Mamlaka kamili ya wananchi haipo Z’bar

Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein akipeana mkono na Shamsi Vuai Nahodha
Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Shein akipeana mkono na Shamsi Vuai Nahodha
Na Shariff Mbukuzi
WAZANZIBARI wapo kwenye shida kubwa. Kweli wanaye rais anawaongoza. Kweli yupo Dk. Ali Mohamed Shein, lakini, ameshughulika kwa malumbano, kuliko anavyohangaikia shida zao.

Na afadhali angekuwa analumbana na viongozi wa Civic United Front (CUF) Chama cha Wananchi, ambao ndio anaoshirikiana nao katika serikali aliyounda.
Rais analumbana na makada wenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwa kuingia katika malumbano na viongozi waliopaswa kuwa wasaidizi wake katika kutekeleza majukumu yake, ina maana Rais amechanganyikiwa.
Ikumbukwe kwamba kupitia CCM, Dk. Shein aliingia kwenye mbio za kutafuta urais. Baada ya kupitishwa kugombea, alipita kwa wananchi akitangaza yale atakayoyapa kipaumbele katika kutumikia wananchi.
Alitangaza wanachoita Ilani ya Uchaguzi, ambayo iliandaliwa na chama chake. Hao makada anaolumbana nao, ndio walioshirikiana katika kuandaa ilani hiyo.
Japo anaongoza serikali ya ushirikiano na CUF – Serikali ya Umoja wa Kitaifa – Government of Nationa Unity (GNU) – kwa sehemu kubwa serikali inatumia ilani ya CCM katika kutumikia wananchi.
Yafuatayo ndio mambo makubwa ninayoona yanawapeleka Rais Dk. Shein na makada wenzake wa CCM, katika kulumbana.
Kwanza, Dk. Shein amegundua sasa kuwa katika baadhi ya hao makada wenzake, wapo walioanza kufanya kampeni ya chini kwa chini ya kumtishia asigombee wadhifa huo kwa muhula wa pili. Wanapanga kumzuia asifikiriwe na chama kugombea tena.
Pili, anaona baadhi ya hao waliotarajiwa kuwa washirika wake katika kupigania kurudi madarakani katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwakani, wanapanda jukwaani ya siasa na kukosoa uongozi wake. Wanalaumu hakuna maendeleo yaliyotarajiwa katika huduma za jamii.
Kwa kuyajua hayo, ameanza ziara ya kikazi akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar ambako anapata nafasi ya kuwatupia shutuma viongozi hao wanaomchanganya.
Alianza wiki mbili zilizopita akihutubia viongozi wa chama ngazi ya mashina zikiwemo maskani za wakereketwa wa chama hicho. Ilikuwa ndani ya ukumbi wa Salama wa Hoteli ya Bwawani, alipowasema wanaohangaika kupita wakisema eti yeye hatogombea tena urais.
Kwa mujibu wa katiba ya Zanzibar, rais anaweza kuchaguliwa tena baada ya kukamilisha kipindi cha miaka mitano. Anastaafu akitimiza miaka kumi.
Alisema kumeibuka aliowaita “watu” wanazunguka kwa wanachama na kusema yeye hatogombea tena urais mwakani. Maana yake ni kwamba wanajitangaza kuwa wanajiandaa kumrithi.
Dk. Shein anasema hajamtuma mtu yeyote kupita akamsemea na hajapanga kufanya hivyo kwa sababu wakati wa harakati za urais haujafika. Anaujua na kuuheshimu utaratibu uliowekwa na chama wa suala hilo.
“Kama mnataka jambo kulijua mniulizeni mwenyewe. Kwanini mnanisemea. Msinisemee mwenyewe nipo,” alitoa kauli hiyo mbele ya Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai Ali Vuai miongoni mwa viongozi waandamizi wa CCM.
Ni maelezo yaliyothibitisha kinachosimuliwa kwa muda sasa kwamba baadhi ya viongozi wakubwa wameanzisha harakati za kutaka kumrithi.
Vyanzo vya habari ndani ya CCM vinasema wazi wapo hao aliowasema Dk. Shein. Mmoja ni Balozi Seif Ali Iddi, msaidizi wake mkuu serikalini, ambaye amekuwa akitajwa kueleza nia yake wakati wa  Bunge Maalum la Katiba, lililomalizika Dodoma.
