Malcolm X alipoizuru Tanzania

Malcom X kushoto akiwa na Abdulrahman Babu kulia
Malcom X kushoto akiwa na Abdulrahman Babu kulia

Hii leo, Desemba 3, imetimia miaka 50 kamili tangu Malcolm X, mwanaharakati wa Kimarekani mwenye asili ya Kiafrika, alipokuwa mgeni wa Chuo Kikuu cha Oxford, Uingereza.  Alialikwa kushiriki katika mdahalo ulioandaliwa na Oxford Union, Jumuiya ya Midahalo ya Chuo Kikuu hicho.

Jumuiya hiyo ni medani ya midahalo yenye sifa ya “babu kubwa” nchini Uingereza. Wengi wa wasemaji wazuri wa Uingereza wenye kusifika kwa ufasaha walianzia huko.  Baadhi yao baadaye walikuwa Mawaziri Wakuu, mawaziri,  wanasiasa, waandishi mahiri au watu walioshikilia vyeo vikuu katika jamii.

Miongoni mwa watu mashuhuri kutoka nje ya Uingereza waliowahi kushiriki katika midahalo ya Oxford Union ni Askofu Mkuu Desmond Tutu wa Afrika ya Kusini, Dalai Lama wa Tibet, kiongozi wa Wapalestina Yasser Arafat, Mama Teresa, Rais wa zamani wa Pakistan Pervez Musharaf, Waziri Mkuu wa Bangladesh Sheikh Hasina na Marais wa Marekani Richard Nixon, Jimmy Carter na Ronald Reagan.

Muhimu kwa Uingereza, taifa lililogawika vibaya kitabaka, jumuiya hiyoya mijadala imekuwa ikitumiwa tangu ilipoasisiwa 1823 kama jukwaa la kuwapa mazoezi ya kujadiliana chipukizi wa kibwanyenye wenye shauku ya kujitosa katika bahari ya siasa.

Malcolm X na hao “watoto wa watu” walikuwa kama mbingu na ardhi. Wengi wakimuona kuwa ni mtu hatari. Wakimuona kuwa yeye ni tashihisi ya mapinduzi, yaani nafsi yake yote ilikuwa ni hatari kwa jamii.

Mdahalo alioshiriki Malcolm X Desemba 3, 1964ni moja ya midahalo ya Oxford Union iliyosisimua sana kiasi cha kuitwa mdahalo wa kihistoria. Wakati huo Malcolm X alikuwa na umri wa miaka 39 na alikuwa amezongwa na mengi.

Idara za kijasusi za Marekani na za nchi nyingine zilikuwa zikimuandama. Hali yake ya afya haikuwa nzuri.Kina Elijah Muhammad wa‘Nation of Islam’ walikuwa nao wakimuandama.

Hata hivyo, hakutishika. Aliendelea kuwapigania Wamarekani wenzake wenye asili ya Kiafrika.

Hoja ambayo akiitetea kwenye mjadala huwa Oxford ilikuwa: “Kutumia siasa kali kutetea uhuru si upotofu; kutumia siasa wastani kupigania haki si uadilifu.”

Umbuji na ufasaha wa Malcolm X wa kuweza kuitetea hoja hiyo katika mazingira ya Oxford Union hauelezeki.Kwa ufupi, usiku huo Malcolm X alicheza na shingo alitoa.

Waliokwenda kumsikiliza usiku ule wa Desemba 3, 1964 wakitaraji kwamba Malcolm X atatumia lugha kali na msamiati wa vitisho kuitetea hoja yake.

Walikosea.  Walimkuta akiwa na silaha nyingine kabisa: ucheshi. Aliwabwaga kwahaiba, bashasha na mvuto wake uliowafanya mara kwa mara waangue kicheko.

Juu ya umahiri wake Malcolm X alishindwa katika mdahalo huo. Alipata kura 137 na mpinzani wake, Humphrey Berkeley, mwanasiasa wa chama cha Conservative,alipata kura 228.

