Wahuni wepi watakaozuiwa 2015?

Balozi Seif Ali Iddi (kulia) ambaye ni makamu wa pili wa rais wa zanzibar na mbunge wa jimbo la kitope kaskazini unguja akizungumza na spika wa baraza la wawakilishi Pandu Ameir Kificho
Balozi Seif Ali Iddi (kulia) ambaye ni makamu wa pili wa rais wa zanzibar na mbunge wa jimbo la kitope kaskazini unguja akizungumza na spika wa baraza la wawakilishi Pandu Ameir Kificho

MAKAMU wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi ameota neno dhidi ya watu aliowaita “makundi ya vijana wahuni” wakati wa uchaguzi.

Anasema serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama, itahakikisha vikundi hivyo ambavyo anasema vimeanza kuandaliwa kuja kuvuruga uchaguzi, itapambana navyo kwa nguvu kubwa.

Balozi Seif, ambaye ni mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), anatilia nguvu kauli yake hiyo kwa kukumbusha matukio yaliyotokea katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Bububu uliofanyika Septemba mwaka 2012.

Kwa bahati mbaya sana, hakueleza kwa ufasaha kilichotokea, isipokuwa kusema tu wananchi walio wengi walishuhudia vitendo vya kihuni vilivyofanya na vikundi vya vijana kujaribu kuvuruga uchaguzi.

Bila ya kutoa maelezo ya kutosha ya anachosema na lengo lake hasa, akasema, “Mambo hayo hayatokubalika kutokea tena kwenye uchaguzi mkuu ujao hapo mwakani.”

Wakati ni jambo zuri kwa maendeleo ya nchi kukemea uhuni, na kuahidi umma kuwa uchaguzi utafanyika kwa amani na utulivu, naona kiongozi huyu hajanyoosha mambo. Anaukwepa ukweli.

Anachokieleza Balozi Seif, Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, anapaswa kukijengea hoja ya ukweli ndipo atarajie kuaminiwa kuwa amekusudia kusema jambo lenye umuhimu mkubwa kwa maslahi ya nchi.

Lakini kwa vile anavyoyaeleza mambo kwa kufungafunga, wakati ukweli wa kilichotokea unajulikana maana ni jambo linalohusu maslahi ya wananchi, anathibitisha asivyo kiongozi muungwana.

Uchaguzi wa Bububu ulifanyika kwa lengo la kuwapa fursa ya haki ya kikatiba wananchi wakaazi halali wa jimbo hilo, kuchagua kiongozi mwingine baada ya aliyekuwepo kufariki dunia.

Salum Amour Mtondoo, aliyechaguliwa wakati wa uchaguzi mkuu 2010, alipoteza maisha. Ikalazimu wananchi wachague mwakilishi mwingine wa kuwasemea katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Nieleze kilichotokea. Makundi ya vijana wa CCM, chama kilichokuwa kinapigania kutetea kiti hicho cha uwakilishi, yalikuwa yamehifadhiwa kwenye matawi na maskani zake, jimboni na maeneo ya karibu.

Eneo la Kibweni, mbele tu ya lango kuu la Makao Makuu ya Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM), lipo tawi la CCM ambako siku hiyo ya uchaguzi mdogo, kama inavyokuwa kwa uchaguzi wote, kulihifadhiwa vijana.

Vijana hao inajulikana hutumika kuongeza idadi ya kura za CCM wakati mwingine kwa kupigishwa kura pale walipostahili kupiga watu halali.

Kawaida, vijana hao waitwao kila majina mabaya, kama vile mamluki na janjaweed, hutawanywa kwenye vituo vya uchaguzi.

Hawa mamluki huzungushwa kutoka jimbo hadi jimbo kusaidia CCM kushinda uchaguzi, hasa maeneo ambako kuna ushindani mkali.

Vijana waliowekwa kwenye tawi hilo la Kibweni, ndio waliomvamia muandishi wa habari na mpigapicha wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Munir Zakaria, kumjeruhi na kuvunja vitendea kazi vyake.

Munir alisimama eneo hilo kuchukua picha za vijana wakitolewa kwenye tawi hilo na kupakizwa kwenye gari maalum na kupelekwa kwenye vituo vya upigaji kura.

Kwa kuamini uovu wao ndio unafichuliwa hapo na kuanikwa hadharani, viongozi wa CCM wakaamrisha vijana wale wahuni wamvamie na kumjeruhi muandishi wa habari na kuviharibu vifaa vyake vya kazi ikiwemo kamera.

Munir anasema waliompiga pia walimuibia fedha alizokuwa amehifadhi kwenye pochi ambayo waliichomoa mfukoni mwake.

