Nachelea tutajalazimika kujenga ukuta

Mojawapo ya bango lenye ujumbe wa kuhamasisha chuki, kama linavyoonekana hapo muembe kisonge
Mojawapo ya bango lenye ujumbe wa kuhamasisha chuki, kama linavyoonekana hapo muembe kisonge

MUDA kidogo niliwahi kupata shauku ya kujadili “uhuni” unaofanywa na baadhi ya watu wanaojinasibu nao ni Wazanzibari. Hawa ni wanamaskani wa Muembekisonge. Nia yangu ilikuwa nieleze madhara ya uhuni wanaoutenda. Niwanasihi waache mtindo mchafu wa kuandika maneno ya chuki kali dhidi ya Wazanzibari wenye asili ya Kisiwa cha Pemba.

Niwakumbushe wanamaskani hao kwamba wanafanya kitu kibaya ambacho matokeo yake yanaweza kuwa mabaya vilevile.

Wanapoandika maneno mabaya kwenye ubao wa matangazo mbele ya maskani yao, wajuwe wanaeneza chuki kwa jamii. Wanajenga picha kuwa Wapemba si watu wema, ila washenzi.

Basi wanapozishawishi chuki hizo kwa wananchi wengine kwa kuziandika kwenye ubao huo, wanamaskani hao wajuwe wanakosea sana kiutu na kisheria.

Wazanzibari hawa ni ndugu tu wa damu na hao wanaowachochea. Si wapo nchi moja yenye utamaduni mmoja unaofungamana na hulka na silka zinazofanana, chini ya serikali moja?

Sikuwahi kuiandika makala inayohusu kunasihi wana-Kisonge kutulia wakatafakari, wakajitambua na wakajiuliza ni haki kweli kueneza chuki kwa kuwasakama Wazanzibari wenzao hao?

Tatizo la Zanzibar, unahitaji kuwa na chombo cha habari cha kila siku, ili kusaidia kuelimisha umma mambo yanayohusu maisha yao, maslahi yao, viongozi wao na serikali yao.

Hamuwezi kuamini, lakini kwa muandishi aliye makini kueleza ukweli, Zanzibar inazidiwa na mambo ya kupasa kuchukuliwa hatua kuelezwa wananchi.

Mambo mengi yanatokea. Wakati mwingine hutokea matatu siku moja, au ndani ya wiki moja na yote yakahitaji kuelimishwa wananchi, ikiwemo kuwahoji wale walioyatenda au kuhusika nayo.

Ilikuwa Agosti nilipofikiria kujadili jambo hilo. Kipindi kilichokuwa na harakati za katiba mpya. Zilitawala akili za wengi. Lile ni jambo zito kwelikweli lililostahili kushughulikiwa kwa nguvu kubwa.

Jambo hili liliandamana na mipango michafu ya watawala na uchafu wenyewe uliandamana na harufu mbaya ajabu ambayo ilihatarisha neva za pua za Wazanzibari wengi kukatika.

Utafutaji wa katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uligubikwa na jitihada za kishetani zilizopaswa tu kutendwa na watu wa jamii ya shetani.

Hawa ni watu ambao kwa kukosa moyo wa hekima na busara, pia walinyimwa hisia za utu na huruma. Walichobarikiwa badala yake, ilikuwa ni kutiliwa akilini mwao chembechembe za ukatili na ufirauni.

Si uongo, kama lilivyoandaliwa na watawala tangu mwanzo, ndivyo hivyohivyo lilivoishia – mashetani hao kujiamini na hata kuthubutu kutumia elimu ya unajimu kufanikisha walichokipanga.

Ile katiba inayopendekezwa ilipita kwa nguvu za kinajimu, maana takwimu zilipangwa, zikachezewa na kupangwa tena na tena.

Zikakaliwa usiku wa manane zinavutwa kwa njia ya watendaji hao kunusa unga wa ndere ili tu wasijijue kwamba wanachokifanya ni haramu.

Pengine walijua kabisa kuwa wakitendacho ni haramu, tatizo kwao ni kwamba walijua walipewa kazi hiyo na watu waliojivika ufirauni – watu waliotokwa na hofu ya Mwenyeezi Mungu, wasiamini kamwe kuwa dhulma ni dhambi kubwa ambayo malipo yake kwa pale alipoumizwa kiumbe wake Rabbana, hulipwa duniani kabla ya mkosaji kukatika.

Leo, nimepata nafasi ya kujadili jambo hilo. Kueleza ubaya wa mtindo wa wana-Kisonge wanaopandikiza na kueneza chuki dhidi ya Wapemba. Ila nitatekeleza wajibu wangu huo wa kuelimisha umma, kwa kuanza mapema kumnasihi Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Dk. Shein nimemsikia akisema kwamba atawashughulikia watu aliowaita “wachochezi” waliopo Zanzibar. Watu aliosema wanania ya kuvuruga amani na utulivu uliopo nchini.

Ningeuliza haraka hapa kwamba hivi Dk. Shein amekusudia kuwashughulikia “wachochezi” wepi hasa? Sio hawa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliopo maskani ya Muembekisonge?

