Salamu za Dk Shein kwa mwaka mpya

Rais wa Zanzibar anayeongoza serikali ya Umoja wa Kitaifa, Ali Mohammed Shein
Rais wa Zanzibar anayeongoza serikali ya Umoja wa Kitaifa, Ali Mohammed Shein

RISALA YA RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI, MHE. DK. ALI MOHAMED SHEIN, YA KUUKARIBISHA MWAKA MPYA 2015

Ndugu Wananchi,

Kwa neema na fadhila za Mwenyezi Mungu, Subhana Wataala tunaukaribisha mwaka mpya wa 2015 Miladiya na kuuaga mwaka 2014 tukiwa na utulivu na amani nchini. Inatubidi tumshukuru Mola wetu kwa kutujaaliya uhai hadi sasa na tumuombe Mwenyezi Mungu awarehemu wenzetu tuliokuwa nao mwaka jana na miaka iliyopita ambao wameshatangulia mbele ya haki.

Kwa kawaida binadamu wengi huupokea mwaka mpya kwa kujipangia maazimio mapya. Hivyo si vibaya, lakini ni vyema pia kutafakari na kuzingatia yaliyopita. Kwa kufanya hivyo, tutaweza kutathmini mafanikio na utekelezaji wa maazimio na dhamira tulizozipanga kwa mwaka uliopita na tuweze kujipanga upya kwa Mwaka Mpya.

Ndugu Wananchi,

Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia hali ya amani, salama na utulivu ambayo imetuwezesha kupata mafanikio katika mambo yetu mbali mbali tuliyojipangia katika mwaka uliopita. Ili tuweze kufanya tathmini ya kina na kuhakikisha kuwa tunapiga hatua kubwa zaidi ya maendeleo katika mwaka ujao, hatuna budi kuiendeleza hali ya amani na utulivu tuliyonayo kwa faida ya kila mmoja wetu. Tunaona, tunasoma na tunasikia kwenye vyombo vya habari, shida, taabu na hasara za maisha zinazowakuta watu wa sehemu mbali mbali za dunia kutokana na kutokuwepo kwa amani. Mwenyezi Mungu atuepushe na hali hio na atujaali tuendelee kuitunza amani, tukae salama na tudumishe utulivu tulionao.

Ndugu Wananchi,

Kutokana na hali ya amani na utulivu nchini, tulifaulu kuwa na usimamizi mzuri wa utekelezaji wa mipango mikubwa ya maendeleo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ikiwemo Dira ya Maendeleo ya mwaka 2020, MKUZA II, Malengo ya Milenia ya 2015 na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010 – 2015.

Katika mwaka uliopita, tulipata mafanikio mengi na makubwa katika nyanja za uchumi, siasa na maendeleo ya jamii. Aidha, tuliweza kudumisha mshikamano na umoja katika jamii. Ni matumaini yangu kwamba sote tunaukaribisha mwaka mpya tukiwa na dhamira na matumaini ya kuyaendeleza mafanikio haya.

Ndugu Wananchi,

Katika risala hii fupi ya kuukaribisha mwaka mpya wa 2015, hivi leo, sitazungumzia mafanikio tuliyoyapata ya kila sekta lakini, apendapo Mola mafanikio hayo nitayazungumza katika hotuba yangu ya kuadhimisha mwaka 51 wa Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964. Naomba niseme tu kwamba uchumi wetu umeimarika na kukuwa kwa kiasi cha kuridhisha. Ukuaji wa uchumi ni suala la msingi kwa sababu ndio kigezo cha maendeleo ya nchi zote. Mafanikio hayo yametokana na juhudi za pamoja za serikali wakiwemo, viongozi na wafanyakazi wote wa sekta zote na wananchi wote kwa jumla. Nachukua fursa hii kutoa pongezi na shukurani zangu za dhati kwa wote hao.

Aidha, nashukuru kuwa mwaka uliopita tuliendelea kushirikiana na washirika wetu wote wa maendeleo na waliendelea kutusaidia kwa kutupa misaada, mikopo na ushauri wa kitaalamu kwenye fani mbali mbali. Kwa niaba ya wananchi wote, natoa shukurani zetu za dhati kwa washirika wetu hao na tutaendelea kuudumisha na kuukuza ushirikiano huu, hasa katika nyanja za uchumi na maendeleo ya jamii kwa faida yetu sote.

Ndugu Wananchi,

Kwa masikitiko makubwa katika mwaka tunaouaga tulishuhudia ongezeko la vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto vinavyofanywa na watu wachache katika jamii yetu ambavyo ni vya uvunjaji wa sheria na vinakwenda kinyume na maadili yetu, dini, mila, desturi na silka zetu. Vitendo hivyo vimeendelea kuongezeka pamoja na juhudi zinazochukuliwa na Serikali za kuvidhibiti kwa njia mbali mbali.

