Baraza la Biashara kufungua milango ya uchumi Z’bar

Rais wa Zanzibar DK Ali Mohamed Shein akiongoza Baraza la Biashara Zanzibar baada ya kufanyiwa mabadiliko makubwa katika utendaji wake huko katika ukumbi wa Bwawani mjini zanzibar.  Picha: Mwananchi
Rais wa Zanzibar DK Ali Mohamed Shein akiongoza Baraza la Biashara Zanzibar baada ya kufanyiwa mabadiliko makubwa katika utendaji wake huko katika ukumbi wa Bwawani mjini Zanzibar. Picha: Mwananchi

Zanzibar. Uamuzi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa wa kulifanyia mabadiliko makubwa Baraza la Biashara Zanzibar (ZBC) umefungua matumaini mapya ya kufungua milango ya kiuchumi ya uwekezaji visiwani humo.

Mpango huo utasaidia kurudisha sifa ya Zanzibar ya kuwa kituo cha Biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na kufanikisha mpango wake wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa wananchi wa Zanzibar (MKUZA).

Biashara Zanzibar ilianza kuzorota mwaka 2000 kutokana na mabadiliko ya kisera na mifumo ya kodi na kusababisha karibu watu 300 wakiwemo wafanyabiashara waliokuwa wakiingia Zanzibar kwa siku kufuata mahitaji ya bidhaa, kupungua kwa kiwango kikubwa visiwani hapo.

Wafanyabiashara wengi walikuwa wakiingia Zanzibar wakitokea katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati wakiwemo wa Mataifa ya Comoro, Kenya, Uganda, Burundi na Tanzania Bara.

Hatua ya kuimarika kwa biashara kulisaidia sana kuongezeka kwa mzunguko wa fedha kwa wananchi na kupunguza ukali wa maisha licha ya wakati huo Zanzibar kuwa katika vikwazo vya wahisani kutokana na matatizo ya kisiasa.

Watumishi wa SMZ pamoja na mishahara kuchelewa hadi miezi miwili lakini waliweza kuishi na familia zao bila ya kutetereka kutokana na mzunguko mkubwa wa fedha uliokuwepo kupitia sekta ya biashara Chini ya mipango ya Rais mstaafu Dk Salmin Amou Juma.

Mafanikio hayo ya biashara ndiyo yalifufua wazo la Zanzibar kuwa na Bandari Huru mpango ambao hadi sasa utekelezaji wake bado unachechemea, licha ya umuhimu wake katika kuinua uchumi wa Zanzibar na kuongeza kipato kwa wananchi visiwa vya Unguja na Pemba.

Hatua ya Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein kuamua kulifanyia mabadiliko makubwa Baraza la Biashara la Zanzibar (ZBC) kumefufua matumaini mapya kwa wafanyabiashara na wananchi katika kumaliza kero za muda mrefu katika sekta ya biashara na kuharakisha maendeleo yao.

Uwamuzi wa Baraza kuipitia upya hati ya sheria namba 47 ya Mwaka 2005 ya kuanzishwa kwa Baraza hilo kutasaidia kuwa na mpango kazi wa pamoja katika kushughulikia matatizo na kero za wafanyabiashara, wawekezaji na wazalishaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi Zanzibar.

Akizungumza katika Mkutano wa nane wa Baraza la Biashara Zanzibari, Dk Shein alisema kwamba chombo hicho kina umuhimu mkubwa katika kukuza sekta ya biashara na uwekezaji na kuwataka viongozi na watendaji kuondoa urasimu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Alisema kwamba kama sekta za kiuchumi zitafanya kazi kama timu mmoja kwa kuunganishwa na Baraza la Biashara la Zanzibar, milango mingi ya kiuchumi itafunguka Zanzibar na kuwanufaisha wananchi wake.

Dk Shein alisema kwamba ni mwafaka kuwapo na Kamati za kisekta za baraza ambazo zitakuwa zikifanya kazi kwa kukutana kwa mwaka mara nne kabla ya kufanyika vikao viwili vya kawaida na mkutano mkuu wa mwaka.

Mfumo mpya wa utendaji wa Baraza Kuu la Biashara Zanzibar litakuwa ndiyo mwamuzi wa mwisho katika kushughulikia kero mbalimbali za wafanyabiashara na wawekezaji pamoja na sekta nyingine za uzalishaji wakiwemo wavuvi, wakulima na wafugaji.

Hatua ya Dk Shein ya kuamua kuimalisha Baraza la Biashara kama itafanikiwa itafufua ndoto ya wananchi wengi kuona Zanzibar inarudisha hadhi yake ya kihistoria ya kuwa kituo cha biashara Afrika Mashariki.

Aidha Waziri dhamana wa Viwanda Biashara na Masoko Nassor Ahmed Mazruy alisema kwamba Baraza hilo lina umuhimu mkubwa katika kufungua milango ya kiuchumi ya Zanzibar badala ya kuendelea kutegemea zao la karafuu na sekta ya utalii katika kuimarisha uchumi wake.

