Zanzibar na Cuba: Hadithi ya Visiwa Viwili

Bw. Hashil Seif. Picha: Ahmed Rajab
Bw. Hashil Seif. Picha: Ahmed Rajab

Na. Ahmed Rajab

HASHIL Seif ni mwenzangu. Ni rafiki yangu na ijapokuwa si wa damu moja, au pengine kwa sababu hiyo, amekuwa zaidi ya ndugu yangu. Yeye ni mtu wa mambo mengi. Ni mtu wa visa na mikasa. Hayo yako wazi katika mashairi na riwaya zake alizochapisha. Mengine yatadhihirika zaidi kitapotoka kitabu chake kipya cha kumbukumbu za maisha yake ya kisiasa.

Hashil Seif ana dosari moja. Kuna nyakati anaweza kuwa machachari na mapepe. Hata hivyo husameheka kwa wepesi kwa vile daima hufanya mambo kwa moyo safi. Pia ni rahisi kuyasahau machachari yake kwa sababu aghalabu huwa ni zao la akili yake inayofanya kazi kama cherehani isiyosita kufuma.

Juu ya mizaha yake mingi akili yake saa zote huwa macho kuangalia wapi duniani haki za binadamu zinakiukwa. Ndio maana kwa muda wa miaka mingi alikuwa akifanya kazi katika Kituo cha Haki za Binadamu nchini Denmark anakoishi.

Tangu utotoni mwake Hashil amekuwa amejawa na raghba ya kupigania haki na shauku hiyo ndiyo iliyompelekea kuzivaa siasa. Alianza na siasa za kiwananchi, za kizalendo, za kupigania uhuru na kumtoa mkoloni. Halafu siasa zake zikapevuka. Zikawa siasa za kitabaka za kuwapigania wanyonge.

Haikuchukuwa muda akiwa kijana kabisa Hashil akawa miongoni mwa wa wafuasi wakubwa wa Abdulrahman Babu tangu Babu alipokuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) hadi alipotoka na kuunda chama cha Umma Party.

Siasa za Hashil zilikuwa za safari ndefu iliyomtoa kwao na kumfikisha Havana, Cuba, 1962. Alikwenda huko kufunzwa mbinu za kupindua serikali. Wakati huo Babu alikuwa amefungwa gerezani na Waingereza. Kuna wasemao kwamba Waingereza walimfunga kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa ZNP.

Hashil aliifunga safari ya kwenda Havana kwa siri kubwa. Alikuwa katika kundi la mwanzo la vijana wa Kizanzibari waliokwenda Cuba wakiongozwa na Hamed Hilal. Wenzao katika kundi hilo walikuwa Said Seif Rahatileil, Ali Yusuf Baalawy, Salim Saleh na Ali Mshangama.

Makundi mingine yalifuata baadaye. Msaada huo ulipatikana kwa jitihada kubwa za Ali Sultan Issa aliyetumwa na viongozi wa chama cha wafanya kazi cha Federation of Progressive Trade Unions (FPTU), Ahmed Badawi Qullatein na Khamis Abdallah Ameir, ende Cuba kutafuta msaada wa kuwapeleka vijana wa Kizanzibari kujifunza mbinu za kupindua serikali kwa kutumia silaha.

Hadithi hii ni ndefu lakini kwa ufupi Ali Sultan alifanikiwa kuwasili Cuba na kupokewa na Raul Castro, aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na ambaye sasa ni Rais wa Cuba baada ya kumrithi kaka yake Fidel Castro. Isije ikafikiriwa kuwa urithi huu ni upendeleo wa kindugu. La, Raul alikuwa miongoni mwa viongozi wa mapinduzi ya Cuba chini ya Fidel walioupindua udikteta wa Fulgencio Batista.

Raul alivutiwa na msimamo wa Ali Sultan. Wote walikuwa waumini wa itikadi moja. Kila wakati walikipembua walichokuwa wakikijadili kwa uchambuzi wa kisayansi.

