Hutuba ya Dk Shein kwenye mahafali ya SUZA

Mwanafunzi bora wa mahafali ya 10 Chuoni hapo Najat Zahor Said akipokea zawadi kutoka kwa Mkuu wa Chuo hicho Dkt.  Ali Mohamed Shein.
Mwanafunzi bora wa mahafali ya 10 Chuoni hapo Najat Zahor Said akipokea zawadi kutoka kwa Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Ali Mohamed Shein.

Ni dhahiri kuwa kila uchao Chuo hiki kinazidi kusonga mbele kwa kasi ya kuridhisha. Jambo hili linadhihirishwa kwa kuendelea kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao wanahitimu na ongezeko la fani za wahitimu ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Itakumbukwa kuwa Mahafali ya Kwanza yalitoa wahitimu wasiozidi 60 katika fani moja. Leo nimefarajika sana kusikia kuwa idadi ya wahitimu wetu imeongezeka hadi kufikia 741 katika nyanja 12. Jambo la kufurahisha zaidi ni kuwa sehemu kubwa ya wahitimu wetu ni wanawake ambao ni sawa na asilimia 64.

HOTUBA YA MKUU WA CHUO KIKUU CHA TAIFA CHA ZANZIBAR AMBAYE PIA NI RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI; MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN KATIKA MAHAFALI YA KUMI
YA SUZA TAREHE 20 DISEMBA, 2014

Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,
Mheshimiwa Waziri Wa Elimu na Mafunzo ya Amali,
Waheshimiwa Mawaziri,
Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi,
Mheshimiwa Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Cha Taifa Cha Zanzibar,
Mheshimiwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Taifa cha Zanzibar,
Ndugu Wahadhiri na Wafanyakazi wa Chuo hiki,
Ndugu Wanafunzi,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.

Assalam Aleikum,
Kwanza, namshukuru Mwenyezi Mungu (SW), Mwingi wa Rehema na Utukufu kwa kutujaalia kukutana katika mahafali haya ya kumi ya Chuo Kikuu cha Taifa Cha Zanzibar tukiwa wazima wa afya na wenye furaha nyingi.

Kwa furaha kubwa napenda kuchukua fursa hii kuushukuru Uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika Sherehe za Mahafali haya. Nami kwa nafasi yangu ya Mkuu wa Chuo nakushukuruni wageni nyote kwa kuhudhuria kwa wingi katika hafla hii na nakwambieni karibuni sana.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Naupongeza uongozi wa chuo kwa uamuzi wa busara wa kufanya sherehe za Mahafali ya Kumi kwa namna ya pekee, ili kuonesha lengo la kuimarika kwa chuo hiki katika kipindi cha miaka kumi tangu kilipoanza kutoa wahitimu mbali mbali. Kupitia sherehe hizi; zilizofanywa Unguja na Pemba kwa muda wa wiki nzima nina matumaini kuwa wananchi wameweza kushuhudia namna Chuo kikuu cha SUZA kilivyoweza kuimarika kitaaluma, kufanya tafiti na utoaji wa huduma mbali mbali kwa jamii.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUZA Prof. Idriss Ahmad Rai akisoma risala ya Chuo katika mahafali ya 10 ya Chuo hicho.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha SUZA Prof. Idriss Ahmad Rai akisoma risala ya Chuo katika mahafali ya 10 ya Chuo hicho.

Aidha, natarajia kwamba wananchi wamepata fursa nzuri ya kuelewa mwelekeo wa chuo na wao kutoa maoni yao kupitia makongamano na vikao vilivyofanyika sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba. Hii ni hatua nzuri kwani inakisaidia Chuo kubaini mahitaji ya jamii na kutafuta mbinu za kuyafanyia kazi. Mahafali haya ya Kumi yanathibitisha kuwepo kwa mafanikio makubwa na tuna haki ya kujipongeza kwa mafanikio yote haya. Hongereni sana.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Napenda ifahamike kwamba juhudi tunazozichukua za kukiimarisha chuo hiki ni utekelezaji wa wajibu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kama ilivyoelekezwa kwenye Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984. Ibara ya 10 ya Katiba ya Zanzibar inafahamisha kwamba:

Kwa madhumuni ya kuendeleza umoja na maendeleo ya watu na ustawi wa jamii katika nchi itakuwa ni wajibu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar:-

(f) Kuhakikisha kuwa zipo huduma za kutosha za kiafya kwa watu wote, zipo fursa sawa na za kutosha za kielimu katika madaraja yote na kwamba utamaduni wa Zanzibar unalindwa, unaimarishwa na unaendelezwa.

