Namsikia Dk. Shein akitamba, ‘Katiba itapita tu’

Shein1

Na Jabir Idrissa

Ni muhimu kusema mapema Dk. Ali Mohamed Shein anahaha. Katika uongozi wake kama Rais wa Zanzibar, yapo mambo yanamsukuma kuhangaika.

Katiba mpya inayotarajiwa ije kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikikubalika kisheria, inamtesa. Anafanya ushawishi ikubalike Kura ya Maoni itakapowadia.

Rais anajua kipindi rasmi cha kampeni bado; hata ratiba yenyewe ya utaratibu wa kura ya maoni itakayosimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) haijatangazwa.

Kampeni rasmi inakuwa ile inayotangazwa na NEC baada ya kuueleza utaratibu kwa mujibu wa Sheria ya Kura ya Maoni iliyotungwa na Bunge la Jamhuri.

Lakini si kosa kwake, kama ilivyo kwa mtu mwingine yeyote, kushawishi umma vipi waje kuiamua katiba.

Viongozi wa upinzani, wakiongozwa na vyama vinne vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wamo kazini, wakiipinga katiba pendekezwa.

Vyama vinavyounda UKAWA ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha NCCR-Mageuzi na Chama cha National League for Democracy (NLD).

Kwa mfano, msaidizi wake serikalini, Maalim Seif Shariff Hamad yupo mstari wa mbele kuhamasisha wananchi waikatae katiba mpya. Anafanya hivyo Zanzibar na Tanganyika.

Dk. Shein, akiwa pia Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, nchi iliyo sehemu ya Jamhuri ya Muungano, ikiwa ni nchi mojawapo zilizoungana, anatumia nguvu kubwa mtawalia.

Amesikika katika mikutano na viongozi wa chini wa CCM katika ziara inayokwenda kiwilaya aliyokwishaifanya Unguja na ambayo alitarajiwa kuikamilisha Pemba wiki hii.

Anafanya hivyo kwa kujua katiba hiyo haikubaliki Zanzibar. Anaihangaikia katiba iliyopitishwa kwa nguvu za unajimu na bunge lililodhibitiwa kwa zaidi ya asilimia 75 na CCM.

Wajumbe wengi walikuwa ni wanachama wake. Bado baadhi ya wengine ni watiifu kwake, japo waliingia wakiwakilisha asasi za kiraia.

Wengi wao walishindwa kuficha ukereketwa wao kwa kushuhudiwa wakitetea maslahi ya CCM kwa mipasho, kejeli na wakafuata kauli za vitisho zilizotolewa na viongozi wa chama hicho.

Sasa Dk. Shein anatumia nguvu kubwa kuipigia chapuo katiba mpya inayopendekezwa akiamini atasaidia kunusuru chama na aibu.

Anapoifanya kampeni ya nguvu Zanzibar, ndio kabisa, inaeleweka haraka ndiko kwenye upinzani na ambako inatarajiwa kwa amani haitapita. Kura ya HAPANA itatawala.

Wananchi tayari wanafahamu vya kutosha wamepelekewa katiba inayolinda maslahi ya CCM na siyo katiba yao. Kote, Unguja na Pemba, wanajua mapema katiba yao iliuliwa kwa ubabe Dodoma.

CCM ilipanga na kuratibu utekelezaji wa mkakati wa kuivuruga rasimu ya katiba mpya iliyoandikwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba, waziri mkuu mstaafu wa Tanzania.

Rafu zilianza mapema walipokuwa wanashiriki mikutano ya wazi iliyoandaliwa na Tume hiyo aliyoiteua Rais Jakaya Kikwete, ya kutoa maoni.

Wanachama wa CCM walisoma maoni yaliyoandaliwa na na kudhihirika yakiendana mmoja baada ya mmoja.

Mkakati wake ulionekana wakati wa mabaraza ya kata kwa Tanganyika, na wilaya kwa Zanzibar; ukiwa ni wakati wa kuijadili rasimu ya kwanza ya katiba mpya.

Ni katika Mabaraza haya yaliyoundwa kwa mfumo uliopangwa na Tume, mara kadhaa wana-CCM walikuwa wakizuiwa na wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, akiwemo Jaji Warioba mwenyewe, kutoa maoni yaliyoonesha kuwa yaliandaliwa.

Mpango wa CCM ulionekana wazi wakati Bunge Maalum la Katiba lilipoanza vikao kwenye ukumbi wa Bunge la Jamhuri, mjini Dodoma.

Kuliibuka mvutano wakati wa utungaji kanuni za bunge maalum, wana-CCM wakitaka kanuni zisizobana kusudi iwe rahisi kuchomeka mambo yao.

