Ukweli tu ndio utamjenga Balozi Seif

Balozi Seif Ali Iddi akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa  jengo jipya la skuli ya msingi ya Ngomeni Wilaya ya Chake chake Pemba
Balozi Seif Ali Iddi akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo jipya la skuli ya msingi ya Ngomeni Wilaya ya Chake chake Pemba

WAZANZIBARI wanaamini haki haitolewi hivihivi (kirahisi). Lakini hatari zaidi ni pale wanaposhuhudia mfumo wa serikali kutumika kunyonga haki yao wananchi.

Imani hii ndiyo hasa inayowasukuma wananchi wasioamini katika uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), au “wapenda mabadiliko” dhidi ya mfumo uliopo, kushikamana na kuzuia jitihada za kukwamisha haki yao.

Wanaonesha msimamo imara wa kulinda haki yao kila unapofika uandikishaji wapigakura; wakati wa uchaguzi, hata wa kujaza kiti kimoja.

Wananchi hao hujikusanya na kuzikandamiza mbinu zinazotekelezwa na watu wanaodhaminiwa na watawala.

Wananchi wanaitikia wito wa serikali kujisajili ili kupatiwa kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, kwa kuamini kama serikali inavyoeleza, ni haki ya Wazanzibari wote Unguja na Pemba.

Kumbe serikali inapotoa hima kwa wananchi kujitokeza kuandikishwa ili kupatiwa kitambulisho hicho, ni kiinimacho. Wanapofika vituoni wanakataliwa kwa visingizio visivyokuwa na nguvu ya sheria.

Wananchi wanashuhudia viongozi wanaotokana na CCM wakitetea msimamo wa serikali kwamba hakuna mwananchi anayenyimwa kitambulisho labda tu kama hakukidhi masharti ya kisheria.

Ndani ya uchochoro huo, maelfu ya Wazanzibari wananyimwa haki yao, huku mawaziri kutoka CCM wakirudia kauli kuwa serikali haivunji sheria.

Lakini, wakati huohuo, wanabainika mawaziri hao wakifadhili makundi ya vijana wanaofundishwa uharamia dhidi ya raia wema kama mbinu ya kuzuia wasipate haki.

Inafurahisha mawaziri wawili wamethibitisha kuwepo watu waliopewa kitambulisho hicho wakati si wananchi halali. Ikaahidiwa watanyang’anywa baada ya uchunguzi kufanywa.

Ni nani aliidhinisha kitambulisho wapewe wasiohusika? Ni kwanini? Nani anafanya uchunguzi kuwabaini hao? Je, uchunguzi umefanywa? Wangapi wamegundulika? Wamechukuliwa hatua gani? Na walioidhinisha kitambulisho kwa asiyehusika wamedhibitiwa?

Mtiririko huo wa maswali unasubiri majibu ya serikali. Bila ya majibu, wananchi wataamini hakuna uchunguzi uliofanywa. Kwa hivyo, ina maana kauli za mawaziri Mohamed Aboud Mohamed na wenzake kutoka CCM, ni za kulaghai umma.

Kumbe mawaziri hawa na viongozi waandamizi wa CCM, hutoa matamko lakini nia yao ni kudanganya dunia huku maelfu ya wananchi wakiendelea kudhulumiwa kwa kunyimwa haki yao inayowafikisha kuchagua viongozi wawatakao.

Maelfu ya Wazanzibari halisa, wengine wakiwa hawajawahi kusafiri nje ya visiwa vya Unguja na Pemba, hawana kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, na wengi wamekosa kusajiliwa kwa ajili ya kile cha Taifa kinachotolewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT).

Wote hao watakosa haki ya kuchagua. Watakosa kushiriki Kura ya Maoni ya kuiamua Katiba mpya iliyopendekezwa.

Hawa ndio wanaolalamikia undumilakuwili wa serikali. Wanataka haki yao. Wanadai kutambuliwa na kupewa haki na siyo haki yao kupewa wasiohusika.

Kwa kuwa wananyimwa haki licha ya kulalamika, na wanaona viongozi wameziba masikio wasisikie vilio vyao na wamefumba macho wasione wanavyolalamika, nao wameamua kuzuia watu wasiohusika kupewa haki wasiyostahili.

