Escrow kuing’oa CCM

Kafulila

Kigoma. Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila amesema licha ya Chama cha Mapinduzi (CCM), kuwadharau Watanzania na kuamini kwamba hawana madhara kwa ustawi wake, kashfa ya uchotaji fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow itaking’oa chama hicho madarakani.

Kauli hiyo imetolewa wakati Rais Jakaya Kikwete akisubiriwa kuchukua hatua kutokana na mapendekezo manane ya Bunge yaliyotolewa na Ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu ukaguzi maalumu wa malipo yaliyofanyika katika Akaunti ya Escrow, uliofanywa na Mdhibiri na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) iliyowasiliwa bungeni hivi karibuni.

Akizungumza alipowasili mjini Kigoma jana, Kafulila alisema kuwa licha ya wananchi kukerwa na tabia ya wizi na ufisadi wa mali ya umma, bado CCM imeendelea kuwadharau kwa vile wananchi hao kila mara wanaunga mkono chama hicho.

“Watanzania wamechoka kulinda wezi na mafisadi, ndiyo maana wakati wa mjadala wa IPTL bungeni nimepigiwa simu nyingi na wananchi waliodai wapo nyuma yangu. Inatia faraja, nami nasema kashfa ya escrow itaing’oa CCM madarakani,” alisema Kafulila.

Alisema nchi ipo njiapanda na hali ni mbaya kwa vile licha ya uchumi kuporwa na watu wachache, Serikali imeshindwa kuwachukulia hatua stahiki wahusika na kuwafikisha mahakamani.

“CCM imeshindwa kumng’oa fisadi mmoja na kumburuza mahakamani. Sasa itawezaje kushughulikia matatizo ya Watanzania ili kuwaondoa katika matatizo?” alihoji Kafulila bila kutaja jina.

Akizungumza na gazeti hili mbunge huyo aliwataka wananchi kuikataa CCM kama kweli wanapenda maendeleo ya dhati.

Alidai kwamba sakata la IPTL limemjenga kisiasa kiasi kwamba anajisikia faraja kupigania masilahi ya umma na kuokoa mabilioni ya pesa ili jamii inufaike na matunda ya nchi.

Wiki iliyopita, mjadala kuhusu uchotwaji wa fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow uliligawa Bunge katika makundi mawili lilipojadili Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu fedha hizo hoja ikiwa; ni nani mmiliki wa fedha zilizogawanywa kwa watu mbalimbali?

Makundi yaliyodhihirika katika mjadala huo ni kundi la upinzani na wajumbe wa PAC ambalo lilitaka viongozi wa Serikali waliolegalega na kusababisha upotevu wa Sh306 bilioni zilizokuwa katika Akaunti ya Escrow wawajibishwe.

Kundi jingine lilikuwa halioni kiongozi wa kuwajibishwa kwa sababu fedha hizo hazikuwa za umma. Hili lilikuwa na wabunge wengi wa CCM, wengi wakihoji mapendekezo yaliyotolewa na PAC wakati hayamo katika mapendekezo ya CAG.

Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani alisema katika mahojiano ya PAC na CAG hakuna sehemu yoyote ambayo CAG alithibitisha kuwa fedha zile zilikuwa za umma, bali limechomekwa kinyemela na PAC. Jambo hilo lilimfanya Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe kusimama na kutoa taarifa akisema kuwa katika mahojiano yao na CAG swali la kwanza lilikuwa ni kutaka kujua kama fedha za escrow zilikuwa za nani.

Alieleza kuwa walijibiwa kuwa zilikuwa na sura tatu, kwa maana ya fedha za umma kwa sura ya kodi na fedha za umma kwa sababu mgogoro wa gharama za uendeshaji ulikuwa bado haujaamuliwa.

Mjadala huo ulilifanya Bunge kuandika historia kwa kumaliza kikao saa 4:49 usiku ikiwa ni mara ya kwanza na Spika wa Bunge Anne Makinda alilazimika kuliahirisha hadi siku ya pili kufuatia mvutano kuhusu maazimio ya Kamati ya PAC.

Katika siku iliyofutata Bunge hilo lililazimika kuunda Kamati ya Maridhioano iliyojumuisha wabumge kutoka chama tawala na upinzani na kuja na maazimio ya pamoja kutokana na Ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu ukaguzi maalumu wa malipo yaliyofanyika katika akaunti ya Escrow, uliofanywa na Mdhibiri na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG).

Akisoma mapendekezo hayo bungeni, Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe alisema: “Kwa kuwa Taarifa Maalumu ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuhusu Ukaguzi Maalumu wa Malipo yaliyofanyika Katika Akaunti ya Escrow ya Tegeta uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), umeonyesha Herbinder Singh Seth wa PAP, James Rugemalila wa Kampuni ya VIP, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Waziri wa Nishati na Madini, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), imeonyesha walihusika kwa namna moja au nyingine na kufanikisha kufanyika kwa miamala haramu ya fedha za Akaunti ya Escrow ya Tegeta, kwenda kwa kampuni za Pan African Power Solutions (PAP) na VIP Engineering and Marketing VIP…”

“Hivyo basi, Bunge linaazimia kwamba, Takukuru, Jeshi la Polisi na Vyombo vingine husika vya Ulinzi na Usalama, vichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, dhidi ya watu wote waliotajwa na taarifa maalumu ya mamati, kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya Akaunti ya Escrow, na watu wengine watakaogundulika kufuatia uchunguzi mbalimbali unaoendelea kuhusika katika vitendo vya jinai.”

Mjadala huo uliibuliwa bungeni na Kafulila, baada ya gazeti dada la Mwananchi (The Citizens kuliibua).

Akaunti hiyo ilifunguliwa kwa ajili ya kutunza fedha za gharama za uwekezaji baada ya kuibuka mzozo wa kimkataba baina ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kampuni binafsi ya IPTL ambayo iliingia mkataba wa kufua umeme na kuliuzia nishati hiyo shirika hilo la umma.

Chanzo: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s