Escrow yamng’oa Mwanasheria Mkuu Jaji Werema

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick

Dar es Salaam. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema amejiuzulu nafasi yake hiyo kuanzia jana kutokana na kuhusishwa na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow. Katika barua yake kwa Rais Jakaya Kikwete, Jaji Werema alisema ameomba kujiuzulu kwa sababu; “ushauri wake kuhusiana na suala la Escrow hakueleweka na umechafua hali ya hewa.”

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ilisema jana kuwa Rais Kikwete amekubali ombi hilo la kujiuzulu na amemshukuru Jaji Werema kwa; “utumishi wake ulioongozwa na uaminifu na uadilifu.”

Jaji Werema ambaye mara kwa mara amekuwa akitetea ushauri katika sakata hilo, amechukua uamuzi huo katika siku ya mwisho ya wiki moja iliyoahidiwa na Rais Kikwete kukamilisha uchambuzi wa taarifa za Bunge na kutoa uamuzi dhidi ya wahusika wa sakata hilo.

Uamuzi wa Werema unatokana na mazimio ya Bunge ya kutaka yeye na baadhi ya vigogo wachukuliwe hatua kutokana na madai ya kuhusika kwenye sakata la uchotwaji fedha katika akaunti hiyo.

Mwanasheria huyo alilalamikia maazimio hayo akisema hayakuwa ya haki kwa wote waliotuhumiwa na uamuzi huo ulifanywa kwa hasira na kufuata mkumbo.

Bunge liliazimia Jaji Werema kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria kutokana na kuipotosha Serikali kuhusu malipo ya Sh306 bilioni kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow, akishauri fedha hizo zilipwe kwa Kampuni ya IPTL iliyo na mkataba wa ufuaji umeme na Tanesco bila ya kukata kodi.

Jaji huyo hakusalimu amri wakati Bunge likijadili tuhuma dhidi yake, akisema anaamini alichofanya na kutaka abebeshwe msalaba. Wakati fulani alishiriki kupendekeza jinsi ya kufikia maazimio ya Bunge dhidi ya watuhumiwa.

Akizungumza na gazeti hili baada ya mazimio hayo ya Bunge Jaji Werema alisema:

“Kilichofanywa na Bunge ni mob justice (uamuzi wa kufuata mkumbo) kwa sababu hata waliowatuhumu, hawakupewa nafasi ya kujieleza. (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna) Tibaijuka na (mmiliki wa hisa za IPTL, James) Rugemalira hawakusikilizwa lakini wamehukumiwa… ilionekana dhahiri jinsi Bunge linavyoingilia uhuru wa Mahakama kwa kutoizingatia hukumu ya Jaji (John) Utamwa,” alisema Jaji Werema.

Bunge lilihitimisha mkutano wake wa kumi na sita na kumi na saba kwa mjadala wa kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow na kupitisha maazimio manane, ikiwa ni pamoja na kupendekezwa kuwajibishwa kwa Jaji Werema, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka pamoja na Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, Eliakimu Maswi.

Bunge hilo pia lilishauri kuwajibishwa kwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco na liliazimia kuwavua nyadhifa zao, wenyeviti watatu wa kamati za kudumu za Bunge ambao ni Victor Mwambalaswa (Kamati ya Nishati na Madini), William Ngeleja (Katiba, Sheria na Utawala) na Andrew Chenge (Bajeti).

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s