Kwa mafanikio tunayoendelea kuyapata katika kutekeleza wajibu huo, napenda kuchukua fursa hii kwa niaba ya wananchi wote wa Zanzibar, kukupongezeni viongozi, wahadhiri na wafanyakazi wote wa Chuo Kikuu cha Zanzibar kwa jumla, kwa juhudi kubwa mnazozichukua katika kuimarisha taaluma chuoni hapa. Kadhalika, natoa pongezi kwa viongozi na wananchi wengine wote ambao kwa namna mbali mbali wamekuwa mstari wa mbele katika kufanikisha dira na dhamira ya kuwepo kwa Chuo hiki. Aidha, nakupongezeni wahitimu wote kwa kuthamini na kutumia vyema fursa zinazoandaliwa na Serikali yenu kwa kufanya jitihada za kutosha zilizokuwezesheni kufaulu vizuri. Hongereni Sana.

Baadhi ya wahitimu wa Chuo hicho wakimskiliza Mkuu wa Chuo (hayupo pichani) baada ya kutunuku shahada zao.
Baadhi ya wahitimu wa Chuo hicho wakimskiliza Mkuu wa Chuo (hayupo pichani) baada ya kutunuku shahada zao.

Napenda kuwahakikishia wananchi wote kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha kuwepo kwa fursa za kutosha za elimu kwa kuimarisha vyuo vyetu ili viwe ni miongoni mwa vyuo bora Barani Afrika. Tumejidhatiti na hili linawezekana. Wahenga walisema “ Penye nia pana njia”.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Ni dhahiri kuwa kila uchao Chuo hiki kinazidi kusonga mbele kwa kasi ya kuridhisha. Jambo hili linadhihirishwa kwa kuendelea kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi ambao wanahitimu na ongezeko la fani za wahitimu ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Itakumbukwa kuwa Mahafali ya Kwanza yalitoa wahitimu wasiozidi 60 katika fani moja. Leo nimefarajika sana kusikia kuwa idadi ya wahitimu wetu imeongezeka hadi kufikia 741 katika nyanja 12. Jambo la kufurahisha zaidi ni kuwa sehemu kubwa ya wahitimu wetu ni wanawake ambao ni sawa na asilimia 64.

Kuwepo kwa idadi kubwa ya wahitimu wanawake katika taasisi mbali mbali za elimu ya juu ziliopo nchini hasa katika miaka ya hivi karibuni ni mafanikio ya jitihada za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuimarisha usawa wa kijinsia katika fursa na shughuli mbali mbali za maendeleo. Hongereni akinamama kwa kuzichangamkia fursa zinazotolewa na Serikali yenu. Haya ni mafanikio ya kujivunia tukitambua kuwa vyuo vingi, hasa Barani Afrika, havijafikia hata idadi sawa ya wahitimu wanawake na wanaume.

Kadhalika, nimeridhishwa na fani mpya za wahitimu zinazoongezeka mwaka hadi mwaka kama ilivyobainishwa na Makamu Mkuu wa Chuo. Kwa mwaka huu tunashuhudia kuongezeka kwa wahitimu wa fani mbili ambazo ni Diploma ya Kazi za Jamii; iliyoanzishwa miaka miwili iliyopita na Shahada ya Kiswahili na Ualimu, iliyoanzishwa miaka mitatu iliyopita. Wataalamu katika fani mbili hizi ni muhimu sana na tumewapata kwa wakati mzuri. Matumaini yetu ni kuwa wahitimu wa fani ya kazi za jamii watakuwa ni chachu ya mabadiliko na watatusaidia katika kukabiliana vyema na changamoto za ustawi wa jamii ziliopo nchini kwetu.

