Watuhumiwa 510 mtandao wa panya road wakamatwa Dar

Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamanda Suleiman Kova
Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamanda Suleiman Kova

Vijana 510 wanaodaiwa kujihusisha na vitenda vya kihalifu chini ya kundi maarufu la ‘panya road’ wamekamatwa na jeshi la Polisi Kanda Maalum jijini Dar es Salaam kwa mahojiano.

Watuhumiwa hao wamekatwa katika mikoa ya kipolisi ya Kinondoni, Temeke na Ilala ambapo jeshi la polisi limefanya msako mkali kuweza kuwabaini lengo likiwa ni kuimarisha ulinzi nchini.

Kamishna wa Polisi Suleiman Kova ametoa wito kwa wazazi wa watoto hao kutofika kwenye vituo ambavyo wamehifadhiwa mpaka watakapo kamilisha uchunguzi wao dhidi yao.

Kamanda Kova amesema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa maeneo mbalimbali ikiwamo kwenye vijiwe huku wengine wakifuatwa katika nyumba wanazoishi baada ya polisi kupata taarifa za kinterenjensia.

“Tulipowapekua watuhumiwa hawa tuliwakuta na vichocheo kadhaa  vya uhalifu ambavyo ni  puli za bangi 113,  kete zake 676, na misokoto 294 na vinginevyo, pia kati yao wapo wakubwa zao watatu ambao ndiyo vinara wa mgogoro”.amesema Kova

Amesema operesheni ya kupambana na ‘Panya Road’ itakuwa endelevu hadi pale jina hilo ambalo limekuwa gumzo jijini litakapotoka kabisa masikioni mwa watu.

Aidha kamanda Kova amesema jeshi la polisi kwa sasa limejipanga katika kutoa mafunzo maalum kupitia wenyeviti wa Serikali za Mitaa  kwa mikoa yote ya kipolisi ili kukabiliana na vitendo hivyo vya uhalifu.

“Ni ukweli usiopingika kuwa vijana wanao fanya vitendo hivi wanafamika kwa wananchi wa eneo husika lakini wanakuwa wasiri kufichua uovu huo hivyo kupitia mafunzo haya yatasaidia kuondoa tatizo hili,” amesema Kamishna.

Januari 2 mwaka huu  hali ya taharuki, hofu na wasiwasi mkubwa iliwakumba wakazi wa jiji hilo kwa saa mbili baada ya kundi maarufu la waporaji la Panya Road, kuvamia mitaa mbalimbali na kupora mali.

Chanzo: Mwananchi

Leave a comment

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.