Lakini yupo pia Dk. Mohamed Gharib Bilali, Makamu wa Rais wa Tanzania, anayetajwa kuwa yumo katika harakati za kuusaka urais wa Zanzibar, ikimaanisha hajasalimu amri.
Dk. Bilali, mwanasayansi gwiji wa elimu ya nishati ya atomiki, na Waziri Kiongozi Mstaafu wa Zanzibar (1995-2000), aliomba ridhaa ya CCM kugombea urais tangu 2000 alipomaliza uongozi wa awamu ya Dk. Salmin Amour Juma.
Hata mwaka 2005 wakati wa maandalizi ya uchaguzi mkuu, wakati ikitarajiwa kuwa Rais Amani Abeid Karume aliyeingia Novemba 2000, ataendelea kugombea ili kukamilisha vipindi viwili, Dk. Bilali alichukua fomu ya chama chake.
Ni hapo baadaye, alinyamazishwa kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Jakaya Kikwete katika urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Inaonekana daktari huyu hajaamini kama aliyonayo ni madaraka makubwa tu.
Dk. Shein itakuwa amegundua kwamba daktari mwenzake huyo hajakata tamaa. Anataka naye lazima aitwe Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Urais huu wa Zanzibar una utamu gani sijui mpaka inakuwa hivo?
Katika hatua nyingine isiyokuwa ya kawaida, Dk. Shein amejikuta akikosolewa na baadhi ya viongozi katika CCM. Rais anaambiwa kuwa chini ya uongozi wake hakujawa na ufanisi katika eneo la maendeleo ya huduma za jamii kama ilivyotarajiwa.
Shamsi alipohutubia wana-CCM katika mkutano uliofanyika uwanja wa Kombawapya, jimbo la Rahaleo, mjini Zanzibar, alisema hajaridhishwa na kiwango cha ukuaji wa uchumi na kwamba matokeo yake huduma za elimu na afya hazijaimarika ipasavyo.
Lakini Dk. Shein akajibu alipokuwa akihutubia wanachama katika mkutano na viongozi wa mashina na wanamaskani wa Wilaya ya Magharibi, eneo la Mfenesini, alisema wanaosema kwamba hajaimarisha huduma za jamii hawalinganishi huduma hizo zilivyo sasa na zilivyokuwa wakati ukoloni na baada ya Mapinduzi.
“Wanapita na kutoa maneno bila nadharia, hawalinganishi kiwango cha elimu, huduma za afya na kukua kwa uchumi kwa hali ilivyokuwa.. maisha ya watu yalivyokuwa…
“Zanzibar ni kati ya nchi za Kiafrika zilizofanikiwa kuyafikia malengo ya milenia kwa kiwango kikubwa.. kupambana na malaria, kunusu vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano, ujenzi wa miundombinu ya vituo vya afya, barabara, madarasa ya skuli, ajira za walimu, usambazaji wa maji safi, na kupunguza umasikini wa kipato.”
Dk. Shein amethibitisha kuwa wanaomsema ni CCM wenzake, aliposema, “Ni ajabu sana unaposikia zikitoka shutuma hizi, tena wanaotoa shutuma ni wanachama wenzetu, wengine tunao humuhumu. Wameishiwa hoja sasa wanasema bila ya kupima maneno. Hawaoni aibu kutamka mambo yanayowasuta.”
Dk. Shein pia akakanusha shutuma kwamba anaongoza nchi kibabe. Anajitetea kuwa anaongoza kwa mujibu wa katiba na kufuata mipaka ya sheria za nchi bila ya kumuonea mtu.
Ukiacha lile linalohusu ugomvi wake na makada wanaotaka kumrithi kiti hicho, shutuma nyingine zimekuwa ndio malalamiko makubwa ya wananchi. Mwingi unamopita, watu wanalalamika huduma duni za jamii.
Ni kweli kama anavyosema, vituo vya afya ni vingi sasa kuliko ilivyokuwa wakati Zanzibar ikiwa chini ya utawala wa wageni na baada ya mapinduzi. Ni kweli skuli zimeongezeka na wanafunzi wameongezeka. Ni kweli.
Ila sasa kiwango cha ubora wa huduma katika maeneo hayo, hakiridhishi hata kidogo. Na hapa ndipo ilipo tofauti kubwa ya huduma za jamii zilivyokuwa wakati ule na sasa. Huduma zilikuwa bora wakati ule ingawa idadi ya vituo vya afya au skuli ilikuwa ndogo. Lakini hata idadi ya watu nayo ilikuwa ndogo.
