Maalim Seif: Kuweni majasiri kutetea haki zenu

Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Shariff Hamad akihutubia katika maadhimisho ya siku ya Haki za Binaadamu mjini Zanzibar
Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Shariff Hamad akihutubia katika maadhimisho ya siku ya Haki za Binaadamu mjini Zanzibar

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wananchi wa Zanzibar kuwa na ujasiri wa kuzijua haki zao za kibinaadamu na waweze kuzilinda na kuzitetea zisikiukwe na vyombo vya dola au wananchi wenyewe kwa wenyewe.
Amesema hayo leo alipokuwa akihutubuia kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Haki za Binaadamu Duniani yaliyowashirikisha wanachama wa jumuiya mbali mbali zisizokuwa za kiserikali katika ukumbi wa kituo cha EACROTANAL mjini Zanzibar.

Maalim Seif amesema vyombo vya dola hutumika kuvunja haki za binaadamu, lakini ni ukweli usiopingika wananchi wenyewe kwa wenyewe huhusika katika uvunjaji huo.

Ameeleza kuwa ni jukumu la kila upande kuhakikisha unatekeleza wajibu wake kulinda na kusimamia haki za binaadamu na elimu ienezwe kwa wananchi kote Zanzibar ili waweze kuzijua haki zao na namna ya kuzilinda zisivunjwe.

Amesema mwananchi kujua haki zake kama binaadamu ni jambo moja, lakini ujasiri wa kuweza kuzilinda ni jambo jengine, na sasa imefika wakati taasisi za kisheria kikiwemo kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar kuanzisha program maalum ya utoaji taaluma kwa jamii.

“Hebu tujiulize vile vilio vya kukiukwa haki za wafungwa na walio vizuizini, ubakaji, watu kunyimwa fursa za kujumuika na kutoa maoni yao, mateso kutoka vyombo vya dola na rushwa havisikiki tena?, alihoji Maalim Seif.

Amesema kwa mtazamo wake vitendo hivyo bado vipo na vinazidi kuongezeka kwa kasi kubwa zaidi siku hadi siku iwe Zanzibar, Tanzania Bara na Duniani, na ndio maana kuna watu hawaoni shida hivi sasa kupoteza maisha ya watu wenye ulemavu wa ngozi au wazee kwa imani za kishirikina.

Jumuiya zisizokuwa za kiserikali Zanzibar katika Tamko lao kwenye maadhimisho hayo zimesema zinasikitishwa kuona baadhi ya taasisi za kusimamia haki za binaadamu zimekuwa ndizo zinazoongoza katika kuzivunja.

Akisoma tamko hilo, Bi. Fatma Said kutoka chama cha waandishi wa habari wanawake (TAMWA) Zanzibar amesema kuna watendaji wa Idara za Mahakama, Polisi, Masheha na mamlaka zinazosimamia ardhi wapo mstari wa mbele kuvunja haki hizo.
Amesema wananchi wasiokuwa na uwezo wa kifedha, watu wenye ulemavu, watoto na wanawake, watu wanaoishi na virusi vya ukimwi na watumiaji wa dawa za kulevya ndio waathirika wakubwa zaidi katika uvunjwaji wa haki za binaadamu hapa Zanzibar.

Tamko hilo limesema hali ya udhalilishwaji watoto na wanawake Zanzibar ni mbaya kutokana na kukithirui kwa vitendo vya ubakaji na udhalilishaji, ambavyo vinachangiwa na kiwango cha juu cha rushwa miongoni mwa vyombo vya kusimamia haki na baadhi ya wanajamii.

Naye Mwenyekiti wa kituo cha huduma za Sheria Zanzibar (ZLSC) ambacho ndicho kilicho ratibu maadhimisho hayo, Profesa Chris Maina Peter amesema kuna haja jamii na wadau wote kuliona suala la kulinda haki za binaadamu ni la kila siku na sio kusubiri wakati wa maadhimisho peke yake.

Amesema jumuiya na taasisi zisizokuwa za kiserikali zina imani kubwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar itaendeleza juhudi za kusimamia haki za binaadamu, ikiwemo kuchukua hatua ya kuzirekebisha sheria zote ambazo zinaonekana kukwaza upatikanaji wa haki hizo.

Maadhimisho hayo yalihusisha maandamano ya jumuiya mbali mbali zisizokuwa za kiserikali, ambapo baadhi ya wanajumuiya walibebea mabango yenye ujumbe tafauti ukiwemo , ‘Elimu ya Sheria itolewe kwa wote’ na Katiba isiyoheshimu haki vijana hatuikubali’.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s