Mwanafunzi bora Najat Zahor Said ambae amehitimu Shahada ya Sayansi na Elimu akipongezwa na mmoja wa wageni walikwa kwa kushinda nafasi ya kwanza kati ya wanafunzi 741 walio hitimu masomo yao mwaka huu.
Mwanafunzi bora Najat Zahor Said ambae amehitimu Shahada ya Sayansi na Elimu akipongezwa na mmoja wa wageni walikwa kwa kushinda nafasi ya kwanza kati ya wanafunzi 741 walio hitimu masomo yao mwaka huu.

Aidha, wahitimu wa Shahada ya Kiswahili na Ualimu watasaidia katika kuimarisha lugha ya Kiswahili na utekelezaji wa dhamira yetu ya kuifanya SUZA kuwa ni chem chem ya lugha hiyo. Ninafurahi sana pale mnaponiarifu kwamba mmejidhatiti kuifanyia kazi rai niliyoitoa ya kuifanya SUZA kuwa “Oxford ya Kiswahili”. Tuendelee kuitekeleza mikakati tuliyokwishajipangia kwa kutambua kuwa jambo hili linawezekana. Naamini kwamba hakutokuwa na PhD ya Kiswahili itakayokuwa bora zaidi ya ile itakayotolewa na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Ni jambo la kujivunia na kutia moyo kwamba hivi sasa kumejitokeza mahitaji makubwa ya Walimu wa Kiswahili hapa Afrika Mashariki na sehemu nyengine nyingi duniani. Hadhi ya Kiswahili ambayo ni lugha ya urithi wetu hapa Zanzibar imekua sana na hivi karibuni Jumuiya ya Afrika Mashariki imeanzisha Kamisheni ya Kiswahili ambayo Makao Makuu yake yatakuwa Zanzibar.

Ni wajibu wetu kuziendeleza jitihada za kuikuza na kuisoma lugha yetu ili tuweze kulimiliki soko la ajira linalotokana na lugha hii. Lazima tujitambue kuwa sisi tuna nafasi kubwa katika kuufundisha ulimwengu lugha hii kwa usahihi wake. Kwa hivyo, ni muhimu kwa uongozi wa chuo kuweka na kutekeleza mikakati madhubuti ya kujitangaza katika vyuo na taasisi mbali mbali zenye mahitaji ya wataalamu wa Kiswahili duniani. Hatua hiyo, itasaidia sana kuwatafutia nafasi za ajira wahitimu wetu pamoja na kueneza na kuitangaza lugha na utamaduni wetu.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Inafahamika kwamba jukumu kubwa la Vyuo Vikuu, hasa vya Serikali, ni kutoa taaluma inayolenga katika kurahisisha utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa jamii au Serikali inayohusika. Kwa mtazamo huu, napenda kuuhimiza uongozi wa chuo kuwa utanuzi wetu wa mitaala, ufundishaji wetu pamoja ufanyaji wa tafiti zetu uelekezwe katika kutoa michango na rai mbali mbali zinazochangia na kurahisisha utekelezaji wa Mipango yetu Mikuu ya Serikali ikiwemo Dira ya Maendeleo ya 2020, MKUZA II pamoja na malengo mengine yaliyowekwa na Jumuiya za Kimataifa kama vile Malengo ya Milenia. Imani yangu ni kuwa uongozi wa SUZA daima unalizingatia suala hili wakati unapotaka kuanzisha fani mpya, isipokuwa napenda kulisisitiza kutokana na umuhimu wake.

Professa Idrissa Rai Dk Maryam Jaffar akiwa pamoja na Dk Mohammed Hafidh katika picha ya pamoja na wahitimu wa chuo hicho
Professa Idrissa Rai,  Dk Maryam Jaffar akiwa pamoja na Dk Mohammed Hafidh katika picha ya pamoja na wahitimu wa chuo hicho

Ndugu Wageni Waalikwa,
Mwaka jana nilivutiwa sana na taarifa iliyoeleza kuwa Chuo hiki kilikuwa kimeanzisha fani tisa mpya za masomo katika viwango tofauti. Nimefurahi kutambua kuwa mwaka huu Chuo kimeanzisha mafunzo katika fani nyengine sita kama ilivyoelezwa kwenye Hotuba ya Makamu Mkuu wa Chuo.