Msikilize Munir anachosema: “Nilikuwa natimiza wajibu wangu wa kikazi. Sijafanya kosa lolote wala kuvunja sheria yoyote ile ya nchi. Ninashanga wamenipiga.”

Munir alipigwa kwa sababu ya kufichua makundi ya wahuni waliokuwa wanasubiri kuzungushwa kwenye vituo vya kupigia kura ili wavuruge uchaguzi.

Mkaazi halali wa Bububu, hata mara moja hahitaji kupelekwa kituoni kwa gari au baada ya kufichwa kwanza kwenye matawi ya vyama vya siasa.

Mkaazi aliye halali anajua wapi vituo vya uchaguzi vimewekwa. Vituo vya uchaguzi jimbo hili vyote huwepo Skuli ya Bububu, kando tu barabara ya Kaskazini Unguja.

Watu wachache, wagonjwa, walemavu na wazee husaidiwa. Na watatokea majumbani wanamoishi, siyo kwenye majengo ya vyama.

Siku hiyo, Mohamed Habib Mnyaa, kiongozi katika Chama cha Wananchi (CUF), aliwaambia waandishi wa habari, “kulikuwa na mienendo mibaya iliyolenga kuvuruga uchaguzi.”

Kwa mfano, alisema, majina ya wapigakura halali yaliyomo kwenye daftari, yalitumiwa na watu wengine wakapiga kura.

Maana yake wapo wapigakura halali, walioshindwa kupiga kura kwa sababu walipofika vituoni, waliambiwa na wasimamizi wa vituo majina yao yanaonesha walishapiga kura.

Sasa, msikilize kiongozi wa CCM, Thuwayba Kisasi, alivyosema siku hiyohiyo, “Si sahihi kujitokeza watu wakazuia wengine kutumia haki yao kupiga kura.”

Ukipima kauli za wanasiasa hao wakubwa nchini, utakuta mmoja anaeleza jambo zuri la maendeleo, mwingine analaghai wananchi kwa kuficha ukweli wa kile hasa kilichotokea.

Mienendo mibaya kwenye uchaguzi nchini inalindwa na dola kwa ajili ya kusaidia CCM. Muandishi Munir alikuwa anaifichua mienendo hii mibaya kwa kupiga picha vijana waliohifadhiwa katika tawi la CCM na kuondoshwa kwa gari kupelekwa vituoni.

Bali Kisasi yeye wakati anatumia mgongo wa haki ya kila mwananchi kupiga kura, anaficha maovu ya chama chao kukusanya makundi ya mamluki na kuwapeleka vituoni kwa gari.

Ni kweli kila mwananchi ana haki ya kupiga kura. Lakini haki hiyo inapaswa kutumika pale panapostahili. Kila mpiga kura ameandikishwa kupiga kura sehemu moja na siyo kutoka eneo moja kwenda jingine.

Bado viongozi wa CCM pamoja na Balozi Seif wanajua wazi wapo wananchi mpaka sasa hawajaandikishwa kwenye daftari kwa kisingizio cha kutokuwa na kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.

Wengi wao wamenyimwa kitambulisho hicho kwa sababu za kisiasa zaidi kuliko za kisheria. Lengo la mpango huo mahsusi ni kuwakosesha haki maana wakiitumia, inaonekana watapigia kura                                           upinzani.

Siku zote za uchaguzi Zanzibar, wanakuwepo watu wakakamavu wanaozuia mamluki kuingizwa vituoni wasimohusika.

Hawa ndio anaowalalamikia Kisasi, mwakilishi wa Fuoni na Naibu Waziri katika Serikali ya Dk. Ali Mohamed Shein.

Kwa hivyo yapo makundi mawili: Kundi la watu wanaozuia mamluki kutumia haki isiyo yao vituoni. Lipo kundi la wanaofugwa kama mbuzi matawini, na kusombwa hadi vituo vya kupigia kura kule wasikohusika.

Je, Balozi Seif anawalenga wepi kati ya makundi haya mawili, kwamba ndio makundi ya wahuni anaoahidi kuwa hawataruhusiwa kuvuruga uchaguzi mwakani?

Ni wepi wavurugaji uchaguzi kati ya makundi haya? Lile linalotumika kujengea mazingira CCM, chama alicho Balozi Seif ili kishinde kwa wizi na uvunjaji sheria, au lile linalozuia mamluki kupora haki ya watu?

Wazanzibari hawapendi kuvunja sheria. Bali pia hawako tayari kuona haki yao inaporwa kihuni. Na hawaipendi serikali inayolea mfumo wa kupora haki ya wananchi.

Ndio maana huzuia kwa mikono yao. Katika kuilinda haki yao, hawaogopi viongozi wasioaminika

Chanzo: Mawio

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s