Anachokiimba Salmin Awadh kimechuja

Mwakilishi wa jimbo la Magomeni, Salmin Awadhi Salmin
Mwakilishi wa jimbo la Magomeni, Salmin Awadhi Salmin

TATIZO kubwa la Salmin Awadh Salmin ni kutoamini kuwa mjiti wa saa ukirudi nyuma ni gharika. Anataka mjiti wa saa urudi nyuma; na bado akiamini hilo likishatokea, saa yake bado ipo nzima – inatembea sawa sawa. Muflisi.

Salmin huyu, tofauti kabisa na alivyokuwa Salmin Amour Juma, rais wa awamu ya nne Zanzibar. Yule daktari alikuwa anajua mjiti ukirudi nyuma, kila kitu kimebadilika.

Nina simulizi ya tabia ya teja ambayo nitaieleza mbele kidogo. Nataka kwanza, nimpongeze Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.

Dk . Shein kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni msaidizi mkuu wa Mwenyekiti Jakaya Kikwete, upande wa Zanzibar. Masuala yanayohusu mwenendo wa chama hicho, anayaongoza yeye.

Basi ni yeye anayezicheza au kuziongoza siasa za CCM ndani ya mazingira ya Unguja na Pemba. Hili nadhani Salmin Awadh halijui. Au labda anaamini kila analoliwaza, basi Dk. Shein ataliridhia.

Kuna kitu Salmin Awadh anakiwaza na kuamini kitafanikiwa chini ya uongozi wa Dk. Shein kama Makamu Mwenyekiti wa CCM. Thubutu! Mbona Dk. Shein keshasema anailinda Serikali ya Umoja wa Kitaifa? Hajamsikia kwa hili? Muflisi.

Salmin Awadh ni kama teja. Nimekuwa nikiyaishi maisha ya mateja (wakiwa wengi) Kinondoni, wilaya iliyoko pembezoni upande wa kaskazini mwa jiji la Dar es Salaam.

Sikuwa naipenda Kinondoni. Hapana. Nilikuwa naiogopa. Wakati huo nikiwa nimelewea zaidi Temeke, wilaya ya pembezoni kusini, na Ilala, wilaya ya katikati ya jiji japo imesambaa zaidi magharibi.

Niliiogopa Kinondoni nilipokuwa naambiwa ni mji wa wajanja. Eti ukitaka uhuni, mbinu za mishemishe, starehe isiyo shida, ni Kinondoni. Watu huchuma wilaya hizo mbili, wakitumia Kinondoni.

Ni Kinondoni ambako mateja ni kama nyumbani kwao. Wapo wengi. Uthibitisho kuwa biashara yenyewe ya madawa ya kulevya imestawi sana.

Basi mateja kila kipembe. Kila mtaa. Huwezi kuwakwepa. Wanaoishi na hata kushinda tu Kinondoni, wamewazoea. Mateja nao ni wachuuzi vilevile kama walivyo Machinga walioenea kote mijini na hata vijijini Tanzania.

Mateja nao wanauza vitu wanavyouza Machinga. Tofauti ni moja: Wanavyouza Machinga wamevinunua na kuuza kwa faida kidogo. Wengi wa Mateja huuza vitu walivyoiba kwa siri au kwa kunyang’anya.

Lakini uongo mbaya, mateja tunaishi nao Kinondoni. Tunakunywa nao kahawa na tangawizi. Wapo wenye akili ya maisha ya Mtanzania. Wanajadili siasa za nchi yao. Wana shauku ya kushiriki michakato ya uongozi nchini pao.

Ila mateja wana utamaduni mmoja. Wakishakula au kuvuta unga, kwa kunusa au kujidunga sindano, lazima watoke udenda. Hapo huwa unga umewalevya. Wenyewe wanasema ndio kukamilisha safari ya majuu, Marekani au Ulaya.

Kama teja, Salmin Awadh naye amelewa. Bali yeye amelewa madaraka si unga. Wote ni walevi wa kutupwa, usijali sana tofauti ya kile kilichowalewesha. Itoshe tu kuamini wamelewa.

Teja ukimkuta midomo imeachana huku akitokwa udenda, ujuwe ameshiba unga; kipimo kimezidi kawaida. Mateja wakishalewa unga hutulia, hawana nguvu na hushindwa hata kupepesa macho. Wanalala huku wakiwa wima au wameketi kwenye vijiwe vya kahawa.

Salmin Awadh, amelewa madaraka sasa. Ni Mwakilishi wa Magomeni, mjini Zanzibar. Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM ambaye pia amekuwa mnadhimu wa wajumbe wa CCM barazani.