Hata hivyo, Malcolm X alionekana kuwa ni mtu shujaa, aliyejiamini na aliyekuwa akitafahari kwa asili yake ya Kiafrika. Muhimu zaidi akijulikana kuwa ni mtu aliyejitolea kupigania usawa na haki kwa watu wake.

Stephen Tuck, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Oxford, ameandika kitabu kizima kuhusu mdahalo huo. Kitabu hicho,‘The Night Malcolm X Spoke At The Oxford Union,’kinaeleza mengi.

Miongoni mwa yanayoelezwa humo ni kwa nini jumuiya ya Oxford Union ilimwalika Malcolm X na kwa nini alikubali kwenda. Kadhalika kitabu hicho, kilichochapishwa mwezi huu, kinaeleza jinsi Malcolm X alivyoathiriwa na ziara yake ya Oxford na jinsi yeye alivyowaathiri wanafunzi waliokuwa wakimsikiliza.

Miezi miwili kabla Malcolm X alikuwa ziarani nchini Tanzania.Kabla ya kuwasili Tanzania alikuwa amekwishazizuru nchi mbalimbali za Afrika ya Magharibi, ya Kaskazini na Mashariki ya Kati.

Ghana, ambako alizungumza na Rais Kwame Nkrumah, alikuwa akikaa kwa Cameroon Duodu, mwandishi ambaye mara nyingi mimi hushirikiana naye katika vipindi vya BBC World Service hasa kile cha kila mwaka cha mashindano cha “the African Quiz.”

Mwaka huo wa 1964 ulikuwa ni mwaka wa safari nyingi za Malcolm X, safari zilizompeleka kwingi na zilizomkutanisha na wengi — viongozi pamoja na wananchi wa kawaida. Kote alikokwenda akieleza madhila yaliyokuwa yakiwafika Wamarekani wenye asili ya Kiafrika na akiutaka ulimwengu uyaunge mkono mapambano yao.

Yote hayo yamo kwenye shajara yake ya 1964, kitabu cha kumbukumbu zake za kila siku.Kitabu hicho, ‘The Diary of Malcolm X – El-Hajj Malik El-Shabazz 1964’ kimehaririwa na Herb Boyd pamoja na Ilyasah Al-Shabazz, ambaye ni binti wa tatu wa Malcolm X.

Boyd ni mtu ninayejuwana naye kwa miaka mingi na amewahi kabla kuhariri kitabu kingine kumhusu Malcolm X. Hiki cha shajara yake ya 1964, kilichochapishwa na Third World Press, kinambainisha Malcolm X aliyepevuka na aliyekuwa na dira maalum aliyoamini kuwa itasaidia kuwakomboa Wamarekani wenye asili ya Kiafrika.

Alipokuwa Ethiopia alikutana na Otini Kambona, mdogo wake Oscar Kambona.Pia huko Addis alionana na Watanganyika wengine kadhaa ambao hakuwataja kwa majina.

Oktoba 3 alikwenda uwanja wa ndege wa Addis kuonana na Abdulrahman Babu aliyekuwa njiani kuelekea Cairo.

Babu na Malcolm X walitoka mbali. Aliyewakutanisha alikuwa Mohamed Ali Foum, mfuasi mkubwa wa Babu katika chama cha Umma Party huko Zanzibar na aliyekuwa katika Ubalozi wa Tanzania Umoja wa Mataifa.

Usuhuba wa Foum na Malcolm X ulikuwa mkubwa kiasi cha kuwafanya wawe wanatembeleana majumbani mwao. Mwingine aliyekuwa akimtembelea Foum kwake alikuwa Che Guevara, mwanamapinduzi wa Cuba.

Majuzi tu, Ashura Hilal (maarufu Ashura Babu), aliyekuwa mke wa Babu, alinikumbusha kuhusu karamu ya chakula cha usiku aliyoiandaa Foum nyumbani kwake New York. Che alikuwa amealikwa.

Baada ya chakula, Babu, Ashura na Foum wakenda Harlem kwenye ukumbi wa Audubon Ballroom ambako Malcolm X alikuwa akihutubia. Babu na Che walikuwa pia wauhutubie mkutano huo lakini Fidel Castro alimzuia Che asiende akichelea kwamba angeweza kudhuriwa na Wamarekani. Che akamuomba Babu amtolee salamu zake.