Imeelezwa kwamba Chuo kimeanzisha Shahada mbili za Uzamili katika masomo ya Kiswahili (MA Kiswahili) na masomo ya Utawala wa Biashara (MBA), Shahada mbili katika masomo ya Usimamizi wa Utalii na Masoko (Bachelor of Arts in Tourism Management and Marketing) na masomo ya Sayansi yanayohusiana na matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), katika kufundishia (Bachelor of Science and IT with Education). Vile vile, Chuo kimefanya uamuzi sahihi wa kuanzisha fani mbili za Stashahada ya Ualimu katika Elimu Mjumuisho na Mahitaji Maalumu na Stashahada ya Elimu ya Michezo. Mabadiliko haya yanayofanywa na uimarishaji wa mitaala ni tafsiri ya vitendo vya kauli mbiu ya Chuo ya kuchochea mabadiliko ya jamii.

Ni wazi kwamba fani hizi zote zilizoanzishwa zitatoa msukumo mkubwa katika kukidhi mahitaji ya wataalamu tuliyonayo katika sekta zinazohusiana na fani zilizoanzishwa. Ni muhimu kwa maendeleo ya uchumi wetu kupata wataalamu wa kutosha katika sekta ya utalii ambayo ndiyo muhimili wa uchumi wetu kwa kutupatia fedha za kigeni na tegemo kubwa la ajira kwa wananchi walio wengi hivi sasa. Ni matarajio yetu kuwa masomo ya utalii yataongeza tija kwa wananchi wetu kwa kukuza ubunifu na kuwapa mbinu mpya zitakazowafanya kuwa wajasiriamali na wawekezaji, badala ya kutegemea kuajiriwa.

Vile vile, Wahitimu wa mafunzo ya matumizi ya TEHAMA katika kufundishia watatusaidia kuimarisha mbinu za ufundishaji na kuiwezesha Zanzibar yende sambamba na mabadiliko ya sasa ya haraka ya Sayansi na Teknolojia.

Kadhalika, wahitimu wa mafunzo ya walimu wa mahitaji maalum yataimarisha uwezo wetu wa kutoa elimu kwa watu wenye ulemavu ambao wanahitaji mbinu mbadala za kujifunza. Kwa hali ilivyo hivi sasa, mbinu hizi za kusomesha watu wenye mahitaji maalum zinapatikana katika maeneo ya miji tu, hivyo programu hii itatoa wataalam watakaosaidia maeneo mengi ndani ya jamii yetu.

10885262_10204107328816905_485096858330982679_n

Ndugu Wageni Waalikwa,
Naupongeza uongozi wa Chuo kwa kuanzisha Mafunzo ya michezo kwa kutambua kuwa michezo ina nafasi muhimu katika kujenga afya na kuibua vipaji vya michezo vya wanafunzi wetu. Inasikitisha kuona kuwa kwa muda mrefu somo la michezo lilikuwa halifundishwi katika Skuli zetu kutokana na ukosefu wa wakufunzi. Matumaini yangu ni kuwa kupatikana kwa wakufunzi wa michezo kutasaidia sana utekelezaji wa mipango tuliyonayo ya kurejesha vugu vugu la michezo maskulini. Kadhalika wakufunzi hao wa michezo watasaidia jitihada za kuimarisha michezo nchini, ili Zanzibar iweze kufanya vizuri kwenye mashindano ya michezo katika ngazi za Kimataifa kama ilivyokuwa hapo zamani.

Vile vile, nakipongeza chuo kwa kuendelea kuandaa mipango ya uanzishaji wa Skuli ya Uhandisi wa Mafuta (Petroleum Engineering), ambayo naelewa kuwa imefikia hatua nzuri. Maamuzi hayo ni muhimu katika kuisadia Serikali kutekeleza dhamira yake ya kuimarisha sekta ya nishati ambapo tayari Serikali imeshasaini mikataba na baadhi ya Kampuni kwa ajili ya kuimarisha sekta hiyo, likiwemo suala la uchimbaji wa mafuta na gesi. Ni jukumu la Chuo kuwa na mpango wa aina hii na kuangalia mambo muhimu ya maendeleo kwa upana zaidi. Dhamira yetu ni kuhakikisha kwamba tunatoa mafunzo katika nyanja zote muhimu kwa maendeleo yetu. Serikali inathamini sana jitihada hizi za chuo na itaendelea kuziunga mkono kwa kila hali. Sote tuamini kuwa maendeleo ya nchi yetu katika nyanja zote yatategemea sana nguvu kazi yenye elimu na maarifa ya kutosha.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Tunaelewa kwamba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar wanalifanyia kazi agizo la Serikali la kuziunganisha SUZA na Taasisi tatu za Elimu ya Juu hapa Zanzibar. Lengo letu ni kukiimarisha zaidi SUZA na kukuza taaluma inayotolewa na taasisi zetu hizi muhimu.