Huyu kilichomlevya hakimnyimi nguvu. Kwa hakika ndio kinampa nguvu zaidi na jeuri kubwa. Anajiona sana, na anaamini ndo amefika na kibosile asiyeweza kushuka tena.

Ulevi wa madaraka unamuandisi kufanya siasa za majitaka. Hajali nidhamu, yumo tu mchezoni, bila ya kujali kama anacheza kwa mtindo wa varange. Ulevi wa madaraka unamkosesha busara hata ya kujua kwamba kwa hayo anayoyaota na kuyapigania, anatafuta kuzusha machafuko.

Salmin Awadh hujui anatumwa au anajitumikisha. Yumo tu anahangaika. Maana ni kuhangaika kukubwa unapoona anatafuta makubwa yanayompita kimo. Hivi hajui kweli madhara ya kuichokonoa serikali ya umoja wa kitaifa?

Sasa kama hajui alipataje ujumbe wa CC-CCM? Kwa kweli anachokifanya ni kuivurugia CCM hadhi yake. Nisingejali kitu maana nafurahia na ningependa hadhi ya CCM izidi kuporomoka. Ni chama kinachohitaji kuzaliwa upya.

Tatizo jitihada za Salmin Awadh zina matokeo mabaya kwa wananchi na nchi yao. Ni jitihada za kubadilisha mjiti wa saa uwe unaotembea kinyume na kawaida. Anataka kurudisha Zanzibar ilikokuwa nchi ya siasa za chuki, fitina, husda, hasama na ufisadi.

Salmin Awadh kwa ulevi tu wa madaraka, kwa sababu ana vyeo kibao ndani ya CCM, pengine kwa kuwa havimstahili, anataka kuibua upya chuki baina ya wapenda siasa wa CCM na upande mwingine.

Siasa zile zilizofutwa kwa vikao vya siri vya Amani Abeid Karume, aliyekuwa Rais wa Zanzibar, na Maalim Seif Shariff Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), ndio Salmin Awadh anazitaka zishamiri.

Wanasiasa hawa katika mwaka 2009 waliamua kisichotarajiwa na Wazanzibari kutendeka kwa mafanikio. Walikutana na kukubaliana kuwa siasa chafu hazina maana, zinarudisha nyuma hamu ya wananchi kuishi na zinazuia nchi kuendelea.

Maafikiano yao yakakomazwa kwa vyama walivyo. Baada ya viongozi wenzao wa vyama kuyadaka maafikiano, kwa kuamini yameleta fursa adhimu ya kupunguza mihemuko ya kuzusha maafa, wakafanikisha yatumike kutandika msingi wa siasa za maridhiano hadi serikalini.

Leo, miaka mitano baada ya hatua hiyo, Dk. Shein anasifia matunda ya maridhiano. Maana yake CCM inaridhika na msimamo wake.

Maalim Seif vilevile anasifia mafanikio ya maridhiano yale. Maana yake CUF inaridhika. Kwa jumla, wananchi wanaridhika kwamba hatua fulani imepigwa. Ni hatua ya kwenda mbele siyo kurudi nyuma. Mabadiliko mema.

Wakati huo ndio mtizamo wa jumla wa mambo, Salmin Awadh na wenzake wanataka mjiti wa saa urudi nyuma badala ya kuufurahia unavyokwenda mbele kama inavyotarajiwa. Nini maana yake sasa?

Maana yake ni moja tu: Hataki amani ndani ya utulivu. Hataki maendeleo yanayoshirikisha kila mwananchi. Badala yake, anataka chuki, fitna na husda kati ya wananchi. Anataka maonevu yashamirishwe dhidi ya wananchi. Tofauti ya itikadi zao kisiasa iwachongee na kugombana. Yale yaliyokuwepo eti yarudie. Muflisi.

Amekuwa akitaka serikali ya umoja wa kitaifa ivunjwe. Alitaka kuwasilisha hoja hiyo kwenye Baraza la Wawakilishi, eti akidai anapeleka hoja yenye nguvu akiwakilisha wananchi anaodai hawaitaki serikali hiyo, eti haiendi vizuri.

Hivi kama haiendi vizuri ndio ivunjwe? Ikivunjwa ndio itakwenda vizuri? Kweli hajui ikivunjwa maana yake tuanze upya, ikimaanisha turudi kule Zanzibar ilikokuwa kwenye siasa za shida? Ndivyo anavyotaka Salmin Awadh.

Umma unamuona huyu muflisi kwelikweli kwa sababu anaimba nyimbo iliyochuja. Si kwa beti wala maudhui, imechuja chuji. Wazanzibari wameamua amani na mshikamano. Ushetani basi!

Chanzo: Mawio

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s