Alisema kwamba Zanzibar kama nchi ya visiwa sekta ya usafiri wa anga na bandari ndiyo njia pekee ya kufanikisha mpango wa kuimarisha uchumi na kupunguza umasikini kwa wananchi wake ikiwemo kuwa na bandari huru visiwani humo.

Ikiwa ni mara yake ya kwanza Baraza hilo kukutana hadi usiku chini Mwenyekiti wake Rais Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein maazimio matatu yamefikiwa ikiwemo Zanzibar kuhakikisha inanufaika na fursa ya soko la pamoja na Afrika Mashariki (EAC) kuanzishwa Taasisi ya Mrajisi wa Kampuni Zanzibar na kuwepo kwa mkakati wa pamoja na kuondosha urasimu katika maeneo ya kiuchumi.

Mikakati ya kuimarisha sekta ya biashara na uwekezaji Zanzibar imekuja wakati muafaka huku Takwimu za mwenendo wa ukuaji wa sekta ya Biashara ukiwa umepungua kutoka asilimia 10.2 mwaka 2012 hadi aslimia 7.7 mwaka jana kutokana na sababu mbalimbali visiwani humo.

Vilevile uagiziaji wa bidhaa kutoka nje umeanguka Zanzibar kwa Asilimia 23. 3 hadi Juni mwaka jana baada ya kuingizwa bidhaa zenye thamani ya Sh2,008,051.87 Bilioni kutoka Sh271.2 bilioni mwaka 2012.

Bidhaa zinazoingizwa kwa wingi ni vyakula vifaa vya ujenzi huku vifaa vya ujenzi vikionekana kupungua pamoja na mitambo.

Usafirishaji wa bidhaa kutoka Zanzibar kuingia katika soko la Tanzania Bara unaonekana kuimarika baada ya kuongeza asilimia 123.4 baada ya kusafirisha bidhaa zenye thamani Sh501.2 bilioni hadi Juni mwaka jana, kutoka Sh224.4 bilioni mwaka 2012. Wakati uagiziaji wa bidhaa kutoka nje ukionekana kupungua kutoka Sh 79.6 bilioni mwaka 2012 hadi 61.8 bilioni mwaka jana sawa upungufu wa asilimia 22.3.

Pamoja na mikakati ya kuliimarisha Baraza la Biashara bado Serikali ya Umoja wa Kitaifa inahitaji kuchukua mikakati ya haraka dhidi ya wafanyabiashara wanaoendelea kukwepa kodi kupitia bidhaa za vyakula na vifaa vya ujenzi ikiwemo saruji kupitia bandari ya malidi Zanzibar

Mfanyabiashara Ahmada Yahya Abdulwakil alisema kwamba Wafanyabiashara wa Zanzibar wapo katika hatari ya kufilisika kutokana na Kampuni za Ujenzi za kigeni kutumia vibaya misamaha ya Kodi wanayonufaika na kuchukua bidhaa za saruji nondo na kuuza kwa bei poa katika soko la ndani visiwani humo.

Alisema kwamba Baraza la Bishara kama litatumika vizuri lina nafasi kubwa ya kusaidia kupambana na vitendo vya ukwepaji wa kodi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kwa kushirikiana na wawekezaji wasiokuwa wamiinifu katika sekta ya uwekezaji na biashara.

Upande wake Mfanyabiashara maarufu Said Salim Bakhresa alisema kwamba malalamiko ya wafanyabiashara Zanzibar kutozwa kodi mara mbili hasa katika biashara ya magari, alisema kilio hicho kinatokana wafanyabiashara wenyewe kutokuwa tayari kufuata taratibu zilizopangwa na Serikali kabla ya kusafirisha bidhaa zao.

Akifafanua Bakhresa alisema kwamba yeye mwenyewe amekuwa akisafirisha magari kwenda Tanzania Bara bila ya kupata usumbufu wowote kutokana na kuzingatia taratibu na kutaka jamii kujenga utamaduni wa kuheshimu taratibu na kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa.

Naye Kiongozi Mwandamizi wa Jumuiya ya Uwekezaji katika sekta ya Utalii Zanzibar, Simai Mohamed Said alisema kwamba Baraza hilo lina umuhimu mkubwa hasa kusaidia Serikali kuondoa urasimu katika maeneo muhimu katika sekta ya Uwekezaji na Biashara Zanzibar.

Alisema kwamba ZATI inaunga mkono msimamo wa Rais kupiga vita vitendo vya urasimu katika maeneo ya huduma za uwekezaji na kutaka watendaji na viongozi kubadilika ili kuharakisha maendeleo ya Zanzibar na wananchi wake kisha wakuu kubadilika ili kufanikisha mpango wa Serikali wa kukuza.

Alisisitiza kwamba iwapo Idara ya Uhamiaji na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) zitafanya kazi kwa mashirikiano kero nyingi dhidi ya wawekezaji zitafanikiwa kupatiwa ufumbuzi ikiwemo upatikanaji wa vibali vya ukaazi kwa wageni na usajili wa miradi ya uwekezaji Zanzibar.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s