ESCROW: Ikulu yazidi kumweka kiporo Muhongo

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Picha: Mwananchi
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo. Picha: Mwananchi

Dar es Salaam/ Zanzibar. Licha ya watu mbalimbali kutaka Rais Jakaya Kikwete kumwajibisha Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuhusiana na sakata la fedha za escrow, Ikulu imesema suala hilo litatolewa uamuzi wakati wowote baada ya mapumziko ya sikukuu.

Hivi sasa Rais yupo katika mapumziko ya Sikukuu za Krismasi inayosherehekewa Desemba 25 kila mwaka na Mwaka Mpya itakayofanyika Januari Mosi.

Akizungumza na wazee wa Dar es Salaam Desemba 22 mwaka huu, Rais Kikwete alisema amemweka kiporo waziri huyo hadi atakapopata ufafanuzi wa mambo kadhaa na kwamba atakapojilidhisha ataujulisha umma.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue aliliambia gazeti hili jana kuwa Rais Kikwete bado hajakamilisha kulishughulikia suala hilo na kwamba litakapokuwa tayari wananchi watajulishwa hatua alizozichukua.

“Unakumbuka Rais alichosema? Bado analifanyia kazi, atakapomaliza tu mtajulishwa, sasa hivi ni kipindi cha sikukuu,” alisema Sefue.

Profesa Muhongo

Hata hivyo, Profesa Muhongo alipotakiwa kuzungumzia shinikizo linalotolewa la kutaka ajiuzulu kabla ya Rais Kikwete kutoa uamuzi wake, aliliambia gazeti hili jana kwa simu kuwa; “Mimi sasa sitaki kuzungumza na waandishi, mambo yangu yote wapo watu ambao wanaweza kuyazungumzia.”

Hata hivyo, katika hotuba yake, Rais Kikwete aliagiza kuchukuliwa hatua kwa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma kuhusu ushiriki wake kwenye kashfa hiyo.

Siku iliyofuata, Sefue alimweka ‘kando’ Maswi na kumteua Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Ngosi Mwihava kukaimu nafasi hiyo hadi uchunguzi utakapokamilika.

Kutokana na kuchelewa kutekelezwa kwa maazimio ya Bunge yaliyotaka viongozi hao kuwajibishwa, Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeahidi kuwasilisha hoja bungeni ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu na kufanya maandamano nchi nzima.

Mpaka sasa viongozi watatu wameshakumbwa na dhoruba inayotokana na sakata la escrow baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema, kung’olewa kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka na kuwekwa kando kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Maswi.

Wapinzani Zanzibar wakoleza moto

Vyama vya upinzani Zanzibar vimeshangaa kitendo cha Rais Kikwete cha kutomwajibisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wakati huko nyuma kuna mawaziri akiwamo Waziri Mkuu waliwajibika kwa makosa yaliyofanywa na watendaji wao.

Katibu Mkuu wa Chama cha Tadea, Juma Ali Khatibu alisema kwamba kuna viongozi wengi ambao walilazimika kujiuzulu kwa makosa ambayo hawakuhusika lili kulinda misingi ya uwajibikaji wa pamoja na kushangaa serikali kuendelea kumlinda Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wakati kashfa hiyo imetia hasara taifa baada ya wahisani kusitisha misaada yao.

Alisema kwamba kama Rais Kikwete ameamua kumuachia Waziri Mkuu kuendelea na wadhifa wake wakati umefika kwa Serikali kuwaomba radhi viongozi wote ambao walijiuzulu nyadhifa zao kwa makosa ya wengine.

Upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed alisema kwamba licha ya kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, hakuhusika kuchota fedha hizo. lakini alitakiwa kujiuzulu ili kulinda heshima yake na kupunguza hasira za wananchi.

“Kwa heshima ya misingi ya Utawala bora Kiongozi hata kama hukuhusika moja kwa moja, unalazimika kuwajibika kulinda dhana ya uwajibikaji wa pamoja.” alisema Mohamed.

Upande wake Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani Abdalla alihoji ni kigezo gani kilichomfanya Mzee Ali Hassan Mwinyi akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Abdallah Said Natepe (marehemu), Shamsi Vuai Nahodha, Dk  Emanuel Nchimbi na Balozi Khamis Kagasheki wajiuzulu lakini  Pinda abaki katika  Ofisi za umma.

Mwinyi hakuwapo  wakati mauaji yaliotokea mkoani Shinyanga, Natepe hakujua kama kina Pius Lugangira, Hatibu Gandhi na Christopher Kadego  waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhaini kama wangetoroka katika Gereza la Ukonga.

Nahodha, Dk Nchimbi na Balozi Kagasheki pia hawakuhusika wala kufika katika eneo la utesaji wa watu wakati utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili.

Bimani alisema kwamba viongozi wote walioguswa na kashfa ya escrow wanatakiwa kufukuzwa, kushtakiwa na mali zao kutaifishwa na Serikali na kusisitiza kama serikali itashindwa kazi hiyo itafanywa na Ukawa mara baada ya kuingia madarakani mwakani.

Makamu Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, Ambar Khamis Haji alisema kwamba maamuzi ya Rais Kikwete yameshindwa kumaliza kiu ya Watanzania  wengi waliokuwa wakisubiri kuona viongozi waliohusika na kashfa ya escrow wanafukuzwa na kufikishwa mahakamani na mali zao kutaifishwa.

Alisema kinachoonekana sasa Serikali imeamua kuwalinda wahalifu, kitendo ambacho hakitasadia kujenga misingi ya utawala bora pamoja na kufanikisha vita dhidi ya rushwa na ufisadi.

Haji alisema kwamba ni jambo la kushangaza Rais Kikwete amekuwa mzito kutekeleza uamuzi ya Bunge, wakati Serikali ni sehemu ya bunge na ilishiriki katika kupitisha maazimio hayo baada ya kamati za uchunguzi kuwasilishwa ripoti za uchunguzi.

Chanzo: Mwananchi

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s