Wajumbe wao ndio waliosababisha mjadala wa aina gani ya kura wakati wa kupitisha ibara za rasimu ya katiba. Walitaka iwe ya wazi, upinzani ukapinga kwa kuhisi itatumika kutisha waliotaka mabadiliko.

Hatimaye, bunge lilipitisha utaratibu wa kura ya wazi na pia ya siri kwa atakayependa kupiga ufichoni. Upinzani ukaweka msimamo kwamba kwa wale wanaounga mkono katiba ya wananchi, wapige kura ya wazi palepale ukumbini.

Dk. Shein anajua Wazanzibari wamegundua mchezo wa CCM kutaka katiba inayoendeleza ung’ang’aniaji madaraka ambao lazima uendane na kuachia mianya ya rushwa na uzembe. Wanataka katiba inayozuia mabadiliko. Hili Wazanzibari wanalijua vizuri.

Lakini lililo kubwa, wanajua katiba iliyopitishwa na bunge ambalo CCM ililiendesha walivyotaka, baada ya UKAWA kuligomea kutokana na kukataa kutumiwa, haina maslahi kwao.

Wazanzibari wameelimika vya kutosha walichotaka hakipo. Haitoleta mabadiliko waliyotarajia. Hakuna mamlaka kamili yatakayoipa Zanzibar uwezo wa kuamulia mambo yake kwa faida ya nchi.

Katika hilo, Wazanzibari wanajua kwa uhakika kinachoitwa unafuu kwa Zanzibar kwamba eti itapata kukopa pasina kikwazo, ni ndoto ya alinacha.

Wazanzibari wameelimika kwamba wakiiridhia katiba hiyo, maana yake wameruhusu kuendelea kunyonywa na kukandamizwa. Tena, hapo itakuwa kwa mfumo uliohalalishwa kisheria.

Tatizo kubwa linaloonekana katika kampeni anayoifanya Rais ni kulazimisha, siyo kujenga hoja ili wananchi wamuamini.

Kwa mfano anasema Zanzibar haitafuti mamlaka kamili maana tayari inayo – ina bendera, wimbo wa taifa, ina nembo, ina mahakama, bunge na serikali anayoongoza. Mamlaka ya kutosha hayo!

ni anamaana kwamba yeye rais anaweza kuamua kutekeleza lolote akishakubaliana na mawaziri wake hata kwa jambo linalohusu mkopo ambao lazima upate idhini ya Serikali ya Muungano inayodhibiti utaifa?

Ni kweli ndiye Rais wa Zanzibar, lakini mbona hajafanikiwa kuitoa sekta ya mafuta kwenye orodha ya mambo ya muungano kwa miaka minne sasa?

Zanzibar ina uamuzi katika suala la sera na sheria za fedha? Usalama wa mitaji ya wawekezaji?

Dk. Shein anataka kusema hayo yatawezekana kwa kuwa Serikali ya Muungano imekuwa ikiridhia mambo yenye maslahi ya Zanzibar bila shida?

Mazoea haya yameanza lini wakati yapo matukio mawaziri wake wamedhalilishwa wanapokutana na Serikali ya Muungano?

Dk. Shein anaposema Zanzibar inayo mamlaka kamili amesahau yaliyotokea kuhusu misaada ya Oman kwa Zanzibar, mbele ya Waziri Bernard Membe?

Nimependa Rais aliposema katiba itapita tu. Angalau anathibitisha serikali ilivyojiandaa kutumia mabavu. Lakini je, rais atakuja kusema nini mabavu yatakapojibiwa kwa mabavu? Maana wasionekane maiti wasioweza kunyoosha mkono wakazuia ukandamizaji.

Nasema, mabavu hayajengi. Nguvu za dola hazitengenezi isipokuwa uasi. Wananchi wanaojengwa ukakamavu hawatakubali kunyang’anywa haki. Naogopa rais anapalilia chuki hata kura yenyewe haijatangazwa.

Maalim Seif anapoahidi kampeni ya HAPANA, inajulikana analenga kulinda haki ya watakaopiga kura hiyo, dhidi ya wasemao “Katiba itapita tu.”

Rais hatendi sawa kuapa udikteta. Ajue hapo haoneshi utawala bora au utii kwa sheria. Hapo analea uongozi varange, anapanda mbegu za udikteta. Hapo halindi maridhiano, analea uhuni kwa gharama ya uongozi mwema.

Chanzo: Mawio

Advertisements

One Reply to “Namsikia Dk. Shein akitamba, ‘Katiba itapita tu’”

  1. Shein rais Wa Zanzibar na wana ccm wote wa zanzibar wanendekeza usisiemu wanacha mambo muhimu ya utaifa, Pesa nyingi zinaibiwa Tanganyika wao kama vile haliwahusu wanachokioga ni kupoteza nafasi zao ikiwa ccm itaanguka Zanzibar.

    Ivi tuwaulize wanategemea kutawala maisha?

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s