Shaka ametumwa kuivuruga Zanzibar?

Naibu Katibu Mkuu wa Vijana, Shaka Hamdu Shaka
Naibu Katibu Mkuu wa Vijana, Shaka Hamdu Shaka

Mwandishi mmoja wa michezo ya kuigiza wa Uingereza  aliyeishi katika karne ya 16 na 17, John Webster alieleza:”We think caged birds sing, when indeed they cry”, yaani tunafkiri ndege aliyekuwa katika tundu anaimba , lakini ukwelii ni kuwa huwa analia.

 
Usemi huu wa hekima niliousikia shule  kwa mara ya kwanza  mwaka 1955 kutoka mwalimu wangu, marehemu Seyyid Ali Kakhtan, huukumbuka  ninapowasikiliza hao wanaoitwa  wanasiasa wa Zanzibar wanaimba nyimbo za uchochezi kufurahisha umati, lakini kwa kweli wanawasha moto  wa chuki ambao ukiripuka sijui mzimaji atakuwa nani.
 
Lakini hujiliwaza na kujiambia haya ndio maisha. Mara nyingi hufikia uamuzi huo ninapokumbuka nasaha za walimu wa dini, kama marehemu Sheikh Abdullla Saleh El-Farsy na marehemu Seyyid Hamid Mansab, za kumtaka mtu apokee ijapokuwa kwa shingo upande kauli anazoziona sio za kiungwana na zilizokosa utu, wema na ihsani.
 
Katika siasa za Zanzibar  za hivi sasa wapo watu  waliovamia siasa ambao wanaonekana kukubuhu kuimba nyimbo za kutukana watu, kuchochea mtafaruku na hata kuzungumzia haja ya kuchinjana na kumwaga damu ili kutimiza malengo yao ya kisiasa. Hii ni hatari kubwa.
 
Ninachoona kimesibu ni kuwa baadhi ya watu hawa ambao ninafikiri labda wanayo mashaka ya kimwili au ya  kiakili (wengine ninasikia, sina hakika wapo  hivyo)  ndio maana hawapendi watu waelewane.
 
Ili kufikia lengo lao hilo wanaamua kubwabwaja matusi yaliyojaa kashfa na kauli chafu za kuchocheya watu wa Unguja na Pemba wafarakane. Baadhi ya watu hawa hata maana ya majina yao yanasibu na hayo wanayoyatamka na kuyafanya hadharani (ya siri siyajuwi).
 
Hivi karibuni mwaka 2014 ulipokuwa unamalazika nilichogundua nilipokuwa kisiwani Pemba ni watu wengi wa huko na hasa wazee kushtushwa na kushangaa na kauli za  mmoja wa hawa watu ambao mwenendo wao una mashaka.
 
Miongoni mwao ni Naibu Katibu Mkuu wa Vijana, Shaka Hamdu ambaye alizungumza katika kijiji cha Ole na watu wa huko kusema ….ole wake kwa kauli zake zile.
 
Mara nyingi Shaka amesikika akizungumzia uwezekano wa kumwagika kila tone la damu ili kile anachoamini vijana wa CCM wanakitaka  kipatikane na amewahi kusema hivyo hata mbele ya Rais Jakaya Kikwete ambaye siku zote amewataka Watanzania kufanya shughuli za kisiasa kwa njia za kistaarabu  katika mkutano wa hadhara uliofanyika Unguja.
 
Lakini  Shaka alinyamaziwa kimya kwa kauli ile na zile za wenzake za kuwabagua watu wa Pemba ambao hivi karibuni walionekana kushangaa kwa nini Shaka na wenzake walikwenda Pemba kuwaomba watu wa huko wakipokee Chama cha Mapinduzi wakati wapo watu katika chama hicho wanawabagua Wapemba na  kuwataka wale waliopo Unguja wahame na kurudi Pemba.
 
Hapa ndipo ninapopata mashaka, sio juu ya Shaka, bali juu ya viongozi wengine wa juu wa CCM wakiwemo Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na kujiuliza kwa nini wanavumilia watu wanaochochea ubaguzi na uhasama?
 
Hivi karibuni, Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, alikuja Unguja na familia yake na kushiriki katika ibada ya Krismasi na anafaa kupongezwa kwa kauli yake ya kiungwana na iliyojaa utu ya kuwataka watu wa Visiwani waelewane na washirikiane  licha ya tafauti zao za kisiasa.
 
Kwa hili, hata wale ambao wanatafautiana kwa mengi na Lowassa, anafaa kupongezwa kwa vile amefanya juhudi ya kuwasaidia watu wa  Zanzibar  kujepushana maafa abayo kila mtu atajijutia yakitokea  na chanzo kuwa siasa za chuki, uhasama na ubaguzi.
 
Nina mashaka makubwa kama naye Lowassa hataandamwa na kutukanwa na akina Shaka ambao kauli kama hizi za kuwataka Wazanzibari kuendelea na mfumo wa Serikali ya moja wa Kitafa (GNU) ili kuendelea amani na maeleano hawazipendi.
 
Shaka amekuwa akiibeza GNU na amekuwa pamoja na hao wanaojiita watumishi wastaafu wa serikali, lakini licha ya umri mkubwa ana wengine wakiwa hawana hata nguvu za kutembea au kusema, wanataka GNU ivunjwe ati wanaiona haina mema wala neema kwa Zanzibar.
 