Hashil na wenzake walishukia hoteli ya Havana Libre na anasema anakumbuka chumba chake kilikuwa ghorofa ya 14. Siku ya pili baada ya kuwasili Havana kiasi cha saa sita za usiku walichukuliwa kwenye mkutano uliokuwa ukihutubiwa na Che Guevara. Ilikuwa katika sehemu ndani ya ofisi yake.

Pamoja na Hashil walikuwa Hamed Hilal, Rahatileil na Ali Mshangama. Walikuwako pia vijana wengine kutoka nchi za Amerika ya Kusini. Kila mmojawao alipewa cigar avute labda ili wasisinzie. Mkutano huo ulifanywa nyakati hizo za usiku kwa sababu Che alikuwa amezongwa na kazi na hakuwa na nafasi mchana.

Che alizungumza kwa Kispanyola lakini alikuwako mkalimani wa Kiingereza. Alizungumzia umuhimu wa kuwa na umoja miongoni mwa wenye kupigana na ubeberu.

Baada ya hotuba yake Che aliwapa fursa ya kumuuliza maswali. Hashil aliuliza lake akajibiwa na baada ya mkutano kumalizika Che alimpa mkono yeye na wenzake akajiondokea.

Hashil anasikitika kwamba Che alipozuru Zanzibar yeye alikuwa masomoni Indonesia. Akina Ali Sultan na wenzake waliokuwa zamani Umma Party ndio waliokuwa wenyeji wa Che Zanzibar na walimpa Mussa Maisara, mmoja wa vijana wa Afro-Shirazi Party (ASP), dhamana ya kumtembeza.

Kwenda Cuba kulimvutia Hashil kwa vile alikuwa akimuhusudu sana Fidel Castro na akitamani akutane naye uso kwa uso. Bahati hiyo ilimwangukia ghafla siku Fidel alipokwenda hoteli ya Havana Libre.

Alipofika hotelini Fidel alifululiza hadi jikoni. Hashil alisadif kuwapo hapo na alisonga mbele kumpa mkono. Hakuwahi kuzungumza naye kwa kina. Alimwambia tu kwa Kispanyola kwamba alitoka Zanzibar. Anadhani baadaye Fidel aliuliza na kuambiwa kuwa Hashil alikuwa kati ya walio Cuba kwa mafunzo ya kijeshi.

Wenye kumjuwa Fidel wanasema kuwa ni mtu mwenye kupenda kujuwa mambo anayependa kuzungumza na kushindana. Fursa hiyo kwa bahati mbaya Hashil hakuipata.

Vijana wa Kizanzibari waliokuwa Cuba hawakuwa na masihara. Muda mwingi walikuwa wakizungumzia vipi watakaporejea nyumbani watapoweza kuipindua serikali.

Mwaka mmoja kabla Marekani ilijaribu kuupindua utawala wa Castro kwa kufanya uvamizi unaojulikana kama ‘Uvamizi wa Bay of Pigs’. Wakati mmoja baada ya vijana wa Kizanzibari kuwasili kulikuwa na uvumi kwamba Marekani huenda ikajaribu tena kuishambulia Cuba. Kusikia hayo kina Hashil walimpelekea barua Waziri wa Mambo ya Ndani wa Cuba Ramiro Valdés Menéndez wakimueleza kuwa walikuwa tayari kusimama bega kwa bega na wananchi wa Cuba kuihami nchi yao.

Barua hiyo iliwakuna viongozi wa Cuba. Kabla ya barua hiyo kuandikwa Wacuba wakitaka kuwaondosha Wazanzibari kambini na kuwapeleka kuwaficha sehemu nyingine. Lakini Hashil na wenzake walikataa na wakaachiwa wabakie kambini.

Mapinduzi ya akina Castro yalikabiliwa na misukosuko mingi. Mbali na jaribio la 1961 la uvamizi wa ‘Bay of Pigs’ Marekani imeiwekea vikwazo Cuba tangu 1959, vikwazo ambavyo vimeudhoufisha uwezo wa serikali ya Cuba wa kuyakidhi mahitaji ya wananchi wake.

Marekani pia ilivunja mahusiano yake ya kiserikali na Cuba. Na isitosheke ilijaribu hata kumuua Fidel Castro zaidi ya mara 600.