Sisi wazee na walezi wa watoto, tuna wajibu mkubwa wa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya watu wanaofanya vitendo hivyo. Kama nilivyoeleza katika hotuba yangu ya tarehe 6 Disemba, 2014 katika uzinduzi wa kampeni ya kupiga vita ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto kwamba kuanzia mwaka huu na miaka miwili ijayo, ni kipindi cha kuvitokomeza vitendo vya udhalilishaji kijinsia nchini kwetu. Leo nairudia tena kauli yangu hio na natoa wito kwa wananchi wote tuazimie kuufanya mwaka mpya wa 2015 ni mwema na utakaokuwa na mafanikio katika kupinga udhalilishaji wa wanawake na watoto. Tufanye juhudi hizi kwa kushirikiana katika familia, mitaa, vijiji na miji yetu yote. Kila mmoja wetu ana wajibu wake katika jambo hili. Kwa hivyo, wazee, vijana, viongozi wa dini, siasa na jamii yote tushirikiane kuyapiga vita maovu haya katika jamii bila ya khofu au kuoneana muhali. Tusiwaonee haya watu wachache wanaowahadaa vijana wetu na kuwanyanyasa wanawake. Nilisema siku ya uzinduzi wa kampeni ya kupiga vita ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto, narudia kusema tena leo, wito wangu kwenu nyote, tuseme sasa na iwe basi. Tusemeni kwa maneno na kwa vitendo. Inshaallah Mwenyezi Mungu Karim atusaidie katika dhamira zetu za kuyapinga maovu haya ya udhalilishaji wanawake na watoto.

Ndugu Wananchi,

Pamoja na hayo niliyoyaeleza, natoa wito kwa wazazi na walezi wa watoto wetu kuwatunza na kuwapa malezi mema. Ni vyema tukawaandalia watoto wetu mazingira mazuri yakuyaendeleza maisha yao, nyumbani na mitaani. Juhudi za kila mmoja wetu na juhudi za pamoja zinahitajika katika kuwapa watoto na vijana malezi mazuri, wayapende masomo yao na wafuate tabia njema za wazazi na walezi wao ili wajipambe nazo na zije ziwafae katika maisha yao. Wazazi na Walezi wafuatilie kwa karibu nyendo za watoto wao, nani wanajumuika nao na nani wanashirikiana nao.

Ndugu Wananchi,

Kuhusu vijana, nawasihi waupokee mwaka mpya kuwa ni wa matumaini na matarajio mema. Wasivunjike moyo kwa sababu ya uchache wa ajira ziliopo Serikalini na katika sekta binafsi. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua hali hiyo kama nilivyowaeleza vijana katika ufunguzi wa maonesho ya fursa ya ajira kwa vijana katika Hoteli ya Bwawani siku ya tarehe 22 Novemba, 2014. Hali hii inawakumba vijana wengi katika nchi nyingi duniani. Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Kazi Duniani ya mwaka 2013, kuhusu ajira inakisiwa kuwa vijana milioni 73.4 duniani hivi sasa hawana ajira. Idadi hii ni ongezeko la vijana milioni 3.5 kwa mwaka, tangu mwaka 2007. Licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yaliyofikiwa na mataifa mengi ya Ulaya, yaliyopelekea kuwepo kwa viwanda vya aina mbali mbali, bado tatizo la ajira kwa vijana, linaendelea kuwepo na katika baadhi ya nchi ni kubwa kuliko ilivyo katika nchi zetu za Afrika. Ziko baadhi ya nchi za Ulaya zaidi ya asilimia 30 ya vijana wake hawana ajira. Katika utafiti wa Mapato na Matumizi ya Kaya uliofanywa mwaka 2009/2010. Zanzibar ilikisiwa kuwa na asilimia 17.1 ya vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 wasiokuwa na ajira. Nataka vijana muyazingatie haya ninayoyaeleza, kwani huu ndio ukweli.

Katika jitihada za kuwawezesha vijana kujiajiri, tumeanzisha mfuko maalum wa kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia miradi watakayokuwa nayo. Kwa hivyo, mwaka 2015 uwe wa vijana kujishajihisha kutumia fursa zilizopo kujiendeleza na kujiajiri. Serikali inayo wataalam wa kutosha wenye uwezo wa kutoa ushauri ufaao kwa vijana.

Ndugu Wananchi,

Katika mwaka tunaoukaribisha nchi yetu itakuwa na matukio kadhaa makubwa ikiwemo Kura ya Maoni ya Katiba iliyopendekezwa na Uchaguzi Mkuu. Mambo mengine muhimu tutakayokuwa nayo ni kukamilisha utekelezaji wa Mipango ya Milenia ya 2015, MKUZA II na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2010-2015. Mambo haya yote yanataka ushiriki wenu wananchi, ambao hautoweza kupatikana bila ya kudumisha amani na utulivu, utii wa sheria, mshikamano na kuvumiliana. Sote kwa pamoja tunao wajibu wa kuyafanikisha mambo hayo kwa kuzingatia utekelezaji wa sera na mipango iliyowekwa.

Ndugu Wananchi,

Kwa kumalizia, risala yangu ya Mwaka Mpya, nakumbusha kwamba, tarehe 12 Januari tutaadhimisha miaka 51 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964. Tutaanza sherehe za maadhimisho tarehe 02 Januari kwa shughuli mbali mbali na natoa wito kwenu wananchi ili mshiriki kwa wingi katika shughuli hizi. Aidha, kama kawaida yetu natoa wito tujitokeze na tushiriki kwa wingi katika kuzifanikisha sherehe hizi za mwaka huu.

Ndugu Wananchi,

Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, natoa salamu za mwaka mpya kwenu wananchi wote wa Zanzibar na Tanzania Bara na kwa ndugu na marafiki wetu wote kokote walipo. Aidha, natoa salamu hizi kwa viongozi wa nchi marafiki na washirika wetu wa maendeleo na mashirika ya kimataifa kupitia mabalozi na wawakilishi wao waliopo nchini. Mwenyezi Mungu aujaalie mwka wa 2015 uwe wa kheri, Baraka, neema nyingi na amani, umoja na utulivu uendelee kudumu nchini kwetu. Tuendelee kupendana na kusaidiana katika kuyaendeleza maisha yetu.

Mungu atupe Baraka za Mwaka Mpya 2015

Ahsanteni

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s