Zanzibar ilikuwa na skuli chache. Wanafunzi na walimu wachache vilevile. Lakini, nchi hii ipo kwenye rekodi ya kuwa moja ya nchi tatu zilizokuwa na maendeleo makubwa katika sekta hizo barani Afrika.
Kwenye elimu, Zanzibar ilikuwa ikikimbia pamoja na Ghana na Misri. Elimu ya kiwango cha kupigia mfano. Elimu ya Zanzibar ilifungamanishwa na mfumo wa elimu ya nchi kadhaa za Jumuya ya Madola chini ya Uingereza – Cambridge.
Mitihani ikichapwa Uingereza na kusafirishwa lakini haikupata kuvuja. Walikuwepo walimu wenye ujuzi na uwezo mkubwa kwa masomo ya sayansi na sanaa pamoja na dini. Zanzibar ilikuwa kitovu cha elimu na utamaduni kwa kanda ya Afrika Mashariki, Kati na Kusini.
Kiuchumi, Zanzibar ilikuwa na uchumi mkubwa. Ikilisha watu wake bila shida na ikitoa misaada kwa nchi nyingine. Zao la karafuu lilitumika vizuri kujenga uchumi na miundombinu ya mawasiliano, barabara na huduma nyinginezo.
Wakati huo, Zanzibar ilikuwa na mamlaka ya kwelikweli ya kujiongoza. Rais wake na serikali yake hawakujenga uchumi kwa kutegemea serikali nyingine zaidi ya misaada ya kawaida iliyotokana na uhusiamo mwema na mataifa na taasisi za mataifa.
Mawaziri wa Zanzibar walifanya kazi kwelikweli. Waliipenda nchi kwa ushahidi hasa siyo nadharia. Ufisadi ulikuwa ndoto. Waliojaribu kutumia vibaya madaraka walidhibitiwa mapema. Watumishi wa umma walipata sifa hadi Ulaya ya utendaji uliojaa huruma, uadilifu na weledi.
Dk. Shein leo anaongoza nchi iliyopoteza karibu sifa hizo zote. Zanzibar leo inaongozwa chini ya amri na maelekezo ya wakubwa wa CCM wanaoendesha Serikali ya Muungano. Leo CCM ndio inaamua bajeti iweje. Bajeti lazima ifungamane na Ilani ya Uchaguzi iliyoandaliwa kwa ajili ya CCM.
Bajeti inatakiwa kuzingatia hali halisi ya mambo ilivyo kwa wananchi, mahitaji yao, ahadi za serikali na viongozi wake wakuu. Bajeti ni muhimu itazame uwezo wa kukusanya mapato. Bajeti inatakiwa kutokana na mapato ya ndani ya nchi, zaidi kuliko kutegemea mapato ya misaada na mikopo.
Serikali inayopanga bajeti kwa kufikiria kwanza maamuru ya serikali ya Muungano, ambako viongozi wake tayari wanajulikana walivyojaa chuki dhidi ya Zanzibar, Wazanzibari na Uislam, haiwezi kupata bajeti ya wananchi. Itapanga bajeti ya viongozi.
Ndio maana mara nyingi bajeti inashindikana kutekelezwa. Kwanza, mapato hakuna ya kutosha, pili rushwa kwa viongozi, tatu utumishi mbovu serikalini, ulaghai na wizi uliokithiri. Siku zote bajeti inakosa kutekelezwa.
Kilicho kibaya zaidi ni pale wananchi wanaposhuhudia viongozi, wakiwemo wakubwa tu katika serikali, wanavyotumia vibaya madaraka kufisidi raslimali za nchi, kuiba mali ya umma, ikiwemo mtandao wa kulipa wafanyakazi hewa. Matokeo yake, skuli hazina vikalio, walimu wanadhalilishwa, skuli za vipaji zimeuliwa, teknohama haijatiliwa mkazo. Tofauti na Rwanda ambako teknolojia ya habari na mawasiliano imeanza kutumika kuanzia elimu ya msingi, kwetu wazo lenyewe halijaingia vema akilini mwa viongozi.
Basi hata pale Rais Dk. Shein anaposema Zanzibar inayo mamlaka yake kamili, ataheshimika tu kwa sababu amesema rais, lakini wananchi hawaamini kitu hicho. Mamlaka yanayotakiwa ni ya nchi kupanga na kutekeleza mipango yake bila ya kutazama fulani anasemaje.
Chanzo: Fahamu
Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s