Wakati huo Tanzania ikijulikana kwa jina la‘Jamhuri ya Muungano ya Tanganyika na Zanzibar’ na ndio maana Malcolm X karibu miezi sita baada ya kuzaliwa Tanzania ameandika kwenye shajara yake kuhusu “Watanganyika” aliokutana nao wakiwa pamoja na “wanafunzi kutoka Tanganyika” aliozungumza nao Addis Ababa hadi saa nne na nusu za usiku.

Malcolm X aliwasili kwanza Zanzibar Oktoba 9. Kwa bahati mbaya alipata usumbufu kidogo kwa vile hakuwa na viza ya kuingilia Visiwani humo.

Oktoba 12 alikwenda nyumbani kwa Babu Dar es Salaam. Ameandika kuwa “Babu hakuwa na mbwembwe hata kidogo na alikuwa na mkabala wa kirafiki. Ni mtu aliye macho saa zote na aliyejitolea kwa anayoyaamini.”

Inavyoonyesha ni kwamba alikuwa akiingia na kutoka nyumbani kwa Babu na hata ofisini mwake. Chakula cha mchana akila kwa Babu.  Kwa mujibu wa Ashura Malcolm X akivipenda sana vyakula vya Kiswahili hasa samaki wa kupaka.

Oktoba 13 baada ya kuchukuwa viza ya  kuingia Nigeria kutoka Ubalozi wa nchi hiyo alitembea kwa mguu hadi ofisini kwa Babu.

Alipokuwa akimsubiri Babu amalize shughuli zake alipiga soga na katibu wake. “Alitoka Zanzibar, mcheshi na mzuri (wa sura).”  Huyo, bila ya shaka, ni Shirin Hassanali ambaye kwa muda wa miaka mingi tangu Babu alipokuwa waziri Zanzibar hadi alipokuwa waziri Dar es Salaam ndiye aliyekuwa katibu wake.

Halafu Babu akamchukuwa Malcolm X nyumbani kwake kwa chakula cha mchana.  Aliwakuta watu wengine wapatao wanne. Malcolm ameandika kwamba akijuwa ya kwamba walikuwa “wakinipima na nilisisimkwa nilipoambiwa kwamba nitakutana na Rais saa 12 za magharibi (hasa kwa vile niliambiwa mapema asubuhi ya leo kwamba haitowezekana).”

Malcolm X akaendelea kuandika kwamba alikutana na watoto wawili wa Babu, “mmojawao (msichana wa miaka minne) alifuatana na dereva kunirejesha hotelini kwangu.”

Huyo binti wa Babu alikuwa ni Salma ambaye siku hizi anaishi Uingereza na mumewe, mwananchi wa Ghana, na watoto wao. Alipokuwa na umri wa miaka mitatu, Salma aliletewa zawadi ya mtoto wa sanamu mweusi na mrefu na mkewe Malcolm X, Betty Shabazz. Zawadi hiyo alikabidhiwa mamake amchukulie.

Ilipotimu saa 12 kasorobo, Malcolm X alirudi nyumbani kwa Babu na wakafuatana kwenda Ikulu. Huko walimkuta Oscar Kambona na Mwalimu Julius Nyerere aliingia saa 12 na robo.

“Ni mtu mwerevu sana, mwenye akili, mwenye kukupoza, ni mtu mwenye kucheka na mwenye kufanya dhihaka sana (lakini kwa uzito kabisa),” ndivyo Malcolm X alivyomuelezea Mwalimu.

Kama miezi sita baada ya kuizuru Tanzania na haikutimu hata miezi mitatu baada ya ule mdahalo wa Oxford Union Malcolm X alipigwa risasi na kuuliwa mjini New York Februari 21, 1965. Aliuliwa katika ukumbi uleule wa Audubon Ballroom ambako yeye na Babu walihutubia 1964.

Chanzo: Raia Mwema

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s