Nimefurahi kusikia kuwa zoezi hili liko hatua za mwisho kwa Chuo cha Taaluma ya Sayansi za Afya kilichoko Mbweni, na Taasisi ya Maendeleo ya Utalii ya Maruhubi. Kwa Taasisi ya Uongozi ya Fedha iliyoko Chwaka bado kuna kazi za ziada ambazo zinahitajika kufanywa ili kufikia azma hiyo. Serikali inaendelea kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa zoezi hili kwa kutambua kuwa kukamilika kwake kutasaidia katika kuimarisha elimu na kupandisha hadhi ya vyeti vya wahitimu wetu wakati wakimaliza masomo yao, jambo ambalo ni muhimu katika kutafuta ajira ndani na nje ya nchi. Kwa mara nyengine, nahimiza zoezi hili lifanywe kwa makini ndani ya wakati uliopangwa ili tuweze kupata mafanikio tunayoyatarajia.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Nikiwa Mkuu wa Chuo, nimeridhishwa sana na dhamira na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Chuo hivi sasa za kuimarisha shughuli za utafiti na ubunifu. Nimefurahishwa na maelezo aliyoyatoa Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Idris Rai, kuwa chuo kimebainisha maeneo ya vipaumbele ya taaluma na tafiti na kuwa maeneo hayo yamewekwa kwa kuzingatia mipango yetu ya maendeleo na mahitaji ya jamii yetu. Hili nalo ni jambo muhimu kwani kutokana rasilimali chache tulizonazo hatuwezi kufanya kila kitu, jambo la busara ni kutafuta maeneo muhimu na tukaweka nguvu zetu katika maeneo hayo.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Nasaha zangu kwa Uongozi wa SUZA ni kuendelea kujenga uwezo wa kufanya tafiti kwa wafanyakazi wake kwa kutumia fursa mbali mbali ziliopo. Hii ni pamoja na kushirikiana na vyuo mbali mbali duniani vyenye wataalamu waliobobea katika tafiti. Naelewa kuwa Chuo kimekuwa kinaingia kwenye maelewano (MoU) na vyuo vyengine au kushirikiana na taasisi nyengine za utafiti kwa nia ya kujenga uwezo wa wanataaluma wake, nasaha zangu kwenu ni kuyatumia mashirikiano hayo ipasavyo ili Chuo kifaidike.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Kwa mara nyengine, napenda kuuhimiza uongozi wa chuo kufanya kazi kwa karibu zaidi na Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais pamoja na Tume ya Sayansi na Teknolojia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (COSTECH) katika kuhamasisha na kuimarisha ufanyaji wa tafiti pamoja na kukuza ubunifu ili kuongeza kasi ya maendeleo nchini. Napenda kukuhakikishieni kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za kufanya tafiti kwa kutekeleza ahadi yake ya kuongeza bajeti kwa shughuli za utafiti kila mwaka na kila hali itakaporuhusu.

Kadhalika, napenda kuagiza kuwa SUZA iendelee na utamaduni wake wa kuzishirikisha taasisi za Serikali katika mafunzo mbali mbali yanayofanyika Chuoni kupitia miradi iliyopo kila inapotokea fursa hiyo. Utamaduni huu unasaidia kujenga uwezo wa watendaji wa taasisi zinazoshirikishwa na kujenga mahusiano mema kati ya Chuo na taasisi hizo. Ni muhimu kufahamu kwamba ili juhudi zetu za kufanya utafiti ziwe na tija, lazima tuhakikishe kuwa matokeo ya tafiti zinazofanywa yanafikishwa kwa watafiti mbali mbali watakaoyatumia matokeo hayo na kuyafanyia kazi. Hili ni jambo muhimu kwa uongozi wa chuo kulizingatia.