Watu hawa sio tu hawayaoni mafanikio ambayo Zanzibar imepata tokea kuachana na siasa za uhasama miaka minne iliyopita bali wanayafumbia macho na badala yake wanafungua midomo yao kubwabwaja matusi kama vile wamepewa jukumu la kutengeneza kamusi la matusi ya Kiswahili.
 
Ni vyema kwa Rais Kikwete na Dk. Shein kuchukua hatua za haraka kuwadhibiti watu wa aina hii, iwe ndani ya serikali, CCM au vyama vyengine, ambao wanataka kuitia nchi katika mashaka kama mwendo wa mashaka wa maisha ya watu hawa ambao wengine unakubaliana na majina yao.
 
Huu mchezo wa kuzungumzia kumwaga damu ili kupata mafanikio ya kisiasa au kutoa kauli za kijeuri za kusema wanaotaka kuleta mabadiliko ya serikali Zanzibar wabebe silaha na sio kutegemea uamuzi wa wanachi kwa kupitia uchaguzi ni wa hatari.
 
Wimbo huu mbaya wa akina Shaka haufai kwa vile unapelekea watu kupoteza imani na kubadilishana uongozi kwa njia ya amani. Tumeona hatari iliyotokea nchi nyingi ambapo watu waliona uongozi haubadilishwi kwa kura na kuamua kuingia barabarani na kupelekea nchi zao kuwa na mashaka na maafa.
 
Tujitahidi, hata tukiwa na mashaka ya kuwepo mizengwe ya uchaguzi au wizi wa kura, tusikaribie huko kwa vile hapatakuwa na mwisho mwema.
 
Kama akina Shaka wanataka kuzusha maafa ya kumwaga damu basi wafanye kwa kuchinja kuku au kama ni lazima kwa familia zao na sio kwa watu wengine na nchi yetu.Watanzania wanataka amani na hawapo tayari kuchinjana, ijapokuwa tunawasikia wengine huko Bara wakitaka kwenda porini kama wazee wa vita vya majimaji, kule Songea, walipoanzisha vita vya msituni.
 
Watanzania waliopo Bara na Visiwani ni watu wa amani na siku zote wamekuwa wakilaani kauli na vitendo vya utumiaji wa nguvu zinazopelekea kumwagika damu, iwe za kuiba mabenki, maduka, viwanda au ujangili wa wanyama pori.
 
Hatukatai zipo njia nyingi kwa mwanasiasa kutaka umaarufu au chama chake kuungwa mkono na hata kupata ushindi, ikiwa pamoja na kutumia mizengwe ya uchaguzi na wizi wa kura.
 
Lakini mambo ya matusi, ubaguzi na  umwagaji damu hayawezi kukubalika hata na baadhi ya wale wenye mashaka ya kimwili na kiakili ambao Wazanzibari mtu kama huyo humwita “ mtoto si rizki”.
 
Kama mtu anataka kutukana basi ajitukane mwenyewe wazee wake na sio wazee wa wenzake na  anayetaka kuuwa auwe kuku na sio watu. Siasa sio kutukanana, kupigana au kuuwana bali ni ushindani wa fikra na nguvu za hoja.
 
Katika dunia ya leo watu wanatafutiana sio kimwili tu bali hata kifikra na bado hii haiwi sababu ya uadui. Hili halina shaka na wenye mashaka basi  ni watu wenye uwalakini wa kimwili na kiakili. Sijuwi huyu kijana Shaka Hamdu yupo katika fungu lipi, labda mwenyewe atatueleza siri yake.
 
Kwa wale wanaozungumzia ubaguzi na kuwataka wenye ndoto ya kuleta mabadiliko ya kisiasa wabebe silaha inafaa wasome  maandishi ya  mwandishi maarufu wa vitabu wa Urusi, Leo Tostoy (1828-1910) ambaye aliandika sana juu ya amani na vita.
Katika moja ya nukuu zake maarufu alisema: ”Everyone thinks of changing the world, but no one thinks of changing himself”, yaani kila mtu hufikiria kuibadili dunia, lakini sio kujibadili mwenyewe kuwa na mwenendo na tabia nzuri.
Ni vyema akina Shaka na wana siasa wote wa Zanzibar, waliomo CCM na vyama vya upinzani, wakazingatia hekima na busara za kauli ya  Leo Tolstoy.
Lakini hata na wafuasi wa vyama vya siasa na kila Mtanzania anapaswa kutilia maanani hekima ya wasia wa Tolstoy ambayo anaheshimika mpaka leo Urusi na kila pembe ya dunia.
Chanzo: Tanzania Daima
Advertisements

One Reply to “Shaka ametumwa kuivuruga Zanzibar?”

  1. ASANTE UMEELEZA MANENO YA MAANA WATU KAMA HAWA HUTUMILIWA TU BAADAE HUTUPILIWA MBALI, HILI JINA PEKE YAKE LINATOSHA WAZANZIBARI WENYE AKILI TIMAM HUJIFURAHISHA NA WATU WAPUNGUFU WA AKILI AJUE YEYE ANA FAMILIA YAKE HAPO ZANZIBAR, KWANZA DAMU ANAYOITAKA KUIMWAGA ITAANZA KUTOKA NYUMBANI KWAKE IKIWA HAJUI MANENO ANAYOSEMA YANAFIKA MBALI IKIWA JUKWAA LINAMLEVYA, ASIJISAHAU AWATAZAME WENZAKE KINA KAMANDO MIDOMO YAO WAPI IMEWAFIKISHA LEO. TUMUOMBE MUNGU AWAKATE KAULI WATU KAMA HUYO SHAKA NA WENZIWE AMIN.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s