Kwangu na hakika kwa Wazanzibari walio wengi, wanamaskani hao waliojichukulia nguvu za kitume, wanaendelea kupanda na kueneza chuki kali dhidi ya wananchi ambao yeye kama rais alikula kiapo kuwalinda?

Wazanzibari wanadhalilishwa na kutishwa na Wazanzibari wenzao lakini humsikii Rais wala Makamu wa Pili, Balozi Seif Ali Iddi kugomba kuwa wanachokifanya wanamaskani hao si haki hata kidogo, na ukweli, ni kosa la jinai.

Ninaona kuwaambia kuwa warudi kwao Pemba wakaishi, au wakatafute katiba yao maana ile iliyopitishwa na bunge lililojaa ma CCM, si yao; au warudi wakatengeneze serikali yao kulekule kwao Pemba, ni kupandikiza chuki kali dhidi ya Wapemba.

Sasa mbona siwasikii viongozi wakubwa hawa wakitaharuki na kuamuru watu wao waache mtindo mbaya huo? Hapana shaka hawajakemea.

Kwa hivyo basi, kwa viongozi hao kutokemea wanamaskani wa Muembekisonge, inatafsiriwa kuwa viongozi wanaridhia kinachotendwa. Je, ni sahihi? Si kosa kisheria?

Haiwezekani kuona kitendo cha wanamaskani wa Kisonge cha kueneza chuki zilengazo watu wa Pemba, kiwe ni sahihi na wanaokitenda waonekane watu watiifu wa sheria, watu wanaostahili kupongezwa.

Wazanzibari wema wanaamini hao ni wakosaji wanaopaswa kudhibitiwa sasa kwa mujibu wa sheria. Si ipo sheria ya kudhibiti wachochezi? Basi itumike kuwakomesha waeneza chuki.

Nayasema haya leo kwa sababu ninaamini kuachia mambo haya yaendelee, si kujenga, bali kubomoa jamii. Ni kuipeleka nchi katika janga ambalo madhara yake hayatabiriki.

Dk. Shein anao wajibu wa kuongoza umma katika kuamini kuwa utawala wa sheria ndio pekee unaoijenga jamii, kinyume chake, utawala usiotii sheria na taratibu, ni balaa.

Kuendekeza uvunjaji wa sheria na kufurahia maovu, kunavutia machafuko. Gharama za machafuko anazimudu? Ni nani anaweza kutabiri athari za machafuko?

Mtindo wa serikali kulea watenda maovu, na ikawa maovu yenyewe yanalenga moja kwa moja kuwasakama wananchi, haufai hata kidogo. Sina shaka mheshimiwa, haufai.

Ona hao wanamaskani wanavotamba kwa kueneza chuki dhidi ya Wazanzibari wenzao, halafu wanachekelewa tu! Mtoto akililia wembe apewe, bali yule atapata funzo akijichinja na kutoka damu. Hawa watu wazima ni wachochezi wa kushughulikiwa vilivyo.

Dk. Shein anapaswa kutambua kwamba hata anapowaachia watu wazima wengine wa mfano wa Salmin Awadh Salmin, Haji Omar Kheri na Shamsi Vuai Nahodha wanaojitahidi kuchafua hali ya hewa, analea waovu.

Hao watatu wanajulikana wametoa matamshi ya kupinga serikali ya umoja wa kitaifa. Hawaitaki. Hii Shamsi kujidai karibuni kuwa kuna watu wanachochea vurugu, ni kujidai tu.

Labda arudi jukwaani au mbele ya vyombo vya habari aseme amejua sasa kumbe serikali ya umoja wa kitaifa imelenga kujenga umoja, mshikamano na utengamano imara kwa Wazanzibari.

Hapo ataeleweka kwa sababu anaendelea kukumbukwa kwa kampeni yake dhidi ya maridhiano.

Maridhiano ndiyo msingi wa kuundwa serikali iliyopo. Shamsi alikuwa mmoja wa viongozi wa ngazi ya juu serikalini kushawishi kupinga maridhiano wakati serikali ambayo alikuwa msaidizi wa Rais Amani Abeid Karume, ilipopeleka azimio la kutaka kufuta siasa chafu.

Nachelea itafika siku wanaoonewa watajihami. Hapo tena, tutaja lazimika kujenga ukuta baada ya kudharau kuziba nyufa.

Chanzo: Mawio

Advertisements

2 Replies to “Nachelea tutajalazimika kujenga ukuta”

    1. Kisonge WAHUNI wanakaa hapo. KWANZA MUJUE KUWA HAWANA ASILI YA UZANZIBARI 100% , PILI HATA IWE VIPI IKIWA WEWE NI MZANZIBARI ASILI HUWEZI KUMTUKANA MPEMBA NADHANI HAWAIJUI HISTORY YA ZANZIBAR WAKATAFUTE VITABU WASOME. WASIKUSHUGHULISHENI HAO TUWAFANYE KAMA MAVI YETU. MSHENZI MSHENZI TU. NA SHENI NDIE ANAEWAAMBIA WAANDIKE IKO SIKU ATAANDIKWA YEYE.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s