Aidha, nakipongeza chuo kwa kuimarisha mahusiano na vyuo vikuu mbali mbali duniani, jambo ambalo ni muhimu katika kukitangaza na kutanua fursa za utafiti, ajira na mafunzo kwa wahadhiri, wafanyakazi na wanafunzi. Kadhalika, naunga mkono uamuzi wenu wa kuanzisha kituo cha televisheni ambacho mmejipanga kukitumia kwa utoaji wa mafunzo na vipindi vitakavyosaidia wanafunzi mbali mbali nchini. Naungana na wananchi kwa kusubiri kwa hamu televisheni yetu hii.
Ndugu Wageni Waalikwa,
Napenda kuchukua nafasi hii kukunasihini wahadhiri na wafanyakazi wote wa Chuo hiki kuwa muendelee kufanya kazi kwa bidii, ushirikiano na maarifa ili muweze kuleta mafanikio yanayotarajiwa na kuzishinda changamoto mbali mbali zinazoweza kuzikwamisha juhudi zenu.

Nakuhakikishieni kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua ya kuimarisha maslahi yenu kila hali inaporuhusu kufanya hivyo kwa kutambua kuwa “Mcheza kwao hutunzwa” nanyi mnatambua kuwa, “Haki na wajibu ni watoto pacha”.

Ni muhimu kila wakati mtambue kuwa jamii, wazazi na wanafunzi wana matumaini makubwa kwenu na wanakupendeni sana. Ni dhahiri kwamba uzalendo mlio nao ndio injini inayotusukuma hadi tukaweza kupata mafanikio haya ya kupigiwa mfano katika kipindi hiki cha miaka kumi. Nakupongezeni kuwa uzalendo huo mlionao uliowawezesha kuvishinda vishawishi mbali mbali vya kutaka kufanya kazi sehemu nyengine hasa nje ya nchi. Lakini mmeamua kufanya kazi nyumbani, kwani mtu kwao ndio ngao. Sote tunafahamu kuwa hakuna malipo wala tunzo itakayokaribia thamani ya kazi nzuri mnayoendelea kuifanya, tunamuomba Mwenyezi Muweza akujaalieni baraka, afya njema na elimu iliyobobea itakayoendelea kuwaletea tija kwa maisha ya hapa duniani na ya kesho akhera.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Nawataka wahitimu mfahamu kuwa wazazi wenu wanategemea kuwa baada ya kuigharimia elimu yenu kwa miaka mingi, sasa umeshafika wakati wa kujitegemea na ikiwezekana muanze kutoa michango mbali mbali itakayosaidia familia zenu. Kwa hivyo, kazi kubwa iliyo mbele yenu ni kutumia elimu mliyonayo kukidhi matarajio hayo katika wakati huu ambapo tatizo la ajira hasa kwa vijana limekuwa ni changamoto kubwa katika nchi zilizoendelea na zinazoendelea.
Nakushaurini kuwa msiwe na dhana ya kwamba ajira lazima iwe Serikalini. Muda hautoshi kurejea nasaha nilizozitoa tarehe 22 Novemba, 2014 kwenye Maonesho ya “Fursa za Ajira na Uzalishaji kwa Vijana” yaliyofanyika katika ukumbi wa Salama kwenye Hoteli ya Bwawani ambayo wengi wenu mlihudhuria. Hata hivyo, ni muhimu kukukumbusheni kuwa msichague kazi na muwe tayari kuchangamkia kila fursa ya ajira inayostahiki. Ni vyema mkafikiria njia bora za kujiajiri wenyewe au kujikusanya kwa ajili ya kuanzisha vikundi vya ujasiriamali kama wanavyofanya wanafunzi wenzenu wanaomaliza vyuo vikuu katika nchi mbali mbali.

Kwa lengo la kupambana na tatizo la ajira, Serikali inatilia mkazo suala la kuwashajihisha vijana kujiajiri wenyewe kwa kujenga mazingira mazuri yanayowawezesha vijana wanawake na wanaume kupata nyenzo muhimu za kuanzisha na kuimarisha biashara na shughuli nyengine za kuendesha maisha yao. Vile vile, Serikali imechukua hatua za kuanzisha mifuko mbali mbali kwa lengo la kupata fedha na kuwasaidia vijana ili waweze kujiajiri. Nakushaurini mzichangamkie fursa hii. Katika wakati huu ambao mnafungua ukurasa mpya wa maisha, nakusisitizeni kuwa msiwe na woga wa kutumia elimu mliyo nayo kwa kujaribu mambo mapya. Tukumbuke ule usemi wa mjasiriamali wa Uingereza ambaye sasa ni Milionea na maarufu kutokana na kufaulu kwa kujaribu mambo mapya katika maisha yake Bwana Richard Branson usemao:

“You don’t learn to walk by following rules. You learn by doing and by falling over”.
“Hujifunzi kwenda kwa kufuata sheria, ila hujifunza kwa kufanya kwa vitendo, ambapo hujumuisha kupepesuka au kuanguka”.

