, Kibandamaiti, mjini Zanzibar.

Wakati huo Mansour, aliyeshika uwaziri katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa miaka 13 mfululizo tangu awamu ya uongozi ya Dk. Salmin Amour Juma, alikuwa gereza kuu la Kilimani, baada ya kesi yake kuahirishwa kwa siku 12.

Mama Jinja, mmoja wa wanawake maarufu Zanzibar, amekuwa imara katika msimamo kwa sababu ameona kuna uonevu Zanzibar inafanyiwa kutokana na ushirikiano wake chini ya Muungano na Tanganyika.

Na msimamo huo ndio aliouchukua na kuusimamia kinagaubaga Mansour, tangu akiwa bado serikalini na kama mmoja wa viongozi waandamizi katika CCM.

Katika mazungumzo na gazeti hili hivi karibuni, amekiri kuwa huo ndio msimamo hasa uliomchonganisha na viongozi wakubwa wa CCM.

“Wapinzani wangu waliutumia kunifitinisha ndani ya chama,” anasema.

Kwa kuwa hakushituka na mipango iliyokuwa inasukwa dhidi yake, hakutetereka. Aliendelea kuamini hajamkosea mtu yeyote kwani aliona ni wakati muafaka wa Zanzibar kurudishiwa mamlaka yake kamili ili ipate kujiongoza na kujisimamia kikanda na kimataifa.

Hapo alikuwa akitamka waziwazi kuwa msimamo wake ni kuwa Zanzibar inahitaji na ni haki yake kupata mamlaka kamili yakiwemo ya kutumia raslimali za kiuchumi ilizonazo ili kujenga uchumi wake bila ya kulazimika kushauriana na nchi yoyote.

Mansour wakati huo alikuwa ametoka kuwa waziri anayeshughulikia sekta ya kilimo na maliasili, ambako raslimali ya mafuta na gesi asilia inayoaminika ipo ndani ya mamlaka ya Zanzibar, ilikuwa imeshatolewa azimio la kutolewa katika orodha ya mambo ya Muungano.

Ndio kusema ni uongozi wake kama waziri uliofanikisha serikali kutoa azimio hilo, kwa kuwa alitekeleza uamuzi wa Baraza la Wawakilishi, uliozingatia maoni ya wajumbe kwamba Zanzibar inahitaji kushughulikia yenyewe sekta ya mafuta badala ya kutegemea Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aliondolewa uwaziri pale ilipodhihirika kuwa amekuwa na msimamo mkali wa kupinga mwenendo wa Muungano unaoinyonya Zanzibar na kuidhoofisha kiuchumi.

Msimamo huo ulikuwa umeingia vifuani mwa wananchi wengi Zanzibar waliokuwa wakimsifia na kumpa moyo kwa kujitoa mhanga na kuinua sauti kwa kaulimbiu maarufu ya “Tuachiwe Tupumue.”

Mama yake alipotokeza na msimamo imara, alijua hana chaguo isipokuwa kusimama na mwanawe kwa kuamini kuwa ni chuki binafsi tu walizonazo wapinzani wake ndani ya chama zilizomponza.

Alithibitisha hiyo kwani Mansour alikamatwa na Polisi ya Mkoa wa Mjini Magharibi, tarehe 6 Agosti, 2014, akapekuliwa nyumbani kwake eneo la Chukwani, nje kidogo ya mji wa Zanzibar, na hatimaye kufunguliwa mashitaka ya jinai mahakamani.

Madai yaliyoko kwenye hati ya mashitaka, ni tuhuma za kumiliki silaha na risasi kinyume cha sheria za Zanzibar. Ametolewa nje kwa dhamana iliyoidhinishwa na Mahakama Kuu Zanzibar.

Sasa baada ya kukaa bila ya kusema mwelekeo wake wa kisiasa, ambao lazima uegemee kusimamia chama cha siasa, Mansour amefanya kile kinachofaa kuitwa “kukata jongoo kwa meno.”