Hofu yangu na yao, isije ikawa wao ndio Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, anawaita wahuni na kuahidi serikali kuwadhibiti utakapofika uchaguzi mkuu Oktoba mwakani.

Pasina kumung’unya maneno, nasema hilo halikubaliki maana si haki na si uongozi bora huo. Itakuwa jambo baya kama ndivyo Balozi Seif na wenzake katika CCM wanavyoamini.

Ndio maana namshauri Balozi Seif awashawishi wenzake kuwa wakweli na waungwana wa nafsi zao. Batili huzuiwa kwa kuchagua haki. Kuifinya haki ni dhambi. Ni muhimu serikali ikarahisisha haki kushamiri na sio kuilea batili.

Kulea batili ni kupalilia chuki. Huko hatimaye kunachochea machafuko. Watakaolaumiwa si wanaodai haki yao, bali ni viongozi wanaoizuia isishamiri.

Viongozi wanaporidhika kuona haki inazuiwa kwa kuwa wanaoidai hawako upande wao kisiasa, ni kupandikiza udhalimu. Ni uhafidhina ambao haufai katika kujenga jamii inayoshikamana.

Hawa viongozi wanahamu mbaya. CCM haiwezi kudumu kwa ushindi wa hila kama inavyoonekana chama hicho kinavyopotea.

CCM lazima iamini sasa kwamba zama za kutangaziwa ushindi badala ya kushinda kwa haki, zimepita. Wala haziwezi kurudi maana wananchi hawakubali.

Zanzibar inataka uchaguzi mzuri unaofuata vigezo sahihi si ghushi. Demokrasia na utawala bora ndio ngao zama hizi. Ndio msingi muhimu unaosaidia nchi kuendelea na matunda ya maendeleo kugusa maslahi ya wananchi.

Uchaguzi unapoendeshwa kwa kuvunja sheria, mshindi anayetangazwa anabaki kuwa si halali. Wananchi wanapotangaziwa asiyehalali kuwa ndiye mshindi, wanajua serikali atakayoiunda si halali. Wataendelea kuamini hivo hata kama serikali hiyo itamaliza miaka mitano.

Wananchi wanajua kura zao zilihujumiwa, sauti yao ilikandamizwa na kuzimwa, kwa sababu wahafidhina ndio walishika hatamu na kuwaamulia nani awe kiongozi wao. Huko si kujenga, ni kubomoa na kuisukuma jamii shimoni.

Haihitaji mtu kuwa na digrii kujua hapo uhuru wa wananchi kuamua huwa umeporwa. Basi imeporwa hatima ya nchi yao.

Sasa, Balozi Seif ni vema akasihi wenzake kuwa Zanzibar, nchi yenye watu wastaarabu, wavumilivu, werevu, wenye utu na kupenda nchi yao, wanahaki ya kusikilizwa na kuheshimiwa.

Si sahihi kutafuta kisingizio kuwaumiza. Kwa sababu wapo katika nchi huru, walindwe na haki zao zilindwe; na utu wao na matumaini yao yaenziwe. Wanatumaini kujenga nchi yao. Sheria na Katiba ndio iwe dira ya kuwafikisha huko.

Nchi hujengwa kwa mipango mizuri na iliyo endelevu ambayo hupatikana kwa kuwepo utulivu serikalini. Uongozi mwema ndio utamudu kubuni mipango mizuri na itakayoleta tija.

Kwa miaka mingi Zanzibar imekosa hayo. Inayo amani lakini roho mkononi. Amani isiyoruhusu wananchi kushiriki kwa pamoja kujenga nchi yao siyo.

Inayoonekana ni mipango iliyotokana na maandalizi ya zimamoto. Asiye mtiifu kwa CCM hafai kuishauri serikali. Hiyo ni dhambi kubwa, CCM haimiliki nchi.

Viongozi wafike mahali waamini sasa kwamba Wazanzibari wanataka serikali ya viongozi waliopata ridhaa halali. Katika hilo, Balozi Seif atavutia umma akiwa mkweli.

Chanzo: Mawio

Advertisements

One Reply to “Ukweli tu ndio utamjenga Balozi Seif”

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s