Hivyo, mafunzo mliyoyapata hapa chuoni tayari yamekufikisheni katika umri wa kwenda, inukeni na muanze kwenda. Daima msiogope kupepesuka au kuanguka, ikitokezea hivyo, inukeni na endeleeni. Kwa uwezo wa Mungu, mtaweza kupata ajira ambazo zinakidhi ndoto na matarajio yenu, Inshaallah!. Aidha, nawahimiza kwamba msitosheke na elimu mliyo nayo, muwe tayari kujiendeleza katika fani mlizosomea au maeneo mengine mapya, ikiwa fursa ya kufanya hivyo itatokezea. Kwani Waswahili wamesema, “Elimu ndio mwongozo uongozao” na “Elimu hushinda nguvu”.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Nachukua nafasi hii kuwakumbusha wale wote ambao walipata fursa ya kupata mkopo Serikalini au sehemu nyengine yoyote kwa ajili ya masomo yao kuwa waadilifu na kurejesha fedha walizokopa mara tu hali itakaporuhusu. Ni vyema wakazingatia kuwa kuna wanafunzi wengi ambao wanahitaji kupata mikopo ya aina hiyo ili nao wapate kuendelea na masomo yao kama mlivyofanya nyinyi. Ni muhimu mkatambua kuwa pamoja na kuongeza bajeti yetu ya mikopo na kuimarisha urejeshaji, bado mahitaji ya fedha za mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ni makubwa kuliko fedha zinazotengwa kila mwaka. Wito wangu wa siku zote ni kuwa waliokopeshwa wazingatie kwamba “Kukopa harusi na kulipa iwe harusi” na isiwe matanga kwa kufanya hivyo wananchi walio wengi watafaidika.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Napenda kuwakumbusha wanafunzi ambao bado mnaendelea na masomo muitumie fursa ya kuwepo hapa chuoni kwa vizuri. Huu ni wakati adhimu ambao thamani yake mtakuja kuijua baadae. Utumieni wakati huu vizuri kwa kuongeza kasi na ari ya kusoma, fanyeni yanayokuhusuni na jiepusheni na yasiokuhusuni na kwa hakika msiyafanye yasiokuhusuni. Kuweni wajasiri wa kuvishinda vishawishi vinavyoweza kuwapeleka msipopatarajia.

Ndugu Wageni Waalikwa,
Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru wale wote ambao wamekuwa wakikisaidia Chuo hiki katika kutimiza dhamira yake ya kuwa chuo bora si Afrika Mashariki tu bali ulimwenguni kote. Serikali inathamini sana michango yao ambayo imekuwa ni chachu ya maendeleo ya Chuo chetu. Nawanasihi wasichoke kufanya hivyo na Serikali itatumia juhudi zake zote kuona kuwa, kwa pamoja tunaifikia Dira ya chuo hiki.

Namalizia hotuba yangu kwa kuwapongeza tena wahitimu wote waliomaliza masomo yao kwa ufanisi. Kadhalika, nachukua fursa hii kuipongeza Jumuiya nzima ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa makubwa na kupelekea wanafunzi wetu kufaulu kwa wingi. Nakutakieni nyote kila la kheri katika kuendelea na juhudi zenu za kutimiza malengo ya Mapinduzi ya Januari, 1964 ya kuwapa wananchi elimu bora bila ya ubaguzi wowote.

Mwenyezi Mungu akujaalieni nyote afya njema na kheri ya mwaka mpya wa 2015. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aufanye mwaka 2015 uwe ni mwaka wa baraka kwetu sote na mafanikio kwa chuo chetu, wananchi na nchi yetu kwa jumla.

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s