Amejiunga rasmi na CUF kwa kukabidhiwa kadi ya chama hicho na Katibu Mkuu Maalim Seif mbele ya umma uliohudhuria mkutano wa hadhara katika kijiji cha Paje, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja, wiki iliyopita.

“Nimeamua kujiunga rasmi na chama hichi kwa kuwa anakiamini kuwa ndio chama kinachosimamia ukombozi wa Mzanzibari. CUF ndicho chama kinachobeba matumaini mapya ya Wazanzibari,” anasema.

“Leo ile siku imefika, nimeamua kwa hiari yangu kuchukua kadi ya chama cha CUF siyo kwamba nimefanya hivyo kwa kuichukia CCM lakini naipenda CUF kwa nia yake ya kuikomboa Zanzibar. Nawaambia ninasonga mbele,” anasema.

Mansour alishaeleza kuwa utakapofika muda wa uchaguzi mkuu, atarudi jimboni Kiembesamaki, na kuomba ridhaa ya wananchi kwa tiketi ya chama kingine, si CCM, kile alichoingilia Baraza la Wawakilishi, na kuteuliwa waziri baada ya uchaguzi mkuu wa 2000.

Alieleza msimamo huo alipoulizwa hatima yake kisiasa baada ya kufukuzwa CCM tarehe 23 Agosti 2013, baada ya kuvuliwa uanachama kwa kutuhumiwa kusaliti chama hicho.

Mansour alianza kuonekana mpinzani ndani ya chama alipojitokeza waziwazi akishabikia mfumo mbadala wa muungano badala ya serikali mbili uliopo.

Wakati akijiunga na CUF, tayari amekuwa akitekeleza majukumu mbalimbali aliyopewa baada ya kujumuishwa katika timu ya mkakati wa kuhakikisha Maalim Seif anaingia madarakani utakapofika uchaguzi ujao.

Watu wengi wanamuona Mansour kama damu mpya inayohitajika ndani ya CUF kwa kuwa itasaidia kuimarisha nafasi ya chama hicho kushika hatamu ya uongozi huku Maalim Seif atakayesimama tena kuwania urais, akiwa ametamka rasmi kuwa hatawazuia tena vijana wa CUF kudai haki yao wakiamini wamedhulumiwa.

“Katika uchaguzi mkuu wa 2010 nilifanya kazi kubwa ya kuwazuia vijana wasifanye vurugu pale hoteli ya Bwawani. Mwanzo niliwatuma wasaidizi wangu waende kuwaondosha, lakini hakuna aliyesikia hadi nilipo kwenda mwenyewe.

“Tena waliondoka kwa shingo upande kabisa. Kwa hivyo uchaguzi mkuu ujao sina namna yoyote yta kjuwazuia vijana kutetea haki yao,” amewaambia wananchi kwenye mkutano wa kijijini Paje.

Maalim Seif amekumbusha kilichotokea wakati Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Khatibu Mwinchande alipokuwa akisubiriwa kutangaza matokeo ya urais yaliyocheleweshwa katika mazingira yaliyozusha hofu kwamba kura zinachakachuliwa.

Kundi la wananchi walizingira geti la kuingilia Bwawani, na kutaka kuingia ndani ili wafuatilie kinachoendelea ndani ya ukumbi wa kutangazia matokeo, wa Salama.

Wakati huo, kulishaenea taarifa kuwa kamati ya maridhiano ya Mzee Hassan Nassor Moyo, ilikuwa inahangaika kumshawishi Maalim Seif akubali matokeo ya ushindi wa Dk. Ali Mohamed Shein wa CCM.

Umma wa Wazanzibari, ulikuwa ukitarajia kusikia tangazo la ushindi wa Maalim Seif.

Mansour yumo katika kamati hiyo, pamoja na Mohamed (Eddi) Riyami wakiwa CCM wakati huo, na Ismail Jussa Ladhu, Salim Abdalla Bimani na Abubakar Khamis Bakary kutoka CUF. Riyami alishahama CCM.

Kamati hiyo ndiyo iliyofanikisha maafikiano ya siasa za maridhiano kati ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume na Maalim Seif walioanza vikao vya siri Novemba 2009.

Chanzo: Mawio

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s