Ni wiki iliyopita tu Rais Barack Obama wa Marekani alipotangaza kwamba Marekani inabadili msimamo kuhusu Cuba na itaitambua na kuwa na mahusiano ya kawaida nayo.

Obama ametambua kwamba sera zao dhidi ya Cuba hazikufua dafu.

Kama kuna utawala unaostahiki kuwa na kaulimbiu ya ‘mapinduzi daima’ basi labda ungekuwa wa Cuba kutokana na vitimbi unavyofanyiwa na Marekani. Kaulimbiu kuu ya Cuba ni ‘patria o muetre, venceremos’ (‘Watani au kifo, tutashinda’), yaani tutaupigania watani wetu, nchi yetu, mpaka tufe na tutashinda. Hiyo ni kaulimbiu ya kizalendo.

Kwa hakika, katika nadharia za Kimarx ipo dhana inayoitwa ‘mapinduzi ya kudumu.’ Dhana hii ilianza kutamkwa na Karl Marx lakini baadaye ikawa moja ya nguzo za madhehebu ya Ki-Trotsky katika itikadi ya Kimarx. Waumini wa fikra hiyo wanamfuata Leon Trotsky, mmoja wa wanamapinduzi wa Urussi ambaye baadaye alihasimiana na Vladmir Lenin.

Trotsky alipendekeza dhana ya ‘mapinduzi ya kudumu’ kuelezea jinsi mapinduzi ya kisoshalisti yanavyoweza kutokea katika nchi zisizokuwa na ubepari mpevu.

Huku kwetu ‘mapinduzi daima’ inatumiwa kama dhana ya kihuni, ya kubagua watu kikabila au kisiasa. Wenye uchu wa madaraka wanazificha dhamiri zao ovu nyuma ya ‘mapinduzi daima.’

Hashil Seif na Mapinduzi ya Zanzibar walizaliwa tarehe moja. Januari 12, 1964 Hashil alitimia miaka 24. Alikuwa ameshapikika kisiasa na alikwisharudi Zanzibar kutoka Cuba. Alikuwa ni mmoja wa vijana wachache waliokuwa na ujuzi wa kutumia silaha na waliokuwa na nadharia za kimapinduzi.

Siku ya Mapinduzi alipewa vijana wapatao 15 awafunze kutumia silaha. Pia aliamrishwa na Maalim Aboud Jumbe akiteke kituo cha mawasiliano cha Cable & Wireless (ilipo sasa Serena Hotel). Aliowaongoza walikuwa pamoja na Adam Mwakanjuki na Kadiria Mnyeji, mfuasi mwengine wa Umma Party.

Jukumu jengine alilopewa Hashil pamoja na mwenzake Amour Dugheish aliyekuwa naye Cuba ni kukiteka kituo cha polisi cha Malindi. Hiyo ilikuwa kazi pevu kwani palizuka mapigano makali hapo.

Aidha Hashil alikuwa katika kikundi kilichoongozwa na Hamed Hilal kuiteka jela ya Kiinua Miguu. Walikuwa pamoja na Dugheish, Rahatileil, Tahir Adnan na Tahir Ali Salim.

Hii leo Hashil Seif akikaa na kuyatafakari yote hayo yaliyopita huingiwa na uchungu kuona jinsi Mapinduzi yalivyopotoshwa na Zanzibar ilivyopoteza mamlaka yake.

I wapi Zanzibar ikilinganishwa na Cuba? Chini kabisa. Cuba ina madaktari Zanzibar. Kwa hakika, ina madaktari na wauguzi wapatao 50,000 katika nchi 60. Isitoshe, Cuba inaongoza duniani kupambana na maradhi ya ebola.

Madaktari wa Cuba wamewatibu bure wagonjwa wa macho milioni tatu katika nchi 33. Hata Mario Teran, sajenti wa Bolivia aliyemuua Che Guevara kwa kuamrishwa na shirika la ujasusi la Marekani la CIA, miaka 40 baadae alifanyiwa operesheni ya macho na madaktari wa Cuba. Alikuwa haoni na sasa anaona.

Sisi Zanzibar tuna nini cha kujivunia na kaulimbiu ya ‘mapinduzi daima’?

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s