CAG Profesa Assad asema moto ni uleule

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na familia ya  Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) Profesa Musa Juma Assad Ikulu jijini Dar es Salaam jana.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na familia ya Mdhibiti na
Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) Profesa Musa Juma Assad Ikulu jijini
Dar es Salaam jana.

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mpya, Profesa Mussa Assad amesema ataanza kazi kwa moto uleule ulioachwa na mtangulizi wake, Ludovick Utouh aliyestaafu.

Akizungumza jana mara baada ya kuapishwa na Rais Jakaya Kikwete Ikulu, Profesa Assad aliyeteuliwa Novemba 5 kushika wadhifa huo alisema: “Ninasubiri niingie ofisini nianze kazi… nitaendeleza yote yaliyoachwa na mwenzangu, sitatoka nje ya mstari.”

Profesa Assad alisema yuko tayari kusimamia utendaji kazi wa kisasa kwa kusimamia misingi ya ofisi yake, ili kulinda hadhi na heshima aliyopewa na Rais katika uteuzi huo.

Kuhusu Ripoti ya Akaunti ya Escrow, Profesa Asaad alisema anasubiri kukabidhiwa rasmi taarifa hiyo na maagizo yote yaliyotolewa na Bunge kwa ajili ya kutekeleza yale yaliyopo chini ya ofisi yake na kuendeleza yale ambayo yalishaanza kutekelezwa.

Alisema moja ya mambo ambayo atayafanyia tathmini na kupatia majibu ni kutotajwa moja kwa moja katika Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kama fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow iliyofunguliwa kwa pamoja na Tanesco na IPTL ni za umma au vinginevyo.

Utoh anena

Akizungumza katika hafla hiyo, Utouh alisema kuwa amemkabidhi Profesa Asaad ofisi yenye watendaji wanaofanya kazi kwa ari na ufanisi katika kutekeleza majukumu yao.Alisema amefurahishwa na uteuzi wake na kusema anaamini ataendeleza uwajibikaji na umadhubuti wa ofisi hiyo kwa manufaa ya Taifa.

Utouh alimkabidhi Profesa Asaad mwongozo maalumu wenye kurasa 78 na kueleza kwamba utampa mwelekeo wa namna ofisi hiyo ilivyo na iwapo kuna upungufu yuko tayari kutoa ushirikiano.

Spika Makinda

Akimzungumzia Profesa Asaad, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema mtikisiko uliolikumba Taifa kutokana na Kashfa ya Escrow umelifanya lijenge misingi mizuri zaidi ya kiutendaji na uwajibikaji katika kuhakikisha matumizi mazuri ya fedha za umma.

Alisema anaamini CAG mpya ataingia na mfumo wa kisasa zaidi na kusaidia kuweka miundo bora zaidi ya kuhakikisha kunakuwa na nidhamu ya hali ya juu katika kusimamia mapato na matumizi ya Serikali.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s